.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

NJAA NA SHIBA !

Related links

NJAA NA SHIBA (Suali)!

Date: 27 August, 2006

Yafuatayo ni mashairi mawili yenye jina NJAA NA SHIBA. La kwanza ni suala na la pili ni majibu yake. Suala limeulizwa na kijana Muhammed Suleiman ambae hapo alipotunga shairi hili mwaka 1982 alikuwa ndio kwanza anajifundisha kutunga na munaweza kuzigundua kasoro kidogo za utungaji. Alimpelekea Sk. Khamis bin Nassor Al-Nabhani, Mola amrehemu, ambae amemjibu kama munavyoona.

Njaa na shiba ilivyokusudiwa unaachiwa msomaji ufafanuwe.

  1. Nimengiya kwenye pango - Kubwa tena ni katile
    Kwa yangu yote mipango - Nashindwa kutoka mule
    Wewe ni mwenye mipango - Naomba uniokole
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  2. Nimezongwa mote mote - Nashindwa kufika mule
    Kwa kakara zangu zote - Nashindwa kutoka mule
    Nabaki kutema mate - Kama nyoka kipilile
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  3. Nimekuja huko kwako - Wewe unisaidile
    Niokowe ami yako - Nitoke pangoni mule
    Ufanye akili zako - Kwani zako ni za kale
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  4. Shiba ikiwa tumboni - Njaa haikai mule
    Si mchana si jioni - Kabisa haipotele
    Yazunguuka uwani - Kidogo yafika pale
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  5. Shiba ikiwa tumboni - Ikitazama kwa mbele
    Kiona njaa njiani - Yaja kwenye tumbo lile
    Haikai asilani - Yatoka bila sumile
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  6. Mambo haya ni magumu - Nawauliza wa kale
    Nyinyi ni mulo khitimu - Akili yenu imbele
    Nami bado ni hirimu - Akili ni ya chechele
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

  7. Hapa ndio kituoni - Kabisa siendi mbele
    Jibu liweke nyumbani - Nikija nilikutile
    Mimi naja karibuni - Tamaa usikatile
    Hii njaa naye shiba - Aliye bingwa ni nani

Mtungaji : Muhammed Suleiman

NJAA NA SHIBA (Jawabu)!

  1. Nakuja nakaa sungo - Niseme unisikile
    Nikuonyeshe mlango - Penye wazi upitile
    Utoke huna kinyongo - Ufurahike milele
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  2. Nikupayo yakamate - Na tena uyatumile
    Ya watu usifuate - Nakwambia kwa kelele
    Ashibae ni kiwete - Mwenda wazimu mpole
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  3. Kitini kaa kitako - Ulo nalo unambile
    Useme maradhi yako - Madawa nikusagile
    Nikutibu wende zako - Wende ukanitambule
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  4. Shiba ina kisirani - Uvivu ndiyo umbole
    Shiba ikiwa tumboni - Njaa hupiga kelele
    Huwaita majirani - Wafike wampokele
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  5. Katu shiba huioni - Kwa hayo usitongole
    Hayaingii kichwani - Kwa hayo usinambile
    Njaa ikija mjini - Huzinga nyumba ingile
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  6. Hayo ni mambo adhimu - Sikiliza nikwambile
    Nikwambie ufahamu - Ukae ukumbukile
    Yamo ndani ya dhulamu - Wala usiyafichule
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

  7. Tamati sendi usoni - Bora sasa nipumule
    Nami nipo uwanjani - Ukija nikupokele
    Nikujibu kwa undani - Uchukuwe utumile
    Njaa ni bingwa wa ndwele - Na shiba ina huzuni

Mtungaji : Sh. Khamis bin Nassor Al-Nabhany Mola amrehemu

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004-2006 Zanzinet