|
|
UTENZI WA KISA CHA NABII YUSUF (A.S.)
Date: 5 September , 2003
- Bisimilahi Kahari, Ya Rabi Mola Jabari, Mmoja uso akhiri, Wala mwanzo kuanzia
- Naanza kwa lako jina, Mola wetu Subuhana, Mtukufu wetu Bwana, Wa pili asotokea
- Twamsalia kaumu, Sote ndugu Isilamu, Mtume Bani Hashimu, Sayyidil Arabia
- Sote Rabi Ya Rahimu, Twamsalia Hashimu, Na tunu nyingi salamu, Twamtakia Nabia
- Nina kisa maarufu, Cha tumwa wake Latifu, Mtume mwema Yusufu, Wao Isirailia
- Mtume wake Wahabu, Yusufu tumwa Habibu, Baba yake Yaakubu, Jinale tawatajia
- Mzazi wake wa pili, Jinale ni kama hili, Aitwa bibi Rahili, Mtukufu wa muruwa
- Yusufu ndie Rasuli, Aloletwa na Jalali, Kwa bani Isiraili, Kaumu isosikia
- Nduguze kuwahisabu, Kwa majina ni taabu, Samahani masahibu, Idadi tawatajia
- Ana kumi wa awali, Kwa baba na mama mbali, Na mdogo ni Rakili, Kwa baba na mama pia
- Walikuwa majabari, Wasiogopa shari, Shujaa walo hodari, Dhiki ikiwafikia
- Alipokwisha kuzawa, Na ndugu wakachukiwa, Wamuhasidi na ngowa, Maradhi yalokomaa
- Sababu yeye kwa kweli, Alikua na jamali, Uzuri wake rasuli, Akipendeza Nabia
- Ni mrembo mtulivu, Mwenye busara mwerevu, Na mwilini hana kovu, Uzuri umezidia
- Yusufu alipokaza, Kwa wazazi kupendeza, Ndugu yakawachukiza, Mabaya kukusudia
- Ndugu walifanya wivu, Na kila la uwerevu, Wamtendee uovu, Kumwangamiza dunia
- Siku moja ya utoto, Amelala hako mato, Yusufu kaota ndoto, Ajabu nawaambia
- Ndoto hiyo ya kioja, Jua na mwezi pamoja, Na nyota kumi na moja, Vyote kumsujudia
- Muda alipogutuka, Hapo alipoamka, Alikimbia haraka, Kwa baba kumwelezea
- Baba kwake ujuzi, Akaifahamu wazi, Ndoto ya jua na mwezi, Na nyota kumi na moya
- Na baba asinyamaze, Ndipo amsisitize, Mwanangu siwaeleze, Nduguzo nakuusia
- Mwanangu stahamili, Siwaambie asili, Yusufu usikubali, Siri ya ndoto zuwia
- Mungu atakukhitari, Akufunze tahariri, Ya ndoto na ya khabari, Waja wasizozijua
- Hapo ndipo auladi, Hao kumi mahasidi, Ikashtadi hasadi, Wakawa na jicho baya
- Hasadi ya jicho ovu, Kwa kumuonea wivu, Ili wamtenze nguvu, Yusufu mmwema nabia
- Ndio waliokutana, Wote ashara vijana, Wasijizuie tena, Moyoni kuvumilia
- Faragha walionana, Wote kushauriana, Mwisho wakasikizana, Maovu kuazimia
- Wakatoka taratibu, Vijana hao kidhabu, Wakenda kwa Yaakubu, Baba yao kumwambia
- Wakafika pasi khofu, Maneno kumuarifu, Kwa kumtaka Yusufu, Ruhusa kumuombea
- Wamtaka ndugu yao, Yusufu mdogo wao, Ili asafiri nao, Huko wanakokwendea
- Hila waliyoisema, Kwa wao mtu mzima, Ni Yusufu kuandama, Kwenda kucheza pamoya
- Hapo baba kashangaa, Na kwanza akakataa, Akajua ni hadaa, Wana walomwelezea
- Maana alitambua, Hila yao kuijua, Yusufu wamchukua, Lakini hatarejea
- Mola aliyoandika, Ni uongo kufutika, Ni lazima kutendeka, Kwani yote yamwelea
- Na baba kwa takilifu, Ya wanawe wapotofu, Moyo ukafanya khofu, Lakini kavumilia
- Ikawa hapana budi, Baba yao kuburudi, Akamtoa fuadi, Yusufu kuwaachia
- Vijana wakaondoka, Na mji wakautoka, Pamoja na muhibbuka, Yusufu tumwa Jalia
- Wakawa wasafarini, Wapotelea porini, Na huku wamachungani, Walisha katika njia
- Wakawasili makini, Kando ya mji njiani, Kwenye mji Dausani, Mji walioingia
- Kufikia kisimani, Mmoja wa ikhiwani, Ambae ni wa mwanzoni, Umri alozidia
- Akalitoa shauri, Kuwapa ndugu khabari, Akasema jambo zuri, Yusufu kumtendea
- Mimi katu sikubali, Tulivyowaza awali, Ni lazima liwe hili, Jengine sitoridhia
- Yusufu tusimuweni, Sote na tumshikeni, Tumtupe kisimani, Haya kwake ni kifaya
- Ikawa budi hawana, Asili kutoshindana, Mkubwa aloyasema, Wadogo wakatikiya
- Hapo tena kwa upesi, Wakamvua libasi, Ambayo ndio khalisi, Yusufu alovalia
- Na kisha wakamshika, Wakamtupa haraka, Kwenye kisima cha nyoka, Kirefu chenye udhia
-
Kwa uwezo wa Rabuka, Hata si robo dakika, Jibrili akashuka, Ajabu ilotokea
- Kufumba na kufumbua, Jibrili keshatua, Yusufu kumuokoa, Kabla hajaumia
- Jibrili kamnyaka, Kabla chini kufika, Taratibu kamuweka, Mahali pema nabiya
- Baada ya kutendeka, Kisa hiki kufanyika, Nduguze wakatoroka, Wakanza kukimbia
- Wenda wakifurahika, Waongea wakicheka, Wakajua kwa hakika, Yusufu keshajifia
- Kumbe wamehadaika, Na bure kuadhirika, Na Yusufu hana shaka, Bukheri kajikalia
- Hata kwa muda saghiri, Wakazuka wasafiri, Wenda mji wa Misiri, Wa katika yao njia
- Ulikua msafara, Ulotimia imara, Wafanyaji biashara, Wasafiri wa ngamia
- Hapo bila ya kungoja, Maji ndio yao haja, Wakamtuma mmoja, Maji kwenda watekea
- Ndoo ikashika papo, Yusufu hapo alipo, Akashika papo hapo, Kamba ilomlekea
- Kamba alipoipata, Akawa yuwaivuta, Na aliyeikamata, Uoga ukamwingia
- Uoga na taharuki, Kwa kamba yake kusaki, Ndoo haitaharuki, Yusufu ameigwia
- Katizama kutafiti, Kujua kilo tiati, Mara ikaja sauti, Kisimani kutokea
- Kwa nguvu zake Kahari, Ndipo tena wasafiri, Hapo pasi kusubiri, Kutafuta kila ndia
- Ikawa ni pata shika, Waume kushughulika, Kamba zimekusanyika, Kisimani zangojea
- Yusufu kwenye kisima, Akatolewa mzima, Ameokoka salama, Kama hakutumbukia
- Basi hapo mtukufu, Mtume mwema Yusufu, Akawa yukwenye safu, Na wasafiri pamoya
- Wakawa wasafarini, Na Yusufu yukundini, Hadi Misiri mjini, Wendako kuwasilia
- Nduguze bila kungoja, Wote kumi kwa umoja, Kutimia yao haja, Walianza kurejea
- Wenda bila wasiwasi, Ndiani wakihadisi, Pamoja nayo kamisi, Walomvua nabiya
- Na mipango walofanya, Ya hila na kudanganya, Ili kwamba kuwaponya, Baba wanapomwambia
- Walingia kwenye kazi, Ya kumkamata mbuzi, Kumchinja kwa ukuzi, Ovu lao kufidia
- Wakaipaka libasi, Yusufu yake kamisi, Kwa hiyo damu najisi, Ya mbuzi walomuua
- Nyumbani wakawasili, Na baba kumkabili, Na la kwanza ni ajali, Ilowakumba na njia
- Wakazidi kutongoa, Na kamisi kuitoa, Ilokua na madoa, Ya damu iloingia
- Uongo walouzuwa, Walosema ndugu hawa, Yusufu ameuawa, Kwa mbwa kumrukia
- Baba kusikia yale, Ya wanawe muda ule, Na huzuni pale pale, Alianza na kulia
- Baba alisema kua, Kwa mwanangu yalokua, Si mbwa alomuua, Wallahi nawaapia
- Ni uongo uso shaka, Wa kanzu kutoraruka, Hata tundu kutoboka, Na mwenyewe akalia
- Yusufu kumdhulumu, Nawaachia Rahimu, Ndie mwenye kuhukumu, Yote Mola yamwelea
- Sasa Yusufu Misiri, Kafika na wasafiri, Maliki akaghairi, Na Yusufu kubakia
- Kampeleka makani, Mtume wa Rahamani, Ambapo ni mnadani, Ili kwamba kunadiwa
- Na kwa bahati nzuri, Akatokea waziri, Kadawaa kwa uzuri, Aliopewa nabiya
- Kamnunua Yusufu, Kwa bei ilo pungufu, Kama mtumwa dhaifu, Asiye na manufaa
- Waziri akamtwaa, Yusufu nae kukaa, Kama mwana wa kuzaa, Mahaba yalomwingia
- Baadae atamke, Kumwambia mke wake, Zulekha mwana mshike, Mola katujaalia
- Waziri bila ya khofu, Akaishi na Yusufu, Asimpe taklifu, Kwa kila lenye udhia
- Waziri akamsifu, Kwa wake uaminifu, Akimpa maalufu, Mali kuyasimamia
- Sasa hapa tufahamu, Umri aliotimu, Ndiyo apewa ilimu, Na hikima zote pia
- Ili kufunzwa khabari, Ya ndoto kuzibashiri, Na akawa ni hodari, Kujua mambo ya ruya
- Hata kwa muda fulani, Hapo Zulekha nyumbani, Ndipo yuwaanza zani, Maovu kuazimia
- Kila siku yamoyoni, Iwapo mili ya ndani, Yusufu kumtamani, Kumuwazia mabaya
- Zulekha yalikithiri, Mapenzi kumuathiri, Na hapo akamghuri, Ibilisi kumwingia
- Kukicha azidi huba, Vitendo vya ukahaba, Ili yake matilaba, Yapate kumnyokea
- Tangu akipenda siri, Na mwisho asisubiri, Mambo yakawa dhahiri, Kwa huba kumtokea
- Na siku hiyo yakini, Waziri hako nyumbani, Mumewe yusafarini, Ndipo aanza udhia
- Na ndiyo siku hakika, Zulekha kufedheheka, Na yake kutotendeka, Aliyoyaazimia
- . Wakati ulipofika, Hiyo siku aloweka, Zulekha akatamka, Na Yusufu kusikia
- Alimwita faraghani, Zulekha kwake chumbani, Amueleze kanuni, Hilo alokusudia
- Yusufu akamwitika, Zulekha bibi labeka, Kwa upesi akatoka, Alikoitwa kungia
- Hata akifika ndani, Akasubiri makini, Asikize jambo gani, Bibi alilomwitia
- Ndipo basi atamke, Huyu baa mwanamke, Amwambie haja yake, Yusufu kumwelezea
- Akatamka machafu, Zulekha bila kukhofu, Yusufu kumuarifu, Na nguvu kumtilia
- Kasema kwa yake dhati, Zulekha muhasharati, Kila njia kutafiti, Amghilibu rasua
- Akazidi ubazazi, Akanena ya upuzi, Kumpa Yusufu wazi, Lake alohitajia
- Moyo wako burudika, Niridhi ninalotaka, Na huna la kukufika, Lolote lenye udhia
- Yusufu hapo rasuli, Kupata hino kauli, Ilimdhuru akili, Na moyo kushitukia
- Moyo ukabadilika, Yusufu kukasirika, Akaanza kumwepuka, Kabisa kutoridhia
- Kasema Yusufu katu, Jambo hilo sithubutu, Sitendi yaso na utu, Ya kumuudhi Jalia
- Basi ndipo hapo hapo, Zulekha pake alipo, Katambua yaliyopo, Yake kutomnyokea
- Akainuka haraka, Ili kutaka mshika, Na Yusufu kaepuka, Zulekha kumkimbia
- Zulekha kwa zake kasi, Asimshike khalisi, Ila kugwia qamisi, Muda alimtapiya
- Alimshika kwa nyuma, Akaivuta kwa hima, Libasi ikamwandama, Qamisi kuipasua
- Ikawa kuchoropoka, Yusufu akaokoka, Na vazi limepasuka, Wakati ajitetea
- Zulekha uchungu wake, Kwa Yusufu amwepike, Kapasua nguo zake, Na makucha kujitia
- Maana ya hiki kisa, Nguo zake kuzitesa, Ilikua ni siasa, Yusufu kumchongea
- Kusudio ni kunena, Arudipo wake bwana, Kumtilia fitina, Yusufu kumzulia
- Ghafula mara waziri, Karudi kwenye safari, Akingia yake dari, Mlangoni kufikia
- Ndipo kuwahi matata, Mwenyewe akayakuta, Kwa kushuhudia vita, Vya mkewe na nabiya
- Moyowe ulishituka, Kwa mambo kubadilika, Si kama alivyotaka, Mbele ya kusafiria
- Moyo mengi ukahisi, Khofu ndani ya nafusi, Akazidi wasi wasi, Kuona yalivyokua
- Waziri kumtangaza, Zulekha kumueleza, Hebu bibi nieleza, Ni vipi umechukiwa
- Niambia tafadhali, Ijapokuwa qalili, Niondowe mushikili, Zulekha bibi nambiya
- Na Zulekha kajibu, Kwa nyingi zake ghadhabu. Kumpa mume jawabu, Kisa kilomfikia
- Bwana unavyoniona, Wala sina la kunena, Ni mambi ajabu sana , Mtu akiyasikya
- Akaanza kwa mpango, Zulekha wake uongo, Kumtakia kifungo, Yusufu pasi na njia
- Alimwambia mumewe, Yalonikumba ujuwe, Yote dhamana ni wewe, Bwana ulonitakia
- Nimetendewa vituko, Mume wangu nawe huko, Na Yusufu mtu wako, Huyo uloniletea
- Ni jambo la kipumbavu, La kunishika kwa nguvu, Anifanye tendo ovu, Nami nikakatalia
- Tena akanisumbuwa, Ni lazima lake kuwa, Nguo zangu kupasuwa, Kutaka nigeukia
- Na mara bila ajizi, Kijana kasema wazi, Mbele yao kubarizi, Na wote wakasikia
- Kwa nguvu zake Karima, Mola mwingi wa rehema, Mwana mchanga kasema, Bila khofu kumwingia
- Alinena hivi sasa, Sote tufanye siasa, Tutamjua mkosa, Ni yupi alokosea
- Tuliyopo hapa sisi, Tupeleleze tukisi, Tuitazame qamisi, Kwa ilivyonyanyuliwa
- Upande ulopasuka, Nguo hio kunyanyuka, Tutamjua hakika, Vita alotangulia
- Na qamisi ndio ile, Nyanyuko likwa mbele, Hapo hapana kelele, Yusufu amekosea
- Au tukiitazama, Imepasuka kwa nyuma, Zulekha ana lawama, Na ndie mwenye khatia
- Kijana alipokoma, Mwana mchanga kusema, Ikawa ni rai njema, Ushahidi alotoa
- Hata walipochungua, Qamisi kuangaliwa, Nyuma imepasuliwa, Wote kuishuhudia
- Basi kwa hichi kiwango, Tushaujua mpango, Zulekha ndie muongo, Yusufu kumzulia
- Mwishowe kimtangaza, Wanawake kueleza, Zulekha ni miujiza, Kwa yeye kutenda haya
- Kwani hawajaamini, Banati hao yakini, Kujua yuhali gani, Uzuri wake nabiya
- Khalafu wakatamka, Banati wakamtaka, Ili Yusufu kufika, Wapate mshuhudia
- Hapo Zulekha mwenyewe, Akasikia mwishowe, Kwa kumsema wenziwe, Khabari kumtokea
- Ndipo ghera kumshika, Kwake akawaalika, Na vyakula akaweka, Wote wakahudhuria
- Akapitisha sharuti, Mbele yao mabanati, Wakayakubali dhati, Zulekha alowambia
- Yusufu alipopita, Banati wakamkuta, Kwa visu wakajikata, Bila ya kufahamia
- Wote kodo macho mbele, Ajabu ya maumbile, Wakakatika vidole, Kwa urembo wa nabiya
- Ni hapo kujulikana, Hapo walipomuona, Kuwa ni mzuri sana, Yusufu wameridhia
- Mwanena lawama kwangu, Kwa hasira na uchungu, Jitizameni wenzangu, Nanyi yalowafikia
- Nanyi mumeadhirika, Kushinda yalonifika, Na vidole kukatika, Bila ya kuzingatia
- Wakazidi kina mama, Waeleza kua kama, Zulekha hana lawama, Yusufu katimilia
- Basi mwisho akapuza, Kwa hasira kumkaza, Zulekha luwaeleza, Wenziwe kuwaambia
- Yakuwa asipoweza, Yusufu kunisikiza, Nyumba yake ni gereza, Lazima ataingia
- Namweleza ya muanga, Yangu anapoyapinga, Hakika nitamfunga, Kiapo namuapia
- Kisha tena awambiye, Hao mabibi wenziye, Na nyinyi semeni naye, Huenda akasikia
- Zulekha kumpa nguvu, Kwa alosema maovu, Wakafanya uerevu, Tumwa kumkazania
- Ndipo wakamuarifu, Kwa nguvu na takilifu, Wakamwmbia Yusufu, Ya bibi yako ridhia
- Ikawa asitamke, Yusufu asiyashike, Maneno ya wanawake, Hayo waliyomwambia
- Kwa hayo aloambiwa, Akaona hana dawa, Ila ya kuomba dua, Kwa Mola wake Jalia
- Na Yusufu dua yake, Ni machafu yamwepuke, Kalingana Mola wake, Hapo akaombolea
- Ya Rabi Mola ujuwe, Yashanishinda mwenyewe, Uiwezae ni Wewe, Shida yangu yakwelea
- Nihifadhi Bwana Mola, Kwani sina tena hila, Kwangu kheri kwenda jela, Kuliko huno udhia
- Mungu aliyakubali, Maombi yake rasuli, Kwa mujibu wa kauli, Ya dua yake nabiya
- Akamkinga Jalali, Na wa Zulekha muhali, Rabi akatakabali, Na gerezani kungia
- Ikawa si muda tena, Zulekha kungoja sana, Ndipo aanze fitina, Uongo kuuchochea
- Maana alipojuwa, Atakalo halikuwa, Tena ameadhiriwa, Khabari zimeenea
- Akamwambia waziri, Mume wake kasisiri, Bwana nnayo khabari, Tafadhali nisikiya
- Nakuomba kwa hisani, Yusufu mtie ndani, Mpeleke gerezani, Kwani amenikosea
- Mji wote ni sherehe, Yusufu kunifedhehe, Katu usimsamehe, Idhara imeenea
- Na kwa hapo ndipo mume, Asijibu asiseme, Ya mkewe aandame, Bila ya kufikiria
- Waziri akawa radhi, Ili bibi amridhi, Mkewe asimuudhi, Ijapo ni jambo baya
- Kamtia kifungoni, Yusufu korokoroni, Hali hako makosani, Badili kumuonea
- Yusufu akenda ndani, Na wawili ithinani, Walokua khatiani, Kwa yao walokosea
- Walifanya ukhalifu, Mfalume kaarifu, Wafungwe wawe madufu, Na adabu kuwatia
- Kwa kutokea ubishi, Kwa ndoto za ushawishi, Waloota watumishi, Jela walikofungiwa
- Na wakenda kwa Yusufu, Kwa shaka na takilifu, Kwani ashawaarifu, Kua ndoto zamwelea
- Saiki ndie wa kwanza, Aliyejitanguliza, Ndoto yake kueleza, Yusufu kuisikia
- Akasema jana kua, Nimeota kuchukua, Sinia iliyokua, Na vinywaji vimetiwa
- Na mwendo wangu wa shime, Njiani nisisimame, Nenda kwake mfalume, Vinywaji kumwandalia
- Yusufu akamjibu, Kama ilivyo wajibu, Kumpa njema jawabu, Ndoto kumfasiria
- Saiki akajibiwa, Ndoto ikaaguliwa, Kifungoni kutolewa, Tumwa kumbashiria
- Akanena langu shika, Wala usifanye shaka, Wewe jela utatoka, Kazi yako kurejea
- Mara hapo akaruka, Mpishi akatamka, Ili hakika kutaka, Kumjaribu nabiya
- Asifikiri ninini, Yakamwingia kichwani, Akaanza ubishani, Kujifanya yamwelea
- Na hapo bila kusita, Ndoto yake kufuata, Kusema aliyoota, Yote yalomfikia
- Yusufu kabwaga shingo, Kuusikiza uongo, Upangwavyo kwa mpango, Bila ya kuona haya
- Ewe nabii wa Mungu, Yusufu mkubwa wangu, Nimeota ndoto yangu, Nimejitweka sinia
- . Nimejitweka kichwani, Na mikate imo ndani, Naipeleka nyumbani, Kwa mkuu wa raiya
- Nilipokuwa njiani, Kaja ndege wa angani, Kaudona siniyani, Mkate kauchukua
- Mkate akaudona, Kabaki nimedangana, Ndipo Yusufu kanena, Ndoto kumfumbulia
- Fasiri ya ndoto yako, Haina salama kwako, Utakatwa kichwa chako, Lazima utauwawa
- Mpishi akaduwaa, Akawa ataataa, Ikawa hana tamaa, Kwa alivyobashiriwa
- Akamwambia mwalimu, Yusufu bwana fahamu, Hayo nilotakalamu, Ni dhihaka nakwambia
- Yusufu ndipo kusema, Ujuwe huna salama, Utauliwa lazima, Kama nilokwelezea
- Siku nyingi zisitimu, Kwa rehema za Karimu, Mungu akamrehemu, Saiki kafunguliwa
- Mwenziwe yule laimu, Aliyengiwa na hamu, Ikatolewa hukumu, Akenda akauwawa
- Na siku ya kuachana, Na Yusufu kuagana, Hapo Yusufu kanena, Saiki kumwashiria
- Akamba leo watoka, Kwako nnalolitaka, Siwache kunikumbuka, Yakumbuke mazoweya
- Ewe wangu muhisani, Sinisahau mwendani, Na kunitaja nyumbani, Kwake mfalume pia
- Saiki kenda kuanza, Kazi yake kufanyiza, Shetani kamsauza, Kutekeleza wasia
- Ikatukia azizi, Maliki kwenye malazi, Alipitiwa na njozi, Mno kaigutulia
- Muda alipogutuka, Malazini kuamka, Akangiwa na wahaka, Wasiwasi kumwingia
- Akawataka maliki, Watumiao falaki, Watizame kisa hiki, Cha ndoto ilomjia
- Kawaita makuhani, Wakuu wanavyuoni, Wote walio mjini, Kuja kumbashiria
- Nimewaita wajuzi, Muifanye yangu kazi, Ya ndoto munipe wazi, Jawabu ilo na njia
- Bidii munvyoweza, Munipe ya muangaza, Kwani yamenishangaza, Sasa nawatamkia
- Nimeota waungwana, Usingizini kuona, N'gombe walodhofu sana, Saba katika ruwiya
- Huwala walionona, N'gombe sabaa mabwana, Kisha nikaota tena, Baada ya mambo haya
- Nikayaota mashuke, Yaso kitu ndani yake, Na mengine yalo pweke, Sabaa yaliyojaa
- Ikabidi makuhani, Kutazama vitabuni, Kuiona hawaoni, Akili zimewashia
- Kushindwa kwa watu hao, Maliki kazidi mwao, Akawa hana makao, Wasiwasi kuzidia
- Saiki akagutuka, Ghafula kamkumbuka, Yusufu akatamka, Maliki kumwelezea
- Saiki katakalamu, Kumwambia muadhamu, Mimi bwana nafahamu, Wakati nilipokuwa
- Nimefungwa gerezani, Nilimkuta mwendani, Mfadhila na hisani, Ajuaye mambo haya
- Na Yusufu kakariri, Bila ya kuyafikiri, Ndoto akaibashiri, Alivyombashiria
- Ni miaka ya neema, Sabaa ya wakulima, Watavuna vuno jema, Chakula cha kuzidia
- Ikisha miaka hiyo, Yenye shibe iso choyo, Itakuja mengineyo, Saba ya watu kulia
- Kilio kiso nyamaa, Kwa kungiliwa na njaa, Iwe ni kuu balaa, Chakula kuwashilia
- Kupata hayo Saiki, Mambo yakamuafiki, Akamwambia rafiki, Yusufu tuonye njia
- Yusufu yake kalima, Kampa jawabu njema, Nawalime wakulima, Mavuno yakiwadia
- Mupatafute mahala, Muvitie kwenye ghala, Shida ikija ghafula, Mupate cha kutumia
- Basi hapo ikabidi, Bwana Saiki karudi, Na kamili ushahidi, Wa kwenda kuwaridhia
- Hata akifika ndani, Kwa mfalume nyumbani, Akaeleza makini, Yote yaliyotukia
- Alimpa tafsiri, Ya ndoto yake dhahiri, Mambo yatakayojiri, Ambayo yatatokea
- Papo kastaajabu, Mfalume kwa jawabu, Mno kaona ajabu, Kwa ujuzi wa nabiya
- Na pale pale kwa hamu, Maliki katakalamu, Saiki kumlazimu, Upesi jela rejea
- Mwite Yusufu haraka, Umwambie ukifika, Mfalume akutaka, Haraka akungojea
- Kufika kwenye kizimba, Asingoje akamwamba, Yusufu bwana aomba, Wende kwake akwambia
- Kukangiya walakini, Kuwa haiwezekani, La kutoka gerezani, Yusufu kakatalia
- Akasema kumjuza, Saiki kumueleza, Mimi katika gereza, Sitaondoka sikia
- Salamu zangu zifishe, Mfalume mjulishe, Mpaka athubutishe, Yakua sikukosea
- Na kisha kwa hiki kisa, Awajuze watu khasa, Yakuwa sina makosa, Zulekha ndie mbaya
- Awaite vilevile, Banati wa siku ile, Walojikata vidole, Na Zulekha wote pia
- Ni kua apeleleze, Maliki awaulize, Wanawake wamweleze, Ni yupi alokosea
- Saiki akaushika, Ujumbe kaupeleka, Yote aliyotamka, Yusufu kumwaridhia
- Alipokwisha ambiwa, Maliki kuelezewa, Maneno yakamtuwa, Pingamizi kutotia
- Ndipo hapo apeleke, Mfalume mtu wake, Wakaitwe wanawake, Na wote wakafika
- Banati wakiwasili, Maliki kawakabili, Kisha akawasaili, Mfalume kuwambia
- Musiogope muhali, Baina hawa wawili, Mwenye makosa kwa kweli, Mwaweza kunitajia
- Ni Zulekha na Yusufu, Mkosa muniarifu, Yupi alo mpotofu, Huyo alo na hatia
- Wanawake wakasema, Kwa upole na heshima, Bwana mwenye na lawama, Zulekha ndie mbaya
- Na Zulekha baadae, Akiulizwa na yeye, Asili asikatae, Akajibu ya sharia
- Yakua wangu ulimi, Leo uongo sisemi, Mwenye makosa ni mimi, Hakika nakubalia
- Mfalume ufahamu, Yusufu simlaumu, Bali niemedhulumu, Na tena kumzulia
- Zulekha akalingana, Ya Ilahi Subhana, Nakubali mimi Bwana, Yakua nimekosea
- Na makosa kua kwangu, Nakuomba Bwana Mungu, Nisamehe dhambi zangu, Ya Rabbi Mola Jalia
- Yote maneno ya watu, Yusufu imethubutu, Si mkosa huyu mtu, Hakika imetokea
- Imethubutu Yusufu, Kua mtu mtukufu, Sababu hana machafu, Maovu kujizuiya
- Zulekha alitamka, Kua alighilibika, Ndie aliemtaka, Sasa amekubalia
- Tushafahamu Yusufu, Kwamba hana ukhalifu, Zulekha ndie mchafu, Kosa lilomwelemea
- Alipopata ukweli, Maliki kwa jambo hili, Ikawa yastahili, Yusufu kwenda tolewa
- Ndipo Saiki atoka, Kwa furaha na kucheka, Kwa Yusufu akifika, Akawa atmwambia
- Itunze yako nafusi, Usiwe na wasiwasi, Zulekha ndie mkosi, Makosa ameridhia
- Wameitwa watu tele, Kaulizwa mambo yale, Akajibu yale yale, Kama yalivyotokea
- Yusufu iliyobaki, Sasa twende kwa Maliki, Usiwe mwenye hamaki, Kufikiri mambo haya
- Yusufu akaitika, Gerezani akatoka, Kwa Maliki akafika, Vizuri akapokewa
- Maliki akasimama, Mtukufu wa heshima, Akampa taadhima, Sitaha kumfanyia
- Maliki kamkubali, Kuwa ni mtu wa kweli, Tena ni mwenye akili, Yusufu kajaaliwa
- Yusufu akataraji, Awe waziri wa mji, Awe ni mtazamaji, Neema ikitokea
- Mfalme karidhia, Na kumsafia nia, Akamba nakuachia, Fanya litakalofaa
- Yusufu asighairi, Wala asitaakhiri, Akashika uwaziri, Cheo hicho kupokea
- Ndipo yaanza neema, Chakula mji mzima, Furaha kwa wakulima, Hadi waliobakia
- Wala vyema wakishiba, Na vyengine kwa akiba, Muda wa miaka saba, Njaa kuwaepukia
- . Kwa furaha wakakaa, Muda wa myaka sabaa, Hapo ikangia njaa, Raha kuwapungukia
- Lakini wao hakika, Japo njaa imefika, Waliishi pasi shaka, Wakila bila udhia
- Ila ilizidi dhiki, Kwa miji iliyobaki, Kwa majirani rafiki, Njaa ikawafikia
- Ndipo ilipomsibu, Njaa kuu Yaakubu, Kumfikia taabu, Ya wanawe wote pia
- Yaakubu hapo basi, Akazidi wasiwasi, Wakati alipohisi, Chakula kimeishia
- Na baba yeye mwenyewe, Akawajuza wanawe, Kuwaambia wajuwe, Njaa ile ilongia
- Ili kwamba wasafiri, Wende mji wa Misiri, Na wana wakakhiari, Baba kumkubalia
- Wakenda wana ashara, Ila wa hidaashara, Hakua na msafara, Nyumbani akabakia
- Aliebaki nyumbani, Kutokua safarini, Ni huyu Binyamini, Ndie aliesalia
- Mwana huyu mtukufu, Na tena nawaarifu, Ni mdogo wa Yusufu, Kwa baba na mama pia
- Basi kumi walobaki, Wakenda na yao dhiki, Kuitafuta riziki, Misiri wakafikia
- Wakawasili vijana, Hata walipopambana, Yusufu akawaona, Kwake walipoingia
- Walipofika ikawa, Yusufu kuwatambuwa, Na wao kutomjuwa, Yakuwa ni ndugu moya
- Yusufu akafuliza, Na wao kuzungumza, Na hali kuwauliza, Na wao kumwelezea
- Yusufu yakamtosha, Nduguze walompasha, Nae akayakinisha, Ni nduguze wote pia
- Khalafu mwisho akaze, Yusufu awaeleze, Awaambie nduguze, Hao walomjilia
- Katamka akanena, Enyi ashara vijana, Munaporejea tena, Hapa mukifikilia
- Ndugu yenu muje nae, Aandamane na nyie, Ili hapa afikie, Nipate mshuhudia
- Hilo hakika nawapa, Nisipomuona hapa, Na chakula sitawapa, Munachokihitajia
- Wala musinifikie, Kwangu musikaribie, Huko huko mubakie, Sitaki washuhudia
- Ikangia tafauti, La kusema hawapati, Ikawa kwao sharuti, Ndugu hao kuregea
- Wakapakiliwa tweka, Za chakula walotaka, Ili wapate ondoka, Makwao kurejelea
- Walipowasili kwao, Kufikia ndugu hao, Wakampa baba yao, Khabari ilotukia
- Walipofungua tweka, Nyoyo ziliwapasuka, Kwa furaha kuwafika, Ya mali kuregezewa
- Hata chakula kikisha, Ndiyo siku ikatisha, Wana kujitayarisha, Safari kuandalia
- Baba wakamshauri, Ili wao kwa uzuri, Kwa huyo mwana saghiri, Ili wende nae pia
- Na watoto wakasema, Kumpa baba kalima, Baba hakyna hekima, Tutakayokufanyia
- Utupe Binyamini, Awe nasi safarini, Usiwaze asilani, Salama atarejea
- Na baba yakamtanza, Halijui la kufanza, Akakumbuka la kwanza, La Yusufu kupotea
- Baba alifanya khofu, Akidhania machafu, Yalomkumba Yusufu, Na huyu atatendewa
- Khalafu akakariri, Kuwapa wana khabari, Akasema mwafikiri, Kua nitakubalia
- Na wana yao kauli, Kumtoa mushikili, Wakasema ilo kweli, Baba yao kumwambia
- Hakika amtakae, Ili sisi twende nae, Ni waziri asemae, Ndiyo alotwelezea
- Kwa nyingi taabu, Akanena Yaakubu, Wanawe akawajibu, Kwa hilo sitaridhia
- Hendi hadi ushahidi, Munipe kweli ahadi, Yake Ilahi Wadudi, Yakuwa atarejea
- Na ijapo ni ajali, Jambo lisokua hili, Siwalaumu asili, Apendalo Mungu huwa
- Na wana wote walipo, Ikawa kula kiapo, Wakasema papo hapo, Kwa Mungu kushahidia
- Wallahi twenda na yeye, Khofu isikuingiye, Baba tutakuja nae, Mwanayo atarejea
- Baba kwa hino ahadi, Ya ashara auladi, Moyowe uliburudi, Imani ikamwingia
- Basi baba akaridhi, Moyo wake kuwa radhi, Mwanawe kuwakabidhi, Wanawe walosalia
- Ndipo baba amtake, Binyamini afike, Na alipokuja kwake, Mara kamkumbatia
- Yaakubu akanena, Na mwanawe kuagana, Kwaheri ya kuonana, Na kheri nakutakia
- Safiri Binyamini, Kwa salama salmini, Na urudi mara thani, Kwa umri na afiya
- Hapo muda ukajiri, Hapana tena shauri, Vijana wakasafiri, Hidaashara pamoya
- Wakenda mara ya pili, Vijana kama awali, Kwa Yusufu kuwasili, Misiri wakafikia
- Kuwasili ikhiwani, Yusufu kwake nyumbani, Kwapanga ithineni, Wawili chumba kimoya
- Yusufu yake akili, Kwatenga mbalimbali, Ndugu wawili wawili, Mdogo akasalia
- Ndipo basi masikini, Kabaki pweke mwendani, Yaani Binyamini, Hapo kaanza kulia
- Mambo yakamtatiza, Yusufu kumshangaza, Kisha akamuuliza, Mdogowe kumwambia
- Nieleze kwa makini, Likulizalo ni nini, Walizwa na jambo gani, Nambia nipate juwa
- Binyamini kasema, Kwa sauti ya huruma, Kumpa yake kalima, Yusufu kumwadithia
- Lau yuhai Yusufu, Leo mimi pasi khofu, Singepata takilifu, Kwa haya kunifikia
- Yusufu nae kajibu, Wasemaje mahabubu, Leo ni wako sahibu, Binyamini sikia
- Yusufu na ndugu yake, Wakangia chumba pweke, Na Yusufu atamke, Siri hapo kuitoa
- Kampa la burudiko, Biyamini tamko, Mimi ndie ndugu yako, Yusufu alopotea
- Na muda ulipofika, Ndugu chakula kutaka, Ili wapate ondoka, Kwa haraka kurejea
- Wote wakamiminiwa, Magunia kujaziwa, Bila ya kulia ngowa, Na Binyamini pia
- Lakini gunia lake, La Yusufu ndugu yake, Yaani mdogo wake, Huyo aliyeletewa
- Humo mwake guniani, Kwa huyo Binyamini, Kaificha pishi ndani, Yusufu kumtilia
- Ndipo ndugu wakafisha, Safari kutayarisha, Mizigo kuipandisha, Kuwabebesha ngamia
- Na mara kwa muda huo, Kuepuka ndugu hao, Katika safari yao, Wanjiani warejea
- Askari nae basi, Akakimbia upesi, Akawakuta khalisi, Bado wangali na njia
- Muda alipowapata, Asikari, kuwakuta, Kwa kelele kawaita, Mkono kuwapungia
- Askari kanena, Kuwajulisha vijana, Nasema kwenu mabwana, Jambo nilowaitia
- Nimeambiwa nifike, Na Maliki niwashike, Imeibwa pishi yake, Ya chakula kupimia
- Na vijana wakafika, Kwa khofu kutetemeka, Khalafu wakatamka, Askari kumwambia
- Twaapa kwa Mwenye enzi, Twakupa ilyo wazi, Sisi bwana sio wezi, Pishi tulowaibia
- Yusufu kasisitiza, Mwishowe kuwauliza, Ni nini yake majaza, Pishi aliyeitwaa
- Walipoulizwa hayo, Wakamjibu kwa payo, Jaza yake mtu huyo, Adhabu kumfikiya
- Ikatazamwa vizuri, Kwa ndugu hao kabiri, Na ikawa asikari, Pishi hakuivumbuwa
- Basi kawa imara, Askari kuchakura, Hadi vijana ashara, Kwenye yao magunia
- Askari kakazana, Hata wa kumi kijana, Na pia hakuiona, Pishi kuishuhudia
- Kuja kutizama nadani, Kwa huyo Binyamini, Humo mwake guniani, Pishi hio ikagwiwa
- Kufika wakatongowa, Uongo wakauzuwa, Kwama huyu hana dawa, Si mwanzo kufanya haya
- Na huyo ndugu wa mbele, Alimwivi vile vile, Hata tembe ya mchele, Akiona huitwaa
- Yusufu katabasamu, Moyoni katakalamu, Ni uovu ulotimu, Machoni kunizulia
- Bwana ufanye imani, Twakuomba kwa hisani, Muwache Binyamini, Tafadhali twakwambia
- Twaomba kwako Maliki, Na sote kutuafiki, Mmoja wetu kubaki, Badili kumfidia
- Yusufu yake kauli, La ndugu asikubali, Kushika mtu badali, Hilo hakukubalia
- Hapo akazidi chuki, Ndugu mkubwa hataki, Kanena mimi sitoki, Misri nitabakia
- Kuwasili kwa mzazi, Na mema maamkuzi, Kisha lao simulizi, Baba kumuhadithia
- Siri hawakuiziba, Wakampa wazi baba, Baba mwanao kaiba, Nasi kumshuhudia
- Na baba yake kauli, Kajibu hili si kweli, Hilo ni yenu nakili, Ni hila mwaniletea
- Kwa yote haya madhara, Inshalla niko imara, Mungu tanipa subira, Njema ya kuvumilia
- Kisa hiki kumfika, Ndipo alipokumbuka, Yale ya kwanza mashaka, Ya Yusufu kupotea
- Akanena kwa uchungu, Rudini enyi wanangu, Kwenye aridhi ya Mungu, Musiogope udhia
- Nendeni pasi nakhofu, Musijali takilifu, Mumtafute Yusufu, Na Binyamini pamoya
- Wakafika kwa heshima, Kwake Yusufu salama, Na wote wakainama, Hishima kumfanyia
- Khalafu kisha waanze, Wakatamka nduguze, Yusufu wamueleze, Wanalolihitajia
- Ewe mwingi wa fadhila, Tuna haja ya chakula, Sisi na yetu aila, Tusije kufa na njaa
- Nasi hatuna thamani, Wala kitu mkononi, Ila ni bidhaa duni, Isiyo na manufaa
- Yusufu kasikitika, Wazazi kawakumbuka, Machozi yakamtoka, Hawezi kuvumilia
- Sasa ndio wapambana, Yusufu na hao wana, Maswali kujibizana, Siri Yusufu atoa
- Yote mambo ya zamani, Ya kutupwa kisimani, Ndipo hapo yabaini, Yusufu alotendewa
- Yusufu awaambie, Ni nani wapili yeye, Alofarikana nae, Baba alompotea
- Ndugu wakamuarifu, Wakasema bila khofu, Jina lake ni Yusufu, Mwana aloangamia
- Na ndugu wakatongowa, Yusufu akajibiwa, Mwana huyo kauawa, Na mbwa mwitu kuliwa
- Yusufu akatamka, Kweli mbwa kamshika, Au nyinyi kwa hakika, Kisa mumemtendea
- Yusufu kasema tena, Na ndugu kujibishana, Hamukufanya khiana, Kisimani kumtia
- Na papo wakajibiwa, Na Yusufu kuambiwa, Jee aliemuuwa, Ni nyinyi wenu mmoya
- Ndugu nao kwa upesi, Wakanena kua sisi, Tutauwaje nafusi, Bila kisa kutokea
- Basi Yusufu kakaza, Kuzidi kuwaeleza, Yote waloyafanyiza, Mpaka kuishilia
- Na hiyo si dhambi katu, Kwa huyo mbwa wa mwitu, Hiyo ni dhambi ya watu, Yenu mulokusudia
- Ajabu yao ni kua, Vipi Yusufu kujua, Ni kama aliekua, Yuko na wao pamoya
- Baadae ndipo tena, Mmoja wao vijana, Alama akaiona, Yusufu kamtambua
- Na hapo kwa nyingi khofu, Kanena kwa takilifu, Wewe kwani ni Yusufu, Bwana hebu niambia
- Yusufu nae haraka, Na mara akatamka, Mimi ndie pasi shaka, Yusufu alopotea
- Ndie Yusufu wenzangu, Mimi mtume wa Mungu, Na huyu ni ndugu yangu, Aliyeniandamia
- Akazidi kukariri, Kuwapa ndugu khabari, Hakika ukisubiri, Mja kwa kila udhia
- Nao ndugu wakaanza, Yusufu wakamweleza, Mola amekutukuza, Kwa dhiki kuvumilia
- Kwa hili Yusufu kuwa, Mungu akujaze sawa, Kwa uliyoyachukuwa, Mambo tulokufanyia
- Yusufu nae kasema, Kuwajibu ndugu vyema, Leo hakuna lawama, Kwenu nyinyi ndugu pia
- Na mola wetu Karimu, Tawasamehe Rahimu, Ndie mwenye kurehemu, Viumbe wake Jalia
- Kisha nae atamke, Yusufu kwa ndugu zake, Qamisi muipeleke, Nawatuma nyote pia
- Twaeni yangu libasi, Tena haraka upesi, Mufikapo na qamisi, Kwa baba mukiingia
- Musimpe mkononi, Nitakavyo ikhiwani, Mumbwagie usoni, Macho yatamrudia
- Na khalafu baadae, Murudi pamoja nae, Nyote kwangu mugurie, Pasi mtu kubakia
- Muje na wote jamaa, Na wala kutokataa, Tuje pamoja kukaa, Hapa kwangu kuguria
- Walipotoka nyumbani, Kwa Yusufu ikhiwani, Wakali bado ndiani, Muda wakisafiria
- Yaakubu mtukufu, Akasikia harufu, Ya qamisi ya Yusufu, Puani kumuingia
- Ilokwenda kwa upepo, Muda huo hapo hapo, Kwa Yaakubu alipo, Harufu kumfikia
- Yaakubu kabashiri, Kwa walokua hadhiri, Akawapasha khabari, Akasema kuwambiya
- Naisikia harufu, Ya mwanangu maarufu, Al-waladi Yusufu, Fuadi alopotea
- . Jamaa wakamjibu, Kumweleza Yaakubu, Yuko wapi aloghibu, Alokufa kurejea
- Mara kwa chache dakika, Saa kutomalizika, Hapo wana wakafika, Kwa shangwe wakatokea
- Na mbele ya kujilisi, Ili wapate marisi, Waliibwaga qamisi,Usoni kumtupia
- Akarejea kuona, Kama zama za ujana, Na kisha ndipo kanena, Yaakubu kutongowa
- Kujuza wale mabwana, Mbele ya kuja vijana, Kwa harufu kushindana, Wakati wakiongea
- Yaakubu katongowa, Mambo nnayoelewa, Najuwa musoyajuwa, Mimi sikuwaambia
- Kwa kufupisha maneno, Mambo yakawa manono, Furaha iso mfano, Kwa baba na wana pia
- Na hapo baba na wana, Wote kukumbatiana, Dhambi kusameheana, Wana waloyakosea
- Ikawa baba kuhama, Wana pamoja na mama, Wakawasili salama, Kwa Yusufu kuguria
- Kawakaribisha vyema, Aila ilomwandama, Kwa adabu na heshima, Yusufu kuwapokea
- Furaha ikawa kuu, Wana hadi wajukuu, Si shangwe mambo makuu, Furaha kuwazidia
- Kisha ndipo kawaweka, Wazazi wake katika, Kiti chenye mamlaka, Heshima kuwafanyia
- Na mara baba na mama, Na wana wakaandama, Kwa furaha kuinama, Wakasujudu pamoya
- Walipokwisha pumuka, Kwa furaha na kucheka, Wakashukuru Rabuka, Kumhimidi Jalia
- Na muda huo haraka, Yusufu papo kafika, Ndoto yake kakumbuka,Ya zama zilopitia
- Akamweleza mzazi, Babake kumpa wazi, Huno ndio uwaguzi, Wa ndoto nilokwambia
- Alizidi akinena, Wa ndoto niloiona, Katika wangu ujana, Leo yatufunukia
- Siku leo imefisha, Ya Mola kutonyesha, Haki amehakikisha, Ilahi Pweke Mmoya
- Tena Ilahi Karima, Kanitendea na wema, Kuniokoa salama, Jela kunifungulia
- Na nyinyi akawaleta, Niliko kunifuata, Mukaja mukanikuta, Kwa salama na afiya
- Kwa uwezo wa Rabbana, Kawaleta nyinyi tena, Tukaja tukaonana, Kujumuika pamoya
- Na mwisho wake khalafu, Mtume mwema Yusufu, Kamshukuru Latifu, Huku akiombolea
- Ewe Bwana Mtukufu, Uliyenipa sharafu, Ufalme uso khofu, Bwana Ulotimilia
- Ukanipa na uweza, Ndoto za kimiujiza, Uwaguzi kunifunza, Tafsiri kuzijua
- Ewe Mwenye enzi Mungu, Ya Ilahi Mola wangu, Uloumba ulimwengu, Na ardhi zote pia
- Ya ilahi niongowa, Nipite hali ya kuwa, Kila haki kuijuwa, Na kwako kunyenyekea
- Njia njema nionyeshe, Na wema nilahikishe, Yaani nikutanishe, Na wetu wema Jalia
- Na hapo akamaliza, Yusufu aloeleza, Pasi moja kulisaza, Shukurani kutumia
- Kwa hivyo wote wendani, Wakakutana yakini, Kama zama za zamani, Siku zilizopitia
- Kufikia kwa Yusufu, Aila ilo tukufu, Wakaishi bila khofu, Kusahau yote pia
- Kwa furaha wakadumu, Kwenye makao timamu, Nyoyo zikatabasamu, Hadi kuaga dunia
- Kwa kufupisha niseme, Yusufu kawa mtume, Kapata na ufalume, Mola kumjaalia
- Basi hapa waungwana, Yatosha niloyanena, Ya zaidi tena sina, Samahani ila haya
- Sasa ndio nasimama, Kisa chetu kimekoma, Na dua kwake Karima, Naanza kuombolea
- Ni wewe Mola Mmoja, Muumba wa sote waja, Itimize yetu haja, Ilahi watusikia
- Twakuomba Ya Manani, Isilamu ikhiwani, Tuongoze kwenye dini, Imani kutuzidia
- Tupe nguvu za nafusi, Tumshinde Ibilisi, Asiipate nafasi, Njia mbovu kututia
- Twakuomba Ya Wadudi, Machafu yawe baidi, Na waovu mahasidi, Yao kutowanyokea
- Ya Ilahi Ya Karimu, Tupe akili timamu, Ya dini na ya ilimu, Tushike bila udhiya
- Tulinde tuwe wekevu, Tuyaepuke maovu, Na nyoyo ziwe na nguvu, Machafu kuyakimbia
- Tuepushie na dhara, Kwa dini tuwe imara, Twaiomba na sitara, Ya akhera na dunia
- Dua ifike ulipo, Na kabuli ije papo, Utupe na njema pepo, Hiyo ulotwandalia
- Amina Rabi amina, Amina Mola amina, Utukabalie Bwana, Kwa baraka za nabiya
- Na hapa ninamsifu, Mola wetu Mtukufu, Mkubwa Mtakatifu, Taala Rabi Jaliya
- Na mtume Muhammadi, Mjumbe wake Wadudi, Kila siku turadidi, Swala na salamu pia
- Bwana Saidi Karama, Mungu takwegesha pema, Akupe na nyingi hima, Malenga usiye doa
Mtungaji : Said Karama - Lamu
Mletaji: Saleh Barkey
|