.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Jamanani Mbona Vishindo!

 

 

 

 

 

 

Related links

Jamanani Mbona Vishindo!

Date:  20 April, 2006

  1. Jamani msiwe kando, Muone ya duniani
    Zilizali kwa vishindo, Vimbunga na matufani
    Vinagonga kama nyundo, Havisiti abadani
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  2. Tsunami ilibashiri, Kimbunga cha baharini
    Indonesha Kashimiri, Bara Hindi na Japani
    Ikafika taathiri, Hadi kwetu visiwani
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  3. Katirina kikafwata, Kikaja kikinguruma
    Mvua bila kusita, Na upepo wa naqama
    Miti ilikatakata, Na majumba yakazama
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  4. Kikaja kimbunga Rita, Dharuba ya ufukweni
    Kilipiga na kusita, Ikawa ni afueni
    Kwa haraka kikapita, Mitaa ya pwani pwani
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  5. Kukazuka zilizali, Bara hindi Afghani
    Kilishitadi ukali, Nchini Pakistani
    Roho pia amuali, Hasara iso kifani
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  6. Sasa bara Afrika, Ukame umeenea
    Njaa isiyosemeka, Miti haitaki mea
    Mazao yaatilika, Na roho zinapotea
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  7. Baharini na barani, Ufisadi wadhihiri
    Bila hofu ya Manani, Maasi yanakithiri
    Hatujali hatuoni, Tunavamia kikiri
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

  8. Wapi tunaelekea, Mbeleni hatutizami
    Ina ghururi dunia, Tunaona hatusomi
    Hatutaki kusikia, Tunazidi hatukomi
    Ufisadi wadhihiri, Baharini na barani

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet