|
|
JAHAZI!
Date: 18 May, 2006
- Liembete na mongoti, tanga kwa lingi shauri
Hautukuti ukuti, imetuwama bahari
Hata mai hayavuti, tutapatae bandari?
- Ngurudi imeshopoka, mai ngamani hujiri
Haitaki kuzibika, na hata kwa misumari
Kuyafua tumechoka , mikono hutuhairi
- Tumekosa taratibu , hatuna tena shauri
Na bandari si karibu , hakupiti manuwari
Zimetutanda dharubu , metuzunguka khatari
- Hatuisi la kutenda , tumeshindwa kufikiri
Kiza kingi kimetanda , kote kimepija dori
Ni heri mwamba kupanda , kama hunu utiriri
- Hatuna ila Manani , wa kumuomba Jabari
Atwegeshe nasi pwani , yapokuwa kwa kihori
Tuokowe Rahamani , waja wako tusitiri
- Suwali si la jahazi , hili katika shairi
Litambuweni wayuzi , mafundi mulo hodari
Wa mtoni wende mbizi , muzizamiayo duri
Limetunga tarehe 21-3-2002 na Ustadh Mahmoud Ahmed Abdul Kadir (MAU) kutoka Lamu - Kenya.
Limeletwa na Sheikh Saleh Barkey
|