.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MUME)

 

Related links

UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MUME)

      Utenzi unaofuata ni utenzi wa pili uliotungwa na Ustadh Mahmoud Ahmad Mahmoud (MAU) wa Lamu – Kenya katika mwaka 2004 wenye maudhui yale yale ya Ramani ya maisha ya ndoa. Utenzi wa kwanza ulikuwa wa nasaha kwa wanawake na huu wa pili ni kuwanasihi wanaume. Kama ulivyo utenzi wake wa mwanzo, mtungaji ametumia lugha tamu na nasaha za hekima ambazo ameeleza kua ni wasia kwa mwanawe wa kiume Yahya lakini pia amemkusudiya kila mvulana ili asitupe mila na afuate maamrisho ya dini yetu.
      Baadhi ya maneno yaliyotumika katika utenzi huu ambao umeandikwa kwa lahaja ya Kilamu yameorodheshwa moja kwa moja baada ya utenzi huu pamoja na maana yake kwa madhumuni ya kumsaidia msomaji anayehitaji msaada huo.

Burudikeni na UTENZI WA RAMANI YA MAISHA YA NDOA (MUME)

1. Kwa ina la Rahamani – Naanda nudhuma hini – Ina ya pili ramani – Namwandikiya Yahaya
2. Kwenye ramani ya kwanda – Banati naliwafunda – Na hini nimeiunda – Wavulana kuwambiya
3. Na asili ya kwandika – Nahisi wana wataka – Baba piya kadhalika – Mimi alinandikiya
4. Baba bwana Ahmadi – Atamjazi Wadudi – Kwani alijitahidi – Kunandikiya wasiya
5. Hapo zamani za yana – Ndiyo la wasiya yina – Alonandikia bwana – Babangu kaniwatiya
6. Nami katika ramani – Tayipinda kubaini – Yale ninayoamini – Yaweza kusaidiya
7. Tanena naloyatuma – Na yale niloyasoma – Tazitaya na hekima – Kwa watu nilopokeya
8. Yale nitayakusanya – Mbali mbali kutanganya – Lengo langu ni kufanya – Kama la maisha boya
9. Boya hili la maisha – Katu halitozamisha – Ashikao tamvusha – Bandari tasikiliya
10. Mwanangu ukiazimu – Kuowa kwanda fahamu – Kuteuwa ni muhimu – Ni amri ya shariya
11. Mtumi alibaini – Akatwambiya owani – Mwanamke mwenye dini – Mungu tawabarikiya
12. Mwanangu sitake mke – Kwa wema wa umbo lake – Nasaba na pato lake – Mayutoni utangiya
13. Wala dini haineni – Owa shuguu la uni – Kishuna kilo na dini – Kukiowa si hatiya
14. Mwenye nasaba tukufu – Na kwa Mola mtiifu – Hawi mtu mekhalifu – Kama huyo kuzengeya
15. Na mke alo na chake – Sikwambii simtake – Bora awe dini yake – Meshika hakumbiriya
16. Dini ni kama bureki – Humziwiya hatoki – Mipakani na haruki – Akiwa taitumiya
17. Na dini humziwiza – Kutenda yasopendeza – Na ndipo kakuhimiza – Mwenye dini kwangaliya
18. Dini ninayoinena – Sikuwa nayo ni ina – Dini ni kwandama sana – Amri zake Jaliya
19. Ni dini kwenye maisha – Mtu iwe humwendesha – Si dini ya kuonesha – Watu kuwahadaliya
20. Ni dini iliyo ndani – Iliyokita moyoni - Ndiyo huwa ni sukani – Ya kumuongoza ndiya
21. Ni ukisa kuamuwa – Ni Fulani tamuowa – Fanya mambo sawasawa – Sandame ya jongo ndiya
22. Usifanye ya sheshegi – Kama watu wenye gogi – Siipeke zigizagi – Harusi nimekwambiya
23. Kula ikiwa ni pesi – Huwa ni bora harusi – Fanya mambo ya kiasi – Kwa gharama ngoma piya 24. Makubwa usiyatake – Na mipaka usiruke – Piya upande wa mke – Waeleze kama haya
25. Zikiwa nyingi gharama – Na mayuto ni lazima – Ngoma zikisa kukoma – Ni lawama husaliya
26. Fanya mambo ya kadiri – Sitake mno fakhari – Nakuusiya sikiri – Hafula za maasiya
27. Hafula za isirafu – Na za magoma machafu – Na kuwa tutu kwa ufu –Dini hayo huzuwiya
28. Mila yetu usiwate – Mfano kuvisha pete – Si yetu usifuate – Wengi wangakazaniya
29. Ni mila ya kinasara – Kuiwata ndio bora – Wangawa watakukera – Waja kwa kutoeleya
30. Na kwenda kupa mkono – Usikiri tangamano – Hata alo nduyo mno – Simuate nawe kuya
31. Nyumba yako siasisi – Kwa msingi wa maasi – Taivutiya nuhusi – Na ukorofi kungiya
32. Na maasi ninenayo – Ni kula mambo ambayo – Mola ayatukiayo – Na kula aloziwiya
33. Moya moya sitoweza – Kutondowa kukweleza – Nimekupa muangaza – Wa ndiya kufuatiya
34. Nimekupa ni kiyasi – Kitumyie nawe basi – Kwa mangineyo kukisi – Kwa mizani kutumiya
35. Nyumba njema ni msinji – Tamu ya chai si ranji – Wengi metiliwa tanji – Kwa fakhari kuzengeya
36. Kiwa ni lazima sana – Hilo la kuandamana – Shemegiyo mvulana – Andamanani pamoya
37. Au mwengine yoyote – Maharimu na fuate – Ajinabu simuate – Mkeo kumwangaliya
38. Rafiki simuamni – Ukamtiya nyumbani – Ila dharura fulani – Sikuye ikitokeya
39. Rafiki usimliche – Ni zaidi huyo mche – Kwa wao mambo ya cheche – Huwa usolidhaniya
40. Zizini kutiya simba – Ni kama moto na pamba – Mara moya huzisumba – Na yivu likasaliya
41. Rafiki kingiya ndani – Sikuye ukatamani – Sambe ona ni nyumbani – Hee utayitongeya
42. Hiyo kwetu siyo mila – Kungiya kula mahala – Pasi hodi na sumila – Siyo yetu mazoweya
43. Yalinakazi madaka – Ni wageni kuwadaka – Madaka ni kuwaweka – Na ndani kutotungiya
44. Ila awe ni mgeni – Wa kushukiya nyumbani – Hungiya na hamuoni – Aliyo ndani mmoya
45. Na uchenda safarini – Kashukiye hotelini – Sipende sana nyumbani – Ila ni kupita ndiya
46. Ukimwendeya nyumbani – Mwenye toto masikani – Au alo masikini – Taabuni humtiya
47. Na iwapo huna budi – Hukufanya kwa kasidi – Siku tatu usizidi – Siongeze hata moya
48. Na hilo wewe sitende – Ila mambo yakushinde – Mteremko sipende – Nyongo hukutumbukiya
49. Lojingi kiwa hapana – Au mfukoni huna – Nenda kwa hadhari sana – Kama kupoteya ndiya
50. Kiwa mtu mekwalika – Ni wajibu kuitika – Shughuli kimalizika – Musiweke mazoweya
51. Na wewe kwako nyumbani – Siifanye mno duni – Kuwa mtu wasitani – Kwa mapambo kuyitiya
52. Mtiliye mke wako – Zitu kwa kadiri yako – Ikiwa nafasi iko – Sibane ukaziwiya
53. Iwe maridadi nyumba – Na kwa zitu kuipamba – Fesheni ambazo kwamba – Kama yeye hutumiya
54. Mtiliye kula kitu – Awe kama wende watu – Simwambiye mimi kwetu – Haya sikuyazoweya
55. Akiwa mbwa minazini – Ukimueta muyini – Simuwate kutamani – Za wende kishuhudiya
56. Ukiwa umeamuwa – Muyini kumtukuwa – Mfanyie sawasawa – Sambe si ya kwenu haya
57. Simwambiye zitu hizi – Kwenu kupata huwezi – Kwenu ni kama kizizi – Hukuona mazuliya
58. Na chakula kadhalika – Mpe anachokitaka – Ambacho tafurahika – Mwenyewe mekizoweya
59. Akipenda biriyani – Mpe mwana simkhini – Maadamu mfukoni – Akiba imesaliya
60. Siku akitaka sima – Simwambiye ewe mama – Kula mtee lazima – Mimi sitaki udhiya
61. Muatiya na khiyari – Apendacho akhitari – Simkaze si uzuri – Masharuti kumwekeya
62. Ila kilicho haramu – Hilo sikiri fahamu – Haramu na kula sumu – Shariya imeziwiya
63. Ama kuhusu mavazi – Ya kaye na siku hizi – Sikiri ya kwenda wazi – Mishono yaso na haya
64. Kwetu sisi Isilamu – Mavazi kitu muhimu – Na sisi yatulazimu – Ya zipimo kwangaliya
65. Mpe mwenyewe nafasi – Ya kuteuwa libasi- Lako wewe ni fulusi – Towa za kununuliya
66. Mpe yako masharuti – Za mshono kudhibiti – Akikhalifu mehiti – Ni haki kumziwiya
67. Ama kitambaa gani – Kikuuliza mwendani –Au ni ipi launi – Wewe waifurahiya
68. Hapo makosa hapana – Kikuuliza kunena – Rangi hini naiona – Matoni imeningiya
69. Ama kiwa ni tamasha – Wataka mfurahisha – Si haja kumuonesha – Maoniye kwangaliya
70. Kata utakachopenda – Umtunukiye nyonda – Nawe hili ukitenda – Chochote takongoweya
71. Mke wako simdhiki – Simwambiye sina hiki – Na nyingi mno sitaki – Sizoweye kutumiya
72. Mpe kwa yako kadiri – Usifanye taqtiri – Ni twabiya si nzuri – Ubakhili kwenye haya
73. Na wewe upande wako – Ipambe kiyasi chako – Bora usivunde miko – Khatiyani ukangiya
74. Kuwa mtu maridadi – Utunge yako jasadi – Hata kufukiza udi – Ukiweza si khatiya
75. Iweke uwe nadhifu – Sionekane mchafu – Hini ni sunna tukufu – Ya tumwa wetu nabiya
76. Kiwa nyee umeweka – Zangaliye kadhalika – Siwate kusokoteka – Shungururu kusaliya
77. Ikiwa wafurahika – Mkeo akipambika – Yuwa nayeye hutaka – Nawe uwe huvutiya
78. Hiyo naye ndake haki – Takuwa hafurahiki – Iwapo hushughuliki – Muilio kwangaliya
79. Naye piya hutamani – Akikuona ndiani – Uwe nawe hisabuni – Penye watu utangiya
80. Au kiwa yako kazi – Kutenda haya huwezi – Wisapo vuwa magozi – Sivae kutembeleya
81. Sitembee na magwanda – Wala harufu za n’gonda – Fahamu watu hutunda – Na akilini hutiya
82. Na kadhalika ulimi – Ipinde uwe husemi – Yalo mawi huatami – Mke wako kumwambiya
83. Mno sana jitahidi – Kwa maneno maridadi – Wake hutaka zaidi – Yalo tamu kusikiya
84. Nena naye kwa dhihaka – Afurahi akicheka – Mwanamke huudhika – Mno kumnyamaliya
85. Mfanyie na ubishi – Kwa maneno yaso ghashi – Na kwake kuwa mteshi – Bila ya kupindukiya
86. Mwanamke ahitaji – Kuvishwa lasi fataji – Kwa hilo kuwa mpaji – Usichoke kumwambiya
87. Mwambiye kula namna – Sifa zake tena sana – Mfano ukimuona – Nyee mefunga upiya
88. Kiwa mesuka mikili – Au kuruni mawili – Siliwate yambo hili – Bila ya kulitumiya
89. Mwambiye umependeza – Kwa nyee kuzitengeza – Sina budi takutunza – Umshumu mara moya
90. Kiwa ametiya wanda – Mwambiye mno napenda – Siifanye hukutunda – Au hukumwangaliya
91. Kijifunga asumini – Au kikuba kitwani – Sichelewe kubaini – Neno lema kumwambiya
92. Yaani kula wakati – Mwambiye kitu katiti – Na kama bubwi siketi – Au duko tongo piya
93. Piya mpe shukurani – Kwa shughuli za nyumbani – Mfano pilau hini – Mno umeipatiya
94. Usichoke kumsifu – Kwa nyumba kuwa nadhifu – Na ukiona uchafu – Usiwe tamuukiya
95. Na faragha ukipata – Mbee yako kikupita – Usiwe utamuata – Mkono kumpekeya
96. Mshike wake mkono – Wala simkaze mno – Hutosha nukuta tano – Ujumbe kumpekeya
97. Kiwa amekukabili – Siitiye mashughuli – Inuwa yako mawili – Na yake kumwelekeya
98. Wata mato yafumane – Katiti yangaliyane – Kwa ulimi usinene – Lugha ya mato tumiya
99. Mato yana lugha tamu – Hunena mukafahamu – Mato kiungo muhimu - Cha huba kupaliliya
100.Mato yana kuu siri – Na mara hukuadhiri – Kakutoleya khabari – Moyoni uloziwiya
101.Hili nimenena sana – Ni muhimu naliona – Wala gharama halina – Na si kazi kutumiya
102. Walakini si sahali – Kwa kila alo mvuli – Kwa wangine ni thakili – Katu hawakuzoweya
103. Mbinu hizi izoeze – Zitumiye sizipuze – Utaona faidaze – Mwenyewe tashuhudiya
104. Mambo hayana gharama – Kwangaliya na kusema – Na mtu mke daima – Kama haya huzengeya
105. Mke huwa una mwako – Kuyuwa maoni yako – Kusikiya neno lako – Ni haja ahitajiya
106. Yuwa hatosheki mke – Kuvaa na kula kwake – Ataka na utu wake – Na hishima kumwekeya
107. Kula alo mtu mke – Hili ndilo umbo lake – La mapambo hilo kwake – Ni yambo meyazoweya
108. Hutokeya kwa nadira – Kwa hili wasoikera – Hina hapendi kuchora – Na wala wanda kutiya
109. Hana hayo mashughuli – Ni kama mtu mvuli – Ya urembo hayajali – Wala hakuyazoweya
110. Kiwa nawe wako mke – Hilo si shughuli yake – Basi nawe sisumbuke – Mashughuli kuyitiya 111. Na lengine la dharura – Ifunde mno subira – Kuna mambo ya kukera – Maishani yatokeya
112. Hakuna maisha tamu – Yenye raha ya kudumu – Mambo takuwa magumu – Kiwa hutovumiliya
113. Kuna tamu na utungu – Kwenye huu ulimwengu – Yalianda haya tangu – Yalipoumbwa duniya
114. Hini ndino kawaida – Kuna raha kuna shida – Ndiyo ya maisha ada – Na watu huwapitiya
115. Basi na kwako nyumbani – Siote kuwa peponi – Maadamu hapo ndani – Si wewe pweke mmoya
116. Mke wako si kivuli – Bali ni mtu wa pili – Una na yake akili – Una na alozoweya
117. Usitake kwa lazima – Kula yambo ukisema – Alikubali daima – Papo hapo kuridhiya
118. Muatiye makawanda – Anene anolipenda – Na kwa huja kikushinda – Siwe vito tatumiya 119. Ukiona sawa ndake – Ikubali uridhike – Na wala sikasirike – Mdomo kumfungiya
120. Kubali mezolinena – Umuunge tena sana – Na faida utaona – Mambo taandama ndiya
121. Na yeye kikasirika – Wewe usipande shuka – Na akizidi ondoka – Kishindwa kuvumilya
122. Mwanangu moto tizama – Hauzinyiki daima – Bali huzidi roroma – Kuni ukiutiliya
123. Moto kitotiwa kuni – Utazinyika mwendani – Na utesi wa nyumbani – Kunize ni neno baya
124. Ziwiya wako ulimi – Siwe na mwingi usemi – Ukinena hayakomi – Maneno huendeleya
125. Zidi na kuikukusa – Ulimi kutotapasa – Zita zenu zitakwisa – Moto mayi hutatiya
126. Na alo mume hodari – Kishindwa yeye hukiri – Ili kwepuka dothari – Ya ufa sini kutiya
127. Sini ikingiya ufa – Hupunguwa zake sifa – Na mahaba nayo hufa – Ukiwa mwingi udhiya
128. Hakuna katu hakuna – Kiumbe kamili sana – Na watu hutukuwana – Ndipo waishi pamoya
129. Kiwa lazima wataka – Mke alokamilika – Juwa na wewe hakika – Takubidi kutimiya
130. Aso taa ni tomomo – Hunu ni kweli msemo – Watu hupitana zimo – Huzidiyana twabiya
131. Mke kikukasirisha – Jaribu kuyikumbusha – Piya hukufurahisha – Mezani hini tumiya
132. Usiyaone ya jongo – Kwa mema ukawa tongo – Sangaliye penye pengo – Kawata palotimiya
133. Huna budi kupuuza – Na mangine kuyamiza – Ndipo muweze kufuza – Na maisha kwendeleya
134. Mke kitenda makosa – Kumwambiya yakupasa – Kwa hishima na siyasa – Na hikima kutumiya
135. Kosa kulisahihisha – Penye watu hujeresha – Ipinde kupurukusha – Faragha kuizengeya
136. Simwambiye penye watu – Haukiri wake utu – Wala hutengezi kitu – Bali ni kinyume huya
137. Kumsifu ni uzuri – Penye watu na dhahiri – Kulaumu ni kwa siri – Ndipo atakusikiya
138. Mwanaadamu kukosa – Ni yambo limetupasa – Ni sawa kuyikukusa – Mangine kuvumiliya
139. Lisamehe kosa dogo – Kosa likiwa mzigo – Halipeleki kishogo – Zengeya nyengine ndiya
140. Tafauti za nyumbani – Ziwe ni siri za ndani – Sizitowe hadhirani – Watu wakazisikiya
141. Siri za ndani zibane – Usimwambiye mngine – Wewe na yeye munene – Suluhisho kuzengeya
142. Ila mukikosa budi – Kunena ikawabidi – Wazee wawasaidi – Hapo haiwi hatiya
143. Tafauti ikizuka – Ni mikono kuyandika – Yua nde ikitoka – Huzuwa nyingi balaya
144. Khususwa siri za siri – Kunena ni kuadhiri – Ila iwe dakitari – Suali mewataiya
145. Mambo ya tini kwa tini – Yawe ni ndani kwa ndani – Hayo muwe hamuneni – Ila yakiwaemeya
146. Kiwa mno mewaganya – Mukashindwa la kufanya – Kwa hapo sitowakanya – Ushauri kuzengeya
147. Ni bora uwe hodari – Na kushindwa usikiri – Wala usitahayari – Kwa halali kutumiya
148. Ni hiko hiko kitendo – Kiwa wa halali mwendo – Haramu iweke kando – Katu kutokaribiya
149. Wa haramu simguse – Kimuona igegese – Hata nyangwani mpise – Sandamane naye ndiya
150. Usende hata karibu – Epuka hizo iqabu – Utapata na thawabu – Mkeo kumngiliya
151. Elewa sana elewa – Ni jukumu umepowa – Mkeo kumwisa ngowa – Kwa haya nimezotaya
152. Mkeo mtosheleze – Haja yake amalize – Na shauku asisaze – Mparo Ukamwatiya
153. Ongeza wako uyuzi – Wa kufanya hiyo kazi – Mwendo kiwa hamalizi – Fahamu wamkoseya
154. Huwa ni kuu dhuluma – Wewe ukisakukoma – Hutaki geuka nyuma – Na yeye kumngojeya
155. Simalize yako haja – Mngoje mwise pamoja – Hili hataki mmoja – Ni nyote hulizengeya
156. Angaliya ufikiri – Kiwa mwendo taghairi – Na wewe penye bandari – Bado nanga hujatiya
157. Utakuwa hali gani – Usingizi huuoni – Hali hiyo ubaini – Na mwendo humuiliya
158. Atakuwa na mtaro – Na dhiki mno na kero – Na hasira na mfuro – Kiwa hutomridhiya
159. Nyumba nyingi huvundika – Zikikosa muafaka – Kwa ngono kutotosheka – Mke na mume pamoya
160. Kwa hili mukitoshana – Mengi huvumiliyana – Mno hukorofishana – Hili lisipotimiya
161. Na lingine kadhalika – Ambalo kwako nataka – Ni mkeo kiudhika – Usiwe tamfuriya
162. Pangine utamuona – Hufura sababu hana – Muelewe tena sana – Na mno kumuyuliya
163. Ifahamu tafauti – Waliyo nayo banati – Hawezi kuidhibiti – Hali inapowadiya
165. Mke si kiumbe dufu – Walakini ni dhaifu – Moyo wake ni khafifu – Hushindwa kuvumiliya
166. Wanawake wana umbo – Huathirika kwa mambo – Katiti yakenda kombo – Wasi wasi humtiya
167. Katika siku za ada – Ya mwezi hupata shida – Ndipo hata na ibada – Mungu kawapunguziya
168. Mno huwa ya thaqili – Na hubadilika hali – Na chote kiwiliwili – Huwa katika udhiya
169. Huwa sana ni wayavu – Hukosa uvimilivu – Huwa kama ivu ivu – Kutumbuka huzengeya
170. Huwa mno ni wakali – Nadhani hata akili – Haiwi sawa kamili – Na punguwani hungiya
171. Kula mara tamuona – Huwarukiya zijana – Na kwa ukali hunena – Kinyume cha mazoweya
172. Ni muhimu kula mume – Mke wake amsome – Kwa zipimo ampime – Siku zikikaribiya
173. Ukisa kumfahamu – Uwate kumlaumu – Hili mno ni muhimu - Yataka kulizoweya
174. Kuna na muda wa mimba – Mara kwa mara huvimba – Ukaona kana kwamba – Mekuwa hukuzengeya
175. Kukosa yambo katiti – Huwa wewe umehiti – Angaliya kibiriti – Kidarika tete huya
176. Mara nyama haitaki – Ataka nsi wa siki – Alacho hakimshiki – Akitiyacho humwaya
177. Zielewe siku hizi – Mimba na siku za mwezi – Kiwa humbembelezi – Taona wamuoneya
178. Mpembe kama kijana – Tena aliyo mnuna – Ndipo mutasikizana – Na yadumu mazoweya
179. Sharuti uwe mwerevu – Na mno mvumilivu – Usifurishe mashavu – Kiwa naye meteteya
180. Kuna mambo ya umito – Ni makuu si matoto – Wengine hula tototo – Na mtanga hubugiya
181. Ni mambo ya miujiza – Zao hali hugeuza – Kiwa hutobembeleza – Mara taona huliya
182. Mwanamke kwa taabu – Mara hufanya ghadhabu – Hata alo taratibu – Hubadilika twabiya
183. Neno lolote aweza – Hajali kuvurimiza – Ni sharuti kuikaza – Mizani kutopoteya
184. Mara aweza talaka – Akakwambiya nataka – Nawe ukikasirika – Mayuto yatasaliya
185. Akikwambiya niwata – Siwe naye mutateta – Ni kiwingu kitapita – Hakiwezi kusaliya
186. Twalaka siiteleze – Aitakapo mpuze – Wala siitendekeze – Lake kumtimiziya
187. Twalaka Mungu meweka – Kwa dharura kutumika – Iwapo mumedhikika – Mumekosa zote ndiya
188. Kushaliki mushindwapo - Twalaka huwa ni hapo – Na muda uitowapo – Usiizidishe moya
189. Timiza na masharuti – Ya hali piya wakati – Na hukumu zitafiti – Kabula ya kutumiya
190. Kuna watu huwatana – Kisa mara huwaona – Kwa haramu watakana – Zipengee huzengeya
191. Huzengeya muhalili – Fikiriya yambo hili – La kuazima fahali – Mke kwenda mpekeya
192. Na langine kadhalika – Ni kwa mmoya tosheka – Ila kiwa medhikika – Haikupinga shariya
193. Mke siowe wa pili – Ni udhiya kweli kweli – Na ingawa ni halali – Ni uzito kutumiya
194. Na wanawake si sawa – Kwa wengineo ni dawa – Utaiyuta kuzawa – Nimekwambiya Yahaya
195. Kuna wanao ridhika – Wangawa wanun’gunika – Kuna wangine huwaka – Fununu wakisikiya
196. Kuongeza si haramu – Walakini ufahamu – Ni kuu mno jukumu – Mbali na wake udhiya
197. Ikiwa sababu iko – Kwa mfano mke wako – Mepowa mikali miko – Kwa dharura za afiya
198. Labuda hana kizazi – La kuzaa haliwezi – Nawe wataka pumbazi – Yapo ni mwana mmoya
199. Au yale mashughuli – Yeye humpa thaqili – Nawe kusitahamili – Huliwezi hilo piya
200. Kwa dharura ziso budi – Usitende kwa kasidi – Kuengeza wa zaidi – Kitosheleza mmoya
201. Kwa mmoya kutosheka – Ndiyo bora bila shaka – Kuengeza ukitaka – Ni kama nilokwambiya
202. Usiwe kiruka mto – Khasa kiwa na watoto – Kuna hisabu mzito – Akhera takungojeya
203. Usiifanya cha nyuki – Hutuwi na hudiriki – Ukishikwa hushikiki – Mara huwa umeteya
204. Kiwa umependa tunda – Huna budi na kupenda – Mti wake tangu kwanda – Wazee walitwambiya
205. Nawe kimpenda mke – Wapende wazee wake – Wakwe mbwako siepuke – Na hishima kuwekeya
206. Muhishimu wake mama – Piya babake daima – Kuwadharau si wema – Tono nawe tamtiya
207. Kwa uovu siwanene – Itunge siwatukane – Hata kama huyo mwane – Hishima mewavundiya
208. Wewe katu sisubutu – Kudharau hao watu – Hata kama utukutu – Kwao umeshuhudiya
209. Kiwa ni watu matata – Sio nao utateta – Kheri mbali kuivuta – Na mambo kuangaliya
210. Ukiwa una nafasi – La kuwapa sikuwasi – Ila fanya kwa kiasi – Siye dewe kakutiya
211. Kuna wakwe wa wangine – Kwa kupata wadengene – Kiwa nao upembene – Hadhari nakuusiya
212. Wangine ni watu sana – Katu hawakudangana – Hata kiwa haja una – Haandami kukwambiya
213. Hanandi hata nyumbani – Kwa mwanawe katamani – Kucha watu wasidhani – Amekwenda kutawiya
214. Ndiyani mukikutana – Huwa na haraka sana – Hamakiniki kunena – Kwa lilo kulikimbiya
215. Wakiwa wakwe wa wako – Kwao hizi sifa ziko – Basi ni bahati yako – Ni hapo pa kuziwiya
216. Ama wakweo wakiwa – Ni wa kupenda kupowa – Kuwapa hukuzuwiwa – Mkono kuwanyosheya
217. Usiweke kama ada – Kisa takweteya shida – Ila wawe si labuda – Ni watu wahitajiya
218. Wakiwa ni wahitaji – Siwangoje kutaraji – Wakiwa kwako hawaji – Ni sawa kuwapekeya
219. Ukiwa umewaona – Si watu wenye maana – Ni wale wa kudangana – Wa kupenda kupapiya
220. Ziwiya sitowe chako – Na mwambiya mke wako – Ila hutofu sumbuko – Birika mbovu kutiya
221. Ama wasio wazazi – Wajomba na mashangazi – Hapo kuna ngumu kazi – Kwa yetu hini duniya
222. Kwanda usiwatapiye – Keti mbali wangaliye – Ukiyaona mamboye – Ndiya hayakwekeleya
223. Usende sana karibu – Taivutiya taabu – Ni wengi wa kuharibu – Katika nimezotaya
224. Ama mashemegi zako – Dada zake mke wako – Mwanangu sivunde miko – Ilowekwa na shariya
225. Usiondowe mipaka – Kwa mzaha na dhihaka – Mara mambo hugeuka – Kizaazaa kikaya
226. Kheri wambiwe muovu – Kuliko kupata kovu – Kheri wambe una wivu – Kuliko kukuvundiya
227. Wivu ni kama kiungo – Ukizidi ni tewengo – Piya kuyifanya tongo – Uduyuthini hungiya
228. Na kuukosa kabisa – Ingawa ndiyo kisasa – Hiyo si njema siyasa – Ya nyumbani kutumiya
229. Ni lazima kuwa nao – Kwa aliyo ni mkeo – Kikuzumbuwa hunao – Matoni hutomngiya
230. Kuwa nao wa kadiri – Hiyo ndiyo dasituri – Na kwa mke ni fakhari – Kwa wende tayivuniya
231. Na fufnunu ukipata – Kuwa mke ni mtata – Siinuke na kuteta – Kwanda zidi kwangaliya
232. Simtukuliye dhana – Kwa kuwa waja hunena – Hilo ni khatari sana – Mayutoni takutiya
233. Iziwiye usubiri – Uhakikishe khabari – Tena ufanye kwa siri – Pasi na kupija mbiya
234. Ikiwa umetosheka – Hilo ni yambo hakika – Kwa taratibu epuka – Bila sababu kutaya
235. Sitaye yako sababu – Utazidi kuharibu – Zitatangaa aibu – Na si wema kueneya
236. Na hilo kisa kutenda – Huna budi kuipinda – Hata kama una nyonda – Siwe nyuma tarejeya
237. Ipinde ipinde mno – Sibadili lako neno – Mwiso tapata usono – Yatatoka mazoweya
238. Utasukikasukika – Kiwa moyo wamtaka – Fahamu tafedheheka – Kiwa hutoiziwiya
239. Iziwiye ikukuse – Mpaka mahaba yese – Penyenye usiyapise – Moyoni kakurudiya
240. Mwisowe yataondoka – Na wewe utaafika – Kuliko kufedheheka – Na izarani kungiya
241. Lakini nakukumbusha – Kiswa cha nana Aisha – Vurumai walizusha – Mawi wakamzuliya
242. Walionena ni wengi – Wakafanya na magengi – Na zikao za mitingi – Madina zikaeneya
243. Kwa yambo liso asili – Kwa mke wake rasuli – Katu halikuwa kweli – Ni uvumi walitiya
244. Mwangaliye na mtumi – Alikuwa haatami – Aliziwiya ulimi – Mpaka wahayi kuya
245. Yataka mno hadhari – Katika hizo khabari – Siwe mpesi kukiri – Yambo ukilisikiya
246. Tafiti tafiti sana – Hata shaka uwe huna – Ndipo hapo lako nena – Bila sababu kutaya
247. Hapa sasa nitakoma – Wala yote sikusema – Lakini ukiandama – Haya takusaidiya
248. Niya na yangu dhamiri – Kwandika kwa mashairi – Ni kueneza khabari – Kwa wenye kuyasikiya
249. Ni sahali kusikiza – Kaseti moya huweza – Wengi wakapulikiza – Wakasikiza pamoya
250. Lau kama ni kitabu – Wasomaji ni hububu – Wengi huona taabu – Kusikiza mezoweya
251. Kauli yangu tamati – Ni zenu hizi baiti – Wavulana mabanati – Nyote nawakusudiya

MWISHO WA UTENZI.

Mtungaji: Ustadh Mahmoud Ahmad Mahmoud (MAU) – Lamu mwaka 2004

Umeletwa na Saleh Barkey tarehe 28 February, 2005

Maana ya maneno yenye lahaja ya Kilamu ambayo ndiyo iliyotumika katika utenzi huu.

Beti

13. Shuguu la uni = Imekusudiwa asiekuwa na thamani au asie kufu yako
15. Hakumbiriya = Kutupa
18. Ina = Jina
21. Jongo = Ya makosa
22. Sheshegi = Vishindo ; Gogi = Kukinai mpaka kufikiya kudharau
27. Tutu = Mahindi ; Ufu = Nazi
Tutu kwa ufu hapa imekusudiwa mchanganyiko wa wanaume kwa wamawake
28. Wangakazaniya = Ingawa wengi wamekazaniya
29. Kutoeleya = Kutoelewa / Kutojuwa / Kutofahamu
39. Usimliche = Usimuache ; Mche = Muogope
43. Madaka = Baraza ya nje ya nyumba ; Kutotungiya = Kutochunguliya
46. Toto = ndogo
54. Wende = Wenzake
72. Taqtiri = Ugumu ( Hili neno TAQTIRI si katika lahaja ya Kilamu)
73. Ipambe = Jipambe
75. Iweke = Jiweke
81. Hutunda = Huchunza / Huangaliya
86. Fataji = Inayon’gara
92. Katiti = Kidogo ; Bubwi = Bubu ; Duko = Kiziwi
94. Tamuukiya = Utamrukiya
105. Una mwako = Una kiu
116. Una = Ana
118. Makawanda = Nafasi
120. Mazolinena = Alilolinena / Alilolisema
125. Kutotapasa = Kutosema
125. Sini = Harufu ya SIIN “S” mfano sitaki, siwezi, sina, sipendi nk
130. Aso taa ni tomomo = Aso hili ana lile
132. Sangaliye = Usiangaliye
135. Kujeresha = Kutahayarisha
139. Kishogo = Kichogo ( Kwenye ubeti imekusudiwa “Haikurudishi nyuma” )
141. Mngine = Mwengine
146. Mewaganya = Yamewaelemeya / Yamewazidi
149. Igegese = Nenda pole pole ; Nyangwani = Jangwani
158. Mtaro = Sababu ya kutafuta ugomvi
175. Umehiti = Umekoseya ; Kidarika (ikidarika) = Ikigusika ; Tete = Cheche
176. Nsi wa siki = Samaki wa siki
180. Tototo = Matope
188. Kushaliki = Kukarabati
203. Umeteya = Umeteleza
210. Dewe = Khasara
211. Wadengene = Wanapaparika ; Upembene = Umepata mtihani
213. Hanandi = Haji
227. Tewengo = Matatizo ; Uduyuthi = Ubaradhuli / Uzembe
233. Kupija mbiya = Kupiga mbiu / Kutangaza
237. Usono = Kipumbazi
239. Penyenye usiyapisa = Upenyo usitowe / Usitowe nafasi hata ndogo

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet