.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Akanidanganya!

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Akanidanganya

Date:  July 1 - 2004

  1. Akanidanganya, akanambia takuja, hafikwa n'tabu, na mashaka na mauja
    Kaniparaganya, nami meishiwa hoja, yaliyonisibu, meona bora kuyaroja
    Nataka waonya, haya yangu si kioja, na wewe sahibu, upime na kuyachuja
    Yaliyompata Mtoja, yemfika na ..... mmoja. (Kassim Ali)
  2. Akanighilibu, kumbe yeye ni laghai, na hana ahadi, ni vyema kumuepuka
    Mtu wa ajabu, mbaya, tena hafai, na pia fisadi, ni mbovu zake hulka
    Aweza jaribu, kuja kukurai rai, akipiga hodi, kwako mlango shindika
    Yaliyompata Mtoja, yemfika na ..... mmoja. (Kassim Ali)
  3. Amenifisidi, nyingi sana zangu mali, sio mtu mwema, tapeli, mdanganyifu
    Aliniahidi, kwa hila za kifedhuli, kumbe anichuma, jangili mla nyamafu
    Nalizikaidi, nasaha zake ahali, mauja me'kwama, jahili la takilifu
    Yalompata Mtoja,yamemfika na? mmoja. (Ahmed Rashid)
  4. Akanipumbaza, kwa tabasamu na cheko, tegoni hangia, nduyenu hapumbazika
    Sasa kajibanza, vimondo tele mbeleko, mwenzenu nalia, mashaka yamenifika
    Mepondwa cha pweza, mejaa masikitiko, mwenza angalia, usije kuhadaika
    Yalompata Mtoja, yamemfika na? mmoja. (Ahmed Rashid)
  5. Ya nini mayowe, kuteleza ni kusoma, kakushinda tonge, mshinde kwa matoezi
    Hila zitambuwe, usibaki kulalama, usiwe mnyonge, inuka wacha ajizi
    Yawahi mwenyewe, sipembejee huruma, hata awe nge, nguruma aone kazi
    Yaliyompata Mtoja, yemfika na ......mmoja (Saleh Barkey)
  6. Yataka vilinge, hila na ujanja mwingi, ndio umshinde, ukipate utakacho
    Kaweka mazonge, na vingi sana vigingi, wengi maafande, mezagaa kama kocho
    Mefanya vigenge, kampeni na mitingi, ni nini nitende, nimzibe yake macho?
    Yaliyompata Mtoja, yemfika na ......mmoja (Kassim Ali)
  7. Ngoma ivumayo, mwishowe ni kupasuka, miko ni imani, na mipango kuisuka
    Kama huna moyo, lijalo wababaika, atakubaini, akuzidishe mashaka
    Ni mengi yajayo, sikuye nae tafika, uwe furahani, kiteweji kimteka
    Yaliyompata Mtoja, yemfika na ........mmoja (Saleh Barkey)

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet