.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Mja

 

 

 

 

 

 

Related links

Mja!

  1. Mja hutashiba kula, Waona ladha daima
    Mja wakonga na ila, Hujui bora khatima
    Mja hiyo ni ghafala, Na kukutaza si vyema
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  2. Urudi kwa Mola wako, Ghafuru ndio Rahima
    Dhiki na taabu yako, La'ala ndio salama
    Nuwiya kwa dhati yako, Toba isiyo na dhima
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  3. Mja usihadaike, Sikiya yangu kalima
    Bilisi asikushike, Ukasahau Kiyama
    Fahamu safawa yake, Siku hiyo ni hasama
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  4. Mja fikiri mauti, Sikuhadae uzima
    KYAM waliofaiti, Mashujaa hapo zama
    Wasikiya huwakuti, Na hio ndio salama
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  5. Mja khofu siku hiyo, 'L-hashiri wannadama
    Ni siku ya makamiyo, Kufufuliwa 'aama
    Ni wewe na amaliyo, Hiyo siku ya zahama
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  6. Mja ladha ya duniya, Haitakwisha daima
    Mja ufikiri njiya, Sirata 'l-mustaqima
    Njiya inayo baliya, Ndani yake jahannama
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  7. Ewe mja tafakari, Inuka ukiinama
    Wenda ndani ya kaburi, Hapana baba na mama
    Mja khofu munkari, Na fimbo zake za chuma
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  8. Mja mkhofu Jalali, Kwa siku ya mahakama
    Siku ya Rabi kujali, Wa yuhyi 'l-idhama
    Siku hiyo ya kitali, Rabi asiyo huruma
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako
  9. Mja natia tamati, Yangu nasaha nakoma
    Mja duniya sukuti, Quruani kunasoma
    Haihati haihati, Mauti kwako lazima
    Ulipofika simama, Urudi kwa Mola wako

 

Khamis Nassor Al-Nabhany

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet