|
|
GARI!
Date: 16 May, 2008
- Kwa jina lake Muumba, Mwenyezi Mungu mmoja,
Ambaye ameviumba, mwili na roho pamoja,
Leo tungo naipamba, inahusu gari moja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Kuna gari la mtumba, limezidisha vioja,
Laendeshwa kwa kuyumba, kweli mwisho wake waja,
Mijini na kule shamba, kwepeni gari likija,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Gari hili linatamba, mbio mbio linakuja,
Ubavuni lina namba, mwishoni nitaitaja,
Kwa rangi wamelipamba, ziko mbili kwa pamoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Gari moto linapamba, latafuta wateja,
Kila kituo latamba, abiria kuwangoja,
Heri likabebe pamba, tumechoshwa na viroja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Dereva katoka shamba, gari kaja kulifuja,
Konda wake ombaomba, anatafuta natija,
Wapiga debe ni pumba, wapo fedha kuzingoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Wakianza kujigamba, kila jema hulitaja,
Nyimbo nyingi wataimba, ili wakidhiwe haja,
Nendeni nao sambamba, hadi waishiwe hoja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Gari hilo la kishamba, roho za watu lafuja,
Kama sumu ni ya mamba, yaua kila mmoja,
Heri nguo ya mtumba, yaweza pata mteja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Anzeni shimo kuchimba, mlitupe kwa pamoja,
Mlikokote kwa kamba, mlizike mara moja,
Gari lisishike namba, ili tupate faraja,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
- Wananchi kila nyumba, kwepeni gari likija,
Msije kuwa manamba, mkajuta siku moja,
Wenzenu wanajigamba, waliita NAMBA MOJA,
Abiria jihadhari, na usafiri mbovu.
Mohammed Amir,
Morogoro
|