.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

MZEE AMETUTOKA

 

 

 

 

 

 

Related links

MZEE AMETUTOKA

Date:  03 March, 2005

Shairi la kumkumbuka mzee wetu aliyefariki baada ya miezi miwili na nusu ya kusumbiliwa na stroke. Inna lillah wa inna illaihi rajiun. Inshaallah Mola atamrehemu yeye na wote kabla yake Shairi hili limetungwa na mwanawe.

  1. Bisimillahi naanza, Nakusalia nabiya
    Mengi nitoyaeleza, Yafaa kuzingatiya
  2. Namshukuru karima, Nafasi kunijaaliya
    Utenzi kuja kusoma, Wa wetu mtanguliya
  3. Baba Mwema katutoka, Akhera katanguliya
    Machozi kwetu yatoka, Kikumbuka mazoweya
  4. Mlezi kaenda zake, Kamwe hutomsikiya
    Kaondoka peke yake , Molatamu hurumiya
  5. Miyoyo yaingia fundo, Tangu alipojifiya
    Kaondoka kwa kishindo, Mzee katukimbiya
  6. Ugonjwa ulomteka , Akaiwaga duniya
    Tulombali twateseka , Japo kwake karidhiya
  7. Japokuwa kateseka, Maradhi kumpindua
    Hikima yake rabuka, Mola hakumuonea
  8. Dhunubu kumfutia , Peponi apatengiya
    Kwake na kwa sote umma, na waliyo tanguliya
  9. Ashura ni siku njema, Sabahi kakhitajiwa
    Siku yake ya siyama, Raby kamra hisishiya
  10. Ami yetu alopema, Dua aki muombeya
    Nduguye aliyomwema , Kibaki kujinamiya
  11. Maziko yalojazana, Rehema akiombewa
    Kapelekwa kwa amana, Kituoni katuliya
  12. Dhiki zikitusakama , Nani tutamliliya
    Msikizaji kahama, Khofu kwetu zabakiya
  13. Nguzo njema yavunjika , Mola tatusaidiya
    Viumbe sote twapita , Hakuna atobakiya
  14. Ukweli usopingika, Kikumbuka waumiya
    Mwema wetu katutoka, Mzee katangauliya
  15. Haki yaumiza sana, Raby tusahilishiya
    Mrehemu yarabana, Na wote watanguliya
  16. Tuauni subuhana , Tusije tukapoteya
    Twakwita kwa lako jina, Karima Tusaidiya
  17. Mema alotutendea, Vipi tutamlipiya
    Mola alomjaliya, Kwake akijitoleya
  18. Kwa wana na wengi Umma, Sote katusaidiya
    Nini tufanye la mama, Baba kumsaidiya
  19. Tukumbuke wake wema, Dua tukimuombeya
    Kwake Jannatunaima , Mola tam ruzukiya
  20. Tusimsahau Mwema, Usiya alotwachiya
    Fattima Kumtizama, Ili apate ridhiya
  21. Mlezi kutanguliya, Siyo kama kapoteya
    Tatukutanisha naya, Mema tuki jitendeya
  22. Dua njema tupatapo, Na sadaka mtoleya
    Tusalipo tuombapo, Mema tukimtakiya
  23. Mpe nguvu wetu Mama, Na wazazi jumuiya
    Afya na umuri mwema, Walikatika duniya
  24. Yamani tukidhiya, Haja zetu kisikiya
    Wote walotanguliya, Ghafuru Tawajaaliya
  25. Khusunul khatima njema, Tulobaki tujaliya
    Qalima Tukiisema, Tuiwagapo duniya
  26. Tupate wakutuzika, Mema waki tuombeya
    Mzee awe kafika, Peponi Kitungojeya
  27. Muweza wa yote piya, Dua tuta qabaliya
    Kwa pekee msikiya, Kwako tuna tegemeya
  28. Twaitikia labeika, Waja kwako twatubiya
    Situwache kuteseka, Na mwsiho tukapoteya
  29. Amina Raby Amina, Rasuli Twamsaliya
    Kwa baraka zake Bwana, Maombi tu pokeleya

Imeletwa na Anonymous

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet