|
|
UKUMBI UMEDORORA!
Date: 03 January, 2008
- Ukumbi ulidorora, sasa umechangamka
Tulete yalio bora, tusije kuchawanyika
Tusitembeze bakora, kuja kuchanja nyika
Ukumbi huu imara, watu hawatabanduka
- Zitoke kila idara, habari zikitendeka
Wala isiwe kafara, ukumbi kumahanika
Yataka nyingi busara, walolala kuamka
Ukumbi huu imara, watu hawatabanduka
- Tusionyeshe hasira, pale tunapoamka
Tulete nyingi tijara, jua kupambazuka
Tusifanye masikhara, ukumbi kuchakarika
Ukumbi huu imara, watu hawatabanduka
Ali Abdulkadir
UKUMBI UMEDORORA!
Date: 03 January, 2008
- Ukumbi wetu ni bora, si wa kutanga na nyika
Hauhitaji bakora, wala kadi kualika
Risala zaja tikrara, soma bila ya kuwika
Sidhani watabanduka, wasemao wadorora
Professor Ibrahim Noor
UKUMBI UMEDORORA!
Date: 03 January, 2008
- Kweli msemayo ni kweli, Mwinyi Ibrahima na Ali
Kwa yote haya yakifeli, sote kukosa yetu mali
Hasara si za makubeli, na kabwela hana amali!
- Hapa pia natawakali, tangulize yetu imani
Kwani kidogo si a'kali, kukutana sote jamani
Zendjibari ni Biriyani, si mseto wa Makuhani!
- Mwasemaje nyi wanawari, wenye hii njema Bustani?
Kudorora si afu'ali, za kutengana na wandzani
Huyisha yetu Zinjibari, ewe Mola wa Manani!
- Hapa tamati nastakari, yangu tamaa kuvumbika
Na wallahi sijakubali, kuwa Jogoo hatowika
Kiza hufuatwa na nari: yuwapi atakae pinga?
Salim Himidi
|