|
|
KWANUKIA!
Date: 21 January, 2008
- Bismillahi naanza, wa Rehema Rahamani,
Wakili ulo muweza, Subihana Maanani,
Maliki mwenye kujaza, ya dunia na mbinguni,
Wabarakatau walid, mtetezi wa Kuduri!
- Mtoto nipe kalamu, nikae chini nitunge,
Niyasema yalojimu, kwa tungo chache nipange,
Lile niloazimu, la mafisadi nilonge,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
- Kikwete ataliweza, la kumfunga kengele,
Paka mwenye kujikuza, ajaye bila kelele,
Ili watu kuwajuza, hatari iliyo mbele,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
- Au ndiyo imetoka, kama mabasi ya Keko!
Balali kishatimka, katuacha na mbeleko,
Mgonja akichopoka, kama kinyaa na toko,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
- Mapesa wameyachota, Kikwete yu njia panda,
Ni sime atajikita, Jitu Pateli adunda,
Mwenye kupata kapata, walokonda wamekonda,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
- Mramba mtapata, akaishie Maweni,
Au twacheza kalata, magelesha ni yanini,
Na wengine watanata, au ndiyo magirini,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
- Beti zangu zinakoma, usingizi wanibana,
Nyani huyu twamkoma, si Ngabu hilo bayana,
Fisadi tutawazima, kama kupe kuwakana,
Mkapa atiwe pingu, asimamishwe Kisutu?
Makame Haji Ussi
|