|
|
Ukweli !
Date: 06 January, 2007
- Ukweli kitu adimu, katika hii dunia,
Ukweli japo muhimu, watu wanauchukia,
Ukweli watia hamu, kutaka kuusemea,
Ukweli waleta hofu, sababu unaumiza.
- Ukweli taona kiza, ukitaka kuusema,
Ukweli utaumiza, utabebeshwa na dhima,
Ukweli utakimbiza, mamboyo yende mrama,
Ukweli taleta kifo, sababu unaumiza.
- Ukweli unaachisha, kazizenye manufaa,
Ukweli unahamisha, uende usikojua,
Ukweli unafupisha, maisha yaliyotua,
Ukweli unaadui, sababu unaumiza.
- Ukweli waleta chuki, jamaa takuhaini,
Ukweli tapata dhiki, uishipo duniani,
Ukweli ingawa haki, waja hawauthamini,
Ukweli una machungu, sababu unaumiza.
- Ukweli ukishiriki, mpweke utabakia,
Ukweli una mikiki, wenzako takukimbia,
Ukweli hata rafiki, khiyana takufanyia,
Ukweli warusharoho, sababu unaumiza.
- Ukweli utapuuzwa, uonwe usiefaa,
Ukweli utaburuzwa, khofu itakufikia,
Ukweli utakatizwa, furaha ulozoea,
Ukweli taadhibiwa, sababu unaumiza.
- Ukweli ukiushika, watachukia nduguzo,
Ukweli watakuweka, mnyonge bila liwazo,
Ukweli watakucheka, kwa dharau na mabezo,
Ukweli utateseka, sababu unaumiza.
- Ukweli mesisitizwa, na Allah Mola Jalia,
Ukweli umehimizwa, waja watu wajibia,
Ukweli umetukuzwa, kila mtu kuuvaa,
Ukweli ulete haki, ijapo unaumiza.
- Ukweli usidanganye, haki ikatokomea,
Ukweli haki ufanye, japo wengine talia,
Ukweli uutawanye, watu wapate zoea,
Ukweli ulete tija, ijapo unaumiza.
- Ukweli ukizoea, raha yake ya pekee,
Ukweli utazindua, wanyonge wasinyongee,
Ukweli tasimamia, haki kote isambae,
Ukweli sio dhuluma, ingawa unaumiza.
- Ukweli na tuuvae, tuishi kwa usalama,
Ukweli tukumbatie, tuziepuke naqama,
Ukweli tuujengee, hima udumu daima,
Ukweli ulete nema, ingawa unaumiza.
- Ukweli kitamalaki, neema zitajazana,
Ukweli tandoa dhiki, ufisadi na fitina,
Ukweli utadiriki, kusimamia amana,
Ukweli taleta kheri, ijapo unaumiza.
- Ukweli pia amani, tajaa na kufurika,
Ukweli si kisirani, uhasidi tatoweka,
Ukweli si uhaini, bali haki kuiweka,
Ukweli iwe ibada, ingawa unaumiza.
Limeletwa na Abdalla Sani
Mtungaji : Mwanoti A. Abdullah (Pemba)
|