|
|
Subira!
Date: 13 December, 2009
- Salaam waheshimiwa, nawaombea baraka,
Tunaomba kujaliwa, kila kheri na fanaka,
Tupate kuondolewa, mitihani na mashaka,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Subira inatakiwa, mtihani ukifika,
Utajiri ukinyimwa, halafu ukasumbuka,
Usidhani umetupwa, Kakusahau Rabuka,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Na mitihani mikubwa, kama inamiminika,
Tumshukuru MKUBWA, subira hulazimika,
Tuzidi kuomba duwa, hapana kulalamika,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Msiba unapokuwa, dhaifu hutetemeka,
Kama mwehu anakuwa, imani inamtoka,
Anasahau ya kuwa, Mungu hivyo Ametaka,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Na makelele kupigwa, maafa yakimfika,
Na yote yamekatazwa, Mungu Anaghadhibika,
Apenda Kushukuriwa, Mola wetu Mtukuka,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Kuvumilia ni sawa, na imani kuiweka,
Hadhulumiwi muumbwa, kwa haki kinatendeka,
Hakuna cha kuonewa, imani ya nguvu shika,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Yote yamesajiliwa, Mungu Ameshaandika,
Kalamu kuinuliwa, wino umeshakauka,
Mitihani ukikumbwa, hakuna kubadilika,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Tangu bado kuzaliwa, vyote vimeandikika,
Riziki imegawiwa, na ajali kadhalika,
Yote hayo majaliwa, hapana kunung’unika,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Usikubali kushindwa, shetani akakuteka,
Utageuka mfungwa, wa shetani ni mateka,
Hapo umeshaangushwa, na imani kutoweka,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.
- Hapa nafunga baruwa, pengine mmeshachoka,
Tunaomba maridhawa, Mola Apate Ridhika,
Tunaomba kuepushwa, na madhambi kufutika,
Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa
Limeletwa na Saleh Bakey
Mtungaji : Abdallaah Bin Eifan
(Jeddah, Saudi Arabia)
|