|
|
KUUKOMBOA WA'TANI
(Kutoka Katika FZV)
Date: 25 February, 2005
Utenzi huu ulitolewa katika gazeti la Umoja wa Wazanzibari (Free Zanzibar Voice)
mnamo 1968 linaonesha hisia za Mzanzibari mwenzetu akitunadia katika ukombozi wa
Wattani wetu, juu ya fahamu yake kuwa Wattani ndio mama yetu. Ni miaka thalathini na
saba, yaani tangu 1968; lakini yaliosemwa ni madhubuti na ni kama yamesemwa jana au leo.
Hapana shaka Wazanzibari ni wenye uwezo wa kuirejesha Dola yao Huru ya Zanzibar kama
ilivyokuwa kabla ya mavamizi ya 1964. Penye nia pana njia.
- Wat'ani watoja damu, 'tabibu twapiga hodi
Hima hima muadhamu, Sinene nenda urudi
Kukawia ni haramu , na kutoa huna budi
Kwani hii ni Jihadi, kuugomboa Wat'ani
- Mwanao ayayatika, mama muwahi waladi
Mwanao atakutoka, usipofanya juhudi
Kilio chake pulika , kinapasua fuadi
Isaidie Jihadi , ya kugomboa Wat'ani
- Mamiyo alokuzaa , ni mpweke na wahedi
Kakuzaa kwa fazaa , na dhiki mno shadidi
Zengea yake ridhaa , ipate ya Wadudi
Kwani hiyo ni Jihadi , ya kugomboa Wat'ani
- Na baba yako mwanangu, na pia na wako jadi
Usiwatie matungu , hata ukapita hadi
Kumbuka zama za tangu , uwache yako inadi
Wajibu wako Jihadi , kuugomboa Wat'ani
- Mama watoto nyumbani , alozaa auladi
Mkapishana yamini , kukidhi wenu muradi
Wote hao ni Wat'ani , na hao ndio biladi
Unga mkono Jihadi , tuugomboe Wat'ani
- Na nchi yetu tukufu , si maiti ni shahidi
Kwani shahidi si mfu , kila siku ni jadidi
Umma hai mashe khofu, walo mbali watarudi
Wataingia Jihadi , kuugomboa Wa'tani
Mzanzibari
1968
Umeletwa na Farouk Amour
|