.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Nguvu za Mola

Related links

Nguvu za Mola

Date:  20 August, 2005

  1. Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi
    Kula,kunywa na kulala, Mola ndiye mfanidi
    Mwenye hekima na hila, Pia na nguvu shadidi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

  2. Sitaikata tamaa, Kufanikiwa muradi
    Nangojea yangu saa, Saa ya Sada na Sudi
    Dini yetu ndio taa, Yamurika mahasidi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

  3. Ukilea mwana mwema, Mola atampa sudi
    Nazo tumwa za rehema, Za Mtume Muhammadi
    Zitakutunza makama, Siku isiyo baidi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

  4. Ama wanotakaburi, Mashetani wa Biladi
    Kuna siku ya khatari, Anokwenda hatarudi
    Njia yetu ni kaburi, Njia ilo maridadi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

  5. Amali ulizotenda, Ndizo zinokupa kadi
    Roho itakapokwenda, Mbele ya Mola wadudi
    Utaoneshwa sana, Na hilo halina budi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

  6. Waliasi makafiri, Na kujitia taadi
    Wakijiona hodari, Kumtesa Muhammadi
    Roho zao zikiguri, Usiyahi utanadi
    Nguvu zao na za Mola, Ni zipi zilo shadidi

Shairi : Maalim Abbas M. Mdungi
Limeletwa na Salma Said katika Makala ya Nabwa

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet