.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

MUHOGO

 

Related links

MUHOGO

Date: 10 October, 2001

  1. Katika chakula tiba - Hapana kama muhogo
    Ya kwanza una haiba - Ukiwa wa mkorogo
    Uwe mwingi wa kushiba - Usiupike kidogo
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  2. Pakiwa na utowezi - Amma huwa kivurugo
    Ukiupatiya ndizi - Ukate wa mchachago
    Ulainike na nazi - Mafuta yafanye sago
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  3. Muhogo hauwi mwema - Kwa makambare na ngogo
    Shati upatiye nyama - Japo ngozi ya kichogo
    Au likiwa vumbama - Liwe nene kama gogo
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  4. Mshelisheli mweusi - Na mbega una titigo
    Ukiupatiya tasi - Ukiula pana zogo
    Na chumvi iwe kiasi - Isije tiwa kwa wigo
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  5. Kolekole kwa yakini - Ni mtamu kwa muhogo
    Uutiye sahanini - Wala pasiwe na zogo
    Tena upate laini - Usiwe na kiparago
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  6. Muhogo minal-ali - Usiokua mchego
    Utie tuwi kalili - Si jingi la mkobogo
    Na samaki afadhali - Asiwe wa mchunjugo
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi
  7. Kadi tama sitazisha - Zote sifa za muhogo
    Beti saba zinatosha - Kutiya watu mchego
    Jama kulima yapasha - Tuiwacheni mikogo
    Uufaidi muhogo - Pakiwa na utowezi

Maana ya maneno alivyokusudiya mtungaji.

Beti 2   kivurugo = furaha
              mchachago = mdogomdogo
              sago =  kuganda (mfano mchuzi wa mafuta unapopowa)

Beti 3   vumbama = aina ya samaki
beti 4   mbega = aina ya muhogo
             kwa wigo = kwa wingi

Beti 5   kiparago = mgumu (kiparago ni kitu kigumu)

Beti 6    minal-ali = mzuri
              mchego = ambao hauivi
              la mkoboko = la inda
              mchunjugo = mbaya ; mwenye miba; ovyo ovyo
Beti 7    mchego = hamu = raghba
              mikogo = pozi

Limeletwa na Saleh Barkey

Alipewa na Sheikh Khamis Bin Nassor Al-Nabhany

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet