|
|
Ulimi!
Date: 26 August, 2004
- Ulimi ni tamu, ukiutongowa
Wa ama ni sumu, ya kusongonyowa
Uyuwe fahamu, na mwiso huuwa
- Ni nyama laini, haina mfupa
Njema kwa lahani, Mola ametupa
T'unu ya thamani, usio mshipa
- Utatuma wema, kwa wako wendani
Ndugu kukugema, na kuya nyumbani
Lakukusukuma, halipatikani
- Kwa baba na mama, kuwekwa paani
Utakuwa mwema, na kwa majirani
Kuyuwa kusema, ni usulutwani
- Wasokufahamu, wauze ni nyani?
Wafanye hamumu, waje masikani
Na wakuhishimu, wawe wa nyaoni
- Swarifu hisani, uwekewe mbeko
Kwa nde na ndani, na kwa wat'u wako
Daraja ya shani, towa shaka ndako
- Hutowa pangoni, nyoka kaja kwako
Katoka waani, asiche zituko
Yako ulimini, mema matamko
Limeletwa na Saleh Bakey
Mtungaji : Shaha: Ahmed Sheikh Nabhany (Mombasa - Kenya)
|