|
|
NCHA YA KISU KOONI!
Date: 09 March, 2006
-
Nakupeni yalo ndani, ya ng'o hatukubali
Sio ya mkahawani, au baoni ya kweli
Mazito yako kooni, kwao ni kitendawili
Baba fimbo mkononi, watoto na wafadhili
-
Si uvumi pata shika, shinani Kisiwanduwi
Ngumi mtu chupa ruka, wachungu huwaelewi
Mvute nguo chanika, walivyo kama wachawi
Makonde ya mwangaruka, na nyimbo hatuitowi
-
Kaja kutoka mrima, mdogo wa baba yao
Kupatanisha hasama, ya wawili chombo chao
Kwaheri chenda mrama, zimekwisha zama zao
Haya maneno mazima, shikeni yawe ni tao
-
Hazitimu siku tatu, ikafata msijue
Si ya kupigwa upatu, wala beni mtambue
Wevi warudisha chetu, haki yetu tuchukue
Tuijenge ngome yetu, na mazuri tuamue
Maher ( Unique )
|