|
|
Utangulizi
Katika kila ustaarabu, kuna vitu ambavyo huwa ni fakhari kwa wenye ustaarabu huo. Ustaarabu wa Kiswahili si ustaarabu wa jana na juzi, ni ustaarabu wa muda mrefu sana. Moja ya fakhari za ustaarabu huo ni tungo za kishairi. Tungo katika ustaarabu wa Kiswahili zina historia ndefu na si lengo letu hapa kugusia jambo hilo. Hata hivyo kitu kimoja ni lazima Waswahili tujifakharishe kwacho, nacho ni utajiri wa lugha hiyo katika fani tungo. Utajiri uliomo katika lugha hii telezi kuitamka tamu kuisikiliza wa methali, misemo na maneno ya hekima, ni uthibitisho kwamba imetoka ndani ya mifupa ya Waungwana waliojali sana wanachokisema tangu siku za kale. Kwa wataalamu wa lugha hii na historia yake wanajua vyema jinsi msemo mmoja wenye hekima ulivyokuwa ukisubiriwa kwa hamu toka sehemu moja ili kupelekwa maeneo mengine ya Uswahilini yaliyojitandaza katika sehemu kubwa za fukwe za Bahari ya Hindi tangu kale. Hima hiyo ilisaidia sana kuenea methali hizo ambazo kupitia fasihi simulizi, zimeweza kuhifadhiwa kutoka vifuani mwa kizazi hadi kizazi kingine na kutufikia sisi wa kizazi cha leo. Tadaburi katika hima hiyo inaweza kuonyesha ni kiasi gani hekima ilivyorafikiana na kukuwa ustaarabu wa Kiswahili hadi leo hii. Ni mara chache kuona ustaarabu fulani ukihifadhi tarikh yake kupitia tungo za kishairi, lakini hilo ni jambo la kawaida kwa Waswahili. Pia ni chache katika tamaduni zinazotumia mtindo wa tungo za kishairi katika michezo yao ya kuigiza, na majadiliano ya mambo muhimu kwao kama ilivyo katika Kiswahili. Hizo ni miongoni mwa fakhari za Waswahili na utamaduni wao ambazo hapana budi zichungwe na kuhifadhiwa. Hii ni amana toka kwa vizazi vilivyopita kwa ajili ya kizazi cha leo na kesho. Hapana shaka yoyote ni kutokana na kuzingatia jambo hilo ndipo walipokusanyika malenga wa ukumbi wa Zanzineti, unaowakusanya Wazanzibari kutoka sehemu tofauti, na kuendeleza ustaarabu huo wa wazazi wetu, naam, jukumu ambalo si kwa kuwa wamelazimishwa, la, bali ni kwa kuujua umuhimu wake. Ifuatayo hapa chini ni Ngonjera. Ngonjera hii imewashirikisha weledi mbalimbali wa tungo toka kona tofauti za dunia. Ni ngonjera ndefu zaidi iliyowashirikisha watu wengi zaidi toka maeneo mengi zaidi kuwahi kutungwa hadi leo hii. Ngonjera hii imepitia mihula na hatua nyingi. Miongoni mwake ulikuwa ni mjadala kuhusu maana ya neno lenyewe la Muanga. Muanga ni kitu gani? Kuna maana tofauti zilitolewa kuhusu neno hilo, lakini hapa tutanukuu maana moja tu ya kitaalamu iliyotolewa na Dr. Kassim Omar Ali ambaye anasema:
Mti huu unapatikana katika maeneo mengi ya Afrika
ya Mashariki na hutumika kuchongea vitu vya thamani. Kwa kitaalamu mti huu
unajulikana kwa jina la "/Pericopsis Angolensis/" na kwa Kiingereza ni "Afromosa".
Sina hakika juu ya kupatikana kwake katika Zanzibar lakini ni mti maarufu
huko Msumbiji, Malawi, Zambia, Kenya na hata Tanzania.
Kwa kuzingatia maelezo hayo tutaona kwamba mti huo wa Muanga ni mti wenye thamani kubwa. Hata hivyo lililo muhimu hapa ni kwamba muanga unaozungumziwa katika ngonjera hii, si mti unaoota shambani na kutoa matawi na majani. Muanga katika ngonjera hii ni fumbo linalowakilisha kitu cha thamani. Ni kitu gani hicho? Hilo ni swali ambalo msomaji mwenyewe anatakiwa apige mbizi ndani ya ngonjera hii na kulitatua. Msomaji anaombwa pia kuzingatia kibwagizo cha ngonjera hii kwamba Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala.
Ndani ya ngonjera hii mna mijadala mingi ya kuvutia, kuna vilio na malalamiko, kuna nasaha, kuna maswali
alimradi hii si ngonjera tu, bali ni hazina iliyokusanya vito vingi vya thamani. Wakati tulipokuwa tukikusanya beti za ngonjera hii iliyoathiriwa kwa kiwango kikubwa na zama ilipokuwa ikiandikwa, tumeweza kugundua mambo mengi mapya ambayo yamkini hayajawahi kugunduliwa katika utunzi wa tungo, au pengine yaligunduliwa lakini hayakuhifadhiwa kimaandishi. Miongoni mwa ugunduzi huo ni namna tunavyoweza kuthibitisha mfungamano uliopo baina ya urari wa silabi za mishororo ya tungo za Kiswahili na lahani ya usomaji wake. Kama tunavyojua miongoni mwa sifa maalumu za tungo za Kiswahili ni kuchunga mizani katika mishororo yake, kuzingatia muwala katika beti zake, kutumia maneno mahala pake, kuchunga heshima ya mtunzi na msomaji wake na mengi mengine. Lakini kuna baadhi ya wakati huwa si lazima kuchunga mizani ya silabi ya mshororo kama usomaji wa mshororo huo utakwenda vizuri na lahani yake. Hilo linashuhudiwa pale yanapotumika maneno kama tu na Saleh.
Aidha itakuwa ni ukosefu wa fadhila kama hatutawashukuru wote walioshiriki katika ngonjera hii ya rubaiyati (mishororo minne-minne) akiwemo Bw. Saleh Barkey wa Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu aliyetoa changamoto kwa malenga wa Zanzinet kwa barua yake:
Assalaam Alaykum,
Malenga na waraibu wa tungo mtandaoni. Nimeletewa zawadi ya ubeti huu mtamu
sana na sahibu yangu hii leo asubuhi. Amenifahamisha kua ubeti huu uliimbwa
na muimbaji anaeitwa Mbaruku bin Talassam maarufu kwa jina la Mbaruku bin
Mwendo au Mbaruku Kipofu ambae alikua katika kundi la Sitti bint Saad pamoja
na Laila bint Maulidi na Maalim Shaabani na Buda Suwedi na Maalim Subeti.
Nina mgeni kutoka Mombasa na nilipomsomea huu ubeti akanimalizia na
akaniambia wakati wake alipokua baro baro alimshuhudia Sitti bint Saad
mwenyewe akiimba nyimbo hio alipokwenda Lamu zama hizo. Huyu Mbaruku Talasam
yeye ni mzaliwa wa Kibokoni Mombasa wakati huo yote ilikuwa chini ya Sultan
wa Zanzibar. Huyu ndie alieimba ile nyimbo mashuhuri ya BASAKHERA ya asli.
Mwisho ni kwamba ngonjera ya Gogo la Muanga ni changamoto kwa majimbi wa tungo, kujadili mishororo, muktadha na maneno yake na kuyachambua. Pia ni fursa kwa sarahangi wa merikebu inayopiga makasi katika mikondo ya anuwai za tungo za Kiswahili, kuona ni vipi wataweza kustawisha utunzi wao kwa ilhamu ya beti za ngonjera hii. Akthari ya hayo ni kwamba tendo lolote la mkono wa mwanadamu halikosi makosa. Tunakaribisha maoni yo yote kutoka kwa ye yote.
Ahmed Rashid
GOGO LA MUANGA
- Kuna gogo la muanga, njiani limeanguka
Waja mafundi kuchonga, kibanzi kutobanjika
Watu wavunjika nyonga, kwa kupanda na kushuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mzee Mbaruku bin Mwendo)
- Waja wenye mbinu zao, hupanda wakadunguka
Waja na wavamiao, kwa papara na haraka
Wako pia waliao, gogo lipo lawacheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Letu sote gogo hili, kilitaka lakutaka
Afanyae hatambuli, mja huyo asumbuka
Thamani yake ni ghali, wala hili si dhihaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Hili gogo madhubuti, si rahisi kukatika
Tukishindwa tukaketi, bandu mwisho hubanduka
Tukikosa jizatiti, gogo litaja anguka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Bandu humaliza gogo, hilo sheti kukumbuka
Tusijitie mikogo, kudharau kila shoka
Tusilikimbie zogo, pembeni jema kuweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ni tahadhari natoa, kabla mbali kufika
Mazuri kuyatohoa, tulinde gogo sifika
Gogo kutolitoboa, mafunza wakaliteka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid).
- Yataka uwe azizi, upende pasi kuchoka
Macho uyaweke wazi, na mwenendo wa hakika
Gogo huwa ni jahazi, kukuvusha ukafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Kwanza ejaribu Chali, mchanjaji wa Msuka
Kisha akakwea Duli, kwa dhihaka akashuka
Nasabawe Mizamyuli, gogo helitaharuka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Akapanda Sefu Chalyo, baba la miraba nyuka
Akarudi na miyayo, mpwawe Miza mizuka
Alimasi yake yayo, mpini ukapasuka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Seremala hachanjili, apikia kwa nkaa
Nyie mwamleta Chili, mchomaji wa chokaa
Hapa tumtaje Pili, kwa mipingo kachakaa
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Kuna tabia ya waja, hutaka vuka mipaka
Na hao ulowataja, kamwe hawakuzinduka
Wakaruka wakatoja, mughuma ukawashika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Wajao kutoka mbali, mwendo msitu na nyika
Kulifwata gogo hili, kwa vishindo kuliteka
Huzungukwa na akili, gogo lawapa mashaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Si jiti hili ni gogo, kijasho kiliwatoka
Migongo yengia pogo, walichoka wakauka
Kimewashinda kigogo, walia watu wacheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Mashoka yao ya vyuma, wageni mbali metoka
Kuja gogo kulipima, kijasho kikawatoka
Kuona isitiqama, gogo lilivyotukuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo mevuka viunzi, vya kiangazi masika
Limekabili mionzi, bila ya kutetereka
Kalilinda Mwenye Enzi, thabiti halina shaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Muhali gani malenga, na gogo lisochangika
Gogo hili sio changa, kwa kweli limepevuka
Limebeba nyingi kunga, na siri za mamlaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Ukiliona karibu, vile lilivyoongoka
Ukapewa masahibu, na vile lilivyon'goka
Utatamani kutubu, mlinzi Mola Rabuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Wazamani na wa sasa, gogo walilizunguka
Kwa hila walipapasa, wajuzi walosifika
Gogo limekuwa tasa, katu halikupasuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(N-gongele)
- Waliotaraji mbao, walianza kufungasha
Na hata wa kuni nao, walikatisha kukesha
Wa vibenza wajuao, gogo hawakulitisha
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(N-gongele)
- Gogo hili ni la kale, ni la zama kwa hakika
Ni la muanga si mwale, zima limetakasika
Lina shina na viale, matawi metawanyika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wala si kila mahala, gogo hili kupatika
Ardhini limelala, kwa dahari na miaka
Subhana wa Taala, ndiye alolitandika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Weshindwa maseremala, gogo waliolitaka
Dhiki na yake madhila, haliogopi mashoka
Gogo si la mjadala, ni sote tunahusika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Mafundi mlo wajuzi, enyi mloelimika
Wenye macho waangazi, mkae kilimurika
Tujue ving'ang'anizi, katu hawataondoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Na hata ving'ang'anizi, hakuna kitowaweka
Meno tang'oka na vizi, kugwegwena watachoka
Limewashinda wakwezi, watajakuwa mahoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo mekita thabiti, ni katu kula mweleka
Gogo hili la yakuti, lameremeta lawaka
Gogo liko madhubuti, limedumu kwa miaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Mafundi wamevinjari, gogo limewasakama
Kila wakizidi ari, wao hawana salama
Wabaki kushuka ngiri, wakijuta wakikoma
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Barkoa)
- Kofia zimevuliwa, kubuni zao hekima
Haweshi kujizunguwa, wana mafuwa na homa
Kucha hadi kuchwa juwa, gogo linawatazama
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Ahmed Barkoa)
- Mahoka haweshi kero, wadhani gogo ni taka
Silaumu barobaro, wala muliozeeka
Pale mutowapo ndaro, kuwakemea mahoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Waulizeni suali, ni lini wataongoka
Pasiwe tena muhali, musizidi kunyongeka
Gogo la muanga hili, ni tunu iloenzika
Kula ajayye na shoka , katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Na nyie mulohajiri, mashoka kuyaepuka
Tahadhari tahadhari, gogo kulipa talaka
Yamezeni ni shubiri, ela gogo haliuka
Kula ajae na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Kwa sote tulohajiri, gogo bado twalitaka
Daima twalifikiri, na machozi yatutoka
Twaliwaza kwa fakhari, salamu twazipeleka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Katu hatulisahau, gogo lilivyo nyooka
Huwezi kulidharau, kwa haiba lasifika
Hila zote musahau, ni muhali kupasuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Gogo lilivyonawiri, madenda yanawatoka
Ndo mana wakavinjari, wakapandisha mahoka
Wakajitia na ari, wasijali kukatika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Gogo hilo gogo gani, lisokubali kumegwa
Ni gogo kweli jamani, au bomu lilotegwa
Wajuzi tuzinduweni, tusije tukakorogwa
Atakuwaje jamani, mwenye shoka seremala
(Muhammad Faraj)
- Ndani kajificha nani, gogo halitaharuki
Ndani mna subiani, au jini la kibuki
Ndani mna kitu gani, mbona halitikisiki
Atakuwaje jamani, mwenye shoka seremala
(Muhammad Faraj)
- Kama mna mashetani, natoa yangu ahadi
Watatoka walo ndani, kwa shoka langu la jadi
Watakimbia porini, kurudi hawatorudi
Atakuwaje jamani, mwenye shoka seremala
(Muhammad Faraj)
- Shoka si la seremala, bora mpe mchanjaji
Kwa uwezo wa Taala, tutaipata faraji
Aanze kwa bisimillah, kisha kwa upasuaji
Atakuwaje jamani mwenye shoka seremala
(Muhammad Faraj)
- Gogo hili gogo gani, kauli yangu natoa
Liloshinda ikhwani, baro baro waso doa
Zana haziwezekani, bado liwe limepoa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Katu hawi seremala, kula ajae na shoka
Ila watu hawelala, mbioni hawajachoka
Limewashinda suala, vyombo vimekongoroka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Linkua kisirani, nafasi halyebu toa
Watu wako hamkani, gogo linawakomoa
Vyetezo nao ubani, jibu wanalipotoa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Si gogo ila n'jini, mughumani kututia
Haitui akilini, kuhanikiza udhia
Zimemaliza Yasini, sadaka na vyano pia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Na mashine za kisasa, kwa umeme ziendazo
Ni kama gogo kudasa, au jicho mkonyezo
Sawa sawa kupapasa, bembelezo na mchezo
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Gogo ni gogo muanga, si majani ya kufyeka
Limewashinda wakunga, wanotaka kuliteka
Wenyewe wanalikinga, bila ya kutetereka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Katu hawi seremala, mchongaji aso shoka
Zitakwisha zote hila, mbao hazitamfika
Gogo halina sumila, mengi shoka yanataka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Si gogo la mashetani, sisi ndio wahusika
Tunalilinda kwa ndani, na nje, limetukuka
Na hila za mafatani, waso kheri watatoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ni letu sote jukumu, kulinda gogo husika
Bismillahi Karimu, dhamira tumeshaweka
Kushajiisha qaumu, gogo vyema kulishika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo hili tanashati, mja mwema amefika
Gogo lina na shuruti, mbaya budi kutoka
Gogo kito cha yakuti, ni neema ya Rabuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Magwiji toka Mrima, na mbali kunosifika
Wote walirudi nyuma, kwa hofu ya kudhurika
Gogo limekuwa chuma, kwa mbali walisikika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ngongele)
- Jamani gogo li chini, na njia imefungika
Hapaendeki mjini, ila kwa gogo kutoka
Yaleteni majambeni, tumechoka kudhikika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Hassan)
- Mje nayo mabegani, tena mfike haraka
Mje nayo hamsini, idadi ya uhakika
Furaha ziwe nyoyoni, unga ukipukutika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Hassan)
- Gogo likatwe shinani, matawi yakialika
Yapuruliwe majani, moja lisijeoneka
Na kilicho kileleni, kukienzi muafaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Hassan)
- Kupurulika muhali, majani yalipofika
Yatazidi kukabili, yote hayataondoka
Yataota kila hali, muhimu ni kuyafyeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gugu limezonga gogo, uyoga kunawirika
Wakubwa hata wadogo, majembe wameyashika
Ni wakali kama mbogo, gogo letu tasafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Haya kake si majani, ya gogo lilotukuka
Ni gugu liso maani, karibuni litauka
Kwa uwezo wa Manani, madhila yataondoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo latuunganisha, baba, mama, dada, kaka
Ni kwetu kulidumisha, qitali mbali kuweka
Gogo kuliimarisha, hata shoka kinoleka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Liwe kali kama wembe, lenye nguvu kama radi
Halitolitoa tembe, ila cheche zitarudi
Ndipo mtajua kumbe, madhubuti ni shadidi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Ziwapi haziko tena, zenu zama zimekwisha
Na njia leo hamna, siku mkazirudisha
Zimepita kama jana, hazitorudi maisha
Kula ajaye na shoka, katu hawi serema
(Maher-Unique)
- Gogo limekuwa sega, kila nyuki anafika
Wajaza bega kwa bega, asali yabubujika
Matumba yale makega, vifaduro metibika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Imu)
- Gogo limetuokowa, wengi tumefarijika
Leo tumepata dawa, sote tumenawirika
Mashoka yenu ondowa, neema imeshashuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Imu)
- Kulipangika mpango, wa gogo kulifunika
Likafukiwa udongo, juu pakaekwa nyoka
Kwani sie ni machongo, nyoka kabanwa na fyuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Muanga ukabarizi, Subhana ya Rabbuka
Umeruka usingizi, aliye ndani katoka
Tutaimba kwa mapozi, na vifua kutanuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Gogo ni letu daima, tumelirithi miaka
La pwani si la Mrima, Manani ameliweka
Na hata wakinguruma, nani atatetemeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Akili zetu timamu, zote zimekamilika
Tunalilinda kwa hamu, twachunza yao mashoka
Hilo kwetu sio gumu, makini kulimurika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kake Mnyonge wa Nyali, usemayo ni hakika
Timamu zetu akili, tu macho tumeamka
Kumlinda mwanamwali, kuepuka mfaraka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Pia na kake Salehe, ya kwako hayana shaka
Hizo siku za sherehe, hapana budi kufika
Jecha, Nshazume, Shehe, wote watafurahika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Salehe wavyaa shari, na wa kwako washirika
Waitibua tabiri, kupinda yalonyooka
Mbaruku si ambari, kuizindunia shaka
Gogo haliebu shoka, likweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Talasani hakukhuni, usiya aliyoweka
Japo hakufika thani, ubeti ulomtoka
Salehe wepata nini, kumjazia vihoka
Gogo haliebu shoka, likweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Hebu wape ahueni, uwaondolee shaka
Nataka nikuamini, urithi ushaushika
Heusia talasani, gogo libambwe kwa shoka
Gogo haliebu shoka, likweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Kwanza gogo liko chini, halihitaji wakweka
Tena gogo si la kuni, bali la muanga-fika
Bure mwaishika kani, kuishurufu dhihaka
Gogo haliebu shoka, likweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Sumileni aje Chani, hapo litacherezuka
Huyo atoka Jozani, kwenye miti ya mirika
Salehe acha utani, muanga si mtonoka
Gogo haliebu shoka, likweche lakerezuka
(Sultan Ahmed)
- Tani wafanya utani, mie sitaki kucheka
Wayajuwa ya zamani, na haya yalozumbuka
Ati kweli huyaoni, sinifanyie dhihaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Ya Talasani muruwa, wasia uloneneka
Kama kwamba kayajuwa, hapo kale ya miaka
Sasa khatuwa khatuwa, alonena yafunuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Kanenea la muanga, kimurimuri murika
Yakhe kwabwagwa manyanga, Chani yuwatetereka
Wengine watangatanga, watafuta pa kushika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Nekuona kidunguni, wawika Tani wawika
Hebu nenda Utaani, tumbo utakorogeka
Ufike hadi Limbani, moyo utamung'unyuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Sie hatufanyi zogo, lakini twachangamka
Kulishangiria gogo, gogo la kuaminika
Hadi siku ya mikogo, ya gogo kunusurika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Urithi ni wetu sote, si wa kwao peke yao
La Muanga letu wote, gogo si geni li pao
Haki ya wana tupate, wa kuleya ende kwao
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Waliona tumelala, kumbe ni dhana potofu
Hawakujua mahala, tulipo kama siafu
Na sasa hawana hila, wamo mbioni kwa khofu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Si dhihaka kupasuka, zimekwisha zao hila
Hata waje na mizuka, na wakubwa wa kabila
Tarudi walikotoka, waliwache limelala
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(N-gongele)
- Gogo hili ni la mwavi, kabisa halibwenzuki
Wachanji watoka mvi, gogo halitikisiki
Wanatumia vitinvi, kutaka kulihiliki
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Muhammed A. S.)
- Ni hiyo ndio dhamiri, gogo lisitizamike
Kwanza ilikuwa siri, yakatumika makeke
Mola ameyadhihiri, na ari naitumike
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Msemao nyie nani, kuacha zenu shughuli
Wenye gogo wajueni, ni wenyewe wa asili
Ni sisi twenye mpini, nyie shikeni makali
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Abduu Salim)
- Gogo letu gogo lile, nawapasulia kweli
Tena wembe ule ule, musidhani nakejeli
Tulieni sote tule, musilete mushikeli
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Abduu Salim)
- Bwana mshika mpini, wadhani twatetemeka
Mtindo huo zamani, dunia ishageuka
Mwajikaza kisabuni, kumbe munababaika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Wembe una pande mbili, hilo mujuwe hakika
Gogo ni kitandawili, kama kinyuri nyurika
Muyapime kwa akili, alie juu kuuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Na mie napiga hodi, jama sijaadimika
Kuona mumeshitadi, ya gogo kuyaandika
Naingia sina budi, nilo nayo natamka
Gogo linaloelea, vipi taingia shoka
(Miminae)
- Wenzangu nimeemewa, vipi gogo kusifika
Kila sifa limepewa, bado naona mashaka
Hili jini lakupewa, ni tabu kujaondoka
Gogo linaloelea, vipi taingia shoka
(Miminae)
- Mwalimu kaja na fani, gogo kutakaliteka
Kapata kitahanani, moyo ukimripuka
Usingizi hauoni, kutengeneza mashoka
Gogo linaloelea, vipi taingia shoka
(Miminae)
- Gogo lipo kiwanjani, ameliweka Rabuka
Hali juu wala chini, viumbe twaadhibika
Gogo haliwezekani, ila kwa Mola kutaka
Gogo linaloelea, vipi taingia shoka
(Miminae)
- Wahenga sinilaimu, kusema niloyataka
Ikiwa metia sumu, hii ni ya uhakika
Sitoitia na ndimu, mchuzi ukachachuka
Gogo linaloelea, vipi taingia shoka
(Miminae)
- Ingawa linaelea, gogo halingii shoka
Ila wamelilemea, wadhani litabanduka
Lini wataendelea, kukubali uhakika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Japo jini la jinani, kuna siku litatoka
Na hila za kishetani, zote zitamalizika
Kibuki likizaini, majivu litageuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Licha chachu cha kupewa, gogo limezifunika
Lakini wameelewa, ni katu kudhoofika
Thabiti litalelewa, kwa uwezo wa Rabuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Katu hukutia sumu, la moyoni kutamka
Bora ngetia na ndimu, mchuzi ukachachuka
Wavyele wakajihimu, kuvikabili vihoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Jitihada ikisibu, kudura hawezi uka
Ila ni wetu wajibu, kulinda haki hakika
Gogo letu mahabubu, tangara tanawirika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Bibi singie majonzi, tamaa ikakatika
Irada ya Mwenye Enzi, haiwezi kupingika
Kuni yakuni tuenzi, dua zetu kwa Rabuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Muanga hauelei, muanga si msanaka
Hilo ni jiti la bei, bibie acha dhihaka
Nakuheshimu chechei, bora ukwepavyo shoka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Muanga si mtondoo, kwenye maji una shaka
Gogo la bibie shoo, viroja waja umbuka
Si mbao ya mpodoo, muanga wameremeka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Zang'ara kama kioo, mbaoze zasugulika
Kwa samani ya viyoo, ndio kwake washirika
Uloona ni msoo, wa kete za bao wika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Miminae ewe nawe, waijua mitonoka
Muanga si mti-bawe, mtumbwi ukachongeka
Hilo ni jiti la sewe, linaishi kwa miaka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Sasa acha ushindani, kuchelea fedheka
Mimi nnaye wa ndani, awezae likwepuka
Hilo gogo lenu deni, mwisho mwaja filisika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Kwanza nazipanga zana, za kufyekea vichaka
Sumeno la Chani bwana, ndilo litalo tumika
Kisha navipiga chana, vifefe vyenu vya rika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Ntakuja na vijana, na zee lao lawika
Utapiga Subhana, mti tukiuzindika
Tutachana na kuchana, na mbao kuzitandika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Seremala wangu Chani, hajui kunoa shoka
Kashinda mabaniani, wenye fani zatajika
Mipanga na maruhani, ya mavani na ya nyika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Kisha tutachana mbao, za mti wetu wa zaka
Halafu wataniwao, walie kina kibweka
Mimi na muanga teo, tu mbali twatweka tika.
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Sultan Ahmed)
- Tani acha kujilabu, Huyo Chani ashachoka
Vijana wana ghadhabu, wefunzwa wakafunzika
Gogo wajao lisibu, puani litawatoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Wavyele hawana pupa, karata zimepangika
Huku wawatoa kapa, huko mrisi ni shaka
Jisu lishagusa fupa, labeka gogo labeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Watambia vyombo butu, ba Tani Alaidika
Zana zishaota kutu, majani shida kufyeka
Seuze gogo la watu, lihimilio mashoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Kujilabu ndio kwao, kwamba gogo watafyeka
Wenda wakirudi zao, ndio kwanza linawika
Zitachuna hila zao, gogo kani limeshika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Janja ya kulikereza, na zana zao kunoa
Vidudu kuvipenyeza, ndani wapate toboa
Wataona miujiza, gogo tukiliokoa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Lileta wataalamu, kazi ije kamilika
Ya gogo kulihujumu, ili sipate kalika
Ni bado mastakimu, baraza inotumika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Ally Saleh - albarto)
- Ajabu ya gogo hili, unapolipa kisago
Kila unapolidhili, linayameza mapigo
Toka siku ya awali, limejenga wake wigo
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Ajae na shoka katu, huyo sio seremala
Hili ni gogo la watu, wenyewe hawajalala
Tena kwa vyombo vibutu, hatafikia mahala
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Mwenye shoka si mjuzi, kazi yake kupasuwa
Huchanja hatengenezi, hachongi kitu kikawa
Ndipo tukasema wazi, seremala hatokuwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Gogo hili li majini, ndu yangu Tani elewa
Katu hulichanji kuni, Miminae ayajuwa
Aliyosema yakini, wewe unayapotowa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Siri ya gogo majini, bado hujaitambuwa
Itafute kwa makini, sirushe na kupopowa
Uliko mbali si ndani, ya kwetu hujayajuwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Ubaya wa kuchupia, tabu yake pakushika
Vyema ukaangukia, pale unapopataka
Sivyo ukatumbukia, ujuwe pashakutoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Kuwa si tabu rahisi, mwenye kutaka hupanda
Ingekuwa ni nyepesi, wewe isinge kushinda
Lakini wapi huhisi, tamaa imekuganda
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Ulikushinda unao, mpini umikononi
Akaja mvunja mbao, na vitasa milangoni
Ukamkabidhi tao, akalitupa njiani
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Leo hulipati tena, gogo limeshapevuka
Huliwezi kubwa sana, kibanzi tabu kutoka
Narudi nasema tena, ogopa kuja biruka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Maher-Unique)
- Kake ntakupokea, manenoyo nimeshika
Utadhani ni sheria, vile yalivyopangika
Gogo lipo kwa murua, kamwe halitaseguka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Waache wajishaue, na mikogo kuiweka
Mijineno watwambie, hakuna atoshituka
Gogo shirika na mie, pekeyo halitatoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Ni muanga si uyoga, matawi metawanyika
Mlo juu mwatukoga, mfanyayo twaudhika
Tutawavalia njuga, mfikiwe na gharika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Kufanya kosa si kosa, kulirudia mashaka
Gogo hili la mikasa, tulisomee sadaka
Likatike mara tisa, pasi hata kualika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Au bora liyayuke, sihitaji kukiuka
Njia yetu isafike, tupite tukipituka
Na hadithi ifutike, mwisho kusahaulika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Mwambie na afahamu,
wakati umeshapita
Bila kuwa na elimu, hata skuli kupita
Hakuna na mwenye hamu, kusikia tarumbeta
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Muhammed A.S.)
- Kuwa na kisu kikali, sio ndio kula nyama
Gogo halistahili, kubeba huku wasema
Mutawacha gogo hili, kwa walio na hikima
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Nami nna haki yangu, kulichanja hutafika
Tutayapiga mafungu, tumjuwe muhusika
Ama zako ama zangu, mashahidi tutaweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Gogo si la msumeno, mulijuwe kwa hakika
Haya si yangu maneno, ya wenyewe washirika
Mutakipata kibano, daima mutakumbuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Mashoka na muyanowe, gogo halitakatika
Ni gumu kuliko mawe, jaribuni kina kaka
Litawatia kiwewe, mushindwe ndani kutoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wanosema ni jepesi, gogo letu nawambia
Uzito wake halisi, nyingi nyingi lukukia
Hakika yake nafasi, ni ya saba baharia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema lapasuka, hebu macho wafumbue
Waache kukurupuka, gogo wasilisumbue
Burudi laburudika, wajue ni letu sie
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema la pamoja, ni rasilmali ya umma
Mbona wafanya viroja, chetu wakidai hima
Twawaona ni wakuja, gogo tasimama hima
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema watachana, na mbao kuzigawia
Wana ndoto za mchana, gogo tawakatalia
Limeshibia kwa sana, vishindo kuvumilia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema tugawane, kila mtu kwa ubale
Ili wapate wavune, ati Omari na Chale
Watabaki na mavune, wakisema asalale
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema wana zana, za gogo kulihasiri
Kweli nafasi hawana, gogo bado ni jusuri
Mashavu yao tatuna, wakipungiwa kwaheri
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wanosema taburura, gogo walitoe kwake
Wajue halitagura, kuzama au kuzuke
Halina hili safura, kwa Kimoto sio zake
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Malenga msiniwache, mwenzenu nikapotoka
Nataka msinifiche, siri ya gogo hakika
Singojee hadi kuche, ukweli ninautaka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Kassim O. Ali)
- Nilisoma dua mbaya, ya gogo kuporomoka
Nikaandaa na kwaya, gogo lizidi omoka
Mesoma zenu riwaya, sasa nimeelimika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Kassim O. Ali)
- Kumbe ni gogo imara, halijawahi toboka
Kila wakati lang'ara, kiangazi na masika
Haligonjwi kwa kafara, mashoka na hata nyoka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Kassim O. Ali)
- Watoto wajikukucha, ladunda likidundika
Wameshindwa mapakacha, fadhilaka wapundaka
Mashoka yao ya bucha, yamezidi kugumuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Wale wenye wasiwasi, wa gogo kuvongonyoka
Kwa hizo zao risasi, pindipo wakizikoka
Hima tufanyeni kasi, wadogo na wangu rika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Mbali tulikoanzia, mengi tumeyavuuka
Wakati umewadia, hadithi kuhitimika
Gogo kulisafishia, tayari kwa kuinuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Ninaupiga upatu, Kiwengwa hadi Msuka
Tusikubalini katu, gogo letu kudhurika
Tukazeni buti zetu, tuikabili shabuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Tulidhania ni mbali, siku ya kula mbarika
Metizama manazili, tutoweni zetu zaka
Tusiifanye zohali, gogo lipate enzika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Meandika beti nane, zitiwe kwenye waraka
Ya tisa msiichane, muhimu kuhesabika
Gogo sio dane dane, tulitemee vichaka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Ngojera hii ni ndefu, ya gogo hili la nyika
Hata watunzi vipofu, wavivu twakokomoka
Kwa tungo zangu nyaufu, nawaaga naondoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Leo umma tawambia, kuna waovu balaa
Rohoni wanaumia, kwa lilivyochichipaa
Siri wataka kujua, undani lilivyokaa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Hila walizovumbua, mashoka hadi patasi
Kibanzi hawebandua, limewapa wasiwasi
Wame ubwia wa chua, gogo lajitanafasi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Walidhani mti ovyo, wenye nyufa zilojaa
Haikuwa ndio hivyo, gogo letu kukataa
Ndio hivi tuonavyo, kila siku tukikaa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Mipango ilitimia, wakipiga darubini
Waje kujichukulia, walipakie melini
Kumbe zito kwa wakia, lingezama baharini
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Wakasema walitose, baharini walivute
Ili watu walikose, chao wakipige pute
Ikawakuta kasese, gogo hali tepetepe
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Wakasema waliteke, gogo liwe mali yao
Kwa mbwembwe pia makeke, wakatangaza ni lao
Waache waweweseke, mewezonga mzubao
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Ndipo wazo likazuka, kuwa gogo walichanje
Mapande yakikatika, na zaidi wayabanje
Lipate kuhamishika, haki ya watu wapunje
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Gogo likasema nipo, karibuni waungwana
Na likala na kiapo, kwa nguvuze likatuna
Na ndo bado lingalipo, zakatikiana zana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - albarto)
- Hapo zamani za
kale, zama na zama miaka
Watu wa huku na kule, wasokwisha kuzunguka
Kuona muanga ule, wakenda kupumzika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Muanga ukawa wao, bukheri kuburudika
Hukaribisha wajao, nao wakasitirika
Kukaja na wapitao, mambo wakayaandika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Kukaja wenye vishindo, tamaa ilowashika
Wakahanikiza vundo, kukawa ni pata shika
Waliiunda miundo, muanga kuuzindika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Muanga wasiuweze, watu wakachangamka
Kukaimbwa Mwana Mize, wakaja waloitika
Wakamba tuusuuze, muanga ukatukuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Ukachipua matawi, muanga ukatanuka
Muanga ukastawi, hakuna kutikisika
Nani haya hayajuwi, gogo lilivyopambika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Kukaja wenye khadaa, kula mti wautaka
Yao wakayaandaa, watu wakafitinika
Gogo welijaza daa, adonae wamshika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Ni vipi tusiyajuwe, kuzushwa yaliyozuka
Kizaazaa kiwewe, pindu pinduka pinduka
Gogoni kawa mayowe, mwenye rungu mwenye shoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Sasa ya leo yawazi, kutaka na kutotaka
Tuepuke ubazazi, kwa pamoja kutamka
Gogo letu l-azizi, wingu lile latanduka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Wayatakayo hayawi, gogo hili kupasuka
Wataka kata matawi, mizizi inong'oleka
Majani ya muangawi, yote pia kuyafyeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hawataweza lidhuru,wakamie kwa mikaka
Mungu atalinusuru,tunamuomba Rabuka
Ataiweka na nuru,imurike na mipaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Gogo lilipokitia, rutuba metawanyika
Lipo kwao asilia,pengine hutaliweka
Kwa hapo limetulia, wapi utalipeleka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kwa makeke na vishindo, gogo halitashituka
Halitafata mkondo, kusiko kulipeleka
Mutaviona vimondo, huu ndio wake mwaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Huu ndio wake mwaka, kwa gogo kuneemeka
Kula aliye na shaka, asubiri itafika
Siku hiyo ya baraka, tayari ishaoneka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Gogo letu ni tukufu, ni mama tulomuweka
Ni hai tena si mfu, ndo mana lanawirika
Si kwamba nnalisifu, gogo hili metukuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Mizizi yake imara, aridhini mejiweka
Hii ni yake ishara, kuwa halitaondoka
Musione masihara, gogo hili lishafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Mwaona linavyongara, japo kiza wameweka
Iyoneni na stara, aibu haikufika
Halitakuwa tambara, mehmeli ya hakika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Shinale la mduara, la gogo menawirika
Sio lile la uchwara, jembamba kama mahoka
Gogo hili la tijara, si hasara walotaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Majaniye menawiri, kijani kilokozeka
Mesimama kimahiri, si yanayopukutika
Tena yaliyovinjari, si yaliyodamirika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kiangalie kilele, nacho kilivyopangika
Na wapige makelele, mwishowe tutakifika
Hawatakaa milele, daima tukateseka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hili hawatalichanja, kwa nguvu zake Rabuka
Watamaliza ujanja, chini watateremka
Kama asali meonja,mzinga hewechongeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hayakuwa asubuhi, katu hayawi jioni
Ikiwa hawakuwahi, basi tena abadani
Kama tuliwastahi, sasa mambo hadharani
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Ametwambia wa Nyali, rutuba meizunguka
Chipukizi za awali, sasa nguvu zimeshika
Zinajikita kikweli, nafasi zao meshika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kila palipogunyuka, dawa njema tumetia
Panapona kwa haraka, gome jipya lazibia
Huwa ni gumu hakika, kuliko lotangulia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Magome mapya zinduko, ugumu wao hazina
Kubanduka huwa mwiko, kwa yanavyo shikamana
Kila pigo sikitiko, lakini yanan'gan'gana
Kula ajaye na shoka,katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Magome ya gogo kinga, ya gogo kujilindia
Ndipo gogo linaringa, vikosi vivyopania
Ya tayari kwa muhanga, hadi mwisho wa dunia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Tena kasema tukufu, na hilo naungamia
Limeepuka uchafu, najisi zinakimbia
Hili gogo ashrafu, kalitukuza Jalia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Dua za wetu wavyele, mbingu ya saba kufika
Watakanyaga chechele, gogo hawatalifika
Wahangaike milele, viwinda vikiwashuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wadau na tujikaze, kikurubu seremala
Njia natuwapoteze, kwa nguvu zake Jaala
Madogori wakacheze, ngoma yao ya asila
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wasokwisha masuali, gogo kulipekechua
Wajua ndani asali, kugema kwawasumbua
Tone kwao si halali, roho tutawadungua
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremela
(Ally Saleh albarto)
- Jawabu nnamwambia, seremala ya hakika
Asije kukaribia, mbigili tutatandika
Vitanzi vyanin'ginia, asithubutu kufika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kwa maneno
yamekwisha, sote tuwe nguvu moja
Harambe kuhamasisha, kuungana iko haja
Gogo kulisimamisha, wapate ona viroja
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Kwa fitina tusitimbwe, tusiwe kubaguliwa
Wajukuu na virembwe, waishi wote muruwa
Madua mengi yaombwe, mahasidi kung'olewa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Na mimi fundi mangungu, uwanjani naibuka
Ufundi ni fani yangu, magogo nondo nasuka
Mikoba ya kilimwengu, mefunzwa nikafunzika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Masiku tangu na tangu, ukumbini munawika
Ati gogo liko chungu, halichanjiki kwa shoka
Mimi kwa maoni yangu, si kweli ninatamka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Tumelikata madungu, mtini likaanguka
Tukavichonga virungu, na mipini ya mashoka
Mabanzi fungu kwa fungu, twetumia kwa kupika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Misumeno ya kizungu, sasa ndio yatumika
Kwereche huko na kwangu, twalimega lameguka
Tushachonga vitu chungu, kwa gogo hili sifika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Nahisi maoni yangu, wengi watachokozeka
Nasubiri ya wenzangu, ni nini watatamka
Gogo hili ni la tangu, ila sasa lachongeka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Ewe fundi ulosoma, bwana uloelimika
Maneno unayosema, tumeambiwa miaka
Gogo lipo mesimama, juu ya yenu mashoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wengi hatuebu shari, sivyo tulivyoleleka
Ela twaona khatari, kwa mnavyotupeleka
Kujifanya majabari, kwa kuwa mna mashoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Misumeno ikereze, fundi anavyotamka
Misuri na waikweze, jasho jingi tawatoka
Watafanya wasiweze, gogo halitavunjika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Sina budi nitongoe, fundi anitia shaka
Kama gogo ni
mamae, vipi alitie shoka
Iweje alikamie, atambe lakerezeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Fundi aja akitamba, asema litakatika
Amejiweka sambamba, na wale wasohusika
Walokuja kwa manamba, leo mbele mejiweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hakika inashangaza, fundi anavyodemka
Ngoma haijamaliza, mwezi bado unawaka
Asidhani wataweza, kuunda wanavyotaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hilo haleanza leo, kani kwa gogo kuweka
Haya ni maendeleo, nyuma yalikoanzika
Tuulize tujuwao, tangulia si kufika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Tumeona mikakati, mingi iloandalika
Sheria na masharti, kochokocho waloweka
Kwetu hiyo si tamati, twendako hatujafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Tumeviona vishindo, kutishwa wanotishika
Wakajiita komando, na vyeo kujibandika
Hewebadilika mwendo, kwa muruwa tulitweka
Kula ajaye na shoka,katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wakajiita masimba, sifa zisizo mipaka
Wakatuna wakitamba, miguu tumepachika
Tunalo twenda sambamba, iko siku itafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Gogo wamelikosea, si leo tena hakika
Njia waliyozowea, sasa haitapitika
Basi kuwachekelea, wakati umeshafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kimya tulinyamazia, kwa mingi sana miaka
Kisirisiri kilia, kuona laatilika
Madhali tunayo nia, hili gogo talindika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kwa kuwa weliberuwa, juu chini kuliweka
Kwa hilo haitokuwa, peke yenu wahusika
Tuna haki sawasawa, vyovyote mnavyotaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kimya hatutanyamaa, sauti zitapazika
Muda huo tulokaa, dhana watabadilika
Kumbe wazidi balaa, njama kwa gogo kuweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Sasa tunasema basi, shingoni yametufika
Twaona yaja kwa kasi, yasije kutufunika
Tushangia wasiwasi, kwa gogo kumalizika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Na waje nayo mapanga, misumeno na mashoka
Tushajitoa muhanga, kufa si kuadhirika
Kwa Mola alilopanga, nani atanusurika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Na waifanye mikiki, mafundi wanokereka
Madhali hii ni haki, hakuna atopweteka
Sote ni wanakindaki, zama tumeshaamka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Mbao hawatapasuwa, heweweza kwa miaka
Wabaki kujishauwa, leo tena wazitaka
Yangekuwa ni ya kuwa, hii leo singefika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kipi kilichowashinda, kwa yote hiyo miaka
Gogo juu kulipanda, lakini helegeuka
Majahazi mngeunda, si ndivyo mulivyotaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Fundi kachome chokaa, kwa gogo helewezeka
Madamu limetuzaa, nyie hamutalinyaka
Tutalilinda kwa taa, kama kiza kitafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Fundi una uraibu, kusema yasosemeka
Fundi rudi uhisabu, isiwe kuhamasika
Ni gogo lipi sahibu, si la muanga hakika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Wewe siye wa awali, shughuli kushughulika
Ni mambo tangu azali, huwashwa yakazimika
Nakwambia ni muhali, muanga kuatilika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Mutaubenzua vipi, muanga si nyangarika
Nakueleza mafupi, muanga wafahamika
Muchongayo ni makapi, macho mukahadaika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Uwadadisi wenzio, ila usije udhika
Ujuwe undani wao, yote wanayokumbuka
Uwasikie kilio, huku wakilalamika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Fundi nakupa maneno, matamu ukiyashika
Twende mkono mkono, muanga una baraka
Muanga una manono, wala hautanyambuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Salamuni ndugu zangu, chambi yangu najitwika
Nahisi maoni yangu, bado sijaeleweka
Hili gogo sio langu, bali ni letu hakika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezeka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Lakwerezeka si chungu, fundi mimi natamka
Hiyo ndio kazi yangu, karibu tano miaka
Wapo pia na wenzangu, wazidi nilipofika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Kukwereza gogo langu, si sawa na kulifyeka
Kukereza ndugu yangu, huko ndiko kulisuka
Japo lapata machungu, misumari kilitwika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Gogo limekuwa langu, mimi na wewe na kaka
Tokea siku wazungu, na wale waloliteka
Kwa hasira na uchungu, wenyewe walituvika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Kuchonga bangu kwa bangu, gogo halijashindika
Mtepe dau na rungu, tayari meshachongeka
Twechonga bila ya pingu, fedha ndio yatamka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Chokaa nazo kwa fungu, vipoloni meziweka
Mabanzi ya gogo langu, makumbi mawe kwa twika
Minazi hata mikungu, kuni zote metumika
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Mambo mbona yamenoga, Ally na Saleh wamoto
Kusema yasio soga, wala nyimbo za kitoto
Mwataka litoa gaga, bila ya njia mkato
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Saleh kanena asili, kuwambiya walo lala
Yalosibu gogo hili, ya kweli yaso suala
Gogo linastahili, kunadi bila ya kula
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Jitihada naifanywe, tuungane kiungwana
Ili gogo lisiminywe, pia watu kutwangana
Hata dawa natuinywe, tuwache kubaguwana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Injiniya mwamuona, yeye pia katongoa
Tuwacheni kuchuana, na gogo kuliopoa
Au tutaja lizana, gogo likija potea
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Mohammed A. S.)
- Amekuja kwa vishindo, wetu fundi wa mangungu
Utani eweka kando, macho katoa ukungu
Mepesi yake mitindo, ni haba yake mizungu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Katoa yake kalima, hadharani katangaza
Lakwerezuka kasema, gogo waligaragaza
Chungu vitu mesimama, kwa sauti kapaliza
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Ila mie namwambia, vifaa vilochongeka
Ilikuwa ni hadaa, ridhaa haikutoka
Huko vilikopotea, nyumbani tunavitaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kama ni pawa na miko, au ni viti na mbuzi
Na madirisha yaliko, hatutaki ubazazi
Kuviachia ni mwiko, kuvisaka ndio kazi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Twajua kuna mapande, waliwahi kuyakata
Ni seremala vivunde, walipo tutawafata
Tuwakatie mapande, wakiyaanza matata
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Mbao walizochukuwa, lazima wazirudishe
Hesabu ikae sawa, na kwa hilo wasibishe
Hilo litasimamiwa, chetu wasififirishe
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Na hata unga wa mbao, wote pia mali yetu
Ni mbolea kwa kibao, waipate watu wetu
Yamee yetu mazao, tuzigange njaa zetu
Kula ajae na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kama wameuza nje, zana za gogo la kwetu
Itabidi tuwakunje, yarudi mapesa yetu
Ni muhali watupunje, gogo letu mali yetu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Mpemba akishaguna, usijefanya dhihaka
Bure utakuja nuna, utajitia mashaka
Kwa gogo wanajivuna, tayari kwa mieleka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Na Waunguja hutuna, misuli imewatoka
Huthubutu kujikuna, wala huwezi toroka
Gogo litavyokuchuna, Pu! chini waporomoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Mbona jama hamuoni,kama muliopofuka
Magogo tele mwituni, miti ya kila tabaka
Gogo hili lina nini, naona mmelishika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Amour Rashid)
- Sio gogo asilani, sije mkahadaika
Funza washalila ndani, unga linapukuchuka
Halifai hata kuni, licha mbao kupasuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Amour Rashid)
- Wacha na midoriani, miti unayotamka
Misonobari mwituni, misitu imejishika
Ni katu hailingani, na muanga msifika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huu ni muanga jama, wavyele twaukumbuka
Muanga ulosimama, ni katu kukwerezuka
Gogo la baba na mama, kwa mababu letukuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Hai hati hai hati, yalaiti natamka
Ni nyonda pendo la dhati, ni mwanga ulotukuka
Silifananishe jiti, na gogo lenye baraka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ni gogo lenye thimari, aidha na auraka
Kulipiga misumari, mapanga hata mashoka
Kulijengea tanuri, ni dhambi bila ya shaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Situtwezeshe fiili, wajua za kuumbuka
Kutughilibu akili, gogo baki kulisaka
Tukamwacha mfadhili, angamizwe na vihoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Nudhura yako batili, gogo halitakatika
Umekita mhimili, si rahisi kuchangika
Sifanye mambo thaqili, gogo kulisukasuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Mvule mti makini, acheni zenu dhihaka
Ovyo hauonekani, mvule umefichika
Chekundu chake kiini, hauna mataka taka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Amour Rashid)
- Seremala wa zamani, kwangu musiwe na shaka
Kwa chembeu na jambeni, hakuna wa kunifika
Hulaza kichwa begani, msumeno kiushika
Kula ajae na shoka, katu hawi seremala
(Amour Rashid)
- Jambeni ya kizamani, kidhati imenoleka
Kinoo kwangu cha nini, bado chuma kinawaka
Sithamini wa mashini, hata kama mtacheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Amour Rashid)
- Akhui Bwana Amuri, seremala mtajika
Muanga si mahamuri, kila mtu kuyapika
Gogo linatoa nuri, ghurubi na masharika
Kula ajae na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Limewashinda wahunzi, wale wanotambulika
Walidhani ni muanzi, mwepesi kupapurika
Vikawakwama viunzi, na gogo kutochangika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kama kuwa seremala, ni mtu kubeba shoka
Wangeweza vigagula, walotaka kulifyeka
Wakalinyenda kiswala, hebu gogo gagaduka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huuthamini muanga, ijapo unatajika
Mvule umekuzonga, hutaki kukuondoka
Japo ukawa muhanga, vipande ukakatika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Akhui ni lako gogo, letu sote twalitaka
Mbona walipa kisogo, mpingo umekuteka?
Usiyaone madogo, pulika Bwana amka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kitendawili natega, kitendawili teguka
Sufuria na mafiga, maji yameshachemka
Kutia hari masega, asali kumiminika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Jua linameremeta, jama kumepambazuka
Tuache kuteta-teta, gogo linanawirika
Nuru inametameta, kizazi kuunganika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Wana wa neti wenzangu, kuna nini mewafika
Mimi kwa upande wangu, safari menigubika
Nafunga mizigo yangu, kurudi nilikotoka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Warashidi Ndugu yangu, katega na kutegeka
Gogo letu walimwengu, haliwezi kuibika
Mfano wadudu chungu, twalinda sijeumbuka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Hilo ndilo jibu langu, mwasemaje washirika
Twaweka kando mirengu, wala hatwebu dhihaka
Zaidi twampa Mungu, ikiwa watatuteka
Gogo haliebu shoka, li kweche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Watumiaji wa gogo, sio tu seremala
Huchongwa bila ya zogo, na majini likalala
Kuna na walo wadogo, lakini wenye madhila
Kula ajaye na shoka, katu huwa seremala
(M. Simba)
- Gogo hufanywa ngalawa, kuelea si udhia
Hubeba vitu muruwa, mali pia abiria
Na mchongaji mwajuwa, sie seremala pia
Kula ajaye na shoka. katu hawi seremala
(M. Simba)
- Wapo mchwa pia chawa, gogo ndani ndani wala
Wasi wasi ni kwa hawa, viumbe waso muhala
Mahasidi sawa sawa, waweza litia ila
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(M. Simba)
- Bandu nao ni kipigo, hili wengi mwalijuwa
Mchwa nao kama ngogo, sunami yasingiziwa
Shime kulienzi gogo, kwani laweza ibiwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremela
(M. Simba)
- Mutapiga makelele, sauti zitakauka
Gogo, shina na vilele, hata halitagutuka
Litanawiri milele, kwa nguvu zake Rabuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Bwana Hemedi twajibu, wavyele weshaamka
Nuru hii ya ajabu, ni njia ilonyooka
Dini ya babu na babu, jamii twakusanyika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Mbona mwaacha utamu, Hashili hujasikika
Profesa Burahimu, muda umeadimika
Sasa nanyi yenu zamu, uwanjani kumwagika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Salim Al-Mauly)
- Haliingii ukungu, muanga gogo hakika
Haliliki kama dengu, mchwa wanasikitika
Hata watowe mafingu, fedha za kuchikichika
Gogo halyebu dhihaka, kwereche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Kilichomo kwenye jungu, ni maji yanochemka
Watu wameapa Mungu, makundi kundi watoka
Wazee wenye mabingu, na vijana kadhalika
Gogo halyebu dhihaka, kwereche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Sufuria ndugu yangu, latumika kwa kupika
Taratibu za kizungu, kila kitu kuandika
Ikiwa kapikwa changu, au bunju asolika
Gogo halyebu dhihaka, kwereche lakwerezuka
(Mohammed Omar-Engineer)
- Kuni zake haziwaki, mwajua mulojaribu
Chungu chao hakipiki, bure wasipate tabu
Watajinyonga kwa dhiki, kwa kuni si mujarabu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Viwe vipande miteni, gogo walivyosaliti
Wamimine tarefeni, na wawashe kibiriti
Watasema kitu gani, moto kukosa sauti
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Muanga mti mgumu, kwa moto hauungui
Hata wakiudhulumu, kipande hawabandui
Ndio mana unadumu, viroja havifalii
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kama ilikuwa nia, gogo kulipopotoa
Kisha moto kulitia, nishati kujipatia
Yao wakiongelea, yetu yakiteketea
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Gogo moto halingii, lina kinga ndani yake
Kwa maji limerishai, kwa uzima lijishike
Watazimaliza rai, wabaki waweweseke
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wajuwe hapapikiki, watabakia na njaa
Kuni zake haziwaki, wala yetu mikandaa
Wala kidudu hazuki, uchanja kuwagaia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kwa kuni si mujarabu, kwa gesi chungu chapika
Hilo kwao sio tabu, gesi moto unafoka
Unavima mtiribu, chungu wamekizunguka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Muanga hauchangiki, sasa imethibitika
Walokuja kwa mikiki, leo wameazirika
Gogo vyema limesaki, bila ya kutetereka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ni gogo lilo imara,wenyewe wamelishika
Daima ndilo kinara, hilo limethibitika
Japo linafanywa kwara, lisiweze tamanika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Nawauliza wahenga, wa muanga msifika
Gogo lauka mchanga, huenda likasafika
Vikaondoka vichonga, vyenye nyundo na mashoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Hayo yakajiri kuwa, yakawa ya uhakika
Wavyele wakapumuwa, wataka sasa ongoka
Ni lipi lilo muruwa, la wao kwanza kushika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kunawirisha mauwa, yale yaliyonyauka
Au kwondoa suruwa, viumbe wanoteseka
Kutoujali uluwa, watu wakashikanika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Waatasimu jamia, gogo litanawirika
Yasemwa huu udhia, muanga ukijishika
Wenzangu mumeridhia, hapa tulipopafika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kula wahedi akiri, gogo kutoachwa peka
Tulilinde linawiri, matundaye kuongoka
Lirudi kwenye kiriri, zamani lilikotoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Hayo kweli tadhihiri, mimea kustawika?
Busitani kushamiri, kwa kila cha kusifika
Au twakosha suduri, kuusha yetu mashaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ho! jama yaoneni, mambo hayakufichika
Mwenye kushika mpini, hataacha kuzuzuka
Ujabari kula fani, asiweze kushikika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Huzidi khadaa zake, kupindukia mipaka
Hajali walo wenzake, tena awasusuika
Liwe gogo lake pweke, katu hana kutosheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Huongeza na vituko, upate kubabaika
Yakuchoshe masumbuko, na tamaa kukatika
Gogo uliache huko, ubaki kulalamika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Akushindae kwa tonge, usimuache kucheka
Towelea kwa mabonge, ajuwe huna dhihaka
Ukisha mbele usonge, tena bila ya kuchoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh barkey)
- Gogo ijapo imara, wenyewe wanalitaka
Ila lapata madhara, hilo halikufikichika
Gogo limetekwa nyara, na miba ilochongoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Nuru inaliangaza, hilo nalo la hakika
Mauwa ya Mwanamiza, yameanza kuchipuka
Kubezana kumaliza, mshikano kuungika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Mwanga mithili hauna, hauwekewi mipaka
Iwapo aweza guna, maarifa asotaka
Lakini mezindukana, hata wasofikirika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Majani yalonyauka, sasa yanatononoka
Gogo litanawirika, Allah ahadi kaweka
Wal'ogopa kutamka, kunyamaa wamechoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kipindi nyeti yakini, ni kigumu kupitika
Mwokozi nuri amini, ndipo tutapookoka
Kiunganika majani, gogo litasitawika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Hima mizizi ungeni, na maji kumwagilika
Inawiri busitani, kwa zana zinosifika
Tukimuona zinduni, na ambari atafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo litasitaqimu, magugu tukiyafyeka
Wenye jembe mujihimu, mapanga tumeshaweka
Wavyele ni yao zamu, pori lote litawaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kushikamana muhimu, na nuri isozimika
Kujitokeza kwa hamu, majina kujiandika
Ijulikane kaumu, wenyewe kutambulika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Tulilinde letu gogo, zama sasa zimefika
Sitende mambo upogo, tukaja kuungulika
Sidhani si lako gogo, kakacha jema kushika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Baada kisa mkasa, wazee, dada na kaka
Si wakati wa siasa, ni vita sio dhihaka
Gogo wanalitomasa, wadhani litachangika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada dhiki faraja, nduzangu nawaalika
Asibakie mmoja, wa ngumi na mieleka
Si wakati wa kuroja, gogoni kuna gharika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada moja ni mbili, hivi sasa twadhikika
Watuumisha akili, watupiga tikitaka
Hadi lini jambo hili, wenye gogo twasibika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada vita vigumu, wiki, dahari na kaka
Gogoni mesitakimu, sisi twazidi kunuka
Tupiganeni kwa hamu, si hivyo twaadhirika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada zangu porojo, kwa mabomba na spika
Nondo, panga, mkongojo, jambia, na kadhalika
Na tuianzeni fujo, gogo tupate jitwika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada ya vita hivi, na gogo kuliinjika
Tukaondoa ugomvi, wa Msuka na wa Chwaka
Wakulima na wavuvi, wote wataneemeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada nyingi hasada, gogo limehasidika
Wamekufa kwa mashada, watu hata karakaka
Tufanye nyingi ibada, kila panaposwalika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada ya zetu dua, na nyingi nyingi nafaka
Yafaa kulizingua, gogo liote ukoka
Tuvune hadi mabua, kwa majamvi na mikeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Baada ya beti hizi, langu neno mesikika
Gogo sifungiwe mbuzi, wenyewe twaja tambika
Madhalimu pia wezi, wote watapukutika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Vyereje bila ya hila, gogo kuhaulishika?
Vyereje ikawa mila, ndovu kuweza kuruka?
Vyereje ki-farasila, halili ikakidhika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje kwenye kibula, mbele choo kuchimbika?
Vyereje asiyekula, aweze kunawirika?
Vyereje kwenye hafula, mtu aanze futuka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje kwa kila dhila, mtoto akagawika?
Vyereje asiyelala, akaweza kuamka?
Vyereje uwe wakala, bila gogo kuridhika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje bila ya ila, gogo lianze nadika?
Vyereje kwa kiholela, wajipange walitaka?
Vyereje si mbadala, kama mipini ya shoka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje tuache kula, gogo lisijeteseka?
Vyereje kula mahala, gogo hili lasifika?
Vyereje kwenye risala, gogo lazidi someka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje limetawala, gogo la kufikirika?
Vyereje maseremala, mikono kutetemeka?
Vyereje aje kabwela, gogo aweze liteka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje kwa kila hila, kisunzi gogo kushika?
Vyereje leo ukala, kesho gogo kutoweka?
Vyereje kwa silisila, gogo limeng'ang'anika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Vyereje leo laila, hunuii kutamka?
Vyereje hutoi bila, gogo likanawirika?
Vyereje una suala, kwa gogo unolitaka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Katu hawi seremala, kula ajae na shoka.
Vyereje leo salala, unatoa mashitaka?
Vyereje kila fadhila, na za gogo wazitaka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
(Omar Fakih)
- Huwaje pasipo mvua, maji yakatiririka?
Huwaje pasipo jua, majani yakakauka?
Huwaje bila murua, mipango ikanyooka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje bila ya mimba, mtoto akazalika?
Huwaje pasipo mwamba, ushindi ukapatika?
Huwaje alo mgumba, gogo letu kuliteka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje aso elimu, kitabu akaandika
Huwaje asojikimu, ya wengine kuyashika
Huwaje bila imamu, jamaa ikasalika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje pasi uchungu, moyo ukaungulika?
Huwaje penye majungu, mambo yakasawazika?
Huwaje penye marungu, udugu ukaundika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje pasipo nuri, mwanga ukadhihirika
Huwaje ukidhihiri, ukweli ukapingika
Huwaje latiwa nari, gogo nasi tunacheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje alo na nia, ya usiku kuamka
Huwaje alonuia, kumwabudu Mtukuka
Huwaje kufakamia, chakula bila mpaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje lokusudia, gogo lisile mweleka?
Huwaje anakimbia, mshikamano kuweka?
Huwaje anajilia, wengine wananyongeka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Huwaje asiyejua, lijamu akaishika?
Huwaje penye surua, tabibu akakoseka?
Huwaje mwatusumbua, na njia imenyooka?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Gogo hili sio mwamba, si kwamba li gumu sana
Ona goba la mgomba, shoka inavyopigana
Gugunya hadi riamba, upapi hutouona
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Ovyo makeke ya mamba, gogoni kusukumana
Li majini musambamba, kiligusa takupona
Afadhali kumuomba, akaridhi wake bwana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Mafundi waja kiimba, taire tai wanena
Ubishi kwenye vilemba, gogo halina hiana
Asemaye amba amba, naakeshe hataona
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Natija liliyokumba, yatoka kwa Subhana
Gogo si gogo la pamba, la muanga mwaliona
Ambari ukiikumba, zindu hamujapishana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Lina nuru ya kupamba, huku limeroweana
Bambua yote magamba, cha kutupa hutoona
Wa vitale wa sambamba, wa kudhuru na kupona
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Gogo japo ni jembamba, nuruye yakifu sana
Shida limefungwa kamba, wenyewe kivutiana
Ya Rabbi munanitimba, gogo thubutu kunena
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Khofu na nisiloomba, ni gogo kuja libina
Hapatokuwa mjomba, wala mamaye Amina
Nuruye nguvu za simba, wa kudhuru takiona
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Wa mji na wa mashamba, kaya tabadilishana
Walokuwa omba omba, afiya zao tanona
Vipepeo na viwamba, shehiani tajazana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakihi)
- Weledi tajua kwamba, ufundi ni kazi sana
Iwe mtu amechimba, na kusoma zote zana
Waweza asali ramba, mzinga ukakukana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Omar Fakih)
- Thaqili mambo magumu, ndivyo yanavyooneka
Ghalati kusitaqimu, ndiyo wanoyatamka
Wasopenda baragumu, kupigwa likasikika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ijapo bamba ni gumu, wajibu njia kushika
Tusije kukosa hamu, gogo litajachangika
Janga kukumba qaumu, tuepushe Ya Rabbuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Nuru ingaze sirati, tusije kutetereka
Imani na mikakati, siri ya kuneemeka
Ugomvi tupige buti, ya kwetu yataongoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ni mwito kwa furusani, imani dini kushika
Waondoe saratani, gogo iloligubika
Arejee ahueni, zamani alotoroka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ndugu zetu hawajali, madhali wana uluwa
Wao hawaoni mbali, mambo yao maridhawa
Tutapigana kwa hili, na iwe itavyokuwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Na iwe itavyokuwa, thuma hatutokubali
Vitisho tunofanyiwa, na inda zisomithili
Naapa haitakuwa, njia hatutabadili
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Njia hatutabadili, mbele kwa mbele twendea
Mwishowe ni mara mbili, tatu hatutangojea
Na Mola wetu Jalali, Yeye twamtegemea
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Jambo moja ni hakika, shuruti hili niseme
Umoja tukiuweka, tutawafanya wakome
Gogo halitakatika, tukikazana kwa shime
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Bila ya Faki na Ame, pamoja kusikizana
Wakaamuwa wagome, kuyatenda ya maana
Gogo takwenda machame, wa kijiwe kulizana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Ni vyema kusikizana, tanga pamoja kutweka
Sote ni ndugu na wana, ni wamoja kwa Rabuka
Kikubali kuungana, gogo halitatutoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Ya mgambo hiyo yaja, wana wa Zinjibaria
Njoni tuketi pamoja, gogo kuzungumzia
Wajibu si wa mmoja, ni wetu sote jamia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Tushikamane jamani, tusije tukajutia
Tulinde wetu watani, Mola tatusaidia
Kwani hatujabaini, kuwa gogo lapotea
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wasolitakia mema, kamba wameikazia
Kwao gogo sio mama, hawana hata hisia
Likitota likizama, kwao wao ni sawia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wao watashangiria, wakiliona lazama
Vicheko vitawajia, gogo kupata nakama
Si lao la kulilia, la kwao liko Mrima
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wazifanya kila hila, tafauti kuzitiya
Watugawa kwa kabila, chuki kuzishadidiya
Kwao wao ni madhila, yetu tulodhamiriya
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wametia na ujimbo, husuda kuongezea
Kwao huo ni urimbo, waliotutegeshea
Kuwa wengine wa kambo, wa kuja kudoea
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Tumejaziwa siafu, eti gogo kulilinda
Tunatiwa nyingi khofu, na kutufanyia inda
Wapita kitukashifu, wadhani watatushinda
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Nimefurahi hakika, kukuona we' wa Nyali
Hivyo ulivyofutuka, ukaeleza ukweli
Patakuwa pata shika, ili kutimiza hili
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Mabaya medhamiria, hata imani hawana
Lengo lao kufikia, hata ni kwa kutengana
Wanaingiana pia, na vita wanapigana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Wenyewe wajivamia, maneno kutupiana
Wanajua pia nia, walilokusudiana
Huenda ikawa njia, wema wakaja ungana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Wawili walo pamoja, ubaya kujifanyia
Wakitengeza na hoja, gogo kulishikilia
Wakaanza kuporoja, wote watafuta njia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Mshangao wanijia, mambo yanavyoendeshwa
Wenye haki wanalia, namna wanavyotishwa
Hakuna wa kusikia, tamaa wanakatishwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Mlinzi wa gogo hili, ajifanya mwenye nguvu
Hana hili wala hili, kwake sote wapumbavu
Hebu mustakibali, gogo kutoka utomvu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Na ategemea nundu, kutoka alomwajiri
Ataletewa kwa rundu, wale wataohajiri
Hata kutumia mundu, haki itapodhihiri
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mohammed A. S.)
- Maneno yako adhimu, wapi uliyafundika
Wakati umeshatimu, wa sote kujumuika
Hatuna wa kulaumu, gogo likimomonyoka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Ya-ghulamu ya-ghulamu, sasa basi kubweteka
Tuikusanye kaumu, vijana wa kila rika
Tukomeshe udhalimu, tusizidi athirika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Sote tukiwa tayari, kwa ari si kubwatuka
Kidete tukavinjari, vipi gogo taliteka
Tutashinda asikari, bila hata patashika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Haihitaji mabomu, na bunduki za bazoka
Na wala kumwaga damu, kama tukihamasika
Zetu nyingi tarakimu, silaha isoalika
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Wenzetu sio mahiri, msije kuhadaika
Na zote zao jeuri, ulevi wa madaraka
Kweli itapodhihiri, gogoni watadondoka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Siogope zao ndaro, kama makinda ya nyoka
Watakufa kwa kihoro, umma ukiwazunguka
Tuwazoe kwa pauro, mithili yake vidaka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Tafakari kwa makini, maneno ninayong'aka
Nguvu ya umma yakini, ulaya mebadilika
Ukuta Ujerumani, ghafula ulifumuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Sasa kwa nini tuchoke, na kuzidi fedheheka
Kwa hayo yao makeke, na kwingi kuruka ruka
Gogoni tusipachike, bendera iso kishoka?
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Sasa tufanye juhudi, hakuna tena kudeka
Kampeni kuzinadi, mpaka watapongozoka
Hakuna tena kurudi, nyuma mwiko kugeuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Tujipange uwanjani, kama mchezo wa soka
Tungie barabarani, singoje lao shitaka
Watatulisha chochoni, kama 'sipoerevuka
Kila ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Nguvu zetu waziviza, gogo kitaka lilinda
Juhudi wazikatiza, mbele tusipate kwenda
Mbigili wameeneza, dondola ni yao inda
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Dondola dawa ni moto, hilo hasa twalijua
Sio kazi ya kitoto, iko siku itakua
Ikibidi kwa mshoto, tumba lao kuwavua
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Gogo sawa na mtunda, fadhila zake lukuki
Ila wao tawashinda, imesaki kwao chuki
Ndipo nasi twajipinda, papatu halibanduki
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Faida kwao halina, tungeona ingekuwa
Miaka wamelibana, mengi yangekwisha kuwa
Ila hasara twaona, gogo hadhi wamenyuwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Gogo wamelizunguka, mikononi libakie
Kutwa wanachacharika, usiku walibanie
Libasi zinawavuka, nini niwahadithie
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Watu wamejikusanya, nguvu zao kwa pamoja
Weshajua la kufanya, kazi yao sasa moja
Mabavu yawatawanya, umoja wanaufuja
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kwa wingi wameitana, kila pembe ya Unguja
Pemba wameambizana, mabadiliko ni haja
Kisha wakaamshana, kukumbushana natija
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Majina wakaandika, kwenda kuifanya kazi
Wakazipiku pirika, kutandika mabazazi
Wangoja siku kufika, mambo wayaweke wazi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Siku ikikaribia, vituko navyo vyazidi
Baadhi wanaumia, kwa inda pia hasadi
Kusudi kuwatishia, kinyume wapate rudi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Mikwaju wanacharazwa, nyumba pia wachomewa
Chini wanagaragazwa, na heshima kuvuliwa
Hakuna linalosazwa, dhuluma wadhulumiwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kama askari China, mbele watu wanasonga
Wafanya kutokuona, visago vikiwagonga
Gogo ndio tawapona, patanyoka palonyonga
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Hakuna anaegomba, matendo ya kukikhiri
Watu wote ni washamba, ubabe ni umahiri
Ila Mola twamuomba, siku asiiakhiri
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Siku usiiakhiri, Ya Wadudi twakuomba
Jambo jema lidhihiri, tulifikie na tumba
Asali ituchiriri, tukinywa na kujiramba
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Atakua mas-uli, hilo twajua hakika
Patatakiwa ukweli, uwazi tahitajika
Si bure ya jambo hili, dunia mebadilika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Tutakuwa mashahidi, gogo walolihasiri
Tutafunua fuadi, kueleza yalojiri
Umma nao tashitadi, tajitokeza kwa ari
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Gogo limekuwa zito, washindwa kulichukuwa
Launguza kama moto, kilidasa waunguwa
Wakongwe nao watoto, walinda macho watowa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Gogo lawatia joto, ni vigumu kuchangika
Wenyewe sasa wamato, tayari washaamka
Na walete mkongoto, watu tazidi zinduka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Watu wameshazinduka, kulala hamna tena
Ari imekamilika, hakika tutapambana
Walitakalo wataka, muhali si leo tena
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Vituko tunaviona, vinofanyika gogoni
Wapiga wakitafuna, wana wako mashakani
Mwaka huu tabanana, hapahapa kiamboni
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Lengo letu kileleni, kwenda lisitiri gogo
Tumeanzia shinani, twenda kidogo kidogo
Tushakita matawini, hatujali lao zogo
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Na wailete dondola, hakuna atoshituka
Si wakati wa kulala, huo tumeshauzika
Gogo letu si jalala, kutupiwa kinonuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Na unyonge tulonao, hakuna atosarenda
Watuwekee vikao, wakishuka wakipanda
Kwa mwaka huu tunao, wataona kirindanda
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wakipenda wasipende, gogo hili litalindwa
Kwa walioko Mtende, na wale walio kendwa
Pamoja mbele tuende, chombo chetu kishaundwa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Dalili ya giza nene, karibu kupambazuka
Hivyo tabu msione, sio mbali tutafika
Na twende tusisonone, siku zinahesabika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Siku zinahesabika, gogo tutapolituwa
Pale tutapoliweka, kwa amani na muruwa
Na kila anohusika, matundaye atapewa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Kweli siku ziko chache, ya wana kutozurura
Utani sasa tuwache, tuhimize zetu shura
Tusingojee kukuche, tutalia kama chura
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Gogo tulitoe kwao, mikononi tulipore
Wasije lichanja mbao, likaja potea bure
Tujitokeze kibao, gogo tukaliburure
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Tuzikumte sonono, maudhi pia mavune
Tupune yetu mishono, mbali tusikaliane
Walolala kama pono, hima natuamshane
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Nguvu wao kitumia, nasi tusiwe kalili
Hapa palipofikia, dhambi kustahamili
Imara kusimamia, lisende gelewa mbali
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wingi wao sisimizi, gogo huweza kokota
Tukipangusa masizi, macho yetu yataita
Itakuwa ndogo kazi, kuyakiuka matuta
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Kila mtu zana zake, mkutano msituni
Mtu kwa wakati wake, achomoe kibindoni
Achomeke palo pake, matokeo ni jioni
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh albarto)
- Wa asiliya hajazi, waitakayo mezani
Nawambia waziwazi, umoja ndio ramani
Ya kuifanyia kazi, kufikiya ufukweni
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wenzangu nawaidhi, masikio tegesheni
Ugonjwa si wa baadhi, wote tumo mkumboni
Kushinda haya maradhi, dawa umoja yakini
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wakereketwa wa gogo, kamba na tuikazeni
Tusiyaone madogo, kubwa lijalo jamani
Wataka shari machogo, kwa dondola si amani
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Twaona kila dalili, shari livyokazania
Waufanya ukatili, dondola kulitumia
Watudhalilisha hali, gogo tupate kimbia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Katu hatuendi mbali, gogoni tutabakia
Tavutana kwelikweli, hadi lengo kufikia
Tutalimaliza hili, kushindwa hweturidhia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kurudi nyuma ni mwiko, kwa kifua twatamka
Kwa ngumi na matambiko, bado hatujashituka
Unaalika mkoko, na muanga kadhalika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Wa Mrima wana lao, letu walitakiani
Gogo hili si la kwao, watubugudhi kwanini
Ni yao makusudio, walitupe baharini
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hukaa kitafakari, siku itapowadia
Itapokuwa fakhari, gogo kujinasibia
Kwa sifa zake nzuri, njema za kuridhia
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Daima ni yangu ndoto, nilalapo yanijiya
Nnawaona watoto, wazawa Zinjibariya
Waliojawa na moto, gogo kulisimamiya
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Waitakayo nafasi, neema kutuleteya
Watutoe wasiwasi, ufukara na udhiya
Kwa Mola wetu mkwasi, hakika yatatimiya
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Kula aliye na haki, matundaye atapewa
Haitakuwa hilaki, hakuna atoonewa
Na hii mingi mikiki, yote itaondolewa
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Hatakuwepo dondola, nyuki wala duduvule
Hakutakuwa na hila, huyu siye ndiye yule
Kwa buraha tutalala, usiku na upitile
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Roho zetu zitatuwa, mwanga tukishauona
Yote ni majaaliwa, alotupa wetu Bwana
Ayafanyayo yakuwa, ya usiku na mchana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Maseramala wa kweli, ndipo tutapowaona
Na misumeno mikali, patasi na zao zana
Waijuwao halali, haramu kwao hakuna
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Watakuja tuundia, vyombo vilo madhubuti
Vyenye sifa si bandia, si vile vya marikiti
Sote tutashangiria, muanga sasa ni mti
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
- Maua yananyauka, majani yapukutika
Meli zapigwa gharika, vidau tanga vyatweka
Mambo yamebadilika, mbele nyuma kugeuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Yana mwisho yatajiri, gogo litanawirika
Utarudi utajiri, wa waridi kuchanuka
Asumini kidhihiri, majogoo yatawika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Hawakukosa wahenga, busara walotamka
Saburi mtoa mwanga, ni msingi muafaka
Wakubwa hata wachanga, uvumilivu kushika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Jahazi meshika kasi, muanga waserereka
Chombo hiki hakikisi, karibuni tutafika
Kwa mbali unauhisi, upepo wa kule Chwaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ahadi nayo ni deni, ukweli ninatamka
Beti jama si miteni, zishindwe kukamilika
Ahadi ya khamsini, bado tunaikumbuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ahadi kweli ni deni, mwenzenu medharurika
Naungulika maini, kiona mnavyofoka
Mkiniacha dagoni, nyavu zangu zakauka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Kimya changu siwe shani, iko siku nitazuka
Na nyavu zilosheheni, gogoni tazipachika
Siku ya siku mwandani, sote tutashereheka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Siku ya siku amini, ndipo 'tapobainika
Adui wa Visiwani, 'tapokoma kupayuka
Wataumwa mapafuni, roho kuwakukurika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Wataumwa magotini, miguu kupopotoka
Wapooze viungoni, na matumbo kukovyoka
Na uji wa maskani, utawashinda kunyweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Na uji wa vibandani, 'tachacha na kuchachuka
Walojifanya maponi, mbawa zitawanyonyoka
Na mbio za sakafuni, ukiongoni kutovuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Na mbio za marathoni, wa gogo kutoshindika
Tuingie himayani, pulika mwana pulika
Tuipachike mizani, nchi ya kusadikika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Mizani iwe mezani, haki ipate tendeka
Kila aliye likoni, isiwe kubagulika
Avune nazi laini, sio yale matunguka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Nazi si za wa jikoni, raia tunateseka
Gogo lililo moyoni, dhuluma itafutika
Ndiyo tukawa na kani, chelezo kuchelezeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim Ali)
- Ninatangaza zabuni, ya kuwatunza vizuka
Miaka arobaini, wao wameatilika
Wana pingu mikononi, miili imekoboka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Gogoni tupapandeni, tumechoka bughudhika
Mbele hadi mkiani, kwa umoja na shirika
Na tuikaze demani, safari kuiinjika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Siku ikikaribia, asakamwa seremala
Vikwazo kumzuia, ili kumtia ila
Ila Mola tamvua, yanomkuta madhila
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally saleh - Albarto)
- Kumkana seremala, viamboni wawafuje
Ni kuzusha masuala, kazi tutaifanyaje
Yeye wamtia ila, vibarua takuaje
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ally Saleh - Albarto)
- Yaguju yametamkwa, hayawi wanayotaka
Watazidi kuhemkwa, gogo halitachangika
Ni zumbukuku zumbukwa, kurudi ni kuumbuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kelele za nyungunyungu, hazitufanyi kuuka
Kwa bunduki na kwa rungu, gogo halitaporeka
Aso mtu ana Mungu, wahenga wametamka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kurudi ni kuumbuka, mbele ndiko kwa hakika
Tumeshafyeka Msuka, magugu yametoweka
Twaviondoa vihoka, Paje vilikofichika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Vyaogopa panga kuu, magugu linalofyeka
Kipaza sauti juu, vyahofu vyatetemeka
Wewe si wa mji huu, rejea ulikotoka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Vihoka vyanishangaza, vimemaliza mizuka
Vyenyewe vimejikaza, gogo letu vyalitaka
Lakini mbele ni kiza, vimekwama vyaumbuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Simba anaponguruma, tisho msitu na nyika
Katu haturudi nyuma, jiwe tukajageuka
La haki litasimama, ahadi Mola kaweka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Yalo dhahiri mwaona, hayana siri bayana
Hayafichiki hapana, mmoja asiye ona
Lipi mnataka tena, ushahidi wenye mana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Wamejaribu pabaya, pakubwa waliposhika
Wapi mmeyasikiya, kuchezwa simba wa nyika
Ni ajabu mambo haya, bado hawajashituka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Wamemchokoza kwao, ndani porini mwa boma
Palipo na ngome yao, naye mbele kasimama
Hawajuwi wende zao, au wabakie nyuma
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique ( Maher Fundi )
- Kaa kikosa gandole, haiba humuondoka
Hugeuka kolekole, kwenda asikooneka
Hatima ni ile ile, na hawa itawafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Wanayo ole wanayo, wangamtimba wa Nyika
Mashaka wajitiayo, cha moto kitawafika
Wanatapatapa nyayo, miguu kukukutika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Sakaratulimauti, kikomoni wamefika
Kwenye kibanda makuti, ndani wamejibandika
Hakiwakingi mauti, Ziraili keshafika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Seramala hakaniki, kwa kuwa gogo ni lake
Kashinda yao mikiki, wamempa haki yake
Hakuna kilichobaki, yabaki wakajizike
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Itakuwaje waseme, gogo halikumuhusu
Kama tampa Makame, na Hamadi mruhusu
Kwani wote wanaume, gogoni watadurusu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Wagogo mefarijika, kumuona seramala
Mradi hakupingika, kawafunza mitaala
Haki yake mepatika, wenyewe hatukulala
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Akili kweli ni nywele, kila mja kajitwika
Lakini wenzetu wale, wamejitwika ukoka
Waliyoyafanya Dole, yamevuuka mipaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Katu hawi mtukufu, mvunjaji wa maduka
Ya watu waaminifu, walioacha vizuka
Kudhulumu roho pofu, na wengi wakasibika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Gogoni mesitakimu, mwavuna yasobovuka
Makubwa, mengi matamu, madanzi na matomoka
Imefika yetu zamu, kwa nini mwakasirika?
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Ikwetu zamu ikwetu, mwezi umetumurika
Hatwebu yenu papatu, tumekwisha hamasika
Shahada ni mara tatu, pakacha tapakachuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Njooni Juma na Duchi, waashi na makanika
Tupigane kama kuchi, na wasio sarifika
Walotunyang'anya nchi, sote tukafisidika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Kassim O. Ali)
- Pakachani kuna vuma, pepo tabibu si wao
Mwana wa moyo mrima, hilo ni chaguo lao
Ndicho kizaliwa chema, kilicho asili nao
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Pachawe ajivuniya, acheza kwao atunzwe
Njuga ameyavaliya, kayakubali achezwe
Ana nguvu kapaniya, karata isigeuzwe
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Ung'ongo umefumka, pakacha limeachana
Vilo ndani memwagika, vyote vimeonekana
Mzigo haukufika, wenye mali wamenuna
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Wameudhika kikweli, lakini nguvu hawana
Huko liliko ni mbali, lirudi halina mana
Seuze kumpa kuli, hasara watagombana
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Wameduwaa viwazi, vinywa vyao havifungi
Wanatokwa na machozi, mganga wao hapungi
Na sasa hawayawezi, wamejipiga ushungi
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Unique (Maher Fundi)
- Mfa maji ana lipi, ghairi maji kushika
Nawafanye hata vipi, ngazi wataishuka
Mifano iko mingapi, wa juu waloanguka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Huwaza na kufikiri, akilini husumbuka
Wanapalilia shari, bado hawajaamka
Kwa jeuri na viburi, kutenda yasotendeka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Shari ndiyo sera yao, tangu na tangu miaka
Wafanyweje watu hao, waweze kubadilika
Hila pia mbinu zao, kila siku zageuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Usaliti jambo baya, na hilo halina shaka
Mengi waliyausiya, ya qitali kutoshika
Watu wakaitikiya, ahadi wakaishika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala.
Ahmed Rashid
- Ahadi waloitoa, ni ya haki kutendeka
Wao wangejitolea, hilo liweze fanyika
Kumbe ni kuwachezea, shere na pia dhihaka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Ahmed Rashid
- Watu walipotulia, mizengwe hata mizuka
Vyema walipangilia, na kiapo wakashika
Batili kushikilia, ua, piga na kuteka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
Ahmed Rashid
- Kutanzwa sio kushindwa, ukajikomea mwako
Kukali mwendo wa kwendwa, safari si babaiko
Vigumu navyo hupindwa, kama ushalenga lako
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Safari zina vishindo, vikakusibu vituko
Mawimbi pia mikondo, hukupeleka kusiko
Nawe geuza mitindo, uendelee wendako
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Hata malenga wa tungo, wajuzi wa miandiko
Hubwagiza kwa mipango, wapate mapumziko
Kisha hujaza mapengo, huzidi msisimko
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Ukeni safu kupanga, shikeni yenu mashiko
Musichoke kuyaganga, kujiripo tikisiko
Gogo hili la muanga, musilipe mpasuko
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Saleh Barkey)
- Nami nauingia papo, gogo adhimu baraka
Vitaondoka vipepo, vihodi hata vihoka
Na Muanga ungalipo, ni katu kuterereka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Ijapo hili twanena, moyoni tunasumbuka
Huwaje bangu kuwana, ndugu wanaotajika?
Muono wao mpana, yasemwa si kupayuka
Kula ajaye na shoka katu hawi seremala
(Ahmed Rashid)
- Kwa uwezo wa Karima, Mola wetu mwenye nguvu
Pamoja hatasimama, na watu hawa waovu
Jicho lake la rehema, kwetu takuwa angavu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Mola wetu ya Wadudi, kwako wewe twajikweza
Waondoe mahasidi, uwapaze kama pweza
Wanyooshe wakaidi, ukweli waone kwanza
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Uwaonyeshe ya haki, njia iliyonyooka
Wajuwe kama hutaki, hakuna kinofanyika
Kwako wewe twashitaki, twaomba zako baraka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Kula ajaye na shoka, kuchanga na kuharibu
Mzuwie ya Rabuka, asituzidishie taabu
Muongoze kwa hakika, arudi kwako atubu
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Gogo letu ulilinde, na lipate nusurika
Wabaya mbali waende, pia nao vibaraka
Mashoka na zao pinde, wazione zayayuka
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Tuzidishie rutuba, lizidi kunawirika
Ulijaze nyingi heba, neema kutawanyika
Watoto tupate shiba, na nguvu kuimarika
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Uwashinde mafatani, waliojawa na chuki
Uwape na mitihani, kwa mia na malukuki
Kama hawatabaini, watie kwenye hilaki
Kula ajaye na shoka, katu hawi seramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
- Kwako tumeelekeya, Mola wetu Ya Jalali
Mikono twakunyosheya, kuondoa hii hali
Gogo letu lapoteya, ndugu zetu hawajali
Kula ajaye na shoka, katu hawiseramala
(Mbarouk - Mnyonge wa Nyali)
Watungaji
Washairi walioshiriki kwenye ngonjera hii ni:
1) Mzee Mbaruku bin Mwendo
2) Sk. Saleh Mohammed Barkey (Saleh Barkey)
3) Sk. Ahmed Rashed Ahmed (Ahmed Rashid)
4) Sultan Ahmed Sultan (Sultan Ahmed)
5) Kassim Omar Ali ( Kassim O. Ali)
6) N-gongele
7) Mbarouk Hamad Shariff (Mbarouk -Mnyonge wa Nyali)
8) Ahmed Barkoa
9) Salim Al-Mauly
10) Sheikh Muhammad Faraj
11) Ally Saleh albarto
12) Hassan Omar Ali (Hassan O. Ali)
13) Maher-Unique
14) Imu
15) Abduu Salim
16) Miminae
17) Mohammed Omar-Engineer
18) Mohammed Abdalla Salim (Mohammed A. S)
19) Amour Rashid
20) M. Simba
21) Omar Fakih
|