.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

MATUNDA YA MAPINDUZI!

 

 

 

 

 

 

Related links

MATUNDA YA MAPINDUZI!

Date: 16 January, 2008

  1. Fumbo tena si fumbo, si siri bali dhahiri,
    Kikao wenye matumbo, kiliketi Zanzibari,
    Kwenye mambo na vijambo, kutangaza ubepari,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  2. Ukitaka Uraisi, karatasi milioni,
    Wa kwanza huo ukwasi, pesa zisizo na deni,
    Kwa fukara si rahisi, japo uwe na tamani,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  3. Na kisomo siyo shani, uchao wanabadili,
    Bado kwenye kampeni, na mchujo wa batili,
    Siasa za mumiani, wengine kuwa dhalili,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  4. Ubunge ni laki moja, fomu sasa biashara,
    Ni chama chenye vioja, sasa hivi ni mnyura,
    Kizee chajikongoja, kimepoteza taswira,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  5. Ni ruba sasa si chama, kimeacha maadili,
    Pesa ndio zinasema, imetoweka asili,
    Mfumo huu dhuluma, mimi nisingekubali,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  6. Ningekulikuwa Mjumbe, kamwe nisingeafiki,
    Chama kimekuwa wembe, kwa mnyonge akishiki,
    Unyanyaso kwa viumbe, bila pesa hauvuki,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  7. Japokuwa Udiwani, ulipe elfu kumi,
    Wenye kipato cha chini, umeshakuwa unyimi,
    Wewe uwekwe pembeni, ijapo uwe msomi,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

  8. Milango kwa upinzani, ndio kuliko bakia,
    Tuibadili ramani, kikongwe kumfukia,
    Tena hatumtamani, sasa kibaki mkia,
    CCM ina wenyewe, wengine ni wapagazi.

Abdalla Sani

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet