.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Ondoa!

 

 

 

 

 

 

Related links

Ondoa!

Date:  7 September, 2007

  1. Ondoa toa sitaki, kuasi Mwenyezi Mungu,
    Ya nguruwe mishikaki, na mikuku ya kizungu,
    Minofu iso ya haki, sionji ulimi wangu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  2. Huwezi kunizuzuwa, nipate kizunguzungu,
    Nyepesi nikachagua, hukumu za mwenye mbingu,
    Katu sintopagawa, kuzigawanya mafungu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  3. Sitanii kweli kweli, japo nipigwe virungu,
    Chumo lisilo halali, sizugiki walimwengu,
    Iwekwe na kachumbali, sirambi enyi wenzangu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  4. Nimekhiyari kufunga, lengo niwe mcha Mungu,
    Sili ulovikaanga, vinono vya chako chungu,
    Bora nifuturu chunga, hata kama ya uchungu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  5. Kabla hata kufunga, sikufanya vunja jungu,
    Leo sitegwi kijinga, kheri yazuke majungu,
    Mukisema najivunga, maji yanatosha kwangu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  6. Hata kama nitakufa, kinywa kimefungwa pingu,
    Bado nitapata shufa, chini na kwenye mawingu,
    Na kutesa maghorofa, makasisi si vidungu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

  7. Nangoja siku ya Idi, sana nimtaje Mungu,
    Uso ukimuhimidi, chini liwe paji langu,
    Kwenye busati jadidi, radhi awe Mola wangu,
    Ondoa mlo batili, vya haramu sifuturu.

Al- Habibi Al Mardad,
Dar es Salaam.

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet