|
|
NI MOYO AU AKILI!
Date: 23 January, 2008
- Nauliza mujuao, Mulio na nyingi fani
Watu na elimu zao, Magwiji na Magogeni
Nimekwama hadi leo, Mebaki mushkelini
Unaopenda ni moyo, Au akili kichwani?
- Wengi niwasikiao, Kila kona mitaani
Husema mioyo yao, Meingia mapenzini
Sisikii wasemao, Yamengia akilini
Naulizia Ni Moyo, Au akili kichwani?
- Hodari wasifiwao, Madarasa na Shuleni
Hutajwa akili zao, Moyo haujulikani
Naufikiria moyo, Hapa una kazi gani
Ndio kweli upendao, Au akili kichwani?
- Moyo ndio upigao, Damu ikenda mwilini
Kama tasimama leo, Ni kuzikwa kaburini
Nakubaliana nao, Hapo sina upinzani
Unaopenda ni moyo, Au Akili kichwani?
- Fikira na mengineyo, Hapo ndio mtihani
Kila Ucha na Uchao, Siuoni ulingani
Sijui undani wao, Wamekusudia Nini?
Unaopenda ni moyo, Au akili kichwani?
- Sio watu Peke yao, Bali hata vitabuni
Kila ncha uendayo, Ulaya na Arabuni
Kauli ndo hiyo hiyo, Moyo kitiwa kinywani
Naulizia ni moyo, Au akili kichwani?
- Masuali ndio hayo, Jibuni Mlo Makini
Msikimbilie mbio, Kuna mteno wa ndani
Kuyajua yasemwayo, Kunataka Umakini
Unaopenda ni Moyo, Au Akili kichwani?
- Niliyouliza hayo, Kabisa sio utani
Mimi nina shida nayo, Niondoke utatani
Ka Bakari na wenzio, Jama Nisaidieni
Naulizia ni moyo, Au akili kichwani?
Amour Rashid
|