.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MKE)

 

Related links

UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MKE)

      Utenzi huu umetungwa na Ustadh Mahmoud Ahmad Mahmoud(umaarufu MAU) wa Lamu - Kenya katika mwaka 2004.
      Kama alivyoeleza mwenyewe mtungaji kua ameutunga kwa madhumuni ya kumnasihi binti yake juu ya maisha ya ndoa lakini pia ameeleza kua ni nasaha kwa mabinti wote kwa jumla juu ya maisha haya ya ndoa.
      Kwa hakika ni utenzi wenye mawaidha mazuri na mtungaji ametumia lugha tamu sana na ufundi mkubwa wa utungaji kufikisha nasaha zake za hekima ambazo zinatukumbusha na kutuhimiza kuhifadhi mila yetu na kushika dini yetu.
      Baadhi ya maneno yaliyotumika katika utenzi huu ambao umeandikwa kwa lahaja ya Kilamu yameorodheshwa moja kwa moja baada ya utenzi huu pamoja na maana yake kwa madhumuni ya kumsaidia msomaji anayehitaji msaada huo.

Burudikeni na UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MKE)

1. Bisimalahi Latifu Naanza kuyasanifu Wala sifanyi marefu Mukachoka kusikiya
2. Niya na yangu azima Nataka tunga nudhuma Kumtunukiya mama Nimpe uwe wasiya
3. Mama huyu mukumbuke Binti yangu wa kike Kwani hili jina lake Nda mamangu asiliya
4. Mamangu Mwana Baraka Pema Mungu tamuweka Daima humkumbuka Na dua kumuombeya
5. Na asili ya kwandika Haya ninayotamka Nimeona bila shaka - Wana wayahitajiya
6. Nataka washa fanusi Kumpa bibi arusi Na jamii ya unasi Waweze kuitumiya
7. Ni nasaha ya mzazi Amezopata uyuzi Kwa nyaka nyingi na nyezi Kusoma na kusikiya
8. Ni mambo nimeyaishi Sina kwayo tashuwishi Mwanangu sitakughushi Niya nimekuswafiya
9. Takweleza namnaze Ili na wewe uweze Nyumba yako uongoze Sawa kuisimamiya
10. Jukumu si lake pweke Alo mume tukumbuke Kadhalika wanawake Hupasa kusaidiya
11. Na mke lake jukumu Ni kuu mno muhimu Ndipo ikanilazimu Jukumule kulitaya
12. Na mke kwake nyumbani Ndiye mshika sukani - Kiipinda bandarini Salama husikilya
13. Na akifanya matezo Kiangalie chetezo Badali kuwa fukizo Ni nguo huteketeya
14. Nimekupa ni mfano Nawe taamali mno Sitozidisha maneno Nadhani yamekweleya
15. Sasa taanda kweleza Yale nimezo yawaza Mwanangu nipulikiza Kwa makini nisikiya
16. Nisikiza kwa makini Uyatiye akilini Kisha mwako maishani Jaribu kuyatumiya
17. Sikwambii kwa mfumbo Tayanena wazi mambo Kufanya hilo si kombo Tumwa ametanguliya
18. Metanguliya rasuli Kubaini yao hali Kati ya watu wawili Mke na mume pamoya
19. Alonena kwa lisani Kwa zitendo mebaini Kwa hili nami sioni Chamba hayo ni khatiya
20. Kiwa tumwa hakuhiti Nami khatiya sipati Niendeme siiati Ndia alotunyosheya
21. La kwanda yambo muhimu Mke lilomlazimu Ni mume kumhishimu Kwa kila hali na ndiya
22. Hishima ni pande mbili Ni ya mke kwa mvuli Na alo sawa rijali Mkewe humuekeya
23. Yani kuhishimiyana Ni yambo muhimu sana Nalo likikosekana Na utuvu hupoteya
24. Mke ataka hishima Na kwa mume ni lazima Maisha henda salama Hishima ichendeleya
25. Mume mshikie hamu Twabiaze zifahamu Maisha huwa matamu Ukimwelewa twabiya
26. Mume ni kama kijana Ahitaji mengi sana - Kwako wewe wake nana Nawe mbwa kumtendeya
27. Dharau nawe haoni Kwako wewe asilani Mfano kiya nyumbani - Inuka kumwangaliya
28. Nyumbani akiwasili Wata yako mashughuli Umuyuwe yake hali Lipi anahitajiya
29. Mfano una wageni Mumo mazungumzoni Wambiye kumradhini - Subirini mara moya
30. Wende ukamsikize Haja yake muulize Na papo itekeleze Pasi na kulimatiya
31. Kisa mtake rukhusa Umwambiye mimi sasa - Kurudi imenipasa Wageni kuwangaliya
32. Fahamu ukimpuza Na wageni ukafuza Ni yambo humuumiza Ingawa tavumiliya
33. Na ukifanya hiyau Tadhani wamdharau Wamfanya yauyau Ni mtumishi mengiya
34. Wala sione aibu Kutekeleza wajibu Bali ni hio adabu Yapasa kukazaniya
35 Usione ni udufu Mumeo kumsharafu Wallahi atakusifu Na heshima kukwekeya
36. Ukimtukuza mume Na yeye tafanya shime Ili hilo lisikome Liwe nda kuendeleya
37. Naye atakutukuza Na kwake uwe aziza Kinyume ukimtweza naye takugeukiya
38. Na upande wa chakula Na shughuli za kulala Pa kupumuwa mahala Yipinde kuzangaliya
39. Pika chakula kizuri Si lazima cha fakhari Hata kama ni kidheri Mwenyewe kusimamiya
40. Simwatiye mtumishi Fikiri kunuka moshi Chakula cha tashuwishi Maudhiko humtiya
41. Angaliya na ziungo Kwa zipimo sende jongo Kufurahi ndiyo lengo Si tumbo kushindiliya
42. Upishi wa ustadi Hufurahisha fuadi - Na ladha piya huzidi Na kwa kula huvutiya
43. Pika kitu kwa kadiri Kichache kiwe kizuri Usipende kubadhiri Ili sifa kuzengeya
44. Mfano mume kiyeta Nyama haina mafuta Siwe naye utateta Nyama gani angaliya
45. Na akiwa kula mara Hueta iso na sura Mnabihi kwa busara Kwa mbali kumtaiya
46. Simwambiye yako kazi Ni kuweta zitu hizi - Mtu kupika hawezi Zote towa meeneya
47. Labuda hupata bure Au wapenda bwerere Kwa maneno simkere Kama haya kumwambiya
48. Na kama haya maneno Mwanangu huudhi mno Nimekupa ni mfano Na mangineyo kisiya
49. Mukiwa hula mezani Au huketi jamvini Angaliya kwa makini Zote za kuhitajiya
50. Zitu nusu usiweke Ukiketi uinuke Mara hiki ukumbuke Mara kile huzengeya
51. Kunawa kwa ya bulini Au penye beisini Bora kuliko dishini Watu wengi kunawiya
52. Mai ya mtiririko Bora kwa afiya yako Si bora mkusanyiko Kuosha wengi pamoya
53. Kitambaa cha kufuta Tishu ni bora kipata Khaswa kiwe cha mafuta Chakula mulotumiya
54. Kiwa mumekula nyama Zijiti kama lazima Chakula kikisakama Menoni kina udhiya
55. Na menoni kikibaki Chakula hutiya dhiki Na mara husikiziki Mtu kikukaribiya
56. Khaswa usiku ukila Hakikisha huyalala Kanwa lako kwa jumla Usafi melifanyiya
57. Hunuka kama uyusi Au cha paka kinyesi Mwenyewe huwa huhisi Ni shida kuisikiya
58. Mtu aliyo karibu Hupata mno taabu Kanwa kunuka aibu Ila kuu hukutiya
59. Ya kula nimemaliza Ya kulala nakweleza Kadhalika tafupiza Siwezi yote kutaya
60. Tengeza yako firasha Mahala pa kuyinyosha Pasiwe huwashawasha Na tashuwishi kutiya
61. Wala sitake ya ghali Mafirasha ali ali Hutosha sitiri hali La kufaa kulaliya
62. Kitandike kwa uzuri Ufukize na uturi Hizi mno huathiri Kuona kunusa piya
63. Ukinuka rihi njema Huwasiika mtima Na moyo hufanya hima Mwendo kumkaribiya
64. Zina athari harufu Zilizo njema na chafu Ya asimini na afu Si kama ya jasho baya
65. Chumba chako cha kulala Pawe patuvu pahala Sipafanye ndipo ghala Ya zitu kukusanyiya
66. Katu matandu siwate Wala uchafu wowote Yaandame uyafute Usichoke na kupeya
67. Ipinde kuwa nadhifu Sionekane mchafu Ni amri ya Latifu Na Tumwa wetu Nabiya
68. Safisha wako muwili Ipambe utajamali Kwa kila kilo halali Haramuni kutongiya
69. Mfano nshi kuchonga Wanazuoni hupinga Kwa hadithi za muanga Ambazo zimeziwiya
70. Ipinde ujitahidi Sana kuwa maridadi Uwe ni wako uradi Mno ulouzoweya
71. Siketi kwako nyumbani Kama uliyo mekoni Na wendapo hadhirani Ndipo kuipotoleya
72. Siweke njema libasi Kuvaa kwenye harusi Na nyumbani kawa basi Matambaa hutumiya
73. Mazuri mavazi yako Mvaliye mume wako Ili nde atokako Siwe mate tamiziya
74. Fahamu yeye ndiani Huziona dizaini Na hakosi kutamani Mavazi haya na haya
75. Akiwa nde huona Fesheni kula namna Nyumbani kwake hapana Ila hayo mazoweya
76. Henda akashawishika Na moyo kasalitika Hana budi tatamka Maguu tamtiliya
77. Lakini akiwa kwake Huona kwa mke wake Ya kushiba mato yake Mwengine hatazengeya
78. Takuwa hababaiki Kiona hiki na hiki Atakuwa hashutuki Ni mambo meyazoweya
79. Upambe fanya nyumbani Usingoje harusini Kuwaonyesha wendani Na fakhari kuzengeya
80. Badilisha dizaini Sishike moya fesheni Nyee zako za kitwani Mitaji ukitumiya
81. Zisuke na kuzitana Tena kwa kila namna Kila siku kikuona Akuone ni mpiya
82. Mumeo mtosheleze Mwako wake amalize Ili mate asimize Yawende akisikiya
83. Mtosheleze kingono Hilo ni muhimu mno Huharibu tangamano Ngono isipotimiya
84. Akutakapo siize Mwegeme umpumbaze Na dharura mueleze Iwapo imetokeya
85. Akutakapo kubali Wata yote mashughuli Sambe hili wala hili Na nyudhuru kuzengeya
86. Na katiti ushaufu Kitiya kama harufu Hutiya uchangamfu Na huzidi kuvutiya
87. Ushaufu usizidi Kaona ni ukaidi Hapo nyuma atarudi Ataghairi na niya
88. Kutiya pozi katiti Kwa mudawe na wakati Hawezi kukulaiti Ni mbinu hiyo tumiya
89. Na iwapo takwekeza Ya haramu kufanyiza Katwaani hilo iza Sikiri ukaridhiya
90. Uyuwalo ni haramu Kwako liwe kama sumu Sitwii mwanaadamu Kwa kumuasi Jaliya
91. Usikiri taawili Na za wengine kauli Wanenao ni halali Sifuate mbovu ndiya
92. Kwa mume ipendekeze Na kwa hilo siregeze Mume wako ihimize Mahabani kumtiya
93. Kuna uganga halali Huno ni tamu kauli Ndilo talasimu kali La mume kumvutiya
94. Sambe naye kwa jauri Wala usimtiriri Nakwambiya tahadhari Mara kinyongo hungiya
95. Mumeo usimtune Yalo mawi usinene Ipinde mutangamane Mutukuwane twabiya
96. Na twabiya ya ukali Kadhalika ufidhuli Ni sumu hayo mawili Yepuke khatuwa miya
97. Sambe naye kwa ghadhabu Mambo utayaharibu Hutengeza taratibu Na hufuja kurukiya
98. Simrukiye yoyote Hata mwanao wa kite Twabiya hiyo iate Au utaiyutiya
99. Kuukiya si uzuri Hutiya kuu dothari Kheri mtu msairi Wambe na kunyenyekeya
100. Akiya aso adabu Kitaka kuya karibu Akome asijaribu Hishima kukuvundiya
101. Kama huyo kumpuza Ni bora kiwa taweza Kisimama kumweleza - Hwenda kazidi balaya
102. Umpuze wende zako Sitowe lako tamko Akizidisha zituko Hapo utaangaliya
103. Na kadhalika idhini Ya mumeo ithamini Sende hata kwa jirani Ikiwa huyamwambiya
104. Ya mume wako ruhusa Kuitaka yakupasa Sende mwendo wa kisasa Amri kuishikiya
105. Sitoke kwako nyumbani Mumewe kiwa kazini Au yuko safarini Kabla ya kumwambiya
106. Salamu usimwatiye Kiya fulani mwambiye Mngojee mpaka aye Siwe utaitokeya
107. Wala usiimakini Kwa hana neno fulani Nichendaa harusini Nikiya atasikiya
108. Ingawa hatouliza Wala hatokuziwiza Atahisi wamtweza Hishima kumwondoleya
109. Ruhusa ukimtaka Mwanangu hutotwezeka Utazidi kutukuka Na matoni utangiya
110. Hilo waume hupenda La kwambiwa yambo kwanda Siinuke ukatenda Kisa ndio kumwambiya
111. Yambo ukitaka tenda Yapo nda uti wa wanda Mshawiri yeye kwanda Upate kumsikiya
112. Hata kama hana kitu Wewe hilo sisubutu Hishima na wake utu Ni haki kumtungiya
113. Ukitaka fanya yambo Mfano la nyumba pambo Mwambiye naye kitambo Tangu ukitiya niya
114. Usipompa khabari Mume haoni uzuri Mume ni yake fakhari Shaurile kuzengeya
115. Na hata kama senti Mekosa hata katiti Kwa hilo hawi mehiti Heshima kumwondoleya
116. Na kitu ukinunuwa Kumwambiya ndiyo sawa Mapema apate yuwa Asiye kushutukiya
117. Hata cha thamani duni Mpe khabari mwendani - Asikione nyumbani Kwenye shaka akangiya
118. Mume kikupa tamasha Ipokee kwa bashasha Shukuru na kuitesha Yapo nda shilingi moya
119. Twaa kwa kufurahika Na uso wako kuteka Na yeye tawasiika Furaha moyo kungiya
120. Usidharau chochote Akupacho sikiate Yapo ni ya chuma pete Na kwa furaha pokeya
121. Mkongoweye ayapo Umuwage atokapo Umuyuliye alipo Kurudi kilimatiya
122. Na wala simtiriri Siwe kama askari Kumshikiya amri Ya kutoka na kungiya
123. Kiwa kwake una haja Usiwe utamngoja Akitiya guu moja Nyumbani ukamwambiya
124. Kama jiwe simwatiye Mngoje ndani angiye Kisa ndio wangaliye Sura ya kumwelezeya
125. Ukiona yake hali Una mengi mashughuli Itakuwa afadhali Umngoje kutuliya
126. Kiwa metenda makosa Kumwambiya yakupasa Na kwa ndiya ya siyasa Na hikima kutumiya
127. Yataka sana hikima Katika mambo kusema Sababu mbovu kalima Ni subili kusikiya
128. Na kipumba cha subili Hufuja pipa asali Na ndio mbovu kauli Mengi hukuharibiya
129. La makosa kikutenda Usimize likavunda Kheri mumalize kwanda Kwa ndiya nilokwambiya
130. Maudhiko kufundika Mwishowe hufurijika Mambo kakharabatika Mdangano ukangiya
131. Simize katu mashingo Yatakweteya tewengo Kheri rakibisha jongo Papo linapotokeya
132. Siweke mambo bariyo Maudhiko upatayo Ni kheri safisha moyo Muande mambo upiya
133. Kukizuka tafauti Ulimi wako dhibiti Mara moya utahiti Mayutoni tasaliya
134. Kutupatupa sipende Ulimi wako ushinde Na moyo upige konde Sambe kwanda fikiriya
135. Neno ukitaka nena Mwanangu lipime sana Kiona si la maana Ipinde kuiziwiya
136. Ulimi sana dhibiti Mwanangu hutoiyuti Kunena kuwe katiti Si robo ya kusikiya
137. Usinene uonalo Na kula usikiyalo Pima kwanda neno hilo Mizanini kulitiya
138. Ulimi kiwa mrefu Tena ukawa mchafu Hukweteya uumbufu Katu usiodhaniya
140. Na mwanangu kusubiri Ni yambo huvuta kheri Na ni twabiya nzuri Hukwepusha na balaya
141. Kusubiri izoweze Twabiya hiyo ikuze Mambo mangine yapuze Na mato kuyafumbiya
142. Ifunde na kuhimili Dhiki za wako mvuli Madamu muko wawili Tafauti hutokeya
143. Ifunde uvumilivu Mwanangu siwe muyavu Hio ni tabiya mbovu Watu watakukimbiya
144. Enga kasi na mtungi Hugongana mara nyingi - Lakini haziyitengi Ni pamoya husaliya
145. Na za mumeo libasi Zifuwe upige pasi Na kama boi haisi Simpe kumfuliya
146. Na mtumishi hodari Afuao kwa uzuri Kufuwa ni dasituri Bali ndiyo mazoweya
147. Ikiwa nyumbani huna Mtu wa kazi kijana Wewe mwenyewe kazana Shughuli kuyitendeya
148. Mume simkalifishe Kumwambiya akodishe Kiyeta simrudishe Ni bora tasaidiya
149. Na akiwa na safari Mpangiye kwa uzuri Mkoba usitakiri Hajaze kumtiliya
150. Mtiliye haja zake Zitu zote uziweke Endako asisumbuke Mara tana huzengeya
151. Hilo lingawa ni toto Lina athari nzito Huba huzidi ukweto - Na nyonda hupeleleya
152. Kiya rafiki nyumbani Na mumeo hako ndani Na komee mlangoni Usimliche kungiya
153. Rafiki wa mume wako Au mwana mjombako Kwako na iwe ni miko Siketi naye pamoya
154. Rafikiye simlite Kama chui wewe mte Wengi mambo yawapete Kwa maswahibu wa kuya
155. Hao majumba huvunda Si eo ni tangu kwanda Utauma kumi zanda Wala hupati kimoya
156. Sifanye nao dhihaka Na kunena na kuteka Mayi kisakumwaika Kuzowa siyasikiya
157. Hata wakipija simu Ukisa kuwafahamu Kata papo ni muhimu Sipende kuendeleya
158. Sipende kuzungumza Wala mengi kuuliza Ghafula chombo husoza Na ukapata hatiya
159. Na hili nalikariri Mwanangu utahadhari Kwa dhihaka usikiri Mtu kikutambaliya
160. Sambe na mteza shere Shere itazuwa mare Kisa mambo yakukere Uyiyute mara miya
161. Fahamu kuwa mzaha Hulitumbuwa jaraha Ishike hini nasaha Mwanangu nakutumiya
162. Nawe marafiki zako Hata walio ndu zako Usikiri mume wako Hao kuwakaribiya
163. Na wasifanye ubishi Na wala mwingi uteshi Pana moto penye moshi - Mara yuu hutokeya
164. Aswili usikubali - Fanya miko yambo hili Sikiri wako mvuli - Shemeji kumtezeya
165. Sinene namuamini Nambiani tangu lini Simba alo wa mwituni Mtu mbuzi kumwatiya
166. Simba ngaifanya paka Siku moya hugeuka Kipata nyama hushika Hasahau mazoweya
167. Nao waume wa nduzo Sifanye nao matezo Sababu ni hizo hizo Nimezokwisa kutaya
168. Fahamu kuwata ufa Huzuwa mengi maafa Ndoa nyingi zimekufa Sababu ni mambo haya
169. Walokwimba wamenena Huwa shemegi mtana Na kiza kikifungana Taa zinya hukwambiya
170. Haya mambo si mazuri Na ni mbovu dasituri Dini piya haikiri Ni mila mno mibaya
171. Nyumbani sikaribishe Yipinde uwaepushe- Yalo sawa wafundishe Kwa mwendo sikuwaambiya
172. Alaka hazikatiki Kwa kwenda mwendo wa haki Usiwache makhuluki Ukamuasi Jaliya
173. Na mambo yana mipaka Usikiri kuiruka Na wendo wangakuteka Msimamoni ziwiya
174. Sifanye nao dhihaka Za kunena na kuteka - Mara moya hupomoka Mtegoni ukangiya
175. Tahadhari tahadhari Thuma tena tahadhari Mashemegi usikiri Nyumbani kukungiliya
176. Kwa mapana na marefu Huno ni mwendo mchafu Ni kheri mara alifu Uwe pweke tasaliya
177. Na ambao wako dada Isiwe ni yao ada Kula wakati na muda Na mzaha kwendeleya
178. Wakiondosha sitaha Kwa matezo na mzaha Mwisho huzuwa karaha Mambo ukayatukiya
179. Kheri hayo kuyakinga Kwa ukuta kuujenga Ungafanywa ni muyinga Bado huyaendeleya
180. Mume ni mwanaadamu Nakwambiya ufahamu Asali maneno tamu Tashuwishi humtiya
181. Humtiya tashuwishi Mara moya kakughushi Huanda kama ubishi Na mara humzoweya
182. Faragha simuatiye Nawe piya iziwiye Siketi na ale nduye Wa kiume ni hatiya
183. Nimenena kwa urefu Ya shemegi kuarifu Kuna mwingi uumbufu Mashemeji huchangiya
184. Ama nduze wa kike Na baba na mama yake Nakuhimiza watake Zidi kuwakaribiya
185. Kwa hawa ikaribishe Suhuba uimarishe Na piya upurukushe Yalo mawi kisikiya
186. Ipinde kutenda zema Zema huzinya khusuma Na pia wema hutuma Na utesi huziwiya
187. Hao siwapige zita Na hata wakikukata Siwe nao utateta Kuteta kuna udhiya
188. Wakikwambuwa ambata Usitake nao zita Na yakizidi matata Hutokuwa na hatiya
189. Iwapo mekosa budi Itenge nao baidi Kwa nidhamu maridadi Na rabusha kutotiya
190. Ukipata mtihani Kuishi nao nyumbani Huyo mamake fulani Na wako ni hali moya
191. Mamake sana mtunge Na usuhuba ujenge Uvumiliye na tenge Litakapo kutokeya
192. Mamama ni tafauti Kuna mamezaa siti Hatukani na hateti Daima ni maridhiya
193. Wengine ni wasaliti Mke makini hapati Angaliya kibiriti Kwa fitina kuzitiya
194. Na ikiwa meswadifu Mwanaisi ni mchafu - Jifunze kuisarifu Kwepuka zake balaya
195. Na mke alo hodari Ayuwao kusafiri Hupeka chake kihori Akaepuka miuya
196. Kukichefuka mtoni Wewe tapiliya pwani Au ambata kokoni Ngoja mawimbi kusiya
197. Penye wimbi siemeze Kheri chombo ugeuze Wangaliye namnaze Bandari upate ngiya
198. Kwemeza usijasiri Mwanangu tayikhasiri Kisa yatazinga dori Lawama kukwangukiya
199. Siri zako za nyumbani Sizitowe asilani Hata kwa nduzo wendani Si wema kuelezeya
200. Siri za nyumbani kwako Nazibaki hokohoko Usitowe matamko Wengine ukawambiya
201. Siri zako zidhibiti Khususa za tafauti Zitokeyazo katiti Ipinde kuziziwiya
202. Jaribuni kumaliza Na mumeo mukiweza - Si uzuri kutangaza Wengine wakasikiya
203. Ikiwa huna namna Mambo yamezidi sana Si makosa ukinena Teuwa wa kumwambiya
204. Siketi na unguliko Nena kwa aliyo wako Mwambiye shauri lako Nimekuya kuzengeya
205. Mtu kutaka shauri Hiyo nda dini amri Mtake alo hodari Na wa mambo kumweleya
206. Zengeya umuulize Ayuwao umweleza Ili naye akwekeze Ndiya njema ya shariya
207. Simuulize yoyote Ili muhimu upate Jawabu ulifuate Hata kama si la ndiya
208. Uliza mwenye hekima Umuyao mesoma Akiwa mtu mzima Ni bora kutegemeya
209. Wengine kiwauliza Huzidi kukupoteza Yaso ndiya hukwekeza Ili kukuharibiya
210. Mumeo kikupa siri Simtolee khabari Kuwa ni kama kaburi Siriye kuifusiya
211. Siri yake iziwiye Mngine simtaiye Hata kikurai iye Usikiri kumwambiya
212. Siri yake ikitoka Fahamu ataudhika Na laiti takushika Lawamani utangiya
213. Maneno ya usabasi Mno hutiya utesi Wewe sitowe nafasi Kwa mwenye kukuambiya
214. Ubajo wa mitaani Siutiye akilini Na wenye nao nyumbani Siwaate kuzoweya
215. Usifanye urafiki Na walio wanafiki - Nakwambiya changu hiki Watakweteya balaya
216. Na zizere zivundifu Ziliyo na nyendo chafu Zitegesha zisarifu Au zitakuvundiya
217. Zizere zina hatari Kuvunda ni zihodari Nenda nao kwa hadhari Ni bora kuzikimbiya
218. Zile ziswa za nganuni Ni za kweli na yakini Hata yeo mitaani Kula mara hutokeya
219. Huya kimesikitika Ati sadaka chataka Kalama kimefutika Mzinga kukwatiliya
220. Na siku ukiambiwa Kua mumeo meowa Sikiri kugogolewa Kutezwa shere na ndiya
221. Keti makini ituze Chombo chako kitengeze Safari yako ifuze Kama hakuna mapiya
222. Wala sifanye matungu Nakuusiya mwanangu Siharibu chako chungu Usikhalifu shariya
223. Jaribu kuikukusa Miyomo kutotakasa Mara moya yatakwisa Yambole talizoweya
224. Na mumeo musitete Na mke mwenza muate Ndiya yake afuate Nawe yako angaliya
225. Tena mwanangu fahamu Mara hutiwa wazimu Si wema wanaadamu hukuzengeleya ndiya
226. Wivu ndio kawaida Kwa watu wote ni ada Siwe nao wa ziada Hisabu zikapoteya
227. Wala si nene na mimi Tamlipa basi nami - Dhibiti wako ulimi Hilo kutofikiriya
228. Kumlipa ni kuasi Amri yake Mkwasi Na kwandamaye bilisi Mawi yake kuridhiya
229. Hishima yako itunge Cheo chako ukijenge Moyo siitiye tenge Angaliya moya moya
230. Usifanye taharuki Na ziumbe sishitaki Watakuzidisha chuki Mambo kukuharibiya
231. Mume kuowa si kosa Walakini yampasa Kuzifanya sawa hisa Pasi na kupondokeya
232. Kiwa mambo yamezidi Kwa hawaa kushitadi Tasahaliya Wadudi Mungu takuhukumiya
233. Katu neno la talaka Siwe utalitamka Ila uwe medhikika Na mambo yamekwemeya
234. Siwe la kwanda la pili Ni kumwambiya mvuli Nitaliki kama kweli Ni mume ulotimiya
235. Kiwa yamezidi sana Wazi wazi huyaona Si makosa ukinena Hakiyo kutaradhiya
236. Hilo wewe siatame Muate yeye aseme Kikuata simwandame Kwenda kumtapiliya
237. Hata kama zake nyonda hushuka zikikupanda Kiwa kosa hukutenda Usende kumwangukiya
238. Kiwa wewe ni mkosa Kurai sitokuasa Na maadamu huesa Hubaze zimesaliya
239. Rai na kutafadhali Si makosa yambo hili Wala maneno sijali Ya waja wakikwambiya
240. Sasa niko kikomoni Nakuusiya kwa dini Kuwa ndiwe namba wani Faradhi na sunna piya
241. Shikamana nayo sana Dini ya Mola Rabana Mambo yako tayaona Kwa uzuri hukwendeya
242. Ukimcha Mungu kweli Katu hupati thakili Kwa uzi wa buli buli Na peponi utangiya
243. Mche Mola pweke yake Siwache ziumbe zake Yambo ovu usishike La kukhalifu shariya
245. La mwisho wangu binti Takwambiya siliwati Mume siwange senti Enga dini na twabiya
246. Shika hiki ni kipimo Taka mwenye msimamo Usitapilie tumo Na fakhari kuzengeya
247. Kheri awe masikini Wa kuishi upenuni Lakini wendeme dini Kuliko miliyoniya
248. Mizani siwe ni pesa Na majumba ya anasa Ni kipimo cha makosa Hiko watu kutumiya
249. Nimekoma kikomoni Kuchora hini ramani Ungiyapo safarini Itakuongoza ndiya
250. Ramani muikumbuke Si yake binti pweke Ni ya kula mwanamke Wa Hawa na Adamiya
251. Kusudi nimeichora Iongoze misafara Kwenye safari za bara Na za baharini piya
252. Rabi tiya tawfiki Fali yangu iyafiki Wawe kwa kitabu hiki Watu ndia hungokeya

MWISHO WA UTENZI.

Mtungaji: Ustadh Mahmoud Ahmad Mahmoud (MAU) Lamu mwaka 2004

Umeletwa na Saleh Barkey tarehe 25 February, 2005

Maana ya maneno yenye lahaja ya Kilamu ambayo ndiyo iliyotumika katika utenzi huu.

Beti

3. Nda = La . "Nda mamangu" = "La mamaangu"
7. Amezopata = Aliepata ; Uyuzi = Ujuzi ; Nyaka = Miaka ; Nyezi = Miezi
12. Kiipinda = Akijipinda yaani akijitahidi au akijikaza ; Husikiliya = Hufikilya
15. Taanda = Nitaanza ; Nimezo yawaza = Niliyo yawaza
20. Hakuhiti = Hakukosea ( Kuhiti = Kukosea)
22. Mvuli = Mvulana
23. Utuvu = Utulivu
26. Mbwa = Wa ( Mbwa kumtendeya = Wa kumtendeya)
30. Kulimatiya = Kuchelewa
33. Hiyau = Hivi ; Yauyau = Hivi hivi
37. Ukimtweza = Ukimdharau
39. Kidheri = Aina ya chakula cha mchanganyiko wa maharage na mahindi
44. Kiyeta = Akileta
45. Kumtaiya = Kumtajiya
56. Kanwa = Kinywa
57. Uyusi = Mfu
63. Mtima = Moyo ; Mwendo = Mwenzio
66. Matandu = Nyumba ya buibui
69. Nshi = Nyusi
71. Kuipotoleya = Kujipamba (Kujipodowa)
80. Nyee = Nywele
82. Mwako = Hamu
84. Siize = Usikate ; Mwegeme = Mkaribiye
86. Katiti = Kidogo
87. Ushaufu = Kujishauwa ; Kukulaiti = Kukulaumu
89. Iza = Kataa (Usikubali)
95. Usimtune = Usimkere kwa kurudiarudia maneno yale kwa yale ; Mawi = Mabaya
98. Mwanao wa kite = Mwanao uliemzaa mwenyewe (Kupiga kite = Kujikamua wakati wa kuzaa)
107. Usiimakini = Usijimakini ; Nichendaa = Nikienda
111. Uti wa wanda = Kijiti cha wanja
121. Mkongoweye = Msherehekee
130. Mdangano = Kutoelewana
131. Tewengo = Maudhiko
143. Muyavu = Usieweza kustahamili
144. Enga kasi = Angaliya kata (kata ya maji)
145. Haisi = Hajui
151. Toto = Dogo ; Huzidi ukweto = Huzidi kukita
154. Yawapete = Yamewapata
155. Si eo = Si leo
169. Zinya = Zima , (Taa zinya = Taa zima)
173. Na wendo wangakuteka = Na wenzio wangekucheka
186. Zema = Wema ; Huzinya = Huzima ; Hutuma = Huchuma
191. Tenge = Fujo
192. Mamezaa = Mamkwe
194. Mwanaisi = Wifi
195. Hupeka chake kihori = Hupeleka mtumbwi wake ; Miuya = Mawimbi yasiokuwa na fujo
197. Siemeze = Usijasirishe
198. Kisa yatazinga dori = Kisha yatakurudia kinyume
210. Kuifusiya = Kujizika
211. Iye = Vipi
214. Ubajo = Umbeya
218. Ziswa = Visa
219. Kalama = Kumbe
219. Sikiri kugogolewa = Usikubali kuchezwa shere
223. Miyomo = Midomo ; Yambole = Jambo lake hilo
231. Kupondokeya = Kupita mpaka
238. Huesa = hujesha

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet