|
|
UTENZI WA KISA CHA NABII AYYUB (A.S.)
Date: 7 September, 2003
- Bismillahi Qadimu, Arrahmani Rahimu, Mwenye enzi ya kudumu, Muumba ndiwe Jalia
- Uloumba ulimwengu, Arshi juu ya mbingu, Ukapanga na mafungu, Waja kuwamiminia
- Aridhi ukatandika, Ziumbe ukawaweka, Hukuwa na mshirika, Ni kazi yako Moliwa
- Ukanyesha na mvua, Ukalitowa na jua, Miti nayo ikamea, Ikanawiri dunia
- Hakuna mtenda kazi, Ila ni wewe muyuzi, Mwenye mkubwa uyuzi, Ndiwe wa kutegemewa
- Ukaumba majabali, Makubwa yaso mithali, Ndani yake muna mali, Na aridhi kuziwiya
- Ukakusnaya milima, Ya mitanga ilokwima, Meupe ukiiona, Na raha kuyangalia
- Yote ni kazi ya Mola, Asokula asolala, Na kwake huna muhula, Popote utarejea
- Katengeza kwa udongo, Na tope zenye mavundo, Mwanadamu lake umbo, Quruani yatwambia
- Ukayaweka mauti, Kwetu sisi ni sharuti, Huja pasi na wakati, Siku zikisikilia
- Tahadhari mwanadamu, Yataka ujifahamu, Siku zikishakutimu, Budi huna nakwambia
- Ewe mja usojali, Kumbuka huna mahali, Mauti hayako mbali, Popote hukungilia
- . Ghafula hukukabili, Mauti hayako mbali, Na jina likabadili, Wendo wakakulilia
- Nakuomba ndugu yangu, Tafadhali nisikia, Roho si ya ulimwengu, Hakuna cha kubakia
- Wawapi wanazuoni, Matajiri masikini, Na wenye nguvu wendani, Kama hawakuzaliwa
- Wako wapi wenye nguvu, Akili na uwerevu, Hawakuwa watukivu, Leo wameshika ndia
- Mamako alihajali, Mimba yako kahimili, Uzito kama jabali, Hakushindwa katukuwa
- Kwa kite kaitukuwa, Henenda akijishuwa, Na mangi akiongowa, Kwa kazi yake Karima
- Ukazawa mwanadama, Huna mbele wala nyuma, Kakuyeya wako mama, Kwa uwezo wa Karima
- Ulimwengu si makazi, Kwa kila alomuyuzi, Ni mapito ya wemuzi, Ya kwenenda mui mwema
- Baada haya kunena, Nina kiswa waungwana, Cha Ayubu tumwa mwema, Nimependa kukitowa
- Nimependa kufasiri, Niwape zake khabari, Nimeona ni uzuri, Mupate kumuelewa
- Babake alitajiri, Alina mali kathiri, Alihai kadhukuri, Mali nda mwane nabiya
- Alipokufa babake, Kayashika mali yake, Ayyubu ndie pweke, Mali kaikusanyia
- Alitajiri ajabu, Wa majumba na dhahabu, Na wana wenye adabu, Mola memruzukia,
- Alikuwa na hekima, Za fahamu ya ilima, Na akili zilo tama, Yote kampa Jalia
- Alikuwa mahabubu, Kwa watu na maswahibu, Akipendeza Ayubu, Kwa watu ni maridhia
- Uli na nguvu muili, Na sura zake jamali, Na biashara amali, Ndio alokifanyia
- Kamuoa mwana mwema, Rahama binti Fartima, Babu yake nitasema, Ndie Yusufu nabiya
- Ayyubu alioa, Wake watatu sikia, Wawili wakakimbia, Rahama akabakia
- Riwaya ilopokewa, Watoto walozaliwa, Ni kumi kuongezewa, na wanane kutimia
- Kawaeya wake zake, Pamoja na wana wake, Hawakumuata pweke, Kwa raha na mazowea
- Mkubwa mtoto wake, Kawalika ndugu zake, Harimala jina lake, Kwake akawatukua
- Kawapikia chakula, Ndugu yao Harimala, Haukupita muhula, Balaa zikawangia
- Balaa zikawafika, Kwa msiba ulotuka, Ya ukuta kuanguka, Wanawe wakajifia
- Mali yakataharika, Mno akafilisika, Yali yakipuputuka, Kila siku kupungua
- Ali na mengi majumba, bustani na mashamba, Na wanyama wa kutunga, Wote hawakubakia
- Maradhi yalimshika, Siku nyingi na miaka, Hakuwa akipunguka. Ila kuzidi nabiya
- Maradhi ya kiajabu, Yalompata Ayubu, Hakusaza matibabu, Na wanaojua dawa
- Mabombwe yalikitoka, Na ngozi ikatanika, Mkewe akashutuka, Kamba unani nabiya
- Muili hukushanuka, Na mabombwe hukutoka, Nawe umebadilika, Na wazidi kwendelea
- Hata naona ajabu, Yalonipata muhibu, Ni kazi yake Wahabu, Ilahi yamueleya
- Kamba wewe hufahama, Yalonipata Rahama, Mitihani ya Karima, Nami taisubiria
- Maradhi ya miujiza, Ya ngozi yake kuoza, Wadudu wakitapuza, Muilini kwa nabiya
- Hakuona la sahali, Ugonjwa kauhimili, Mkubwa ulo thaqili, Mola aloqadiria
- Rahama kamuhimili, Kenda nae huko mbali, Nti yenye majabali, Kibanda kamjengea
- Kenda nae taratibu, Kamueka kwa adabu, Hakusikia dharubu, Za mikukuto ya ndia
- Kali chakula hakuna, Wala maji ya kunwa, Ndaa ilipowabana, Rahama hakungojea
- Kateremka mjini, Rahama katumaini, Tapata mwema mwendani, Riziki kumpatia
- Watu walipomuona, Kwa umoya wakanena, Ndoo kwetu wata bwana, Shere wakimtezea
- Rahama hakukubali, Waloyasema rijali, Kaomba Mola Jalali, Amlinde na mabaya
- Ayyubu akamwita, Kamba wewe huniata, Ni gani wenda tafuta, Nambiya nipate juwa
- Kamba wewe mume wangu, Nakuapia kwa Mungu, Sitakutupa bwanangu, Wala sibadili nia
- Kanena na moyo wake, Ni wapi mimi nifike, Kakumbuka mwanamke, Upesi akamwendea
- Mlango akaubisha, Akataka kukopesha, Nikipata tarejesha, Kanena wangu nabiya
- Mwanamke kwa umbeja, Kishipa kikampija, Akanena kwani ngoja, Lilokueta nambiya
- Hukuya nyumbani kwangu, Ila kunipa matungu, Akuone mume wangu, Apate kukuridhia
- Rahama akamjibu, Mwanamke kwa ghadhabu, Nina wangu Ayyubu, Nilopewa na Jaliya
- Mimi sitokukiridhi, Kwani mimi meniudhi, Una kitu chenye hadhi, Ukitaka niatia
- Ali na nyele safira, Rahama zalikin'gara, Mwanamke kwa hasira, Makasi kamuetea
- Kazikata nyee zake, Akampa mwanamke, Kabeba mikate yake, Mumewe kampekea
- Rahama akadhahabu, Akafika kwa Ayubu, Mumewe kataghadhabu, Maneno kimwelezea
- Mumewe likamkera, Kutoa nyee safira, Zilikua nyee bora, Ni ndefu zikin'garia
- Akamwapia Jalali, Mbee za wake rasuli, Si haramu ni halali, Chakula nilokwetea
- Mla wewe mume wangu, Nimeuza nyee zangu, Nimekwapia kwa Mungu, Maovu kukutendea
- Kanena tahakikisha, Na hadi taipitisha, Mboko mia takutwesha, Ninapopata afiya
- Kiwa na afiya yangu, Tachunguza mke wangu, Ili nilipe matungu, Na kufuata sharia
- Rahama akamjibu, Kwa sitaha na adabu, Kwamba uovu Ayubu, Siwezi kukufanyia
- Rahama ayatamke, Amwambie mume wake, Amuombe Mola wake, Mateso kumwondolea
- Kamwambia mke wangu, Naona haya kwa Mungu, Mestarehe na wanangu, Ashara wa thamania
- Tasubiri Mola wangu, Na balaa za matungu, Maadamu moyo wangu, Na ulimi mebakia
- Na ulimi nibakishe, Ilahi nikukumbuke, Dudu usimuoneshe, Ulimini kuningia
- Walitoka kwa muili, Wadudu wote wawili, Tiati wamekabili, Ayyubu changaliya
- Wa kwanza katumbukia, Mtoni akaingia, Mai yakamtukua, Ayyubu kionea
- Wa pili kapanda bara, Kwenye jangwa la sahara, Akawa mnyama bora, Asali yake ni dawa
- Hapohapo Jibrili, Kwa Ayubu kawasili, Yali mikono miwili, Kudhumani metukua
- Metukua kudhumani, Metoka nayo peponi, Amepewa na Manani, Ayyubu kumwetea
- Ayubu katakauli, Kamwambia Jibirili, Menikumbuka Jalali, Kunipa yangu afiya
- Jibirili kamjibu, Menipa Mola Wahabu, Dawa yako kukutibu, Matunda ya jannatia
- Akamwambia simama, Ayyubu tumwa mwema, Kwa amri ya Karima, Inshalla utatulia
- Mimi nimetumwa kwako, Nipoze ugonjwa wako, Piga tini guu lako, La upande wa kulia
- Yakatoka maji moto, Meupe yalo mazito, Akapowa tumwa wetu, Maradhi yakapungua
- Kamwambia Jibirili, Upige nao wa pili, Wa kushoto sikuvuli, Maji yakaitokea
- Mabaridi ya kutosha, Jibrili kamnwesha, Mola akamrejesha, Kama zamani nabiya
- Maradhi yake kapona, Tumwa akawa mzima, Akarudi kama zama, Kwa uwezo wa Jaliya
- Ayyubu akanawiri, Kan'gara kama qamari, Ukarudi utajiri, Wake na watoto pia
- Riwa nyengine hunena, Alibaki na Rahima, Kazaa wangine wana, Na mali yakarejea
- Haya yaliyomsibu, Kumpata Ayyubu, Mitihani ya Wahabu, Nae kaisubiria
- Mola anatufundisha, Kutaka kutuonesha, Maana ukiondeshwa, Sibabaike sikia
- Uyatie akilini, Usubiri kwa Manani, Ndake Mola mitihani, Quruani yatwambia
Mtungaji: Muhammad Abdulla Shatry wa Lamu.
Umeletwa na Saleh Barkey
|