.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Naliya!

Related links

Naliya!

  1. L-akhi nakuja kwako, Kukupa niliyo nayo
    Ni mbali nitokeyako, Nakuja kwa haja hiyo
    Nakuja kwa sikitiko, Na tena nna kiliyo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  2. Naliya nasikitika, Kuninyima harusiyo
    Naliya nahuzunika, Sijuwi niyasemayo
    Naliya nikikumbuka, Kunikhasimu kakeyo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  3. Naililiya suhuba, Nzuri tuliyonayo
    Naliya hipiga toba, Hiyakumbuka mamboyo
    Naliya hii dharuba, Ni kubwa unipigayo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  4. Naliya sikukudhani, Waweza kufanya hayo
    Naliya nimebaini, Kuwa ndiyo tabiayo
    Naliya nna huzuni, Nawe fanya upendayo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  5. Naliya nikifikiri, Ni mengi niyawazayo
    Naliya sina nadhari, Kwa hayo nikumbukayo
    Naliya nikisubiri, Nayangojeya yajayo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  6. Naliya hiomboleza, Katu furaha sinayo
    Naliya sitanyamaza, Roho yangu yenda mbiyo
    Naliya chaniumiza, Kidonda cha dundumiyo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi
  7. Naliya natiya tama, Shairi niitungayo
    Naliya siwezi sema, Nnafikiya upeyo
    Naliya yananikwama, Mabaya unifanyayo
    Naliya ndani ya moyo, Kwa kuninyima harusi

(Kidonda cha dundumiyo = Kidonda cha kooni)

DUNDUMIYO = koo = koromeo

Khamis Nassor Al-Nabhany

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet