|
|
Kimbia Ugwe!
KIMBIA UGWE, USIJAONA NG'OMBE ni shairi lililoanzishwa
na Sheikh Saleh Barkey na kuchangiwa na watungaji
waliotumia ufundi wao wa lugha yenye utajiri wa namna
yake usiochosha kuusoma na kurudia mara kwa mara.
Maana ya neno "UGWE" ni kamba kama alivyotuelezea
Sk.Kassim Abdulla, ambaye ni mjumbe mwenzetu mashuhuri
katika zanzinet na mmojawapo walioshiriki katika
ngonjera hii ya kimbia ugwe.Katufahamisha kuwa neno
"ugwe" linalotumika katika msemo "kimbia ugwe,
usijaona ng'ombe", lina maana ya "kamba" na hii ni
hakika kabisa wala hakuna mushkeli wowote.
Na maana ya jumla ya msemo ni kumtahadharisha mtu
akimbie chanzo cha matata kabla matata yenyewe
hayajamfika.Utaona dhahiri kwa maana ya neno "ugwe"
iliyokusudiwa katika msemo huu ni "kamba". Maana
nyengine ya hili neno "ugwe" abayo ni "uanguke"
haioani wala haisadifu na usemi wenyewe kama
ilivyofafanuliwa kwenye mjadala. Huwezi kumwambia mtu
"kimbia uanguke" na wakati huo huo ukawa
unamtahadharisha na pembe za ng'ombe!.
Haya yanatokana na kawaida za kikwetu na namna ya
ufugaji, ambapo ng'ombe hufungwa kamba kichakani kwa
malisho na inakuwa si rahisi kujuwa kajifichia wapi
kwa kuona kamba yenyewe na ndio ukaja huu msemo kuwa
uwe na hadhari kubwa kwa kuwa huwezi kufahamu
atakutokea wapi, na dawa ya yote bora kimbia ugwe
kabla hujaona ng'ombe.
KIMBIYA UGWE USIJAONA NG'OMBE
-
Yakueleya vizuri, fahali limechachama
Hakuna cha ujabari, ukweli ukisimama
Ukijitiya kiburi, pembe zitakuandama
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Saleh Barkey)
-
Nakuomba ya akhii, siri uifafanuwe
Alokusudiwa hii, ya pembe simraruwe
Leo miye sikwachii, hadi huyu nimjuwe
Ataye kimbiya ugwe,asije kuona ng'ombe
(Maher Fundi)
-
Kimbiya ugwe n'nini, jamani musinikhini
Nambiyeni hadharani, nami nione ya ndani
Sina raha asilani, hivi nimo mashakani
Ng'ombe huyo ni wanani, alokimbiya zizini
(Juma Salim)
-
Dudu unalolitaja, hakuna asolijua
Kutwa limo kubwabwaja, na pia hujihashua
Harufu chenza kangaja, apitapo lagwavua
Natuufunge mkaja, ajuwe tumeamua
(S.Hashil)
-
Kimbiya ugwe kimbiya, yupo avuma kipole
Mkinzi utaja liya, kusudi haina pole
Akhuyi geuza njiya, sitende yale kwa yale
Kushazuka ruhaniya, ganja na moja kidole
(Saleh Barkey)
-
Kimbiya sije jibana, ng'ombe hajuwi salama
Kimbiya ugwe kijana, ng'ombe atakuandama
Kimbiya leo si jana, tafuta mahala hama
Kimbiya sije kuona, hakuwachi takuchoma
(Salma Khamis)
-
Jidhatiti barabara, ili usije teleza
Pembe zake ni imara, tena sana zaumiza
Uhitajilo tambara, ng'ombe kuweza mcheza
Mjipange mduwara, mumtiye makengeza
(Said Suleiman)
-
Kheri bora kutuliya, nikachemsha akili
Mti tauparamiya, kuiepuka ajali
Nikigwa nitaumiya, kwa makwato ya fahali
Inuka simama dede, upate mcheza ng'ombe
(Said Suleiman)
-
Dede tumeshasimama, fahali kuja mcheza
Hata akija kwa wima, ngao tumeshatengeza
Tumeshazijuwa njama, pembe tutazikwereza
Katu haturudi nyuma, kidete tunamwangaza
(miminae)
-
Shemere tutamvika, pasi kuwa na khabari
Na amri kuiitika, pasi na lake shauri
Kiona tacho mfika, maisha yake takiri
Pahala pake kafika, pakutolewa jeuri
(Abdulla Al Harthy)
-
Ukimpima kichwani, hana ukali pembeni
Hawamuogopi nyani, wala watoto nyumbani
Asomjuwa ni nani, ngombe wa aina gani
Muache aje nyumbani, tumtiye mikononi
(Abdulla Al Harthy)
-
Dua ndugu iondowe, ng'ombe kumwita nyumbani
Ng'ombe humjuwi wewe, ni ng'ombe wa majangwani
Khuyi sijifaraguwe, huyo hachezewi ndani
Hadhari uichukuwe, pembeze zina medani.
(Walii Genderi)
-
Kiburi si maungwana, tuliza yako akili
Hodari ungajiona, dume usilikabili
Ubingwa ja huo huna, wa kumcheza fahali
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Kassim Abdullah)
-
Usijifanye shupavu, ya akhi kimbia hima
Utaanguka kibavu, ng'ombe akikuandama
Kimbiya kama mwerevu, usisubiri nakama
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Kassim Abdullah)
-
Haya yangu usilumbe, kwa hakika nakwambiya
Ukija kutogwa pembe, ndugu utajijutiya
Neno hilo usiambe, ya kwamba tamchezeya
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Kassim Abdullah)
-
Nikwambiayo wafiki, yafikiri na kupima
Usende kwenye hilaki, kipigo kitakuuma
Maji ya goti huvuki, utawezaje ya pima?
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Kassim Abdullah)
-
Majuto ni mjukuu, daima huja mwishoni
Nakupa wasia huu, usikilize akini
Utaja vunjika guu, wakubwazo kikhaini
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Kassim Abdullah)
-
Yakhe usijipe tabu, hili sikio la kufa
Si rahisi matibabu, ni mithili ya kifafa
Mwache ujifanye bubu, usimpe maarifa
Asitafute sababu, kashindwa kuziba ufa
(Assad Abdullah)
-
Haya huyo n'nani, anojitiya hodari
Ng'ombe akamzaini, kumtiya mtegoni
Kila siku hamkani, watu wako mafichoni
Akhuyi aweze nini, mwenyewe yu taabani
(miminae)
-
Kimbiya wako uwovu, ng'ombe asijekubana
Kwani huwi muwerevu, na mjinga uso mana
Ukaondosha uvivu, kuwa naye mbali sana
Ukanusurika shavu, ng'ombe akaja kuchana
(miminae)
-
Ukiambiwa makini, hadhari iwe kichwani
Ng'ombe bado yu mwituni, hujuwi kichaka gani
Kambaye iuwanjani, alama uhatarini
Ujuwe wazi huponi, akikutiya mbaroni
(miminae)
-
Mbinu zenu zimeshindwa, fahali kumchezeya
Sio yule wa kupandwa, sanamu lilo bandiya
Ni mwingi aliyefundwa, ghafula hukutokeya
Kikushika utapondwa, huna utapobakiya
(miminae)
-
Siyo kwamba ni hodari, mwenye nzito asili
Bali nina ujasiri, wa shida kuikabili
Kinachonitiya ari, na kule kutokubali
Ni kupewa tahadhari, ya dudu liso akili
(Said Suleiman)
-
Kwangu ng'ombe atadunda, kwani mimi ni mchunga
Pembe zake zitapinda, najiamini kwa chenga
Mwishowe nitampanda, hali huku ninaringa
Nitalifanyia inda, likome kutanga tanga
(Said Suleiman)
-
Hata angekuwa ndama, usingeweza mpanda
Seuze ng'ombe mzima, mwenye nguvu za kuwanda
Atakunyanyuwa wima, kikutupa uwe sanda
Bila hata ya huruma, na mengi atakutenda
(Maher Fundi)
-
Pokea wangu wasiya, uepukane idhara
Usikae kungojeya, dunia kukuburura
Mambo umejioneya, mebadili yake sura
Walopewa ruhaniya, tano na moya vitara
(Maher Fundi)
-
Gombe lifanyie shime, uchunga wake mpevu
Hilo na tuliandame, hadi litoke mapovu
Baadaye umpime, kama yeye ni mwerevu
Halafu umtazame, kumbe si mkakamavu
(S.Hashil)
-
Mimi nimeligundua, kwamba halina halani
Watu kimsujudia, ni hapo kale zamani
Leo wanalizomea, na kulita punguwani
Wallahi linaridhia, lajuwa li taabani
(Said Suleiman)
-
Macho yake kufumbua, ni nadra ubaini
Pembe zake tazivua, bila hata ubishani
Tambara kimtupia, yeye aona majani
Sasa leo wanambia, tabishana kwa ruhani?
(Said Suleiman)
-
Usemayo si utani, limebaki hamkani
Lajifanya kama nyani, lachupa kutwa mitini
Haaminiki yakini, buluu kwake kijani
Siruhani si shetani, ni joka kwenye majani
(S.Hashil)
-
Asemayo si muhimu, asijifiche chakani
Aangaliwe kwa zamu, asitoweke kizani
Sote tunamfahamu, kiumbe wa kizamani
Apenda kumwaga sumu, jengine yeye haoni
(S.Hashil)
-
Alaa kumbe hukomi, wajifanya mjuaji
Usijeleta magumi, na kutafuta majaji
Na majeshi kukuhami, usipate kufa maji
Ng'ombe aja hasimami, haraka kimbiya mji
(Assad Abdullah)
-
Simtetei akhui, uwazi mbele machoni
Anadhani hatujui, mwana khaini nchini
Kaona hatutambui,wake wizi lo'zaini
sasa nakimbiye ugwe, asije kuona ng'ombe
(miminae)
-
Huyo tushambaini, hana lake la makini
Twembeba mgongoni, akenda kutukhaini
Leo yuwatutamani, ela kambini hafani
Mungu keshambaini, sasa hayuko nyoyoni
(Abdulla Al Harthy)
-
Ya ng'ombe si fani yao, idhara waitafuta
Ugwe ishingoni pao, kama kisu yakeketa
Ng'ombe meirusha kwao, na sasa yawafuata
Akhuyi utaja toka, mtini si ngao shuka
(Salma Khamis)
-
Inawatafuta mwao, mule walimojificha
Wawe na nyundo na ngao, salama wakizificha
Kitoa shauri yao, bora mapema ku'm'cha
Akhuyi utaja toka, mtini si ngao shuka
(Salma Khamis)
-
Muwapi mlojikumba, kujiweka viamboni
Kuwa mnakuja komba, vilivyo vyetu vya ndani
Mkashindwa kuviwamba, mkabaki mabondeni
Ng'ombe akawa ni simba, ugwe akakufungeni
(Maher Fundi)
-
Kwa vipazo mkitamba, bila watu viwanjani
Matokeo tumesomba, ngome iko mikononi
Sisemi tunajigamba, ukweli umebaini
Ng'ombe alofungwa kamba, ndiye kakumalizeni
(Maher Fundi)
-
Mkamiya hanywi mayi, funda moja hachubui
Muache aliye ngoyi, Mshazume habagui
Jecha Shumba hakugwiyi, sambe arambaye tui
Hata ugwe agwegwenye, kuukata hatambui
Ahmed Rashid)
-
Kuukata hatambui, hata ugwe agwegwenye
Kaja na kituitui, hata wajane anyonye
Kumbe kipole hajui, yuko wima kinyekinye
Hadaa kafanye huko, Ole wamekubaini
(Ahmed Rashid)
-
Ole wamekubaini, hadaa fanyeni huko
Kimbiya ugwe fulani, kijiwe hiki si chako
Ndugu wakiwa vitani, enenda kondeni kwako
Halahala ncha hino, hoho tatoja matoni
(Ahmed Rashid)
-
Hoho tatoja matoni, halahala ncha hino
Umeshindwa umetani, wagaagaa kipono
Waropoka mitaani, kwa goli la kisigino
Haja matao ngomani, ugenini jalalani
(Ahmed Rashid)
-
Mtenda mwenye ujuzi, hababaishwi na tao
Ila awe mwanafunzi, wakujipachika cheo
Akipita pande hizi, sikiza chake kilio
Hawahi vuta pumzi, watu wajilia vyao
(Said Suleiman)
-
Sitishike asilani, kwa shani yake ya jana
Muangaze kwa makini, pakukupiku hakuna
Kesha tokeya zamani, sasa atumiya jina
Hako wakumuauni, Aanza kwanga mchana
(Said Suleiman)
-
Sikiza wangu azizi, ujuwe hii hakika
Shina meacha mizizi, na chini limeshang'oka
Gogo latoa vibanzi, majani yanakauka
Nzige mefanya kazi, mbuyu unaanguka
(Maher Fundi)
-
Safari ya kwenda mbali, mwanzowe hatua moja
Waufahamu ukweli, sifasiri sina haja
Tulipo hatuko mbali, yanjiani yanakuja
Tumepaniya kikweli, twaisubiri faraja
(Maher Fundi)
-
Sitouka abadani, kwa kelele za mlango
Nishaliona zamani, kama halina mpango
Unamuogopa nini, ng'ombe alo na mapengo?
Yake macho hayaoni, sikwambii hilo bongo
(Said suleiman)
-
Mapengo ni yake shani, hayo katu hatumii
Zilokuwepo kitwani, akhui huzizuii
Amepewa na Manani, hata humjuilii
Ndugu ngiya safarini, mbinde hazisaidii
(Walii Genderi)
-
Mlango haukuwepo, usifanye ukaidi
Ujuwe na Mungu yupo, akhuyi sinikejeli
Kimbiya urudi papo, utizame yalofeli
Bora wewe hukuwepo, ng'ombe alipo vinjari
(Walii Genderi)
-
Yaeleweka zamani, mpanda ngazi hushuka
Ila hili hayawani, naona laporomoka
Limechoka taabani, popote lajipweteka
Limeishiwa na fani, kazi linababaika
(Saidi Suleiman)
-
Kwake kwenda malishoni, nako pia ni mashaka
Mana macho hayaoni, nuru imeshamtoka
Anategemeya nini, upupu au ukoka?
Hao wakumuamini, kijasho kimewatoka
(Said Suleiman)
-
Ni mkubwa mtihani, yakupasa ubaini
Nakuona taabani, wajikaza kisabuni
Ya ng'ombe kubwaga zani,kutiya hofu mjini
Kimbiya sio utani, asikutiye machoni
(Assad Abdullah)
-
Yaliwashinda malenga, tena malenga wa kweli
Ikawa watangatanga, wahaha kila mahali
Wakiitafuta kinga, ya vishindo vya fahali
Ng'ombe kwake akitinga, nani wakumkabili
(Assad Abdullah)
-
Yalielezwa zamani, na wajuzi wa maana
Kwamba haiwezekani, kuichezeya amana
Si muhali asilani, ukipokonywa dhamana
Katu ng'ombe si haini, wala hafanyi hiyana
(Assad Abdullah)
-
Mshari ni kama nani, kugombanisha wendani
Wenziwe hawathamini, leo wamembaini
Tutamchukuwa pwani, tukamchovye majini
Tufanye yetu dhamiri, katu harudi nchini
(Abdulla Al Harthy)
-
Yasemwayo kumbe kweli, ng'ombe kang'olewa pembe
Kaziye fanya ajali, mkali kuliko wembe
Kadhoofu yake hali, na suraye ya uzembe
Kuona kwake si mbali, hajiwezi hata chembe
(S.Hashil)
-
Sikwamba ni ushabiki, ng'ombe kumjaza sifa
Mikubwa yake mikiki, kikupata ni maafa
Na nguvu zake lukuki, mwenye mbio kama zefa
Akhuyi nyuma sibaki, sipuuze utakufa
(Assad Abdallah)
-
Situone twakughasi, yote haya ni mahaba
Mana wewe kwetu sisi, unapendeka si haba
Wala baya usihisi, sisi nduguzo kwa baba
Kwa hiyo ukituasi, mateso utayabeba
(Assad Abdallah)
-
Woga umekuzidiya, Shuruti unatetema
Amini ninokwambiya, kweli alikuwa chuma
Zama zimempitiya, hawezi tena kuchoma
Madhali ana bidaya, na nihaya ni lazima
(Said Suleiman)
-
Walojifanya vidume, wangapi wameshaenda
Wakajifanya mitume, watakalo wakatenda
Akina Mkamandume, pia na Jabu Mponda
Basi na lilo likome, lishapata ndugu donda
(Said Suleiman)
-
Khuyi huu ni usiya, upate yako salama
Kama hutaki sikiya, ungali wajitutuma
Atakuja kuvamiya, ushindwe na la kusema
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Saleh Barkey)
-
Usijitiye umbeya, ujionee huruma
Khatari kuichezeya, huo si mchezo mwema
Vipi utajiteteya, dume likija kufuma
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Saleh Barkey)
-
Tafuta umtakaye, umchukuwe pembeni
Huyu niachiye miye, nikamfunge mtini
Usiwe na kazi naye, humuwezi ni wa nini?
Asishughulishe kamwe, ng'ombe huyu wa utani
(Abdulla Al Harthy)
-
Amtaka ulonaye, amtiye mikononi
Mikononi awe naye, amdhibiti ugweni
Ugweni chini akaye, amjuwe yeye nani
Nani yeye ajuaye, asiye penda undani
(S.Hashil)
-
Huyu sitampa mtu, Mtashindwa ishi naye
Ana wake utukutu, nao naujuwa miye
Alinikhasimu kwetu, kuwa sisemi na yeye
Ng'ombe huyu wa mzimu, ni wangu si wenu nyiye
(Abdulla Al Harthy)
-
Akhuyi sifanye manza, kuzidi kumkebehi
Ng'ombe alifungwa kwanza, ndio mbio ukawahi
Ugwe wake umetanza, nakuwapia Wallahi
Lau angekusabahi, ungeangukia Mwanza
(Walii Genderi)
-
Sauti mnazotoa, ng'ombe hamjamfika
Ya bure mnatongoa, au woga mewashika
Parakacha akitoa, mbona mnatawanyika?
Akhuyi huyo si nyoka, sifanye kumchokoa
(Walii Genderi)
-
Zama ulipoambiwa, kiona ugwe kimbiya
Akhuyi hukutakiwa, hoja kutuhubiriya
Shauri kila kipewa, waja na jawabu miya
Lipi utaja twambiya, ng'ombe akikuraruwa
(Walii Genderi)
-
Nyingi hamrere zako, bado hujaona ng'ombe
Majigambo ndiyo yako, huku waogopa pembe
Umewafata wenzako, kumpiga kwa vijembe
Ugwe maneno ni hako, je kiona mwepembe
(Walii Genderi)
-
Takupa kisa cha kweli, Pemba kilichotukiya
Cha yule aliyesali, karibu sana na njiya
Akatishwa kweli kweli, sala kamtengukiya
Basi nawe zingatia, tumia yako akili
(Dr.Hassan)
-
Kaambiwa anosali, hasemi anasikiya
Kipole ng'ombe mkali, keshakata atujiya
Endelea na kusali, ela miye nakimbiya
Khushui ikapotea, kwa bwana mwenye kusali
(Dr.Hassan)
-
Kimbia mwana kimbia, kimbia sirudi nyuma
Kimbia mbali kimbia, kimbia sione nyuma
Kimbia kule kimbia, kivumbi uwache nyuma
Nyuma huko ndio nyuma, siyatafute kimbia
(Walii Genderi)
-
Habari ulisikia, za bwana mwenye kusali
Yaache kuyarukia, ya ng'ombe yana kejeli
Wengi alowazukia, wamekufa chalichali
Huyo kweli ni mkali, dume lilopindukia
(Walii Genderi)
-
Watupie wenye ngeli, wanotamani mauti
Wamcheze kwelikweli, japo kafungwa na mti
Wakiiona batili, weshakuwa mahututi
Shujaa wa atiati, imedumbwa yake hali
(Walii Genderi)
-
Mja unayo khiyari, kwambwa ukaambilika
Au kudhani hodari, ukakumbwa na mashaka
Kushapewa indhari, geuza njia haraka
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Dr.Hassan)
-
Tamati natamatiza, sina tena niendako
Yangu usijeyabeza, nakuasa ndugu yako
Ugwe ukiuangaza, usijipeleke huko
Akhuyi kimbiya ugwe, singoje kuona ng'ombe
(Dr.Hassan)
|