|
|
Kiwera!
Date: Jan - Feb 19, 2003
Assalam aleykum
Wapenzi wa mashairi na wanaukumbi kwa jumla
Baada ya kukamilika shairi la Kiwera,leo ninafuraha
kukuleteeni shairi kamili la beti 81 pamoja na
utangulizi wa Professor Ibrahim Noor Shariff na majina
ya watungaji wote wa shairi hili.
UTANGULIZI
Watunzi waliotunza tungo za watungaji wetu wa kale
wameturithisha idadi nzuri ya tungo za zamani ambazo
zinatupa taswira ya maana inayotuwezesha kuona ujuzi
waliokuwa nao watungaji waliotutangulia. Kuna tungo za
mvyele wetu aitwaye Fumo Liyongo ambaye, inasemekana
aliishi zaidi ya miaka elfu iliyopita, na kuna tungo
za wengi walioishi baada yake. Kuna tungo zenye
maudhui mbalimbali - tungo za kidunia na za kidini, za
kufanyiana mizaha na za kutiana vishindo vya kivita;
kuna na za kusifu na za kuumbua; kwa ufupi, kuna tungo
za maudhui mbalimbali zilizotungwa na Waswahili.
Ninadhani kuwa hakuna watu wowote katika Afrika ya
Kati, ya Mashariki na ya Kusini ambao wana utajiri wa
aina hii katika fasihi yao.
Katika aina kwa aina za maudhui ya tungo zilizotungwa
kwa bahari mbalimbali; bahari zisizopungua kumi na
tatu - utenzi, wimbo, shairi, tumbuizo, wawe, kimai,
Dura Mandhuma, Inkishafi na kadhalika - hakuna aina
inayopendwa na Waswahili wengi kama tungo za
kujibizana. Tungo za kujibizana si za bahari maalumu
wala maudhui maalumu. Huweza kutungiwa kwa bahari ya
wimbo, shairi, utenzi na kadhalika. Pemba, kwa mfano,
kuna ngoma ya kibati (mdebe au cherewa) ambayo watu
huimbana papo kawa papo bila ya matatizo. Ule uhodari
wa kujibizana papo kwa papo na, aghlabu kwa maneno ya
kutaniana, watu wakafurahi na kucheka, kumewapa
wachezao ngoma hiyo sifa kubwa kwa wenye kupenda tungo
za aina hiyo. Halikadhalika, katika mji wa Amu (Lamu)
kwenye hafla za harusi upande wa wanawake, kulikuwa na
tumbi ya mama zetu waliokuwa wakiimbana usiku kucha
kwa nyimbo za kupigiwa mfano walizozitunga hapohapo
ngomani, ndipo wakale wetu wakaturithisha msemo
unenao: "wimbo hutoka ngomani."
Uswahilini kote kulikuwa na wazee wetu ambao walikuwa
wakitungiana mashairi na kujibizana papo kwa papo, au
kwa barua na katika miaka ya karibuni, katika magazeti
pia; na hii leo mila na utamaduni huo unaendelezwa
katika ZANZINET. Mola Karimu Rahimu awape kila la
kheri na baraka waliouanzisha mtandao huu ambao lengo
lake ni la kheri; lengo la kuwaunganisha Wazanzibari
popote pale walipo.
Katika zanzinet kuna wajuzi wa fakhari katika kutunga
na kujibizana kwa tungo zenye uzito wa thamani kubwa.
Nilitaka kutoa mifano ya uhodari wa kutunga
unaoonekana humu katika chombo hichi cha fakhari cha
zanzinet, lakini nikaona kuwa watungaji ni wengi na
tungo za fakhari ni nyingi na mwenye kusoma na kuelewa
hahitajii kutolewa mifano ya udohoudoho. Mwenyewe huwa
anasoma na kustaladha kila akutanapo na haluwa za lozi
za aina hizo ambazo huandaliwa kila mara.
Leo tunakuleteeni, kwa ukamilifu, mashairi ya
kujibizana yenye maudhui ya KIWERA ambayo yametungwa
na idadi ya wanazanzineti. Tunatumai utastaladha na
utamu uliomo katika tungo hizi.
Ili kuzidi kuonea raha yaliyozungumzwa, inataka uelewe
maana ya "kiwera" ; na si maana ya "kiwera " tu, bali
makusudio yaliyokusudiwa; kwani neno "kiwera" katika
mashairi haya haina maana ya humbo au neema ya wingi
wa dagaa au samaki. "Kiwera" ni "neema" ya aina
nyengine kabisa iliyowafikia watu wa nchi ya jirani.
Sasa nakuachilia msomaji unaposoma utose katika ubongo
wako makusudio yaliyokusudiwa ili ustafidi na kuyaonea
raha mashairi haya kama wanavyoingiwa na shauku wenye
kupenda mafumbo na fani ya kujibizana kwa tungo. Soma
ukishasha...
Ibrahim Noor
Kiwera!
-
Twaanza Bismillahi, utungo kuucharaza
Beti hizi ni nasahi, kwa kila mwenye kuwaza
Kuna jambo tuliwahi, si jambo la kupuuza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Mvuvi kashuka pwani, kwenye usiku wa kiza
Karabai mkononi, na nyavu kaning'iniza
Samaki wingi wa shani, wezuka kwa kushangaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Hakuweza kuamini, kadhani ni miujiza
Samaki wa mkondoni, bandarini kutokeza
Leo kumezidi nini, au apaazwa pweza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Katoa chombo nangani, akaanza kucheleza
Nyavu zake za thamani, kataka zitandiliza
Na mishipi kibindoni, ikibidi kurambaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Samaki walioshuka, walishitushwa na kiza
Ndipo walipoibuka, juu mwanga kufatiza
Chini walihangaika, kiza kiliwapoteza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Hata zilizotoboka, nyavuni waliingiya
Walolala meamka, mikondoni mekimbiya
Nyavu zikawa mkeka, kiziona walaliya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Mishipi ikawa kamba, wakiona wapandiya
Ndoana wakiziramba, bila chambo kuzitiya
Madema yakawa nyumba, vururu wakiingiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Shime yapatilizeni, wakati umewadiya
Juhudi tuongezeni, uzio na juya piya
Leo ni leo jamani, mavuvi kumaliziya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Yapatilizeni shime, kiwera kimechagiza
Inukeni mukachume, mukumbe mukijaliza
Muwe wavuvi vidume, damu musije ilaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Munamuona mwenzenu, wa heko kumpongeza
Kuibaini fununu, hakunena ngoja kwanza
Werevu na kila mbinu, mvuvi vyombo kajaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Kiwera kilichongiya, hakitadumu milele
Haitakuwa sawiya, jambo hilo mlijule
Kesho tukiamkiya, kiwera si kilekile
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Aweza vuma wa kusi, vyombo kuvitetemesha
Ikawa ni wasi wasi, roho zetu kuzirusha
Ikaingia nuhusi, wavuvi kuwazamisha
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Kake mnyonge wa Nyali, usemayo yaneleya
Kiwera hiki kikali, mtu asije teleya
Ingawa bado thakili, ya Kisumu kuja Mbeya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kimeingia chavuma, kiwera mbele na nyuma
Kaskazi kisimama, kusi si hasha kuzima
Ikawa kushika tama, leo mbona yamekoma?
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Wapo washatuambiya, mwaota mwajipumbaza
Kiwera mwashangiriya, wala hamutakiweza
Hachinjwi ng'ombe mkiya, mafumbo watufumbiza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Wasoona ya duniya, kwa kiyoo kuwacheza
Wakawa wang'ang'aniya, kiwera hiki kubeza
Wajuwe tushanuwiya, mambo yatawashangaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Mambo yatawashangaza, wajue tushanuwiya
Pamoja tutawekeza, jamii yote sawiya
Tushauona mwangaza, nyuma mwiko kurudiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Wenye tamaa kukata, kwa nini wajiumbuwa
Kiwera kilichokita, ni haki kukinyakuwa
Na wale wanaoteta, macho yao kufunguwa
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Hata uvume upepo, wa kaskazi na kusi
Ama kwa hapa tulipo, chombo chetu hatukisi
Kiwera chetu kipapo, nasi twaongeza kasi
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Watu walidhani ndoto, kiwera kilipozuka
Walidhania ni moto, wakaratasi mewaka
Kuripuka si kokoto, hata chuma meyayuka
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Na sasa hauzimiki, unawaka baharini
Vilo juu vyaghariki, Jivu halipatikani
Mkali haushikiki, unaelea majini
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Nauona waripuka, bahari yote yawaka
Wavuvi mechangamka, wanavua wakitweka
Maji chini yachemka, samaki wahangaika
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mhhhhh-Miminae)
- Shime jamani shimeni, kiwera ki-uwanjani
Shime tujikusanyeni, tuingieni chomboni
Samaki tuwavueni, tufaidike jamani
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(mhhhhh-miminae)
-
Kwa kiwera kilomaki, hakitaki makelele
Na aliyemo hatoki, asiye takaa kule
Mwenye macho hapingiki, chomboni tajaa tele
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Kama tumeshatongowa, ya muhimu kwa kiwera
Ni kipi kukizongowa, cha mazonge udodora?
Wasije kuzikongowa, nyavu mashua za mbura
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Wavuvi wafanye nini, nawauliza wahenga
Na wavyele watendeni, nawadadisi wakunga
Samaki wako jikoni, na shume limetuzonga
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Wana wa kwetu imani, tuime tushikaneni
Ya kiwera si mageni, yashatokea nyumbani
Tushike sisi mpini, makali kwao usoni
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Yashatokea nyumbani, ya kiwera si mageni
Ndio hasema watani, mavuvi yamalizeni
Watumbatu na Kusini, Jadida na Mtemani
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Kwani twasubiri nini, na kiwera kingalipo
Vyombo tweunda zamani, vyetu sio vya mkopo
Tuvishushe baharini, tuvitegeshe upepo
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Ikiwa ni manahodha, wamejaa washupavu
Tena wasio bughudha, wenye macho maangavu
Wasafi hawana adha, sifa yao ni werevu
Kumeingiya kiwera, Shime yapatilizeni
(Mabrouk Mnyonge wa Nyali)
-
Yaliyopita si ndwele, sasa tugange yajayo
Wembe uwe ule ule, tusivunjikeni moyo
Kiwera kilicho mbele, kisivuuke machweyo
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Wavyele tuwasomeshe, wasijefanya zohali
Wavuvi tuhamasishe, wa karibu na wa mbali
Tusilale na tukeshe, kiwera tukikabili
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Si moja linofumbika, hapalaliki nangani
Mawimbi yateremka, mbao zinadata chini
Mashariki zafyatuka, nasi tumumo chomboni
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Nahodha tuchangamke, tueleke bandarini
Hapa tusiteremke, tutazama mkondoni
Uwache utupeleke, hadi tufike gatini
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Maher-Unique)
-
Kwa mwenye kutabaruku, matumaini haachi
Mola ataturuzuku, tushinde kiwera hichi
Takapokucha usiku, furaha mejaa nchi
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
- Jahazi meshika kasi, na tanga lapeperuka
Chombo hata hakikisi, mpingo waserembuka
Kuvua jama rahisi, kazi kupata nafaka
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kiwera meshika kasi, wavuvi wa Mgongele
Wavuvi wavua ngisi, pweza,changu kwa makole
Wavuvi sisi kwa sisi, ni wa Chaani na Kwale
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kumeingia kiwera, yapatilizeni shime
Tuiondoe sitara, tuyasafishe mahame
Tusije kutekwa nyara, samaki wasituhame
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kazi kupata nafaka, samaki tushawavuwa
Eshiriki dada,kaka, chombo hawakuchaguwa
Efanya nini Mahoka, jamii inatambuwa
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kwa hapa tulipofika, ndio tumesharidhiya?
Majahazi kuyatweka, kiwera kuyajaziya
Kwa miye sijatosheka, bado hayajaningiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Kiwera kimaridadi, kwa nguvu chashadidiya
Chataka tujitahidi, mavuvi kumaliziya
Na aliye mkaidi, si hasha haoni njiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Yataka tujitahidi, mavuvi kumaliziya
Tuvue kwa ustadi, isiwe kwa kutupiya
Nnawapeni ahadi, nanga mwishowe tatiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Patu na mabaragumu, zipigwe kwa kuchagiza
Huko Mrima zihimu, zipukutike ajiza
Wauke wenye naumu, kwa mavuvi kutangaza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Wajuwe utamu wake, wajute kujilemaza
Kila mtu zana yake, mavuvi kufululiza
Katu tusiweweseke, kazi tutaitimiza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Tumekutupa makwetu, tumewaacha wageni
Kiwera sasa mtutu, tujenge wetu watani
Tusirudi nyuma katu, tuelekee fukweni
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(mhhhhh-miminae)
-
Tusiruhusu wageni, kuingia kiwerani
Wageni wana kunguni, walojaa tendeguni
Siwaoni na huweni, kunyonya damu mwilini
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Wengi walichangamka, kiwera kilipongiya
Haba walojipweteka, kuendekeza uviya
Mavuvi kimalizika, sote tutafurahiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Vyombo tukishavijaza, bandarini kuingiya
Hata wachokoa pweza, nao watashangiriya
Neema tasheheneza, ipate yote jamiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Nyota njema ikitoka, mweye macho aiona
Na yule asiyetaka, la kumfanya hakuna
Kiwera kikamilika, naapa tutagawana
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Pamoja tutagawana, kiwerani tulongiya
Siyo kwa kubaguwana, ni nyeupe zetu niya
Qasama bila sonona, tupate sote sawiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Na tukivue kwa ari, nguvu moja insiya
Hakuna la kusubiri, wakati watukimbiya
Huu wetu utajiri, tusiache ukaviya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Walo juu ufukweni, kiwera kiangaliya
Tukawahamasisheni, kwa makundi kuingiya
Tusiwawache jamani, tuwaonyesheni njiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Angenda juu kipungu, hafikilii mbinguni
Ama kwa Mwenyezi Mungu, kubwa hakuna yakini
Tutapata letu fungu, Inshallah kwa karibuni
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Wale wanaotucheka, huku wakishangiriya
Iko siku itafika, akili zitawangiya
Kiwera tukikiweka, ndani ya zetu siniya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Wacheka nnawaomba, jambo moja kulijuwa
Kwa wetu Mola Muumba, hakuna lisilokuwa
Takwenda nao sambamba, kwenye jua au mvuwa
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
-
Nimepata mnong'ono, nataka wasimuliya
Ya wale samaki mbono, tunaowakimbiliya
Ati akina Machano, wapanga kutuibiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Wapanga kuzorotesha, kukifisidi kiwera
Wameanza tisha tisha, kule upande wa bara
Lazima kuwakomesha, wasitutie hasara
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Kassim)
-
Samaki wengi wa shani, umma umejivuliya
Kutoka mwambao pwani, maziwani nako piya
Wenzangu tahadharini, wakioza tutaliya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ibrahim Noor)
-
Kazi pevu i-jikoni, kwa jifya wanapikiya
Jiwe moja hulioni, mawili yamesaliya
Imani hima jamani, tuondoshe mabakiya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ibrahim Noor)
-
Matoke hayapikiki, sima watuvurugiya
Na mwiko hauzunguki, ziko kombo sufuriya
Nazo kuni haziwaki, mbichi tukiangaliya
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ibrahim Noor)
-
Tengeni yalobakiya, tutumie seridani
Na wapishi nao piya, hali zao taabani
Umuri walofikiya, ni mkorogo mekoni
Kumeingiya kiwera, Shime yapatilizeni
(Ibrahim Noor)
-
Korojo sufuriyani, mapishi yasiyolika
Twaumiya matumboni, nyongo tunazitapika
Takaudi tuwapeni, wapishi kupumzika
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ibrahim Noor)
-
Samaki wako jikoni, meko mawili mabovu
Wachuuzi wa makini, wapishi wengi wachovu
Sukuma wiki mezani, ugali u nyovunyovu
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Ugali u nyovunyovu, matoke ya hatarini
Tutaondoa maovu, ja fahali Kisauni
Nyangumi wabaki fuvu, wakapotee jaani
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Vyungu wameviunguza, hakuliki asilani
Si moto kuteketeza, kwa moshi ulio ndani
Harufu mehanikiza, havipiti mdomoni
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(mhhhhh-miminae)
-
Laiti kuwa vyalika, tungepakuwa tukala
Kwa njaa zilotushika, tusingechagua kula
Rojo limeharibika, hatuliwezi kulila
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(mhhhhh-miminae)
-
Roho zinafurahika, kizuri tunapokila
Kupikwa kiloongoka, mapishi ya mwenye mila
Na mafya yanapowekwa, kuenjekwa bila ila
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(mhhhhh-miminae)
-
Chungu chetu cha udongo, udongo wa mfinyanzi
Chungu chetu si cha chongo, chongo mng'ong'wa na nzi
Chungu chetu cha mzingo, mzingo ulo na enzi
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Yapatilizeni shime, wazee yatatupona
Vijana mshike sime, chatu lisije waona
Samaki jike na dume, chunguni kurundikana
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Ewe baba ewe mama, umoja mshikamano
Mabarobaro simama, kukilinda chungu hino
Kesho kesho wanosema, katu si mfungamano
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Ahmed Rashid)
-
Kiwera kilichozuka, ni kiwera cha wavuvi
Tena walio Msuka, sio hawa wa Michamvi
Watu wanalalamika, bado wanakula duvi
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Hassan)
-
Mate Yanawadondoka, wanangoja wachuuzi
Ajabu hawajafika, kunako shehia hizi
Kitoweo wakitaka, washazichoka mbaazi
Kumeingiya kiwera, shime kipatilizeni
(Hassan)
-
Wachuuzi wa Vinyenga, ninawapa indhari
Bei wasijeipanga, kama ile ya jodari
Yawaje vivyo la panga, kuuzwa kama johari
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Hassan)
-
Basi panapo kiwera, wasizuke matapeli
Navioze wenye ghera, ya kuuza bei ghali
Yafaa tuwe imara, tuwadhibiti kikweli
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Hassan)
-
Kiwera tuwe imara, tukishike kweli kweli
Isitupate hasara, bahati si mara mbili
Inshaallah iwe tijara, Mola twaomba kubuli
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Hassan)
-
Na sasa ndiyo tamati, mengi tushayaeleza
Twamaliza hizi beti, kiwera kukitangaza
Kwa ari tujizatiti, hima tusije teleza
Kumeingiya kiwera, shime yapatilizeni
(Saleh Barkey)
-
Ndugu zangu na wendani, tamati tumeifika
Tumuombe Rahmani, Mola aso mshirika
Tumswaliye Amini, Mtume asiye shaka
InshaAllah muwafaka, iwe kun fayakuni
(Ibrahim Noor)
-
Humbo jingi limefura, karibu nasi si mbali
Na kwetu hiki kiwera, Rabbi twaomba kabuli
Mola tupe 'stimrara, neema zako Jalali
Mpunguti ya Adili, kheri yawe midrara
(Ibrahim Noor)
-
Mtukufu mwenye sifa, wa haki Mola Manani
Twondolee makhawifa, i-Kwako enzi na shani
Utupe kila la sifa, nyoyo ziwe furahani
Kafu isiunge nuni, ndiwe Adhimu Razaqi
(Ibrahim Noor)
-
Rabbi Mola taturidhi, atupe kila la jaha
Ajaaliye hifadhi, na iqibali swahiha
Haja zetu azikidhi, zizidi kwetu furaha
Twakuombawe Ilaha, Jalla waAlaa Jalilu
(Ibrahim Noor)
-
Mola wetu tukirimu, utujazi kila mema
Tuyatakayo yatimu, izidi kwetu neema
Inshalla Mola Rahimu, tatuhifadhi daima
Ya Rabbi tupe salama, Duniyani na Akhera
(Ibrahim Noor)
Watunzi
Yafuatayo ni majina ya watunzi wa shairi la Kiwera kwa
ukamilifu:
1)Sk.Saleh Muhammed Barkey (Saleh Barkey)
2)Prof.Ibrahim Noor Shariff (Ibrahim Noor)
3)Dr.Kassim Omar Ali (Kassim)
4)Dr.Mbarouk Hamad Shariff (Mbarouk Mnyonge wa Nyali)
5)Dr.Hassan Omar Ali (Hassan)
6)Maher Moh'd Ahmed (Maher-Unique)
7)Sk.Ahmed Rashed Ahmed (Ahmed Rashid)
8)Bi.M.A.Masoud (mhhhhh-miminae)
|