|
|
Wanichukia
Date: 06 December, 2005
Nawasilisha hapa shairi lililoandikwa na ndugu yetu, Khatib Mohammed Khatib, ambaye baada ya
uchaguzi wa mwaka huu hapa petu ni miongoni mwa wanaokumbwa na vitimbi vya chuki ya ubaguzi
iliyomezeshwa kusudi vichwani mwa Wazanzibari.
Anaishi eneo la Fuoni, Wilaya ya Magharibi, na kuna bwana mmoja ambaye amekuwa akiingia katika
himaya yake na kumfanyia uharibifu wa makusudi huku akijigamba: "Nyinyi ni wakuja tu hapa. Nani atakayenizuia mimi?"
Bahati mbaya, Khatib hajawa mwanachama wa ukumbi huu, lakini aliniomba ikiwa naweza kumpatia
bega la kulilia huzuni zake popote pale pawapo. Nami nikaona katika ukumbi huu muna Wazanzibari wenzake
ambao wanaweza kulia naye kilio.
- Unanichukia bure, sababu usuli wangu
Waniombea nirure, yanishukie machungu
Kwa lolote unikere, usonone moyo wangu
Ni bure wanichukia
- Unanifanyia shere, wauviza utu wangu
Wanipigia misere, hadi barazani kwangu
Wasema hatuwi sare, wanifanyia mizungu
Wanichukia bure
- Waniletea ukware, wanibughudhi kwa vyangu
Nikijikuna upere, waungulika mwenzangu
Kama kikuku kuchere, waniinga nendezangu
Ni bure wanichukia
- Cheo cha mwanasesere, kwako ndiyo hadhi yangu
Wanichomeka mishare, wakazia na marungu
Nipige uniburure, mimi namwachia Mungu
Wanichukia bure
- Nimeshakuwa bwerere, mbeleyako mlimwengu
Wanipiga sasambure, wanivunjia na vyungu
Illahi si “kamzore”, anayo yako mafingu
Ni bure wanichukia
- Tunduni kama “tetere”, taabani haliyangu
Ninahofu, tere - tere, sina hata “sungu sungu”
Wavizia unipore, “yaailahi mola wangu”
Wanichukia bure
- Ya Rabi hapa nikore, nalibana chozi langu
Uwabane waniture, ya Rabi wababe wangu
Migongoni uwachore, “WASALITI ULIMWENGU”
Wanichukia bure
- Nyuso zao wazipare, ziwe weusi wa chungu
Waongezewe upere, wajipare kwa uchungu
Wakome kiherehere, sili sili ziwe pingu
Wanichukia bure
- Kula yao wachekure, wangie kizungu zungu
Nyonga zao waburure, kama kidege makungu
Wajue waja si bure, dhuluma jazaye chungu
Ni bure wanichukia
Limetungwa na Khatib Mohammed
Limeletwa na Mohammed Mohammed
Wanichukia
Date: 07 December, 2005
- Huyo akucheza shere, akuzongezonge pingu
Kelele zisikukere, aso mtu ana Mungu
Yamemshinda Mabere, aweje mramba vyungu,
Ni bure akuonea.
- Utamsibu upere, ajikune rwangu rwangu
Hata mbele ya wavyere, soni hana mpwa wangu
Angie kiherehere, ishamshinda mizungu
Lako shitakia Mungu.
Ahmed Rashid.
Wanichukia
Date: 07 December, 2005
- Napenyeza yangu pyere, ndani ya shairi langu
Ukweli meona gere, gere la haki si jungu
Shairi tamu ya ndere, kuletwa bila virungu
Vumilia,
- Naomba ndugu wa "kureeee!!", uvumilie viwingu,
Usipige "makerere", bora nyamaza kizungu
Sheria kazipekure, pia muombe na Mungu
Vumilia.
Mohammed Omar
Wanichukia
Date: 07 December, 2005
- Ndugu zangu sikizeni, haya ninayowambia
Musiwe malimbukeni, watu kuwatumilia
Mukaingia vitani, bila nyinyi kujijua
Majuto ni mjukuu, Kilio huja mwishoni
- Vita hivi ni ya nani, ndugu mnatumiliwa
Silaha zimkononi, Nyote mmedhamiria
Tusichezee wattani, tutakuja jijutia
Majuto ni mjukuu, kili huja mwishoni
- Kila mshika mpini, silaha kuichezea
Aangalie ni nani, aliyemkusudia
Ni ndugu wa ubabani, au wa mama mmoya
Majuto ni mjukuu, Kilio huja mwishoni
- Tutakuwa simanzini, siku moja nawambia
Tutajiuliza moyoni, kilio tutaomoa
Hatuuoni wattani, sasa umetukimbia
Majuto ni mjukuu, vilio huja mwishoni
- Wa kulaumiwa nani, ukweli utawadia
Ni ndugu wa maduguni, au ni wa tumbo moja
Au ni yule jirani, Ndie alotuchezea
Majuto ni mjukuu , Vilio huja mwishoni
- Watoto wetu mashaka, ndio yatayowavaa
Si mtoto wa Mashaka, Wala wa ndugu Vua
Wote watapita shida, familia itasambaa
Vilio vitawajaa, Majuto yatatovaa.
- Haraka imenizidi, mimi mwingi wafadhaa
Wattani si ufaidi, ugeni umenijaa
Kalamu naweka chini, ninakimbia udhia
Majuto ni mjukuu, Vilio huja mwishoni
Anonymous-126
|