.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

KARAFUU MBOVU

 

Related links

KARAFUU MBOVU (Sehemu ya pili)

Sh. Khamis Bin Nassor (Mola Amrahemu), baada ya kukamilisha utenzi kuhusu karafuu zilizoharibika kutokana na mvua kali iliyonyesha mwaka 1961, aliandika tena juu ya mada hiyo katika mwaka 1962 lakini ameelezea khasara iliyowakuta watu wa Mkoani tuu

  1. Yaliyopita Msuka - Ya mali kuharibka
    Mwaka ulipopinduka - Na Bopwe yalitokeya

  2. Yalizaliwa kwa kweli - Makarafuu ya vuli
    Kwa wingi kila pahali - Kazole zikaeneya

  3. Bopwe kwa kila wendako - Karafuu nyingi ziko
    Mkoani ndiko huko - Khasa zilikohamiya

  4. Kipapo na Kichunjuu - Huwezi tizama juu
    Kwa wingi wa karafuu - Uzazi unatimiya

  5. Zilizaa nyingi sana - Za watu kuonyeshana
    Bopwe nzima hapana - Ambapo panabakiya

  6. Washitiri wakafika - Wa Wete na wa Msuka
    Ikawa ni pata shika - Kupita wakikaguwa

  7. Kila shamba upitalo - Ni zuri lipendezalo
    Nalo ndilo litakwalo - Washitiri wawaniya

  8. Washitiri watamka - Mali hii twaitaka
    Na bei tuliyofika - Yafaa kubarikiwa

  9. Akasema mwenye mali - Iwapo mushakubali
    Tumngoje shekhe Ali - Sasa hivi tatokeya

  10. Shekhe Ali akafika - Hata hajapumzika
    Washitiri kwa haraka - Nao wakamtokeya

  11. Bwana Ali kashakuja - Wala yeye hana hoja
    Ela liko neno moja - Alisema hasikiya

  12. Neno alilodhukuri - Kuwambiya washitiri
    Katazameni vizuri - Nipate wabarikiya

  13. Pana jengine muhimu - Na hilo mulifahamu
    Sharti fedha taslimu - Moja isije punguwa

  14. Akasema shekhe Ali - Taslimu fil hali
    Kukopesha sikubali - Na wala sitaridhiya

  15. Wengine wakakodishwa - Wengi wakahangaishwa
    Wengine wakakopeshwa - Ambao waaminiwa

  16. Mashamba yakakodiwa - Wenye fedha wakatowa
    Wengine wedhaminiwa - Kodo ikategemeya

  17. Basi hapo washitiri - Wakakaa kusubiri
    Zilipokuwa tayari - Kambini wakahamiya

  18. Waliyo na mali yao - Zinatuwa roho zao
    Wawangoja watu wao - Wapate kuwachumiya

  19. Hata siku za kuchuma - Ikaanguka zahama
    Mvuwa ikatuandama - Kubwa haina mithaa

  20. Ilianza Mkoani - Kichunju na Kangagani
    Khususa Mkanyageni - Kivumbi Mtu haliwa

  21. Ukipita Mtambile - Watu wote ni wawele
    Yafaa kupewa pole - Maradhi yanawangiya

  22. Wambaa hata Kengeja - Ilikuwa tafrija
    Mvuwa ya moja kwa moja - Nahari na layliya

  23. Basi Gae la mtungi - Mvuwa ilikuwa nyingi
    Haikutosha msingi - Karafuu zepoteya

  24. Chonga Mkungu Kipapo - Humo mvuwa yekuwapo
    Mtu hatoki alipo - Kwa maji kuwazidiya

  25. Ama upande wa Jonza - Ilikuwa miujiza
    Namna zilivyooza - Siwezi wahadithiya

  26. Mvuwa iliyokuwako - Sehemu za Kunguziko
    Yoyote hana endako - Matope yanaeneya

  27. Mtu hatoki kwa tope - Havai nguo nyeupe
    Na upande wa Kigope - Ukipita wateleya

  28. Mgagadu na Kuyuni - Kulikithiri huzuni
    Watu wote taabani - Kwa kuzidiwa na mvuwa

  29. Mangurumo na umeme - Yalikuwa Jambangome
    Wanawake kwa waume - Nyuso zikawafiziya

  30. Upande wa Mgelema - Mvuwa nyingi ikavuma
    Muda wa wiki nzima - Halionekani juwa

  31. Ukipita Mizingani - Wanunuzi kituoni
    Hawaigusi mizani - Hawana cha kununuwa

  32. Ngwani hadi Chemi - Kulikithiri huzuni
    Watu wote hawasemi - Kazi yao ni kuliya

  33. Waliya hawanyamazi - Kwa huzuni na majonzi
    Hawapati usingizi - Huwaoni kusinziya

  34. Waliya kiomboleza - Hawana la kufanyiza
    Macho yanagiya kiza - Kutwa ni kujinamiya

  35. Ama Sipesi na Kendwa - Mitaa hiyo yekwendwa
    Lakini wote weshindwa - Kodi ikawachachiya

  36. Ikawachachiya kodi - Ikawesha jitihadi
    Ikawa hapana budi - Wengine kufilisiwa

  37. Vizuke hadi Nanguji - Yalimiminika maji
    Yote waliyotaraji - Wasipate hayakuwa

  38. Alikodi moadhamu - Hemedi bin Salimu
    Ilimtoka fahamu - Kidogo akaghumiwa

  39. Akatamka Hemedi - Sina tena jitihadi
    Najuta miye kukodi - Bora ningelipumuwa

  40. Inanipata taabu - Na mashaka na adhabu
    Mali yangu inaghibu - Na nyengine nadaiwa

  41. Tamaa ilinishika - Nisiweze ifunika
    Yananipata mashaka - Na mali inapoteya

  42. Hii ni bakhti yangu - Kunipiga ulimwengu
    Naapa mapesa yangu - Kodi nitaikimbiya

  43. Jonza Khamisi Hemedi - Mali ya watu hakodi
    Na alivyo mkaidi - Yake hataki itowa

  44. Washitiri wakifika - Yeye huwa awacheka
    Nyuma akizunguuka - Hayupo keshakimbiya

  45. Hayupo haonekani - Wala hakai nyumbani
    Hadi saa za jioni - Karibu juwa kutuwa

  46. Utamuona yuwaja - Mwendo wa kujikongoja
    Na hayo si mara moja - Hiyo ni yake tabiya

  47. Wageni hawaondoki - Na kukodisha hataki
    Na wala hasemezeki - Huna la kumwambiya

  48. Mwisho hufanya ubishi - Akasema sikodishi
    Mwenyewe hazinitoshi - Naomba kusamehewa

  49. Ingawa bado ni changa - Lakini banda najenga
    Na hivi natangatanga - Watu wa kunichumiya

  50. Nimeshakusnya pesa - Zi tayari hivi sasa
    Na watu sitawakosa - Wa kuja niokoteya

  51. Sasa niwape mahali - Mwende mukakodi mali
    Karibu wala si mbali - Na jina tawatajiya

  52. Ni bora niwaeleze - Mwende mukabembeleze
    Mufike musikilize - Salehe awangojeya

  53. Shekhe Salehe Saidi - Iwapo muna lukudi
    Mukifika mutakodi - Haja yenu itakuwa

  54. Ana shamba la fakhari - Ni kubwa tena ni zuri
    Naye si mtu jeuri - Bashasha azitambuwa

  55. Salehe ni maarufu - Na shamba lake nadhifu
    Ni zuri wala si chafu - Kila mwaka alimiya

  56. Washitiri wakafika - Salehe hajaondoka
    Nao wakafurahika - Kwa kule kumkutiya

  57. Wakafurahika sana - Kwa Salehe kumuona
    Nao wakaambizana - Bora kumuhadithiya

  58. Wakasema tunakuja - Tunakusudiya haja
    Tukodishe shamba moja - Ndilo tulilokujiya

  59. Na kama iko ya pili - Ikiwa haiko mbali
    Juu yetu si thakili - Pamoja kuzichukuwa

  60. Salehe akakubali - Akawapa shamba mbili
    Kaona ni afadhali - Kama kuwazuiliya

  61. Yakamaliza maneno - Wakaeka maagano
    Watowe elfu tano - Zibaki tisaa miya

  62. Mikono wakapeyana - Shamba wakakodishana
    Tena wakaoneshana - Pahala pa kutumiya

  63. Maneno yalipokwisha - Mabanda wakajengesha
    Kuchuma wakaanzisha - Ikamiminika mvuwa

  64. Kwa hakika watu hao - Ilighibu mali yao
    Wasipate hata nguo - Ikawa kudirikiwa

  65. Hawakupata tijara - Bali wepata hasara
    Kwa mvuwa kuwakwangura - Msiba ukawangiya

  66. Ukawangiya msiba - Kula hawapati shiba
    Wenda wakipiga toba - Pesa zao kupoteya

  67. Mvuwa iliposhtadi - Ikawa kubwa shadidi
    Mchana ukasawidi - Mvuwa ilivyoeneya

  68. Maji yakamiminika - Na maradi kuwalika
    Zote zikaharibika - Zile walizochumiwa

  69. Kilindi na Kuungeni - Huko ilikuwa shani
    Khasara Matwaiwani - Nao ikawashukiya

  70. Watu wa mitaa hiyo - Walikiyhiri kiliyo
    Kwa mali waliyonayo - Na ilvyowachachiya

  71. Shekhe Issa Twaiwani - Alikuwa taabani
    Kutwa yupo barazani - Kimya kanajinamiya

  72. Echuma akazipata - Akavijaza vikuta
    Mvuwa iliponyonyota - Kuchuma akazuwiya

  73. Karafuu zikaoza - Nyumbani akazijaza
    Hata juu ya baraza - Yeye akianikiya

  74. Nyingi zikaharibika - Nyingi zikapukutika
    Hizo zilizokauka - Nyeusi kama makaa

  75. Shekhe Issa akakonda - Asijuwe la kutenda
    Na wala hana pa kwenda - Fikira zikamwishiya

  76. Akasema shekhe Issa - Karafuu nishakosa
    Na ndani sina mapesa - Ya kulipa vibaruwa

  77. Mambo yananishangaza - Sijuwi la kufanyiza
    Sina budi tamuuza - N'gombe wangu wa maziwa

  78. Tamuuza n'gombe wangu - Nifiche aibu yangu
    Kwani ndiyo kilimwengu - Nakhofu kuadhiriwa

  79. Japo tapata khasara - Kuuza n'gombe ni bora
    Naikimbiya idhara - Iliyonielekeya

  80. Basi Chemi kwa Kikasa - Huko mvuwa yepangusa
    Watu wote wakakosa - Waliyoyakusudiya

  81. Wote waliokuwako - Viliwafika vituko
    Ikawa ni sikitiko - Kwa yaliyowazukiya

  82. Nabahani Muhamedi - Kwa Kikasa akakodi
    Elfu kumi lukudi - Pamoja alizotowa

  83. Na hata akishachuma - Elfu yamtazama
    Mbali mambo ya gharama - Shilingi tisaa miya

  84. Hizo ni vile akenda - Na magarini kupanda
    Na za kujengesha banda - Pahali pa kutumiya

  85. Akaja na watu wake - Waume na wanawake
    Akaanza kazi yake - Muda umeshawadiya

  86. Akahamiya akesha - Shamba la kufurahisha
    Kuchuma akaanzisha - Bila ya kukawiliya

  87. Echuma muda wa wiki - Haraka hapumziki
    Lakini hazikauki - Ni mbaya hali ya hewa

  88. Ikanya mvuwa kikweli - Ikaharibika mali
    Uso ukatabadali - Mweusi ukafifiya

  89. Zote ziliharibika - Moja haikukauka
    Na za juu zaanguka - Za chini zakokolewa

  90. Ikawa khasara yake - Pesa za watu na zake
    Na nyengine apeleke - Hana pa kuzizumbuwa

  91. Ikamjiya nadhari - Ende aliko tajiri
    Ili ampe khabari - Kwa yale yalotokeya

  92. Hapo hakutaakhari - Akenda hana nadhari
    Kamueleza khabari - Na huku ajinamiya

  93. Akenda hadi Pujini - Hali yake tabani
    Hajuwi aseme nini - Fikra zinamwishiya

  94. Pujini akawasili - Kwa Salimu bin Ali
    Akashtakiya hali - Mengi akaelezeya

  95. Yote akamueleza - Hata moja hakusaza
    Tajiri kananyamaza - Kama asiyesikiya

  96. Tajiri akatamka - Hayo najuwa hakika
    Lakini sijatosheka - Na wala sijaridhiya

  97. Shamba nilikukodisha - Fedha ukasalimisha
    Zile zilizobakisha - Nazi nzihitajiya

  98. Mengine miye sitaki - Na wala sisemezeki
    Labda shamba la Piki - Ukinipa tachukuwa

  99. Tachukuwa kwa thamani - Au tashika rahani
    Ukinilipa mwakani - Shamba takurudishiya

  100. Muhamedi ndugu yangu - Ni hayo maneno yangu
    Nazitaka pesa zangu - Uwe hali ya kujuwa

  101. Muhamedi kakalimu - Sikiza sheke Salimu
    Kukulipa ni lazimu - Usidhani nakataa

  102. Lakini kwa hivi sasa - Similikimhata pesa
    Kwa sababu nimekosa - Yamini nakuapiya

  103. Shekhe Salimu naapa - Sikatai kukulipa
    Kama napata kukopa - Deni nigelichukuwa

  104. Nikachukuwa kwengine - Hakupa tusigombane
    Na sasa tusikizane - Maliyo takuleteya

  105. Takupa kitu rahani - Ukishike kwa thamani
    Hata tufike mwakani - Panapo majaaliwa

  106. Mwakani takuja nazo - Pamoja zote pesazo
    Kwangu mimi pesa hizo - Siwezi kuzuwiliya

  107. Tajiri hakuyarudi - Maneno ya Muhamedi
    Sababu hapana budi - Kwa hivyo akaridhiya

  108. Shekhe Ali bin Juma - Kitongani alihama
    Ulimpata mughuma - Ole akenda hamiya

  109. Na alipofika huko - Ni vivyo jua haliko
    Likazidi sikitiko - Asijuwe pa kwendeya

  110. Akamwambiya nduguye - Ewe Khamisi siliye
    Si weye wala si miye - Khasara inaeneya

  111. Haya yaliyotufika - Hutokeya kila mwaka
    Wengine husikitika - Na wengi huvumiliya

  112. Mwaka huu yako kwetu - Lakini si peke yetu
    Ni pamoja na wenzetu - Yaliyotufikiliya

  113. Sasa tustahamili - Tumfike mwenye mali
    Tukamliliye hali - Tuombe kupunguziwa

  114. Tena twende kwa haraka - Isiwe kuakhirika
    Pengine ataondoka - Si mtu wa kutuliya

  115. Shekhe Ali na Khamisi - Wakenda mbiyo upesi
    Huku wana wasi wasi - Khofu inawazidiya

  116. Wakamfika tajiri - Pasi na kutaakhari
    Yote wakamkhubiri - Waliyoyakusudiya

  117. Shekhe Ali katamka - Bwana kwako tumefika
    Neno tunalolitaka - Ni vizuri kukwambiya

  118. Tumekuja na mawili - Moja wapo ukubali
    Na ingawa ni thakili - Lakini ndiyo duniya

  119. La kwanza tusamehewe - La pili tupunguziwe
    Na gharadhi tuondowe - Uwe watuhurumiya

  120. Utuonee huruma - Hatuwezi kusimama
    Mwiba uliotukwama - Hatuwezi kuutowa

  121. Inatupata khasara - Yaoneke kwa jahara
    Tena inatukwangura - Na hila zinatwishiya

  122. Ni hayo tukwambiyayo - Nawe sema upendayo
    Wasemaje manenoyo - Jawabu twahitajiya

  123. Tajiri naye kajibu - Shekhe Ali ni muhibu
    Maneno yenu twaibu - Yote nimeyasikiya

  124. Lakini nawaeleza - Mengi mulozungumza
    Ama yananishangaza - Tena yananikuliya

  125. Kwa hayo muliyosema - Kwa uzani hiyapima
    Kwangu hayakuinama - Uzito unapunguwa

  126. Niliwakodisha mali - Rahisi wala si ghali
    Kusamehe sikubali - Siwezi wapunguziya

  127. Kuwasamehe siwezi - Pesa moja sipunguzi
    Na tena kwa siku hizi - Fedha nazihitajiya

  128. Mulivyokubali kodi - Mali yangu hairudi
    Ikiwa hapana budi - Nawapa shilingi miya

  129. Zitabaki alfeni - Hizo tuandike deni
    Muje mulipe mwakani - Rabi akitujaliya

  130. Maneno yangu ni hayo - Wala sina mengineyo
    Fedha ndiyo nitakayo - Nipate kuzitumiya

  131. Kwa hivyo wakaondoka - Na machozi yawatoka
    Nyuso zinasawijika - Majoinzi yanawangiya

  132. Kitongani wakahama - Na deni yawatazama
    Wakajutiya kukoma - Kwa deni kuwakuliya

  133. Ama Abedi Rajabu - Ilimfika taabu
    Ikawa ndiyo sababu - Mali yake kupoteya

  134. Alikuwa akichuma - Mtaa wa Giriyama
    Kila kizitizama - Chungu zimemjaliya

  135. Ikamfika hilaki - Ambayo haisemeki
    Kupewa jema hataki - Kazi yake achukiwa

  136. Akija Mtu Haliwa - Huagiziya kahawa
    Hapokei akipewa - Jinsi alivyoghumiwa

  137. Sheke Abedi Rajabu - Mambo yalimuadhibu
    Akangiwa ni ghadhabu - Zote akazifukiya

  138. Na nyuma viko vikuta - Huku mvuwa yanyonyota
    Kuzichima akajuta - Kwa zilivyomuozeya

  139. Zote zikaharibika - Majamvi yamun'gunyuka
    Na mvuwa yapukutika - Bado haijanyamaa

  140. Akipiga makelele - Apita huku na kule
    Uwanjani tope tele - Hana pa kuanikiya

  141. Kambi yake mlimani - Ina vikuta wanjani
    Karafuu za bondeni - Zote zinakokolewa

  142. Yakmjiya mahana - Hapati kutulizana
    Si usiku si mchana - Kutwa kiguu na njiya

  143. Wale wamchumiyao - Wataka rudi makwao
    Wazitaka pesa zao - Hawana cha kutumiya

  144. Kwa lazima azitowe - Wala asiwasumbuwe
    Zote awape wenyewe - Moja isije punguwa

  145. Pakaingiya mzozo - Abedi pesa hanazo
    Ikawa ni matatizo - Ikaanguka ghasiya

  146. Ikawa ni kugombana - Hapana kusikizana
    Karibu na kupigana - Abedi na vibaruwa

  147. Basi mambo ya Tasini - Kwa Abdul Rahamani
    Naye epata huzuni - Kubwa isiyo mithaa

  148. Abdul Rahamani Khalidi - Mvuwa ilimhusudi
    Zote alizozikodi - Jamii zilipoteya

  149. Zilimpoteya zote - Hata moja asipate
    Kutumwa mtu amwite - Basi huyo akimbiya

  150. Ama Sefu Muhamedi - Kwake mambo yalizidi
    Kwenda huku akirudi - Tasini hawezi kaa

  151. Na huko Mkanyageni - Nako ilikuwa shani
    Abdalla Khalfani - Mughma unamngiya

  152. Ulimpata mughuma - Asijuwe la kusema
    Zile alizozichuma - Zilimharibikiya

  153. Zote ziliharibika - Machozi yakamtoka
    Kwa kazi ya kuanika - Hapati za kuanuwa

  154. Basi Omari Bakari - Cheyameni mashuhuri
    Mvuwa ilimkithiri - Na mengi yakatokeya

  155. Hakika Mkanyageni - Ilikuwa kisirani
    Hususa kwa cheyameni - Mambo yalimkuliya

  156. Akijikeketa meno - Akaeka mkutano
    Akenda hana maneno - Hawezi kukhutubiya

  157. Akamwambiya katibu - Nisemalo likutubu
    Maneno hiyaharibu - Nirudisha hipoteya

  158. Kwa sababu moyo wangu - Si hadhiri ndugu yangu
    Nafikiri ulimwengu - Ulivyonielemeya

  159. Sikodi tena maisha - Na zangu tazikodisha
    Ucheyameni watosha - Hayo nijiaguliya

  160. Mambo ya Mkanyageni - Ya Omari cheyameni
    Na Abdulla Khalfani - Nishawazungumziya

  161. Kangani tusisahau - Zilioza karafuu
    Zilizo chini na juu - Jamii zilipoteya

  162. Shekhe Salehe Hemedi - Ni jusuri wa kukodi
    Khasara ilimzidi - Shamba aliyochukuwa

  163. Yalimpata matata - Akawa yeye ajuta
    Alikosa hakupata - Makusudi hayakuwa

  164. Ama Rashidi Saidi - Kwa khasara alizidi
    Ikawa hapana budi - Maliye kuchukuliwa

  165. Alishikwa akabinywa - Asemayo akakanywa
    Maliye akanyan'ganywa - Yote hakubakishiwa

  166. N'gombe dume na mtamba - Jamaa waliwakumba
    Bakhti yake ni nyumba - Ndiyo aliyoachiwa

  167. Mvuwa yekuwa Chokocho - Pasiwe kipatikacho
    Ridhwani afichacho - Si kazi kufichuliwa

  168. Kwa hakika Ridhwani - Alikuwa taabani
    Kwa shamba la Mchangani - Ndilo lililomuuwa

  169. Ridhwani akasema - Unanipata mughuma
    Hata moja sikuchuma - Nami huku nadaiwa

  170. Mapesa nidaiwayo - Ni mengi wala sinayo
    Mwaka huu ni kiliyo - Kilichonifikiliya

  171. Naye ndugu Juma Kombo - Ekodi shamba kwa Yambo
    Yakamfika majambo - Asiyoyategemeya

  172. Shamba ekodi kwa pupa - Na pesa ni za kukopa
    Asipate cha kulipa - Kodi ilimchachiya

  173. Juma Kombo kimuona - Alivyongiya mahana
    Ukimwita hukuguna - Tena hukunyamaziya

  174. Japo mwite haitiki - Wala hana urafiki
    Kusema yeye hataki - Mara hukuhamakiya

  175. Juma Kombo tumjuwe - Chokocho ndiye mjiwe
    Ridhwani jiraniye - Pamoja wanapokaa

  176. Asubuhi huitana - Mikono wakapeyana
    Ikawa ni kulizana - Kina wakiomboleya

  177. Upande wa Makombeni - Na Mkoano mjini
    Mimi huko nu mgeni - Nilikwenda kutembeya

  178. Lakini niliuliza - Watu wakanieleza
    Karafuu zinaoza - Zahinda kuondolewa

  179. Ziliharibika kweli - Kwa mvuwa kuwa thakili
    Uwanjani kama vuli - Ukipita wachopeya

  180. Ama dalali Kichungi - Epoteza mali nyingi
    Kataa sasa haringi - Maringo yanamwishiya

  181. Yalimwishiya maringo - Akaingiya kinyongo
    Akawa hana mpango - Wala hana pa kwemndeya

  182. Akenda akinadisha - Wengi aliwakodisha
    Mavuno yalipokwisha - Fedha hakurudishiwa

  183. Ikamfika hilaki - Nyumbani hakukaliki
    Probeti hakwendeki - Akhofu kulaumiwa

  184. Sababu mali si yake - Epewa yeye ashike
    Akusanye apeleke - Probeti angojewa

  185. Hayo ndiyo matatizo - Kishungi pesa hanazo
    Yakamwishiya mawazo - Hana pa kuzizumbuwa

  186. Lakini efanya rai - Ya kupita akidai
    Akawa kwake hakai - Kutwa kiguu na njiya

  187. Wengine walimlipa - Wengine hawakuumpa
    Akabakiya kurapa - Roho haikutuliya

  188. Na mwisho alitamka - Mwaka huu kwa hakika
    Khasara inanifika - Nisiyoitazamiya

  189. Hii ni bakhti yangu - Kunipiga ulimwengu
    Nnamshukuru Mungu - Ndiyo hali ya duniya

  190. Kishungi esema hayo - Wala furaha hanayo
    Akanyamaza kiliyo - Lakini akiuguwa

  191. Na kila mwenye shambaye - Hajitambuwi haliye
    Hapotei asemaye - Kuwa nataka semewa

  192. Za chini hazikauki - Za juu hazichumiki
    Mvuwa hainyamaziki - Mali yazidi poteya

  193. Waliyo na mali yao - Walikosa hata nguo
    Khasara ya mwaka huo - Ndivyo nilivyokwambiya

  194. Khasara kubwa ajabu - Wengi iliyo wasibu
    Mali haina hisabu - Nyingi iliyopoyteya

  195. Kuna wapikao uji - Khasara zao sitaji
    Lakini binti Haji - Huyo aliteketeya

  196. Akiupika mseto - Na uji juu ya moto
    Jioni hapana pato - Uji hewenunuliwa

  197. Na asokuwa na kazi - Akichoma maandazi
    Kukaa bure hawezi - Si mtu wa kutuliya

  198. Kukicha alfajiri - Kila chakula tayari
    Angojeya washtiri - Bado hawajatokeya

  199. Hapana mtu ajaye - Wala amuulizaye
    Bi Haji na khasaraye - Hana wa kumpokeya

  200. Bi Haji hapumziki - Huwakaanga samaki
    Atembeza hawatoki - Hayupo wa kununuwa

  201. Mbugwani Bi Mafunda - Biashara yemshinda
    Asijuwe la kutenda - Fikra zikamwishiya

  202. Bibi Asha na Salima - Maneno waliyosema
    Sasa ni bora kuhama - Hapana la kukaliya

  203. Tuwaarifu wenzetu - Tuhame turudi kwetu
    Hapa hatupati kitu - Biashara yapoteya

  204. Salima akatamka - Yapendeza kuondoka
    Mwaka huu kwa hakika - Tumeshaharibikiwa

  205. Sasa ni bora tuhame - Twende kwetu tukalime
    Asemaye na aseme - Kusema ndiyo duniya

  206. Hakika mabibi hao - Ni kubwa khasara yao
    Lukudi ya kwenda kwao - Ikawa kudirikiwa

  207. Ni hayo yaliyopita - Hapana aliyopata
    Na wengine wakajuta - Majuto yasiyofaa

  208. Nami ndiyo haandika - Bukuni nikayaweka
    Yasijesahaulika - Iwe yakikumbukiwa

  209. Mwisho wangu wa utenzi - Kwenda usoni siwezi
    Zatosha baiti hizi - Kiasi cha kuongeya

  210. Utenzi natiya tamma - Kuandika nasimama
    Nijuwayo nishasema - Mengine sikuyajuwa

  211. Sasa nawambiya jina - Ingawa najulikana
    Uzuri kuambiyana - Ili mukanitambuwa

  212. Khamisi jina ni langu - Ni jina la baba yangu
    Nasoro ni baba yangu - Piki nilipozaliwa

Sk. Khamis bin Nassor Al Nabhani [ 1962].

Limeletwa na Saleh Barkey

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet