|
|
Nchi Yangu
Date: 20 August, 2005
- Nimependa, Nimependa hadi
Sitarudi, Pale nilipokwenda
Sitashindwa, Kwa wangu muradi
Nchi yangu
- Nchi yangu, Ndio wangu mama
Ulikwisha, Kumeza machungu
Jina langu, Kupata heshima
Nchi yangu
- Wangu baba, Bwana familia
Unolea, Kwa mema mahaba
Na msiba, Ukifagilia
Nchi yangu
- Ndio mke, Hariri ya moyo
Nipendayo, ulonayo peke
Unishike, Tukishinde choyo
Nchi yangu
- Una shida, Ndani ya hikidi
Maanidi, Wamo wakugida
Shika ngoda, Piga mafisadi
Nchi yangu
- Uchecheme, kujivuta mbele
Ipo ndwele, Fanya usimame
Fanya shime, Inuka mvyele
Nchi yangu
- Siwe nyuma, Muda kumekucha
Kijiacha, Sipo jisukuma
Aja nyuma, Shetani makucha
Nchi yangu
- Nchi yangu, Ninayoipenda
Nchi yangu, Damu inokwenda
Nchi yangu, Haki utashinda
Nchi yangu
Shairi : Maalim Abbas M. Mdungi
Limeletwa na Salma Said katika Makala ya Nabwa
|