|
|
Nyumbani ni Nyumbani!
Date: 28 May, 2006
- Nikikumbuka nyumbani, hukaa najinamia
Hujiona maskini, ingawa navumilia
Ukweli siko rahani, rohoni ninaumia
Ugeni si kitu chema, maskini mtu kwao
- Nyumbani hakurudiki, watu wamekuvamia
maisha yako ya dhiki, wamrima watanua
Uhuru hausemeki, woga umetujalia
Ugeni si kitu chema, masikini mtu kwao
- Ninakumbuka udogo, tulivyo tukitulia
Hakukuwa na vichogo, waungwana weenea
hatukuona mgogo, kahawa kujiuzia
Una karaha ugeni, masikini mtu kwao
- Ninaporudi kazini, kucha ndani hubakia
computer ukumbini, na TV kwangalia
macho hufika huoni, mionzi mekujalia
Masikini mtu kwao , ugeni si kitu chema
- Ibada ni mtihani, swala hujipitilia
Darasa misikitini, hadithini hubakia
Watu hawajali dini, dunia wafikiria
Ugeni si kitu chema, masikini mtu kwao
- Iko siku tutarudi, sisi ni wavumilivu
Na wasomi ikibidi, waje waongeze nguvu
na mola atatuhidi, hatutofanya maovu
Ugeni si kitu chema, masikini mtu kwao.
Anonymous 282
|