.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

BUNGE LOTE LASINZIA!

Related links

BUNGE LOTE LASINZIA!

Date: 12 April, 2008

  1. Raia wa Tanzania, Bara visiwani pia,
    Hivi kweli mnajua, kuwa bunge lasinzia,
    Posho wanajichotea, na ‘mishangingi’ sawia,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  2. Aibu inatokea, picha zinapotwaliwa,
    Wabunge wa Tanzania, bungeni wanasinzia,
    Wageni wanadhania, ni utani si sheria,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  3. Spika kawaambia, ruksa kujilalia,
    Ila amewausia, mkoromo kuto-toa,
    Walale kwa kusinzia, na ute kujitolea,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  4. Chaguzi imewajia, wa Tanzania raia,
    Mbio watawajilia, kura mtawapigia,
    Wabunge tawaambia, mema tutawatendea,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  5. Muswada ukijilia, kwa kura kupitishia,
    Kwa wingi wamezidia, wapinzani wanalia,
    Vijembe tawapigia, na kedi tawafanyia,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  6. Vema mkijiandaa, kura kuzikazania,
    Kuchagua wanofaa, wenye na haki sawia,
    Bunge - enda likafaa, miswada kujadilia,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

  7. Beti nane natulia, nazidi sisitizia,
    Haki kuikazania, viongozi kuchagua,
    Bungeni wende kukaa, macho-pasi kusinzia,
    Bunge lote lasinzia, ndoto ni posho na gari.

Abdalla Sani

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet