|
|
Tahadhari Na Ukimwi!
Date: 17 June, 2006
- Nataka towa nasaha
Ya dhati si ya mzaha Kuhusu kuu jaraha Dunia liloingiya
- Jaraha ni la ukimwi
Janga lake halikomi Limekuwa kama zimwi Hula mmoya mmoya
- Ukimwi dawa hauna
Tena ni khatari sana Kwa wazee na zijana Wake na waume piya
- Ukimwi ukikushika
Yuwa zako zimefika Ni mno utateseka Wewe na wangine piya
- Ukimwi hukukondesha
Damu ukakukausha Sura zikawa hutisha Jamaa wakukimbiya
- Basi ndugu jihadhari
Ukimwi una khatari Kuu mno lake shari Ni nyingi zake balaya
- Jitunge kila wakati
Epuka uhasharati Sifanye hata katiti Mtegoni utangiya
- Hiyo ndiyo yake kinga
aha zote kuzifunga Kubali kuwa mjinga Salama kuipatiya
- Uzinifu si werevu
Bali ni maangamivu Na mangineyo maovu Ni chambo hukuvutiya
- Muangaliye samaki
Kinena chambo sitaki Asilani humshiki Salama atasaliya
- Na wewe mwana Adamu
Mungu mekupa fahamu Huwaje ukanywa sumu Na hali waangaliya
- Fikiri yako maisha
Kwa nini wayafupisha Wanao kuwabakisha Yatima bila hatiya
- Wewe kwa kutaka raha
Wengi wawapa karaha Haya mambo si mzaha Yataka kufikiriya
- Wenda kujitumbukiza
Kwenye janga lenye giza Wenzio kuangamiza Kwa rahaya mara moya
- Wajitiya mayutoni
Wewe mwenyewe mwendani Huu ni ujinga gani Kifo kujitafutiya
- KIfo si chako wepweke
Utamuuwa na mke Watoto waungulike Lipi walilokoseya
- Tuate uhasharati
Na kwa hishima tuketi Ukimwi hautupati Illa tukiuzengeya
- Na zaidi wasichana
Kadhalika wavulana Hawa ndiwo wengi sana Kwa ukimwi kupoteya
- Wasichana barobaro
Jiziwiyeni mparo Hapo utakwenda ziro Ukimwi kutosaliya
- Jiepusheni kabisa
Na za upuzi anasa Hizo ndizo huwatosa Mtegoni mukangiya
- Ukishapija mtindi
Lolote halikushindi Hata koo kwenye landi Mwenyewe utaitiya
- Wewe ndiye muamuzi
Na wangine hawawezi Ukiamua upuzi Mwenyewe utaumiya
- Nasaha naikariri
Tahadhari tahadhari Ukimwi kuu khatari Inatishia duniya
- Kauli yetu tammati
Ni nasaha kwa umati Hayana dawa mauti Ukimwi ni moya ndiya
Mahmoud A. Abdulkadir (MAU) - Lamu, Kenya
|