.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ngoma yataka matao !

 

 

 

 

 

 

Related links

Ngoma yataka matao!

Date: 26 May, 2006

  1. Macheza hawi kiwete, ngoma yataka matao
    wala usiwe na tete, utulie kwa kituo
    wala haitaki kete, ufuate michapuo
    Mcheza hawi kiwete ,ngoma yataka matao

  2. Itabaki kujisifu, yalaiti huwa mwao
    utasikia harufu, hayo si mafanikio
    udume mintarafu, ndio utakiwao
    mcheza hawi kiwete , noma yataka matao

  3. Action ni muhimu, mijadala baadae
    mtaka unda hudumu, haneni kwa ajuae
    itabaki kulaumu, lengo haliji milele
    mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

  4. Shati ufate midundo, sibaki kurukaruka
    la sivyo kaa kando, taishia kuanguka
    unapokuja mkondo, simama kwa uhakika
    mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

  5. ngoma huwa na vishindo, yabidi uwe imara
    itaingia mipindo, usifanye masikhara
    Hamadi kwenye kibindo, silaha huwa ishara
    mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

Anonymous 282

Ngoma yataka matao!

  1. Ngoma haina ujuzi, haichaguwi umbile
    Kwa mchezaji si kazi, ni mdundo na kelele
    Haiwi kiziwi wazi, hulishika tao mbele
    Akawashinda wajuzi, kwa kuona yalo pale

  2. Kama kiwete kilema, kusudi lako miguu
    Kaa ufahamu vyema, kuna mikono ya juu
    Hushika ikasimama, wala si shughuli kuu
    Hawafunzwi kinamama, siwako ukumbi huu

  3. Hutiwa mtu kilema, akashindwa kupuliza
    Na mwili wake mzima, kichwa kikampooza
    Zumari yake hugoma, kwa ukwaju ulooza
    Hubaki mate kutema, Mambo hakuyamaliza

  4. Kucheza kuruka ruka, na khatua kuzifata
    Ndipo ya kweli husaka, kasi unayotafuta
    Mwendo ukaengezeka, karibu ukaivuta
    Ikawa mwako hakika, hufiki utajikuta

Maher ( Unique )

Mcheza hawi kiwete!

Date: 27 May, 2006

  1. Kiwete si maumbile, ni mapungufu fulani
    aso hili ana lile, ni maumba ya manani
    kuna viwete wa fani, ni hali ya Insani
    Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

  2. Huyu mama Senkoro, siasa zimemshinda
    ni kiwete wa medani, aliwekwa njia panda
    Ni daktari makini, wa hospitali za kanda
    Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

  3. Kucheza ni kubwa fani, ukae ukitambua
    watu hupata nishani, kwa kuweza majukwaa
    lazima ujiamini, la si sivyo tajikwaa
    Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

  4. Kwa hili nasisitiza, kiwete sio kilema
    kiwete hugizagiza, na mwingi wa kulalama
    mchana huona giza, hubakia kuyoyoma
    mcheza hawi kiwete ngoma yataka matao

  5. Kutojua si vibaya, natakiwa kujifunza
    usiwe waona haya, ukenda kwa kujibanza
    utaikosa hidaya, tabaki kujiliwaza
    Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka matao

Anonymous 282

Mcheza hawi kiwete!

Date: 28 May, 2006

Sasa nimekuwelewa, nini hasa lengo lako
Uliyonena ni sawa, umempata aliko
Yatokota yake dawa, epuwa juu ya jiko
Mpe chungu atapowa, umwache uwende zako

Maher ( Unique )

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet