.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Yaliyomkuta Sahib yangu !

 

 

 

 

 

 

Related links

Yaliyomkuta Sahib yangu!

Date: 01 June, 2006

  1. Nnasahibu mpenzi,umri wake makamo
    Amejitia kitanzi,moyoni ndimo kiwamo
    Kampata mwanagenzi,mwari na chake kisomo
    Utadhani mbaa'mwezi,mashaalla ana kimo

  2. Alikuja nishauri,kuwa anakwenda posa
    Nikamwambia subiri,ndoa inataka pesa
    Na kanzu ilonzuri,na naali za kisasa
    Hakupinga akakiri,kingoja yangu ruhusa

  3. Nyuma akanizunguka,akenda kwa baba'ake
    Asimkute katoka,mama yupo peke yake
    Maneno yalomtoka,kuwa anataka mke
    Mama roho menutsuka,akamwambia atoke

  4. Machozi yanamtoka,kaja kwangu analia
    Huku akinung'unika,hajui lakunambia
    Mambo yameshamfika,asiyo yatarajia
    Kahisi keshamtoka,hakuna nyengine njia

  5. Tukaifunga safari,kumtafuta babaye
    Ilikuwa laasiri,tulipo onana naye
    Tukampa yetu siri,twamtaka bintiye
    Ni muungwana jasiri,kajibu tukaribiye

  6. Baba katoa shuruti,kwa mwanawe kumtowa
    Anazitaka yakuti,kilo bila kupunguwa
    Apewa nyumba binti,na khati kuandikiwa
    Ndipo atapodhibiti,bintiye kuolewa

  7. Tukapewa wiki mbili,tulete yetu jawabu
    Katuvuruga akili,tukabakia mabubu
    Kuzipata hizo mali,yataka nyingi sulubu
    Hata miaka miwili,sirahisi kwa sahibu

  8. Nikamwambia mwenzangu,kila jambo linakheri
    Limeandikwa na Mungu,Kukuepusha na shari
    Hili sio lako fungu,jikaze onesha ari
    Najuwa unauchungu,sahau nakushauri

  9. Tukakifunga kitabu,kwa nyuzi kukishonea
    Yalo sibu yamesibu,kule hatukurejea
    Ikawa ndio jawabu,baba kumpelekea
    Tulihisi ni aibu,kwake tena kumwendea

Barkoa007

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet