.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ntampiga kwa mbali !

 

 

 

 

 

 

Related links

NTAMPIGA KWA MBALI!

Date: 06 April, 2006

  1. Fundi hatafuti mbili, moja ya ndani yatosha
    Wala sitangi kwa hili, cha mbele huporomosha
    Kama haya hukubali, kiweke takuonesha
    Ntakipiga kwa mbali, kama nnakiamsha

  2. Iwe ndogo ya sindano, tundu ya kiasi hicho
    Umbali uso mfano, kipande ukijuwacho
    Sitouma yangu meno, wala kupepesa jicho
    Ntakitowa kibano, kiruke kisiwe nacho

  3. Sisaki kwenye vichaka, kwa mshare na upinde
    Langu ni pori la nyika, mkuki huwa upande
    Nikirusha nihakika, wateleza na umande
    Ukapiga kwa haraka, akafa na usigande

  4. Sasa nnakuwalika, twende sote usasini
    Shuruti hutoshituka, kuyaogopa majani
    Au vinopukutika, nakuanguka mitini
    Tukamkamate nyoka, tumtiye guniani

  5. Yako ya mbali ifiche, fimbo usije muuwa
    Akitoka bora mche, hapendi kukaribiwa
    Usijifanye macheche, kutaka kumraruwa
    Atakudhuru muwache, ana moto usojuwa

Maher ( Unique )

NTAMPIGA KWA MBALI!

Date: 07 April, 2006

  1. Usianze kumtisha, mfanya hapigi kelele
    Alolala waamsha, mtama kwako uwele
    Wataka taji kuvisha, kalamu zako za kale
    Kubishana kumekwisha, wala sipige kelele

  2. Suala hapa sindano, ukubwa wake mdogo
    Umejifanya mbano, madhumuni ni mtego
    Meno yako sio chano, wala kipande cha gogo
    Napenda wako mfano, kunitekenya kwa zogo.

  3. Hayo yako ni kuwa, husaki kwenye vichaka
    Wasasi wote wauwa, hilo kwako sioshaka?
    Sifa yako watunguwa, kumkosa ni mashaka
    Yako yanokusumbuwa, sababu wajianika..
  4. Umeanza kutapika, usasi wako ukoje?
    Si ndege wala si nyoka, yoyote yule naaje
    Kiumbe akiibuka, yawa mafusho mvuje?
    Muhimu kwako kafika, huulizi kama muje

  5. Wababaisha umati, silaya yako iwache
    Papohapo ni machati, kwanini huanzi cheche ?
    Muingie kati kati, manunguniko yawache
    Sifa yake huipati, milele atabakia ni Che.

Hashil Seif

NTAMPIGA KWA MBALI!

Date: 07 April, 2006

  1. Usasini ni kunyata, wa huko miguu chini
    Chini utawaokota, hadhari uwe makini
    Makini wakutafuta, rangi ya macho kichwani
    Kichwani ukipapata, nyama imo mikononi

  2. Pori lina ushujaa, kuwinda ni kuvizia
    Kuvizia bila taa, ukitega wakilia
    Wakilia huzubaa, ndipo ukauwachia
    Ukauwachia chaa, mkuki ukamwingia
  3. Usingoje akufiye, uwache ukiwa ndani
    Ndani utowe aliye, umbane mikononi
    Mikononi mzuwiye, utowe kisu alani
    Alani hadi shingoye, umchinje kiwa chini

Maher ( Unique )

NTAMPIGA KWA MBALI!

Date: 07 April, 2006

  1. Neno usasi kuua, kisu bunduki mkuki
    Msasi anachagua, kama meno msuwaki
    Kitandawili tegua, au nyanyo Mzandaki?
    Nimechoka kupumua, mbele naona hilaki.

  2. Ushujaa sio pori, yule anaechagua
    Sijui kama ngangari, au ngoma ya kilua
    Hii ni defu safari, ukutanayo yaua
    Hata uwe mwari, kipimo chanisumbua !

  3. Yamwisho kwako mauti, mikononi akufia
    Viko vifo vya njukuti, vyengine moto fifia
    Kitakiwacho si suti, nakudengua kofia
    Hata uwe huna shati, jumba kuu kuingia.

Hashil Seif

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet