.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Mama Musimlaumu!

 

 

 

 

 

 

Related links

 

Mama Musimlaumu!

Date: 18 June, 2006

  1. Imenibidi kunena , kabla wangu wakati
    Sababu nimewaona , mamangu humlaiti
    Mamangu makosa hana , si pweke amezohiti
                      Kosa hili nda ummati

 

  1. Nda ummati hili kosa , na ziyongozi wa nti
    Kosa nda wana siyasa , na mahakimu wa koti
    Kosa nda wenye mapesa , na wasiyo na senti
                       Kosa hili nda ummati

 

  1. Mamangu si Mariyamu , wa Imrani binti
    Mama ni mwanaadamu , meishi hapa tiyati
    Na nyoteni mwafahamu , kuna dhaifu wakati
                        Hushindwa kuidhibiti

 

  1. Mama hakutenda pweke , na labuda hakukiri
    Ali na mwendani wake , aloifanya jasiri
    Ndipo mimi niumbike , mamangu kumuaziri
                         Pasina yangu shauri

 

  1. Ikiwa kuna lawama , lawama nazitanganye
    Mukimlaumu mama , nae baba mumkanye
    Ndipo hapo yatakoma , ubaguzi musifanye
                           Wanawake musifanye

 

  1. Mimi kattu sikubali , mamangu kumlaumu
    Na pweke kumkejeli , huwa ni kumdhulumu
    Kwaye pweke yambo hili , aswilani halitimu
                          
    Hilo nyote mwafahamu

 

  1. Kitendo ni cha wawili , alopawa kapokeya
    Haitokuwa adili , mama pweke kumwemeya
    Halihitaji dalili , wala hoja kuzengeya
                            Ayuwa kulla mmoya

 

  1. Mno huona utungu , kiwasikiya kunena
    Humlaumu mamangu , kwa kuwa mkosa
    sana
    Mimi na wendani wangu , hatupati hata ina
                          Ni sina au sibina

Mahmoud A. Abdulkadir (MAU) -P.O.Box 54 - Lamu , Kenya 7-7-2005

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet