.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

ASO CHAKE !

 

 

 

 

 

 

Related links

ASO CHAKE!

Date: 18 May, 2006

  1. Aso chake hana lake , wala hatambulikani
    Na hata kwa walo wake , yeye hawi na thamani
    Neno ni la mwenye chake , aso chake hunenani?

  2. Aso chake ni muinga , angawa mno mwerevu
    Angawa fundi kupanga , hambiwa ni mpumbavu
    Kwenye mambo humtenga , angaliya nazi mbovu

  3. Aso chake si mzuri , angawaa kama mwezi
    Aso chake si hodari , angawa mno muyuzi
    Aso chake ni jauri , angawa ni mtukuzi

  4. Aso chake ni fidhuli , na sawa yake ni jongo
    Anganena yalo kweli , huwambiwa ni mrongo
    Angawa huona mbali , huonekana ni tongo
  5. Aso chake ni mchafu , naangawa maridadi
    Na aso chake ni dufu , angawa shekhe Biladi
    Hapati umaarufu , angawa mwenyeji jadi

  6. Aso chake rai hana , angawa ni SAQARATI
    Aso chake akinena , wa kusikiza hapati
    Walo wake humkana , hata muda wa mauti

  7. Mwenye chake ndie bwana , mwerevu mwenye busara
    Angawa hana maana , hupewa yeye bendera
    Husoza nasi huwona , hini ni kuu hasara

  8. Na hini ndiyo sababu , ya mambo kuharibika
    Zimetuzidi taabu , na kwetu kumefujika
    Na tamaa ya karibu , hapana kutengezeka

  9. Ni sharuti tubadili , na fikira tugeuze
    Wakisimama wawili , mwenye chake sishunduze
    Tumpe mwenye akili , ili chombo achoweze

Limetunga na Ustadh Mahmoud Ahmed Abdul Kadir (MAU) kutoka Lamu - Kenya.

Limeletwa na Sheikh Saleh Barkey

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet