KARAFUU MBOVU
Huu ni utenzi kutoka kwa mzee wetu Sh. Khamis bin Nassor Al-Nabhany
(Mola Amrahemu) wa Piki , Wete Pemba. Jina la utenzi ni KARAFUU MBOVU ambao ameutunga
tarehe 28 Jamadul Akhir, 1381H (1961). Huu ni utenzi juu ya mambo ambayo
yametokea na hata watu waliotajwa ni hakika wameishi na wengine wako hai
na baadhi yao wengi humu munaweza kuwajua. Utenzi huu ni beti 325.
- Bisimillahi ni jina - Lake Mola Subhana,
Ya Rabbilaalamina - Jalla wa alla taaa
- Ilahi Mola Wadudi - Yupweke Rabbi Wahidi
Na mtume Muhammadi - Sayyidil anbiyaa
- Kwanza nastaghfiru - Kwa Mola wangu Ghafuru
Naomba utunusuru - Na maovu ya duniya
- Dibaji naifupiza - Siwezi kuendeleza
Nakhofu kuja teleza - Makosani haingiya
- Wala sitasema sana - Sifa za Mola Rabbana
Kila mtu aziona - Jinsi zilivyoeneya
- Sasa hadithi naanza - Kiasi kuzungumza
Na kidogo kueleza - Yaliyotupitikiya
- Naanza utenzi huu - Wa kisa cha karafuu
Mazao yetu makuu - Yalivyotuozekeya
- Ingawa siyamalizi - Lakini siyanyamazi
Kuvumiliya siwezi - Haddi yananikuliya
- Ni bora kuyaandika - Bukuni nikayaweka
Yasijesahaulika - Yawe yakikumbukiwa
- Hivi kaeni tayari - Niwaeleze khabari
Na mengi yaliyojiri - Yote tawahadithiya
- Tuanzie Mkoani - Mtambile na Kangani
Kengeja na Matuleni - Tumalizie Ditiya
- Mote humo walichuma - Kwa sherehe na salama
Hata siku za kuhama - Mengi wakaazimiya
- Wakaazimu moyoni- Wasirejee nyumbani
Waendelee usoni - Kutafuta manufaa
- Kwao wasitake rudi - Wakenda walikokodi
Hayo ndiyo makusudi - Waliyoyakusudiya
- Kwalizaliwa hakika - Makarafuu ya mwaka
Kila utakapofika - Matunda yanin'giniya
- Nyoyo zikawatukuta - Kuuza walichopata
Mashamba wakatafuta - Bei kubwa wakatiya
- Ikawa ni jitihadi - Shamba kubwa kuzikodi
Kutwa husikiya hodi - Watu wakuhodishiya
- Kila atakaye kodi - Hufika kwa Masuudi
Akaeleza muradi - Na alilokusudiya
- Na Masuudi husema - Ni bora kwenda tazama
Mali muiyone vyema - Isije kuwahadaa
- Wahitaji hutamka - Shamba tunazunguuka
Nasi tunafurahika - Ghilla tutainunuwa
- Shamba zote tumekwenda - Na mali tunaipenda
Ela pa kujenga banda - Bado hatujapajuwa
- Masuudi huwajibu - Maneno yenu taibu
Tutafanya taratibu - Mupate pa kutumiya
- Baada kuridhiyana - Mali wakakodishana
Kila mtu humuona - Furaha zinamngiya
- Chake Chake na Msuka - Ni hayo yalitendeka
Nami hapa nayaweka - Mengine tawatajiya
- Mengine nitayotaja - Ni jamaa wa Unguja
Nao Pemba walikuja - Sababu walizoweya
- Pemba walipowasili - Wakenda kila pahali
Wakasadiki ni kweli - Karafuu zimezaa
- Tukashikana sambamba - Waunguja na Wapemba
Kuoneshana mashamba - Kupita tukikaguwa
- Mambo yakawa ni hayo - Kila shamaba upitayo
Uambiwe utakayo - Kattu huwezi chaguwa
- Hapo tukakodi mali - Rakhisi wala si ghali
Lakini jambo thakili - Ni kule kudhaminiwa
- Iwapo mapesa huna - Sharti ulete dhamana
Mengi hayana maana - Ni bure hutasikiwa
- Mashamba yakakodiwa - Wenye fedha wakatowa
Wengine hawakupewa - Fedha hazikutimiya
- Ikawa banda kujenga - Karafuu zikechanga
Lakini siku zasonga - Mali wazipapatuwa
- Mara zikawa tayari - Tena zeiva vizuri
Hapo ikawa safari - Makambini kuhamiya
- Tukahajiri watani - Kuhamiya misituni
Mtu kwake humuoni - Usije mkusudiya
- Tukaanza kuzichuma - Na jua linasimama
Mara mande akavuma - Ule upepo wa mvuwa
- Mande alipovunjika - Shuwari ikaanguka
Wingu likamiminika - Kubwa halina mithaa
- Mvua ikanya mchana - Kubwa mfano haina
Kila mtu akaona - Leo tutaangamiya
- Yakawa mambo marefu - Sote tukangiya khofu
Tukaomba takhafifu - Mvua inatuzuidiya
- Hakika yasikitisha - Na mengine yachekesha
Kuyasema sitayesha - Tawakatiyakatiya
- Mambo hayo ni thakili - Wala hayana mithali
Mazito kama jabali - Vigumu kuyachukuwa
- Hadithi ya karafuu - Mazao yetu ya juu
Yanatuvunja miguu - Twafa tunanyon'gonyeya
- Tunangiwa na huzuni - Tajiri na masikini
Hatujuu hatuchini - Kama kozi twaungiya
- Sote twapiga siyaha - Hapana mwenye furaha
Nyoyo zina majaraha - Kwa huzuni kutungiya
- Huzuni ikarefuka - Kwa mali kuharibika
Nyengine zapukutika - Kwa kuzidiwa na mvuwa
- Mvuwa ikatudamiza - Karafuu zikaoza
Hata zikangiya funza - Ikawa kuzifukiya
- Kila utakapopita - Utaviona vikuta
Zishageuka mpeta - Hizo zilizobakiya
- Basi hapo matajiri - Ziliwaruka nadhari
Na wanyonge mafakiri - Wakazidi teketeya
- Mvuwa ya mwezi mzima - Wengi yetutiya homa
Ukatupata mughuma - Akili zikapoteya
- Mambo ni siku ya wiki - Mabovu hayakaliki
Mapesa hayapatiki - Ya kulipwa vibaruwa
- Huona juwa latoka - Upesi tukaanika
Mara mvuwa huanguka - Mbiyo tukenda anuwa
- Shani huko madukani - Ndiko kwenye mtihani
Muhindi haonekani - Hayupo kashakimbiya
- Walokodi taslimu - Hao hawana fahamu
Zinazidi darahimu - Pesa walizozitowa
- Walochuma mali zao - Wanakithiri kilio
Bakhti kupata nguo - Na pesa ya kushonea
- Shekhe Salim Subeti - Ni tajiri madhubuti
Alivichawanya vyeti - Watu wakavichukuwa
- Wengi aliwadhamini - Akitowa pesa ndani
Alfu na alfeni - Mbali wa tisaa miya
- Wengine elfu sita - Watakao wakipata
Hulifunguwa bueta - Watu kuwahisabiya
- Bin Subeti tajiri - Tena ni mtu dusuri
Kwa Pemba ni mashuhuri - Kila mtu amjuwa
- Alizichawanya fedha - Kudhamini na karadha
Na wala si kwa ghamidha - Alivyo akizitowa
- Akitowa nyingi mali - Kuwapa walokubali
Kwa kiasi na dalili - Laki tano zatimiya
- Kwake ilikuwa soko - Kula saa watu wako
Hapati kipumziko - Huyu toka huyu ngiya
- Bin Subeti kwa sasa - Mali yake kaikosa
Kwa mvuwa kutupangusa - Hapana lilobakiya
- Mvuwa inatufilisi - Inatutiya nuhusi
Unyonge bila kiyasi - Uliyotuelekeya
- Inaeneya khasara - Rabbi atupe nusura
Isitufike idhara - Kuja tukafilisiwa
- Unatupata msiba - Alae hapati shiba
Si mwana wala si baba - Msiba umeeneya
- Unaanza Mkoani - Wete hadi Mgogoni
Basi Matangatuwani - Msiba wajipepeya
- Ama Shekhe Mselemu - Alizichuma kwa hamu
Kwa siku sita timamu - Chungu zikamjaliya
- Majamvi akaongeza - Uwanja akaujaza
Karafuu zikaoza - Moja hakuianuwa
- Hayo ni ya Mgogoni - Ilipoanza huzuni
Basi Matangatuwani - Na huko yalitokeya
- L-azizi L-Kiyumi- Yeye ekuwa hasemi
Kwa huzuni na mughumi - Akavunja kutembeya
- Temb eya ufike Konde - Huko ndiko kwenye ponde
Ni kama tope za bonde - Ndivyo zinavyonukiya
- Kwa Rashidi bin Ali - Iliharibika mali
Ikawa kucha halali - Kwa mawazo ya duniya
- L-Khaifi maarufu - Tena mtu wa sharafu
Mvuwa ilimtilifu - Konde akaichukiya
- Hakika shekhe Rashidi - Mvuwa ilimfisidi
Zake na alizokodi - Zote zikampoteya
- Msuka kwa mahabubu - Azizi bin Harubu
Ilimfika adhabu - Kuhama na kuhamiya
- Alikuwa maghmumu - Hakai kichakapumu
Ilimtoka fahamu - Akili ikapoteya
- Akili ikamtoka - Kwa mali kuharibika
Akawa asikitika - Asema kinjiyanjiya
- Basi Msuka na Shumba - Humo watu wetirimba
Ni mitaa ya ndaamba - Karafuu zeeneya
- Mvuwa yenyesha Makuwe - Ikawa kubwa Kinoe
Watu wasijitambuwe - Bule na Maziwanjiya
- Bungala na Kwalegongo - Mvuwa yetiya kinyongo
Ikaharibu mipango - Maksudi hayakuwa
- Tufike na Mgogoni - Ilikuwa tafrani
Basi huyo CHEYAMENI - Alizidi kughumiwa
- Hamadi bin Abdalla - Mchana hataki kula
Usiku hataki lala - Kwa huzuni kumngiya
- Alizichuma kwa inda - Zikajaa tele banda
Mkutanoni akenda - Hawezi kukhutubiya
- Bwana mkubwa Sihaka - Yalimpata mashaka
Kutwa akitaabika - Kuweka na kuondowa
- Akasema ndugu zangu - Naliya na mali yangu
Na harusi ya mwanangu - Naona haitakuwa
- Kifundi hadi Kipange - Mvuwa yetiya unyonge
Wajengao wasijenge - Jengo halikutimiya
- Basi kiumbe mzito - Kulikosekana pato
Zilianikwa kwa moto - Na zote zikaunguwa
- Kwa upande wa Msuka - Ilikuwa pata shika
Mvuwa ikimiminika - Nahari na lailiya
- Wete tusiisahau - Zilioza karafuu
Zikapakiwa kwa dau - Baharini zikatiwa
- Shekhe Sultani Isa - Naye mvuwa yemtesa
Ikamwishiya siasa - Asijuwe pa kendeya
- Maneno aliyosema - Sitaki tena kuchuma
Unanipata mughuma - Fikira zinanishiya
- Basi kwa Abu Muniri - Mvuwa ilimuathiri
Akamwita Hamiyari - Mwanawe akamwambiya
- Hima ingiya njiyani - Ukakodishe Kiwani
Na shamba ka Makauni - Nalo piya walitiya
- Shamba hizo zikodishe - Moja usiibakishe
Na nazi uziangushe - Tunachoka kununuwa
- Hamiyari katamka - Baba siwezi ondoka
Mvuwa ikimiminika - Hapana wa kuondowa
- Mambo yekuwa Limbani - Kwa Jidde na Sefu Chani
Pauro limkononi - Karafuu zafukiwa
- Jidde alichimba shimo - Ikawa zatiwa humo
Na za Sefu humo humo - Na za bi Asha pamoya
- Na katika wanawake - Bi Asha tumkumbuke
Ni kubwa taabu yake - Iliyomtokezeya
- Bibi Asha Muhamedi - Tabu kwake ilizidi
Kwenda huku akirudi - Kutwa kiguu na njiya
- Kutulizana hapati - Wala kitako haketi
Hata juu ya mabati - Yeye akianikiya
- Akizichuma bondeni - Akaja nazo nyumbani
Na zilizo uwanjani - Nazo zajiri poteya
- Bibi Asha akisema - Shamba langu la Kingoma
Linanitiya mughuma - Nikenda natekteya
- Mwisho esema Bi Asha - Kheri ningalikodisha
Kama kujihangaisha - Na wahka kujitiya
- Chasasa kwa Kibeberu - Naye mvuwa yemdhuru
Akasema nashukuru - Liwe litakalokuwa
- Kibeberu katamka - Mali inaharibika
Azma inanitoka - Niliyoikusudiya
- Nalikuwa na dhamiri - Ya kwenda nunuwa gari
Lakini nnaghairi - Fedha haikutimiya
- Akamwambiya nduguye - Kuchuma na tuzuwiye
Vibaruwa tuwambiye - Kuchuma tunazuwiya
- Tuwambiye wende zao - Kila mtu ende kwao
Na hayo mapesa yao - Tumo twawatafutiya
- Mara tukishazipata - Kwa baruwa tutaweta
Sisi hatuna matata - Wala hatuna hadaa
- Na Uondwe hadi Nyali - Mvuwa yekuwa thakili
Ikaharibika mali - Kele na Mpakanjiya
- Chekeya hadi Jambaji - Yalimiminika maji
Khasara kwa wachumaji - Nao ikawashukiya
- Daya ilimiminika - Mvuwa kubwa kwa hakika
Kila aliyeanika - Naapa hakuanuwa
- Kwenyesha mvuwa ya sifa - Isiyo na takhfifa
Khalfani na Khalifa - Mughma ukawangiya
- Khalfani katamka - Kuchuma tapumzika
Niendelee na duka - Hwenda nikafanikiwa
- Khalifa alizirai - Asiwezee kutalii
Kutwa ashinda na njii - Chakula alisusiya
- Mkanjuni kulikondo - Kwa ndugu Hamadi Nondo
Yeye alifanya bindo - Azowa akifukiya
- Hamadi Nondo esema - Kukodi nimeshakoma
Ikiwa nataka chuma - Bora kwenda kibaruwa
- Mvuwa ya Makongeni - Ilihamisha wageni
Na waliyo Tondooni - Nyuso ziliwachukiya
- Mvuwa haina kiasi - Tondooni ilighasi
Shekhe Nasoro Khamisi - Ndevu asiweze nyowa
- Niwahadithiye Piki - Ilivyokuwa hilaki
Mtu yundani hatoki - Kazi ni kuchunguliya
- Basi huyo shekhe wetu - Yeye hakisema kitu
Ela Rabi Mola wetu - Tunusuru na Baliya
- Muhamedi bu Khamisi - Hakuwa na wasiwasi
Lolote halimghasi - Hulimezeya kifuwa
- Akisali na kusoma - Na kuomba duwa njema
Rabbi utupe salama - Ya akhera na duniya
- Hushinda msikitini - Kusali na kuadhini
Na kumuomba Manani - Jalla wa Alla Taaa
- Tufike kwa Khalfani - Kutwa kucha humuoni
Hatulizani dukani - Kero linamzidiya
- Khalfani bu Rashidi - Shamba nyingi alikodi
Ikamwisha jitihadi - Zote zikamuozeya
- Vikuta vikajazana - Vyote vikaozeyana
Apitaye akiona - Hahitaji kuambiwa
- Kadhalika na babaye - Ilimtoka suraye
Japo echuma maliye - Huwezi muangaliya
- Huwezi kumtazama - Akaapo huinama
Hanyamazi alalama - Kilemba keshakivuwa
- Hebu twende Kilimani - Karibu na darajani
Karafuu zibondeni - Zote zinakokolewa
- Kambi ya shekhe Saidi - Mtu jusuri wa kodi
Tena dalali anadi - Kina akikaribiya
- Lakini tunavyoona - Milele hakodi tena
Kwa khasara kubwa sana - Iliyomfikiliya
- Kiliyo cha shekhe Isa - Aliyerudi Mambasa
Hali yake hivi sasa - Si mzima asinziya
- Kanakonda kama uzi - Kula chakula hawezi
Wala hana usingizi - Kucha ni kujinamiya
- Nami mtunga utenzi - Yalinipata majonzi
Sikuwa na usingizi - Na wala sikusinziya
- Zangu nilizoanika - Nyengine zilikauka
Dukani hazipeleka - Basi zilikataliwa
- Khasara ikanisonga - Kutwa kucha nikitanga
Haja tembezewa kanga - Hashindwa kuzinunuwa
- Nyumba yangu ni nyeupe - Hataraji nizikope
Muuzaji asinipe - Na tena akachukiwa
- Kanijibu kwa ukali - Kukopesha sikubali
Neno hilo ni muhali - Sitaki kulisikia
- Jambo la kukopeshana - Linaondoka hapana
Kama taslimu huna - Kanga zangu nachukuwa
- Kwa khabari ya kukopa - Khamisi siwezi kupa
Najuwa hutanilipa - Ndiyo hakukataliya
- Miye nauza kwa haja - Sitaki ambiwa ngoja
Kubaki shilingi moja - Siwezi kukuachiya
- Hamwambiya tafadhali - Niachiya kanga mbili
Kijana hakukubali - Hayo niliyomwambiya
- Kanga mbili hazikosa - Sababu sina mapesa
Nikabakiya kupwesa - Sina za kunuliya
- Kinyikani hadi Gasi - Kulizidi wasi wasi
Shekhe Sefu bu Khamisi - Mvuwa yemuharibiya
- Alialika wajima - Nduguze wakenda chuma
Vikuta avitazama - Hana pa kuanikiya
- Echumisha kwa mpanja - Akaujaza uwanja
Akakataa kuwinja - Wenziwe wamngojeya
- Aliwambiya wenziwe - Mainji sasa yasiwe
Siku hizi tupumuwe - Hakuinjiki kwa mvuwa
- Akawambiya jamani - Kwa sasa tupumuweni
Hakwendeki msituni - Mainji hayatakuwa
- Mwenye yake akatende - Kuinja leo tusende
Mwituni kuna umande - Nguo zetu zitarowa
- Siku hizi tusiwinje - Mainji na tuyavunje
Tuwe nyumbani tukunje - Mvuwa ikitutokeya
- Basi Khamisi Kinenya - Mambo yalimkanganya
Watu akiwadanganya - Waliomdondoleya
- Akiwambiya nendeni - Murudiye majumbani
Nami hirudi dukani - Fedha nitawaleteya
- Nyote murudi makwenu - Mukafanye kazi zenu
Na yote mapesa yenu - Takujawapelekeya
- Vibaruwa wakajibu - Kinenya watughilibu
Leo twataka hisabu - Hatuna cha kutumiya
- Hatuwezi kuondoka - Tena tulipe haraka
Pesa zetu twazitaka - Tumechoka kungojeya
- Kinenya twakukhubiri - Leo utupe shauri
Hatuwezi kusubiri - Tunachoka khadaliwa
- Kama wataka matata - Tayari utayapata
Maishayo utajuta - Kila ukikumbukiya
- Kinenya akenda mbiyo - Kwa babaye na kiliyo
Maneno amwambiayo - Babaangu niombeya
- Baba nakuja unipe - Yule dumeo mweupe
Hamuuze nikalipe - Vijana wataniuwa
- Akamjibu mwanangu - Dume mweupe si wangu
Nami nna deni yangu - Kubwa nnayodaiwa
- Yule ni n'gombe wa watu - Kumuuza sithubutu
Nami ndani sina kitu - Hakupa ukenda towa
- Wangu ni yule mtamba - Yule mweupe mwembamba
Huyo siwezi mkumba - N'gombe wangu wa maziwa
- Sasa bora wende zako - Ukauze vitu vyako
Ulipe madeni yako - Yaliyokushughuliya
- Baba kiume jikaze - Funga susu uchuuze
Mwanagu usipuuze - Utakujashitakiwa
- Baba tafuta pesangwa - Hima ulipe malingwa
Kinenya huwezi fungwa - Kifungo kina udhiya
- Ukifanyiza mchezo - Utapata matatizo
Iwapo pesa hunazo - Basi utateketya
- Saidi Ali Mjaka - Yalimpata mashaka
Ilikuwa aanika - Lakini hakuinuwa
- Hapo uwanjani pake - Akisema peke yake
Ni kheri nipumzike - Saidi nitaumiya
- Najiona natilifu - Machumi yenda uchafu
Siwezi kujikalifu - Afadhali tapumuwa
- Zote karafuu zangu - Zinapoteya kwa wingu
Aidha na ndugu zangu - Wasema nawaibiya
- Nami naapa qasama - Shamba lao sikuchuma
Aliyechuma ni mama - Ndiye aliyedondowa
- Kinyikani watu hao - Pamoja na wenzi wao
Ni kubwa khasara yao - Iliyowafikiliya
- Basi Piki Mchangani - Palikuwa na mgeni
Kwake ilikuwa shani - Namna ilivyokuwa
- Hadharmi wa Unguja - Naye Pemba alikuja
Yalimfika maoja - Pemba akaichukiya
- Na maalim Hemedi - Mali nyingi alikodi
Ikamshadidi hadi - Zote zikampoteya
- Taabu ikampata - Ya watu alioleta
Mvuwa iliponyonyota - Wote walimkimbiya
- Wakabakiya wawili - Wenye ahadi ya kweli
Wa tatu aitwa Ali - Muuzaji wa kahawa
- Kubwa lililomfika - Ekuwa asikitika
Zote ziliharibika - Zile alizochumiwa
- Mgoli na Mavuika - Na fimbo hadi Kinyika
Mvuwa ikimiminika - Wala haikinyamaa
- Makaani na Kinyuji - Yakimiminika maji
Watu walivyotaraji - Hata moja halikuwa
- Mtanga mzee Khelefu - Hadithi yake ni refu
Akenda kama kipofu - Macho hayaoni njiya
- Sababu alizochuma - Hepata moja nzima
Basi alingiya homa - Akenda akiuguwa
- Khelefu kiliyo chake - Halilii mali yake
Aliya kuhama kwake - Na muradi haukuwa
- Akarudi meli mbili - Taabani hana hali
Yunifomu ya skuli - Selemani hekatiwa
- Selemani akasema - Yunifomu ni lazima
Sikupata sendi soma - Na skuli takimbiya
- Khelefu akamjibu - Mwanangu utaharibu
Kutoroka ni aibu - Nami nitalaumiwa
- Wakinikuta walimu - Sana watanilaumu
Ikiwa ni yunifomu - Baba takununuliya
- Baba jikaze kiume - Wende shule ukasome
Duniya uitizame - Huko tunakokwendeya
- Kodi ya bwana Khelefu - Ilikuwa ni dhaifu
Na tena hakusadifu - Wala hakufanikiwa
- Na Shamisi Zaharani - Aliyeko Kisiwani
Watu wekwenda muhani - Kama aliyefiliwa
- Na waliokuwa Finya - Karafuu zewavunya
Wasijuwe la kufanya - Fikira zikawashiya
- Wa Pandani na Masipa - Walikuwa wakirapa
Wa kule hafiki hapa - Maji yalivyoeneya
- Kadhalika wa Takao - Ilioza mali yao
Mambo kwa jirani zao - Bwagamoyo na Bogowa
- Patini na Bahanasa - Humo mvuwa yepangusa
Huoni mtu na pesa - Ambae aitumiya
- Waliyozidi Patini - Kwa Saidi Selemani
Yeye hakitoka ndani - Kwa khofu ya kudaiwa
- Shekhe Saidi Riyami - Alikithiri naumi
Kwa zile elfu kumi - Fedha alizozitowa
- Taabu ikampata - Eshindwa la kutafuta
Pesa moja hakupata - Na deni yamngojeya
- Na shekhe Salim Sunda - Khasara ilimpanda
Kama uzi akakonda - Kwa mali kumpoteya
- Maneno aliyosema - Bora nisingalichuma
Afadhali ningelima - Roho ingelituliya
- Kuliko kutaabika - Kuanuwa hianika
Na hata zikikauka - Sina wa kumuuziya
- Toba Ya Rabbi sitara - Imenipata khasara
Mambo yote yanarura - Hapana lililokuwa
- Amma janibu za Gando - Kulikithiri kishindo
Hakupitiki kwa vundo - Labda uzibe puwa
- Junguni hadi Mkote - Jumla ya watu wote
Wekuwa kama viwete - Maguu yanyon'gonyeya
- Ali Hemedi wa Raha - Ilimtoka furaha
Akipita na siyaha - Imkononi kofiya
- Kofiya haivaliki - Na Raha hakukaliki
Gari haiendesheki - Mughuma unamngiya
- Ikawa apiga yowe - Akawambiya wanawe
Leo bora mupumuwe - Sitaki kuanikiwa
- Japo mukazianika - Bure hazitakauka
Wingu likimiminika - Itakuwa ni udhiya
- Akausiya wanawe - Leo Kheri mupumuwe
Magari musiyatowe - Maji yanaziba njiya
- Ela bora niwatume - Mwende hima mukaseme
Vibaruwa wasichume - Kishamba cha Madaniwa
- Basi skuli Ziwani - Sheke wetu Slemani
Alikuwa taabani - Kwa alivyoozekewa
- Khasara walishikana - Njema ikawa hana
Mabovu yakajazana - Asipate pa kukaa
- Mkasa wa Magogoni - Kwa Rashidi Sultani
Amma ilikuwa shani - Siwezi wahadithiya
- Mali iliharibika - Kambini nzima yanuka
Mwenyewe akaondoka - Mali akaikimbiya
- Maneno mengi aseme - Wanawake na waume
Atakaye akachume - Zote natowa atiya
- Na Muhamedi Saidi - Khasara ilimzidi
Ikamwisha jitihadi - Na mali yampoteya
- Akamwambiya mwanawe - Tufunge tusichumiwe
Machumi yenda kwa gowe - Hwenda yakatuchachiya
- Ama shekhe Muhamedi - Mengi aliyaradidi
Ikawa hapana budi - Kidimni kuhamiya
- Alipohamiya huko - Alizidi sikitiko
Mradi kila endako - Hana faka ya kukaa
- Barawa hakukaliki - Kidimni hakwendeki
Harubu kwenda hataki - Kwa huzuni kumwingiya
- Msiba umemfika - Aliya asikitika
Zile alizoanika - Nazo zimemvimbiya
- Akamwambiya babaye - Baba kheri utuliye
Kazi taifanya miye - Nikichoka tapumuwa
- Kutakao Hababuu - Aliumiya miguu
Kwa kuoza karafuu - Hanyamaziki kuliya
- Aliyo akitamka - Mwaka huu ndiwo mwaka
Khasara ilonifika - Nisiyoitegemeya
- Asema kiliyo changu - Yananizidi matungu
Mali ya watu na yangu - Jamii imepoteya
- Sililii hizi zetu - Muhamedi sina kitu
Naliya mali ya watu - Sina pa kuivumbuwa
- Azizi Saidi Komba - Nae mvuwa yemkumba
Asilijuwe la kwamba - Kelele zikamwishiya
- Zikamwishiya kelele - Jamaa zake wa Ole
Wakenda kumpa pole - Hawezi waitikiya
- Neno alilotamka - Naliya hisikitika
Zote zinaharibika - Zile nilizochumiwa
- Inanifika hilaki - Kichemi hakukaliki
Na Ziwani hakwendeki - Kwa kero la vibaruwa
- Saninga siwezi kwenda - Nikenda roho yadunda
Maji yanajaa banda - Nikifika naghumiwa
- Barawa kwa masharifu - Kwa Alawi bin Yusufu
Kulikuwa na uchafu - Ziligeuka makaa
- Zikawatiya kinyongo - Yakawashiya maringo
Zilikuwa kama dongo - Tope za kukandikiya
- Hapo esema Alawi - Myaka yote sidaiwi
Mwaka huu siyajuwi - Mambo yatavyokuwa
- Yusufu nakueleza - Mambo yamenishangaza
Hidaiwa nitauza - Shamba la Tumbi wa kaa
- Yusufu akamjibu - Kwa maneno ya ghadhabu
Neno hilo si muhibu - Kwa miye sitaridhiya
- Tumbi wa kaa kuuzwa - Alawi tutamalizwa
Barawa tukifukuzwa - Wapi tutakimbiliya
- Utatupata mughuma - Tusiweze kusimama
Nasi Shumba tushahama - Haijuzu kurudiya
- Tukiuza mali yetu - Hatutakuwa na kitu
Tukipita kwa wenzetu - Si hasha kutuzomeya
- Kanambe hadi Makumbi - Maji yepiga msingi
Watu wakavunja kambi - Wengine wakakimbiya
- Wakavunja kambi zao - Wakarejeya makwao
Sababu mabanda yao - Mengi yewavunjikiya
- Bakari Abdrahmani - Ilimtoka imani
Akasahau hisani - Kubwa aliyofanyiwa
- Alikodi akachuma - Kwa sherehe na salama
Mali akiitazama - Nyingi kajikusanyiya
- Lakini mvuwa yenyesha - Bakari hajakausha
Kazi ajishughulisha - Fikira zinamwishiya
- Akawa mtapitapi - Hana khofu haogopi
Vibaruwa hawalipi - Kaziye awahadaa
- Ubaya akawafanya - Vibaruwa kuwabinya
Mwisho aliwanyan'ganya - Pesa moja hakutowa
- Basi wachumaji hao - Hakuwapa pesa zao
Na yeye hana kituo - Deni inamzidiya
- Vibaruwa wakasema - Bakari si mtu mwema
Kazi yake ni dhuluma - Ndiyo aliyozoweya
- Na Omari Athumani - Kwa kodi hawezekani
Ni jasiri kwa yakini - Sifaye mtu hupewa
- Shamba nyingi alikodi - Kwa shime na jitihadi
Alfu nane lukudi - Fedha alizozitowa
- Akaweka watu wake - Kuchumiwa mali yake
Waume na wanawake - Wote wakaimchumiya
- Zikachumwa kwa haraka - Mali ikakusanyika
Wingu likamiminika - Nahari na lailiya
- Hapo alipoziweka - Ekwenda akazishika
Zinavimba zatumbuka - Akazifanya mboleya
- Akawambiya wanawe - Nendeni mukazizowe
Zote mukazikokowe - Sitaki zishuhudiya
- Muzizowe kwa mabamba - Zote muzirovye shamba
Mashimoni mwa migomba - Mupite mukizitiya
- Athumani kaondoka - Machozi yapukutika
Na Musa asikitika - Kwa yale yalotokeya
- Watoto wakalizana - Kina wakiambiana
Baba yetu pesa hana - Za kodi na vibaruwa
- Kikaanguka kiliyo - Na maneno yasemwayo
Baba mapesa hanayo - Hwenda akashitakiwa
- Shekhe Omari kasema - Deni linaniandama
Unaningiya mughuma - Fikira zinanishiya
- Hii ni bakhti yangu - Kunipiga ulimwengu
Mali ya watu na yangu - Yote yananipoteya
- Wanangu musiogope - Roho naziwe nyeupe
Tauza mali nilipe - Deni nnayodaiwa
- Kwanza nitauza nyumba - Na kikataa cha shamba
Na n'gombe wangu mtamba - Tamuuza atakiwa
- Azizi shekhe Salimu - Ekodi mali kwa hamu
Akawaita hirimu - Ili kuja mchumiya
- Akachuma zikaoza - Iikawa zamshangaza
Hata siku ya kuuza - Mali haikutakiwa
- Vibaruwa wamdai - Wataka pesa za chai
Salimu awalaghai - Kina akiwazuzuwa
- Vibaruwa wakajibu - Salimu watughilibu
Hima fanya taratibu - Hatutaki zuzuliwa
- Salimu sibu shauri - Hima usitaakhari
Na tena twakukhubiri - Khadaa zitakwishiya
- Salimu yake maqali - Sina kitu sina hali
Bora mustahamili - Nami nawatafutiya
- Vibaruwa wasemayo - Itakwisha khadaayo
Pesa zetu hii leo - Tupe bila kupunguwa
- Twazitaka pesa zetu - Haraka turudi kwetu
Jawabu ya sina kitu - Hatutaki kuambiwa
- Hapo Salimu Nasoro - Kikamjiya kihoro
Akajifanya mtoro - Atoroka vibaruwa
- Jamaa wa Kibochano - Na wale wa Meli tano
Wote wakishika vyano - Karafuu zafukiwa
- Birikau na Mavungwa - Mabanda yameshajengwa
Wachumaji wakapangwa - Siku ya kwenda hamiya
- Siku ya uhamiaji - Yakamiminika maji
Yote waliyotaraji - Wasipate hayakuwa
- Shangafu Hindi na Jojo - Khasara kubwa na fujo
Wakakata mikongojo - Fimbo za kuchechemeya
- Kokole na Pondeyani - Na N'gambwa na Miburani
Zilioza majamvini - Zilishinda kuanuwa
- Muradi kila wendako - Ukifika mvuwa iko
Mkanjuni ndiko huko - Watu walikoumiya
- Nasoro bin Majidi - Na L-baqashi Asedi
Shilingi arba ziadi - Ndiyo aliyochukuwa
- Walikodi shamba hiyo - Watu wakaliya choyo
Pato lao ni kiliyo - Kina wakiomboleya
- Waliya wakiongeza - Kwa mali yao kuoza
Na hizo zilizosaza - Ni bahati kutakiwa
- Basi tukenda usoni - Kuna kijana Amani
Alikodi Kuungani - Pamoja na Tundauwa
- Bwana huyo wa kimanga - Khasara ilimsonga
Kutwa kucha akitanga - Kwenda kiguu na njiya
- Waliyopata maoja - Siweshi nikiwataja
Pemba hapana mmoja - Ambaye alibakiya
- Ikatufika dharuba - Pasiwe mwenye akiba
Hata nusu ya kibaba - Sikwambii kwa guniya
- Na hizo zilizosaza - Hapana pa kuziuza
Wahindi watufukuza - Nao zinawajaliya
- SI-JI-EE ukiifika - Ni vivyo kutaabika
Ukipewa pa kueka - Kupima utangojeya
(SI-JI-EE = C.G.A. = Cloves Growers Association)
- Aibu ya SI-JI-EE - Ukenda sharti ukae
Karani akuringie - Uwe wampembejeya
- Karani huyo taringa - Kina akikusimanga
Aseme zina mchanga - Ni lazima kutolewa
- Ni mbichi zikakaushwe - Zina taka zisafishwe
Nzima tuzipasishe - Karani atakwambiya
- Moyo takupiga fundo - Akufanyiye kishindo
Sharti utaje magendo - Ndipo utakubaliwa
- Kama magendo hutowi - Ujuwe hupasishiwi
Karafuu hupimiwi - Wallahi nakuapiya
- Ukifanya ukaidi - Utakwenda ukirudi
Mwisho uwe huna budi - Maliyo kuichukuwa
- Magendo ukikubali - Zitapasi hazifeli
Tena kwa muda qalili - Fedha utahisabiwa
- Tena pana wachukuzi - Wanakaa domo wazi
Iwapo huwakonyezi - Hawaligusi guniya
- Hilo sharti ulijuwe - Wote wataka wapewe
Ulichonacho mugawe - Pekeyo hutaachiwa
- Sasa twende kwa Wagunya - Tujuwe walivyofanya
Nguo walizochawanya - Watu wakazichukuwa
- Wakiwakopesha watu - Vitambaa na viyatu
Khasara wageni wetu - Nao ikawashukiya
- Hiyo siku ya kudai - Huondolewa kwa rai
Na kupigwa ulaghai - Na nguo zishavaliwa
- Yamini naweza apa - Jamii waliokopa
Hapana aliyelipa - Na mwisho walikimbiya
- Amma yewafika mambo - Watembezaji urembo
Shida kuu na vikumbo - Kutwa kiguu na njiya
- Hutanga na mabahasha - Kupita wakikopesha
Bure kujihangaisha - Na fedha zikapoteya
- Waliondoka Mambasa - Kuja tafuta mapesa
Wasipate wakakosa - Nauli ya kurudiya
- Na mafundi charahani - Wakishinda barazani
Sabaha hadi jioni - Hawana cha kutumiya
- Hushinda kutwa mchana - Huoni fundi kushona
Wengine huambiana - Tushoneni sidiriya
- Tutashona tukiuza - Watu wengi wauliza
Nyengine tutatembeza - Mwenye pesa tanunuwa
- Na hao wenye magari - Ziliwesha tazbiri
Dereva na matajiri - Wasijuwe pa kwendeya
- Huona gari zapita - Hawana walichopata
Hata pesa za mafuta - Ilitabu kutimiya
- Garini watu hujaa - Wasipate pa kukaa
Ashukae hushangaa - Hana pesa za kutowa
- Na wapikaji miseto - Kutwa huchezeya moto
Jioni hawana pato - Uji hewenunuliya
- Hatokei mnunuzi - Apitae haulizi
Huwapata bumbuwazi - Mseto unachelewa
- Na wachinjao magombe - Hawana faida chembe
Wakiuza hata pembe - Mikamo wakifukiya
- Na wakifanya hisabu - Pato lao ni taabu
Pesa zao zinaghibu - Nyingi zinawapoteya
- Apatae sigireti - Akikosa kibiriti
Mawili yote hupati - Usijeyatumaniya
- Kila mwenye biashara - Ilmpata khasara
Mambo yote yalirura - Hapana lililokuwa
- Kasoro iliyopita - Wengi iliyowapata
Kila unayemkuta - Ana kiliyo aliya
- Yaliyopita ni hayo - Na zaidi mengineyo
Hayo ndiyo matokeyo - Pemba yaliyotokeya
- Na sasa nakhitimisha - Mwisho hapa nafikisha
Mengi nnayabakisha - Siwezi kuendeleya
- Haya niliyoandika - Hata nusu sikufika
Naona yakirefuka - Hwenda nikaja poteya
- Ndiyo nikatiya tamma - Kuandika hasimama
Fahamu sinayo vyema - Na kutunga sijajuwa
- Ni kazi kubwa kutunga - Na maneno kuyapanga
Nami bado ni mjinga - Moyo haujatuliya
- Moyo sijatulizana - Nikabaguwa maana
Ela nawambiya jina - Mupate kulitambuwa
- Niwambiye jina langu - Na jina la baba yangu
Jina la mtaa wangu - Nalo nitawatajiya
- Jina langu ni Khamisi - Mtu fakiri mchesi
Lolote halinighasi - Hulimezeya kifuwa
- Nasoro ni baba yangu - Mpenzi wa moyo wangu
Piki ni mtaa wangu - Ndipo nilipozaliwa
- Ni mzalendo wa Pemba - Na mimi nakaa shamba
Kazi yangu ni migomba - Kupanda nikilimiya
- Kadi tamati utenzi - Nimechoka sijiwezi
Kwa yote siyamalizi - Mengi sikuyatambuwa
TAMMA
Sk. Khamis bin Nassor Al Nabhani [28
Jamadul Akhir, 1381H (1961)].
Limeletwa na Saleh Barkey