.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Tujitahidi na Sunna

Related links

Tujitahidi na Sunna

  1. Wazee na as-habu, Akh-wa na ukhtina
    Nimeandika kitabu, Kiasi kukumbushana
    Kidogo nimekutubu, Si ila kuambizana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  2. Faradhi iwe kamili, Tujitahidi na sunna
    Tufunge tena tusali, Kwa usiku na mchana
    Na tukimiliki mali, Twende Maka na Madina
    Tujitahidi na sunna, Tukamilisha faradhi
  3. Aidha zaka tutowe, Kwa amri ya Rabbana,
    Walokhusika wapewe, Bila ya kupendeleana
    Kwa kipimo wagawiwe, Pasi kudhulumiana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  4. Tukae tukikumbuka, Kua uhai hapana
    Wengi waliotutoka, Wala hawarudi tena
    Jambo jema la kushika, Ni kumtii Rabbana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  5. Tunyanyueni mikono, Tukisikia adhana
    Tusali na sala tano, Na dua kuombeana
    Tuombe masikizano, Jamii muuminina
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  6. Tujitahidi na dini, Ndio jambo la maana
    Na sadaka tutoweni, Ina ubaya khiyana
    Tumlaani shetani, Laanahul mal-una
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  7. Tuitambuwe dunia, Kua si kubwa ni duna
    Hii dunia ni njia, Twapita si maskana
    Dunia yatuzomea, Na huku yatutafuna
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  8. Pana safari lazima, Kubwa mfano haina
    Sote inatuandama, Aasi na msalihina
    Habakii mtu nyuma, Babu na baba na mwana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  9. Soteni lazima kwenda, Mbele yake Subhana
    Kila tuliyoyatenda, Wenyewe tutayaona
    Mwenye lake talipanda, Sayyia au hasana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  10. Dhalimu na madhulumu, Walo wakikopeshana
    Wakae wakifahamu, Siku ya kwenda kutana
    Wanaekewa zakumu, Chakula cha kulishana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  11. Wako wapi watukufu, Walokuwa na majina
    Ambao ni maarufu, Na sote tukiwaona
    La mwisho ni udhaifu, Hali zao hairana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  12. Waliokuwa na raha, Wanangiwa na mahana
    Wote wapiga siyaha, Kina wakiambiana
    Hayupo mwenye furaha, Jamii wanadangana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  13. Tuwatazame wazuri, Walio wakijivuna
    Maringo na ujeuri, Fedhuli na kujiona
    Unakwisha uhodari, La kulifanya hawana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  14. Wako wapi maridadi, Wa vikoi na fulana
    Kwenda huku wakirudi, Na kujiona wapana
    Sasa hawajisafidi, Unawapata mdhana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  15. Iwapi ile suhuba, Watu kutemebleana
    Kila wendapo washiba, Karamu kupikiana
    Jamii wapiga toba, Na wote ni mahuzuna
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  16. Tuwatazame walevi, Waliowakilevyana
    Na ukali kama uvi, Na watu kuwatukana
    Unawishia ujuvi, Khatima wachukiana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  17. Ndugu zangu nawambia, Kama kunabihishana
    Ni kali mno dunia, Yauma tena yabana
    Atakaeichezea, Ajuwe watapambana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  18. Kuna adhabu akhera, Ya namna kwa namna
    Toba ya Rabbi sitara, Allahu mustaana
    Tuombeni maghfira, Kwa Rabbil-aalamina
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  19. Niliyowahadithiya, Ni ya kweli si ya dhanna
    Kwa maneno yangu haya, Ni kama kuzinduana
    Na iwapo ni mabaya, Nawaomba samahana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi
  20. Tammati sina la kwamba, Ni bora tatulizana
    Lakini radhi naomba, Kwa wazee na vijana
    Musije mukanigomba, Ikawa kununiana
    Tujitahidi na sunna, Tukamilishe faradhi

Khamis Nassor Al-Nabhany

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet