|
|
Msalieni Nabiya (S. A. W.)!
Date: 19 April, 2006
-
Mola amemswalia, Kipenzi chake Hashimu
Kisha wakafuatia, Malaika wakarimu
Na nyinyi umma jamia, Swalini mumsalimu
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Na Swahaba zake pia, Ziwafikie salamu
Wao walitangulia, Kunusuru Isilamu
Yarabi Mola Jalia, Waja wako warehemu
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Kifua kapanuliwa, Hana shaka wala dhana
Utajo kanyanyuliwa, Kwa shahada na adhana
Mizigo kaondolewa, Dini yake ikafana
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Katuletea risala, Ujumbe kaueneza
Kaamsha walolala, Wakauona mwangaza
Mefika kila mahala, Nuru ameisambaza
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Kakileta Jibrili, Mtume kakipokea
Kitabu kilo kamili, Kiso shaka Katwambia
Na vizimwe vibatari, Mwanga ushatufikia
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Kandili zote zimeni, Tunacho cha kuonea
Maneno Yake Manani, Risala ilotimia
Uwongofu Qur-ani, Kwa amchae Jalia
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Kote zimeshaenea, Baraka za Subuhana
Nuru katufikishia, Muhamadi kwa amana
Nasi tumeipokea, Jamii muuminina
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Kitabu hiki adhimu, Mola ameweka wazi
Kupitiwa na kalamu, Za viumbe hakiwezi
Jinni wala binadamu, Kakihifadhi Mwenyezi
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Sunnah ilotahirika, Kufuata ni lazima
Mafunzo yenye hakika, Ilimu na tarjima
Ni kauli ziso shaka, Maneno aliyosema
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
- Awe ruwaza njema, Annabiyul khatimu
Tusiwe tu twasema, Tufuate kwa timamu
Kufuata ndiko kwema, Uzushi hautodumu
Msalieni NabiyaNa ali zake kiramu
- Ya Rabbi Mola Adhimu, Tunakuomba atiya
Ya Rabbi utukirimu, Utuweke na Nabiya
Na Sahaba wakarimu, Walofuata yake njia
Msalieni Nabiya, Na ali zake kiramu
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
|