|
|
Mumetusaliti!
Date: 10 January, 2006
-
Wambie wambie, twaafiki, uliyotwambiya
Kawahutubie, wanafiki, wasio na haya
Sema wasikie, yastahiki, kuwapasuliya
Walimwengu tupo twasikiya!
-
Kila msaliti, na yeyote, anayewasifu
Na akawasuti, sifa zote, za watakatifu
Huyo afiriti, si lolote, ana hitilafu
Sio muungwana ni mdanganyifu!
-
Iwe ni Padiri, wa dhehebu, linalotajika
Shekhe wa kadiri, kwa vitabu, alivyovishika
Hebu tafakari, kwa karibu, anayotamka
Wake umahiri unatia shaka!
-
Wasomi kalamu, na wenzao, walionyamaza
Hutaka zidumu, kazi zao, kwa kuwapongeza
Hawa madhalimu, basi nao, bora kupuuza
Na ikibidi kuwaapiza!
-
Na hao wengine, waadhama, uliowataja
Zao dane dane, sio njema, Pemba na Unguja
Damu kwa matone, kwa majuma, kwetu ikivuja
Kwao wao si kioja!
-
Mwisho sina budi, kuungana, na wetu malenga
Kwamba Mohamedi, vyako vina, umevikuunga
Wewe si baidi, tunga tena, nyoyo ukikonga
Ndipo utaona raha ya kutunga!
Kassim O. Ali
|