|
|
RISALA KWA MAALIM HASHIL!
Date: 30 April, 2008
- Maâlim Hashil sogea, leo tupate ongea
Haidari kachochea, Wakomoro kupokea
Kwa haya yalotokea, haki yako kutetea!
- Kwa kweli umebobea, na haya yakuelea
Bob Denard kutulengea, mamluki kutupondea,
Komoro yateteketea, hapana pa kusemea!
- Haya yote nakwambiya, Faransa imepania,
Komoro kuangamia, faida kujipatia
Mayotte kuikalia, msingi wa hayo pia!
- Hawa kina Haidari, wao kweli mahodari
Ngazija si kachumbari, si nguru wala jodari
Wafanyeje ya fahari, nyama imetaghayari!
- Kwa leo nakuachia, ujue si rakhisia
Vituko vya Komoria, ukoloni jahiliya
Jeshi hilo Afrikiya, ni sawa na mabandia!
- Mwisho hapa tunaweka, wino na kalamu pia
Hatuna pakueleka, si kichochoro si njia
Tumeshindwa na kufyeka, seuze pa kufagia!
- Wajibu wako Maâlim, kufunguwa yetu macho
Usingojee ya Muusim, kufichua ujuwacho
Hata ikiwa ni Muslim, usiche jicho la kwacho!
salim Himidi
|