.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Kisa cha Miraji

 

Related links

 

KISA CHA MIRAJI

  1. Nanza kunudhumu kwa isimu ya karima
    Mola Mtukufu wa milele mwenye dawama
    Zimewaenea watu wote zake neema
    Sala na salamu kwa mtume zende daima.
  2. Na jamaa zake na sahaba tuwasalie
    Tupate ya kheri miongoni mwao tungie
    Siku ya kiama wasimame watuombee
    Tupate Nusura, Siku nzito ya jahanama.
  3. Haya yanatosha sendi mno kwa dibaji
    Kwani nina mambo kuyataja nahitaji
    Ni hadithi njema ya usiku wa Miraji
    Ya Mtume wetu kupandishwa katika sama
  4. Ilipowadia Mola wetu kadhihirisha
    Cheo cha Mtume Jibirilu alimshusha
    Akaja nyumbani kwa Mtume akamwamsha
    “Ondoka silale,Mola wako akwita hima”.
  5. Alipoamka Jibirilu alipasua
    Kifua cha Tumwa taka zote akaondoa
    Kisha kikajazwa kila mema kile kifua
    Akaja Buraqi mbele yao akasimama.
  6. Jibirilu Kasema“ mola wako akusalimu
    Tumekuja kwita twende nawe kwake Karimu
    “Upande Buraki kwa heshima na taadhimu”
    Buraki ni nyama ametoka katika sama.
  7. Wakenda kwa mbio wakafika kwenye Madina
    Jibirilu kamba “shuka hapa mwombe Rabana
    “Sali kwa vizuri rakaati mbili za Sunna
    “Kisha umsifu Mola wako kwa sifa njema”.
  8. Wakashika njia wakafika Jabali Turi
    Jibirilu kasema“Sali hapa upate kheri
    Hapa ni mahali Maulana Mola Qahari
    Amemsemeza Nabi Musa maneno mema”.
  9. Wakafululiza wakafika Beti Lahamu
    alipozaliwa Nabi Isa wa Mariyamu
    Jibirulu kasema“Sali hapa penye Makamu
    Muombe Rabuka hapa pia mahali pema”.
  10. Na katika kwenda wakaona jinni njiani
    na kijinga chake amwunguze Nabi Amini
    Jibrilu kasema Soma Dua omba manani
    Nabi akaomba , Mola wake akakizima
  11. Baada ya hayo mambo mengi wakayaona
    Wakaona watu wakipanda mara huvuna
    Jibirilu kasema“Watu hao mujahidina
    Wendao jihadi wajaziwa mema daima.
  12. Baada kidogo ilinuka harufu nzuri
    Jibirilu kamba “ ni harufu ya mwenye kheri
    Msusi wa nywele akisuka watu vizuri
    Binti Firauni akisuka kwake daima”.
  13. Alipomchana na shanuo kumwanguka
    Msusi kasema “Fiarauni amepotoka
    Binti Firauni aliinuka kaghadhibika
    “Takwenda mwambia utakiona chako kiyama”.
  14. Khabari zikenda Firauni akasikia
    Akawakusanya ,mke ,mume,na wana pia
    Ndani ya mafuta yenye moto akawatia
    Ni kaburi lao lifukalo harufu njema.
  15. Na katika kwenda waliona watu wazima
    Zinapondaponda vichwa vyao nyundo za chuma
    Jibirilu kamba “Wasosali sala daima
    Ndio jaza yao wajaziwa kesho kiyama”.
  16. Kisha wakanenda wakaona wasio wema
    Wanalishwa moto , mishubiri na michongoma
    Wapigishwa nyinda utasema wana wa kima
    Jibirilu kamba “Wasotoa zaka,nasema”.
  17. Baada ya hapa wakaona walao nyama
    Wanalazimishwa kula mbovu waache njema
    Jibirilu kamba “ni wazinzi wasiokoma
    “Wake na mume wazinio dom-daima”.
  18. Kisha wakaemda wakaona mto wa damu
    Mna watu ndani wogelea wakila sumu
    Jibirilu kamba “watu hao wala haramu
    Mali yao yote kwa haramu wameyachuma”.
  19. Na katika kwenda waliona watu wabaya
    wakikatwa ndimi kwa mikasi zinarejeya
    Ndio hali yao wakikatwa ndimi humeya
    Jibirilu kamba “wazuwao wanaposema”.
  20. Kisha wakanenda wakaona watu njiani
    waparura nyuso kwa makucha wataabani
    jibirilu kamba “wasemao watu penbeni
    watafufuliwa nyuso zao hazina nyama.
  21. Na katika kwenda walikuta mitume pia
    akawamkia kwa salamu wakitia
    kasha akafika nyumba kubwa akaingia
    Bet Mukadasi nyumba njema yenye heshima.
  22. Walipowasili msikiti wenye baraka
    Waliona nuru pande mbili kimemutuka
    Nuru ya ya kaburi la daudi alotukuka
    Na ya pili nuru ya kaburi la Mariyamu.
  23. Wakaingia ndani wakasali rakaateni
    kaona mitume imejaa msikitini
    Hapo Jibirilu kainuka akaadhini
    Akakimu sala ,hawajui yupi Imama.
  24. Jibirilu kamba “Waambiwa utakadamu
    Na mitume iwe nyuma yako ,wewe imamu
    Ukubwa ni wako na heshima na taadhimu
    Kesho utakuwa muombezi wa wote uma”.
  25. Baada ya kusali kila mtu alishukuru
    Neema za Mungu Mola wake Mola Ghafuru
    Na kila mmoja nema yake akadhukuru
    Neema za Tumwa zikazidi zao neema .
  26. Kisha ikashuka Miiraji-ngazi thamini
    Imepabwa fedha na dhahabu na marijani
    Akapanda Tumwa Muhammadi hata mbinguni
    Wakapiga hodi waingie katiak sama ..
  27. Wakamba “ni nani mwenye nuru yenee sama’
    Jibirilu kamba “ Muombezi wa wote umma
    Akafunguliwa kwa haraka na hima hima
    Wakampokea kwa heshima na taadhima .
  28. Tumwa kamuwona baba yetu Tumw Adamu
    Akamwamkia maamkio ya kiislmu
    Kamba : Marhaba ,mepokea yako salamu
    “Ndiwe mwenye ,mbele na mitume yote i-nyuma”.
  29. Kisha wakakwea wakafika wingu wa pili
    Kabisha mlango wakaingia kama awali
    Kmwona Isa na Yahya wote wawili
    Sura zao moja kama ndugu baba na mama .
  30. Na wingu wa tatu wakaingia kwa taadhima
    Nabii yusufu wakamwona na sura njema
    Akanza salamu Tumwa wetu, ndiyo hishima
    Akakaribishwa akawekwa mahala pema.
  31. Kisha wakafika wingu wane wakamwona
    Nabii Idrisa na watano Nabii Haruna
    Uwingu wa sita Nabii Musa bini-Mrana
    Wingu wa saba Burahimu mwenye adhama .
  32. Kisha wakakwea wakaona hapo walipo
    Beti Maamuri imekaa chini ya pepo
    Wakangia ndani wakaona mahali hapo
    Safu sabiini za malaika –viumbe vyema.
  33. Kisha akataka kuonyeshwa moto mkali
    kaona vituko na adhabu ilo kamili
    Moto unawake kuni zake in majabali
    Na watu wabaya waasio Mola daima .
  34. Kisha wakafika kwenye pepo nzuri sana
    Wakaona mambo hapanaye aliyeona
    Wala myawaza kwa moyoni kamwe hakuna
    Wala msikia mambo hayo akayasema .
  35. Baada ya hapa akapewa aliopewa
    Mambo matukufu mfanowe hutaujuwa
    Kapewa na sala khamsini akachukuwa
    Yeye na umati wake wote wapate mema .
  36. Alipomwendea Nabi Musa alimwambia
    “Sala khamsini kila siku zina udhia
    Bora urejee Mola wako kwa kuombea
    Awapunguzie Mola wetu ana rehema” .
  37. Tumwa karejea kumwomba Mola Karima
    Anawaomba takhfifu wapate uma
    Akapunguziwa na Molawe mwenye rehema
    Zikawa ni tano- natusali basi kwa hima .
  38. Kisha wakashuka na usiku wakawasili
    Beti Muqadasi nyumba njema tangu asili
    Ikawa Buraki kasimama kama awali
    Tumwa kampanda kwa isimu yake karima.
  39. Katika kwenenda wakaona wengi ngamia
    Watokao Shamu mali mengi wamepakia
    Walipomuona Burakiye walikimbia
    Moja kavunjika goti lake kwa kwenda hima .
  40. Kisha wakanenda wakafika Makka na kiza
    Hakujacha vyema akakaa Tumwa kiwaza
    Kujuwa yakini Makureshi watamcheza
    Shere kubwa mno wamwone mwongo daima .
  41. Katika kuwaza aliona tumwa Rasuli
    Mbele yake asi maluuni Abu Jahali
    Akamwuliza kwa dhihaka na kwa kejeli
    “Ewe Muhammadi ! nakuona uso kunama .
  42. “Una jambo gani kubwa mno la kughairi
    Ukabadili uso wako usinawiri
    Hunambii nami nikajua yako khabari
    Siyo hali yako tujuwayo kwako daima”
  43. Akamba “Naam takwambia yangu khabari
    Usiku wa leo nalikwenda mbali safari
    Beti Mukadasi nikafika nyumba ya kheri
    Kisha nikapanda baadae katika sama”.
  44. Akawakusanya maluuni Abu Jahali
    Makureshi waje wawe naye wakinakili
    Alipoweleza kwa utungo wasikubali
    Pakawa vicheko na dhihaka na kumzoma .
  45. Kureshi wakamba “tusifiye Beti Kudusi
    Kama umekwenda hutashindwa tukidadisi
    Ama mbingu saba usemazo hatuziisi
    Kwani katukwenda hatujui zake alama” .
  46. Moyo wake Tumwa ukaingia nyingi shughuli
    Mambo ya usiku asiweze kuyafasili
    Mola kaamuru Jibrilu kuinakili
    Beti Mukadasi mbele ya yake kuitazama .
  47. Akawasifia sifa zake wakazikiri
    Kapima kwa nyayo na dhiraa hata shubiri
    Na Abubakari akisema “Ewe Bashiri
    Ndizo sifa zake umesibu zote alama”.
  48. Wale Makureshi wakanena “Ewe Amini
    Ndizo sifa zake umekwisha kuzibaini
    Tuna watu wetu safarini Bani Fulani
    Twambie na siku ya yao kukoma” .
  49. Kamba “Watu wenu karibuni watatokeya
    Ijumatano ndiyo siku yao yakuya”
    Ilipowadia siku hiyo walingojea
    Wakatoka nje majiani wakasimama .
  50. Wakawatokea watu wao wote idadi
    Jua halijachwa ikatimu yake miadi
    Wakamba “Ni kweli alosema hatuyarudi
    Lakini mchawi , anafanya haya daima .
  51. “Ingawa ni kweli sifa zote alofasili
    Ila ni mchawi kama haya kwake kalili
    Kwani anapenda dini yetu kuibatili
    Hatumfuwati tukaacha wetu sanamu” .
  52. Basi nimekwisha Miiraji kuinudhumu
    Kwa Himdi yake Maulana Mola Karimu
    Sala na Salamu na Baraka na Taadhimu
    Zimwendee Tumwa na Ali na Sote uma .
  53. Rabi turehemu kwa rehema yako Azizi
    Turehemu sote wasomao na wasikizi
    Sote turehemu kwa Baraka ya Muombezi
    Siku ya Kiama utokowe na Jahanama .

Mtungaji: Kadhi Sheikh Abdulla Saleh Farsi
Mosomaji: Sheikh Abdallah A. Bakathir
November 1963
Mfungo Tisa ,1383 .
Umeletwa: Ahmed Rashid

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet