Vyako!
- Vyako ukiviandama - Huja kusibu pekeyo
Vyako vyako ni hasama - Kugombana na wenziyo
Vyako haiji kwa wema - Vyako usijuwe siyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako ujapo ishika - Ukasema vyako ndiyo
Vyako havitatindika - Ukabadili mamboyo
Vyako hukutiya shaka - Uwapo mtu na payo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Ni vyako na kwamba kwamba - Ati na toba sikiyo
Vyako viumbe hugomba - Japo awe ni mwenziyo
Vyako huvunja majumba - Ukamuacha mkeo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako ukiishiriki - Hutembei kwa nduguyo
Vyako hupati rafiki - Huna mwema umrio
Vyako ukiisadiki - Mwema huwa khasimuyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako vyashinda kudhani - Usishike yasemwayo
Vyako hupati mwandani - Huna mwana maishayo
Vyako vingi ni shetani - Imithili nafsiyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako ukiisarifu - Husemi na mpenziyo
Vyako ni jambo dhaifu - Mtu hula manenoyo
Vyako ifanye khafifu - Uisitiri haliyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako vyako ni hasara - Mwisho ni vyako pekeyo
Vyako mtu humkera - Kheri pima akiliyo
Vyako usipofikira - Wavunja mpya nyumbayo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako ndiyo usalata - Shatti uone machoyo
Vyako ukiifuata - Asahi wafa pekeyo
Vyako vyaleta ukata - Ukesha piya mamboyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako waipendeleya - Ya vyako ina kiliyo
Vyako yawaharibiya - Musishike yasemwayo
Vyako mwisho hujutiya - Mwenzangu duniya siyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako ndiyo kudanganywa - Hasa zamani za leo
Vyako chako hunyan'ganywa - Daima ukenda mbiyo
Vyako mwishowe huchunywa - Na wingi wa vizomeyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
- Vyako hakika si njema - Tammati ni kishiliyo
Vyako usipoipima - Waudhika maishayo
Vyako hushikizwa tama - Nawe ukasema ndiyo
Vyako hubadili moyo - Ukagombana jirani
Ali Said Al-Jahdhamy (Kamange)