.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

VITA VYA WADACHI KUTAMALAKI MRIMA

 

Related links

Vita Vya Wadachi Kutamalaki Mrima

Napenda kuwaleteeni utenzi huu mrefu wa beti 632 unaoitwa "VITA VYA WADACHI KUTAMALAKI MRIMA". Utenzi huu umetungwa katika mwaka 1891 A.D. (1307 A.H.) na Sheikh Hemedi Bin Abdallah Bin Said Bin Abdallah Bin Masudi El Buhry. Kwa bahati nzuri katika ukumbi wetu huu wa ZANZINET tunae mwanaukumbi mwenzetu ambae ni kilembwe (au hata kifuta miguu) wa mtungaji wa utenzi huu. Utenzi huu ni moja wapo katika kazi ziliochapishwa kama ni JOHARI ZA KISWAHILI ( Swahili Classics) katika mwaka wa 1955 na East African Literature Bureau wakati huo.

J. W. T. Allen ambae ameufasiri utenzi huu kwa Kiingereza amesema haya kuhusu utenzi huu:

" Vita vya Wadachi is in a different category from other tenzi. We know that umetungwa na means composed and written by Hemedi bin Abdallah and not that Hemedi worked over an earlier version of a poem. We may therefore be certain that the language is as it was originally written, and except for a few doubtful slips, that we have the version as originally composed. Historically it is a remarkable work; no one would expect a poetic dramatization of history only five years old to be strictly accurate in detail; but except for some poetic licence the poem is a plain record of fact and genuine autobigraphy. 'It is psychologically true' and the feelings of the conquered peoples are vivid and convincing."

Burudikeni na Vita Vya Wadachi Kutamalaki Mrima ...

1. BISMILLAHI Ghafari - Al Wahidi 'lKahari - Mwinyi kuhui shajari - Na jinni na insiya
2. Yu pweke ARRAHMANI - Wala hayuko wa thani - Mruzuku duniani - Ila ni yeye mmoya
3. ARRAHIMI siku ya nyota - Tawapeleka janata - Ambao wametakata - Na maasi ya dunia
4. Ndiye muumba Jannati - Ardhi na samawati - Na vilivyo katikati - Muumba ndiye Jaliya
5. Ndiye muumba bahari - Na shamsi na kamari - Na nyota zikakithiri - Ili anga la dunia
6. Ndiye muumba tuyuri - Kuruka pasi shajari - Kwa uwezowe Jabbari - Jalla waala Taaa
7. Ndiye muumba rasuli - Muhammadi mfadhili - Tena akamjamili - Haiba ya mambo pia
8. Kwanza kampa jannati - Ya lulu na mayakuti - Na kushufai umati - Siku ya kiu na ndaa
9. Kampa na Kur'ani - Na sabaa 'lmathani - Na nuru za duniani - Kampa kamuatia
10. Na jamii mashahidi - Akapewa Muhammadi - Mitume yote idadi - Hapana aliyepewa
11. Kampandisha mbinguni - Kwa huba yake Manani - Kamtia na peponi - Kabla kutawafaa
12. Sifa za Rabbi Majidi - Na mtume Muhammadi - Ufantapo jitihadi - Kufuruni hutangia
13 Sasa nashika kalamu - Na karatasi ya shamu - Ambalo nalifahamu - Nilandike moya moya
14. Niname nitafakari - Nipige zangu nadhari - Nelekeze ushairi - Na kwamba utalekea
15. Na moyo nitoe ghashi - Niwakhubiri Madachi - Na nipatalo siachi - Na wenzangu kuwambia
16. Nitulize moyo wangu - Tuwe pamoya wenzangu - Niwakhubiri Mzungu - Awali na akhiria
17. Kwanza nitake auni - Kwakeye Mongu Manani - Na Muhammadi Amini - Na mitume yote piya
18. Nidhukuru Allahumma - Ndiwe mwingi wa rehema - Muabudiwa dawama - Ni jinni na insia
19. Tunusuru waja wako - Vita vya adui zako - Wakataa dini yako - Tusiabudu Taaa
20. Na mtume Muhammadi - Sala 'ILahu Sayyidi - Tuombeeni Wadudi - Tunusurike na baa
21. Na baba yetu Adamu - Na Musa na Brahimu - Tuombeni karimu - Atwondolee udhia
22. Na Nuhu na Idrissa - Shuaybu na Yunusa - Na Zakaria na Isa - Tumbeeni Jaliya
23. Na Isahaka dhabibu - Na Sami waladi Nuhu - Na Yushau na Salehu - Nyanda zenu ni kwinua
24. Pamwe na Ismaili - Yeye Dhu 'lKifili - Muombeni tashili - Rabi kutusahilia
25. Yusufu na Yaakubu - Na Harunu na Ayubu - Tuombeeni Wahabu - Mwinyi ezi na kusaa
26. Daudi na Sulemani - Na Ilyasi yuani - Na Lutu na Lukmani - Na tumwa Hudu pamoya
27. Thuma na tumwa Yahaya - Rabbi ni kutuombea - Atwondolee udhia - Kwa ezi yake Taaa
28. Thuma na Abubakari - Na Sayyidina Umari - Khalifa zake Bashiri - Muhammadi mfadhaa
29. Na Sayyidi Athmani - Na Sheikhe Abu Hasani - Na Abdirahmani - Bin 'Aufi sikia
30. Na Hamza na Abbasi - Mulioshinda Majusi - Tuombeeni Kuddusi - Atunusuru Jaliya
31 Na Hasani na Huseni - Dhuria wake Amini - Kwa Mungu tuombeeni - Dini yetu yapotea
32. Na Taha na Zubairi - Ndinywi wapiga kufari - Kwa saifi na khanjari - Dini mukaiwania
33. Fadhili na Msllemu - Wana wa Bani Hashimu - Waungwana mulotimu - Msio shaka na tuwa
34. Thuma Bin Maadi - Na mwana wa Aswadi - Wazoefu wa hadidi - Kula utambo kungia
35. Amru bin 'lAsi - Yeye ni Bin Unaysi - Tuombeeni upesi - Atwondolee balaa
36. Na Sayyidina Khalidi - Mzaliwa ni Walidi - Na jamii masayyidi - Rabbi ni kutuombea
37 Ewe Mama Mwana Hawa - Mikono yako inuwa - Duayo itapokewa - Uombalo litakuwa
38. Thuma na Mwana Fatuma - Na Khadija wako mama - Pamoja na Mariyama - Binti Imraniya
39. Na Zaina na Sakina - Wewe na Mwana Hasina - Ndinywi mnao majina - Na Ummi Kulthumiya
40. Na Aisha na zuhura - Na Zalikha na Asira - Ndinywi wanawake bora - Mtakalo mwalipewa
41. Na Khatuni na Asiye - Na Halima na Radhiye - Saliha na Atikiye - Leo nawakumbukia
42. Uwapi Mwana Mayasa - Khaulata na Anisa - Mkaomba kwa Kuddusa _ Subhana wa taa
43. Uwapi Mwana Hanifa - Na Zaina na Afifa - Na Salima na Zalifa - Wanawake mashujaa
44. Amina na mwana Hinda - Inuani zenu nyanda - Atende mwinyi kutenda - Atujalie wasaa
45. Nishao hao kutaja - Mtu mmoja mmoja - Ndipo nidhukuru haja - Niliyoikusudia
46. Na mimi kusudi yangu - Iliyo moyoni mwangu - Kisa cha hawa Wazungu - Takacho wahadithia
47. Mwanzo wake hikutubu - Walifunua vitabu - Kususu na marahibu - Vyuo wakaangalia
48. Wakatunza majahili - Taurati na Injili - Vyuo vikawaratili - Kwingiliwa ni wakaa
49. Wakasoma taurati - Wakaona katikati - Kungiliwa na mauti - Wala yasiyo wasaa
50. Wakakiona kitali - Wala kisicho mithali - Na watu wingi kudhili - Katika zote kariya
51. Kuona kwao hakika - Miji haitatuweka - Wakataka pa kushika - Mahali pa kwenda kaa
52. Wakajua kwa dalili - Jihadi itawasili - Wakaona Sawahili - Ndiko kwa kukimbilia
53. Wakauzana shauri - Kuwaza na kufikiri - Wengine wakadhukuri - Wenzi wao kuwambia
54. Sawahili na twendeni - Tukafika tujengeni - Wengine wakabaini - Sisi haya kututua
55. Vyuo vyetu tukitunza - Mbona hatutokuweza - Twakuona kuna jiza - Kama wingu la mvua
56. Nti haitatuweka - Na damu itamwagika - Wengine wakatamka - Ajabu kubwa ajaa
57. Kama ile Sawahili - Watu walio dhalili - Wawezaje kukabili - Kwa harubu na kitaa
58. Hayo musitutajie - Na twendeni tukangie - Tukajenge tukakae - Kwa urembo na wasaa
59. Linalo saza yuani - Twendeni kwa Sultani - Tukamwambie yakini - Kama tuloazimia
60. Atakapo bwana wetu - Sasa hivi twende zetu - Maana hakuna mtu - Awezaye tuzuwia
61. Basi wakafuatana - Kwenenda kwa wao bwana - Kufika akawaona - Kawauliza jamaa
62. Mna nini waalimu - Jambo mlilo azimu - Wote wakatakalamu - Samaa laka wa taa
63. Jambo tunalokujia - Vyuo tumeangalia - Tumeiona Ulaya - Kungia vita ajaa
64. Tumetafuta makamu - Ya kwenda kustakimu - Tumeiona fahamu - Nti ya Sawahilia
65. Twataka tukaikaye - Tumuweke tutakaye - Tumwondoe twondoaye - Tutume tukitumia
66. Tukajenge na majumba - Tukithiri kuyapamba - Na kula mwinyi kasumba - Tumtoe jeuria
67. Ni hilo shauri letu - Wasemaje bwana wetu - Turukhusu twende zetu - Au ni kutuzuia
68. Bwana wao kabaini - Nti hi nambiani - Na jina la Sultani - Nami nipate lijua
69. Kishakwe sema Hamamu - Wote wakatakalmu - Hayo hatuyafahamu - Kuyajua moya moya
70. Wajuao matajiri - Hao wenye kusafiri - Ndio wenye tadbiri - Nti hiyo kuelea
71. Uwatake waje hapa - Kwa haraka na kipapa - Sifa zake watakupa - Jamii watakwambia
72. Akaweta Sultani - Jamii makaptani - Wenendao kwa dukhani - Bahari kuzipasua
73. Na jamii matajiri - Wazoeleo bahari - Jamii wakadhihiri - Kwa kwitika amria
74. Sultani akakuli - Nambiami tashili - Nti gani Sawahili - Nami nipate ijuwa
75. Nimeweta kunambia - Nti hiyo kunelea - Na huyo mwinyi Ulaya - Jinale nahitajia
76. Nambiani jina lake - Na jina la mji wake - Manakhodha watamke - Tusikie Maulia
77. Nti hiyo mbwakhubiri - Iko ndani ya bahari - Bi khamsi ashuhuri - Ndipo waifikilia
78. Sharti wende na maji - Bahari inayo mji - Twenendeya uhitaji - Ila tusingekuja
79. Wapita bahari ngumu - Lujjati na kalzumu - Na uyuni na dhulamu - Jamii utazingia
80. Hata uone ishari - Bahari ya akhadari - Jina lake kerkeri - Jua umekaribia
81. Na bandari ina myamba - Mara dukhani huwamba - Huwezi tupiwa kamba - Kwa bandarize udhia
82. Mji wake mbwakhubiri - Jina lake Zinjibari - Kwanza utaona nuri - Kabla hujafikia
83. Ni jina la mwinyi sifa - Ni Sayyidina Khalifa - Alokuzwa ni Latifa - Kimkuza akakuwa
84. Jina la mwinyi biladi - Khalifa bin Saidi - Mtamalaki junudi - Sharki na gharbia
85. Ni mkubwa wa nasabu - Kabila ya Kiarabu - Na jina la wake babu - Sultani nawambia
86. Ni asli ya Imamu - Jina la mwinyi makamu - Waungwana walotimu - Wasio shaka na tuwa
87. Naye huyo Sultani - Mjiwe u kisiwani - Na sairi buldani - Amriye yasikiwa
88. Maneno utuuzayo - Ni hayo tukwambiayo - Akakyangua kiliyo - Sultani akaliya
89. Mzungu kaliya sana - Na wote maruhubana - Kisha wakanyamazana - Wote wawele nyamaa
90. Wakanyamaza matozi - Wana hamu na simanzi - Kwa kutajwa mwinyi ezi - Na vyuoni wamjua
91. Baada ya kunyamaza - Rahibu wakamuuza - Lipi lililokuliza - Twambie tupate jua
92. Mzungu akatamka - Roho yangu ina shaka - Watu wangu kudhilika - Na baa kuwashukia
93. Maana nina kitabu - Cha tangu abu na abu - Siku moja hajaribu - Usiku hakifunua
94. Hatwaa hasoma sana - Haona kwaja kijana - Himtunza lake jina - Lina fau akhiria
95. Jina lake maalumu - Katikati lina lamu - Mwisho wa yake isimu - Fau imekwishilia
96. Na mwana huyo wenzangu - Ndiye mdhiki Wazungu - Nina hamu roho yangu - Jina mnalo nambia
97. Nambiani sifa zake - Nti na biladi yake - Na hiyo kaumu yake - Msiate neno moya
98. Kimaa kuwauliza - Jamii wakanyamaza - Wakakhofu kurejeza - Kumsifu mauliya
99. Wakakhofu kukhubiri - Kuja yakamkasiri - Khatima akadhukuri - Kwani kuninyamalia
100. Nawauza nambiani - Sifa zake Sultani - Akondoka kaptani - Jina lake tawambia
101. Jina lake maarufu - Ndiye Mushti Kirofu - Moyo akatoa khofu - Mbele akamtokea
102. Akenda mbele yuani - Na chepeu mkononi - Akakipiga na tini - Mara tatu kutimia
103. Khatima akamwambia - Sifa za mwinyi ulaya - Jamii takusifiya - Moja sitakubakia
104. Sifa zake tatamka - Sultani hana shaka - Mzuri wa kuumbika - Simuene na mithaa
105. Wajihiwe mdawari - Wadanda kama kamari - Huwezi kuubusuri - Kwa haibaze sikia
106. Uso wake mdawara - Na pua kama kitara - Na nuru yake yan'gara - Ni ajabu nawambia
107. Na hapo alipokaa - Patia mtu fazaa - Pametuka kama taa - Kwa matandiko ajaa
108. Matandiko ya hariri - Mekundu na akhdhari - Wendapo kuyabusuri - Matoyo hukupotea
109. Johari na mathoreya - Mengapi takusifia - Huwezi kuzangalia - Mato yako kuyenua
110. Barazaye Muarabu - Ni matovu ya dhahabu - Ukenda wataajabu - Kwa hali ilivyokaa
111. Pamejengwa kwa imara - Na mapambo bora bora - Mbaya hungia sura - Ambapo wakurubia
112. Naye huyo Sultani - Kiwasili barazani - Kama simba ghadhbani - Huwezi kumwangalia
113. Mkononi yuna sefu - Na khanjari maarufu - Shujaa hungia khofu - Ru'uba ikamwingia
114. Akakipiga kilemba - Ameketi kama simba - Mnene huwa mwembamba - Endapo kushitakiwa
115. Na moyo wake makini - Hana fazaa moyoni - Ndiye huyo Sultani - Asiye shaka na tuwa
116. Na hukumuye idili - Ukenda hukusaili - Ujapokuwa dhalili - Sharaa utaipewa
117. Ayna bi 'layni - Udhna bi 'ludhuni - Wa sinna bi 'ssini - Auwaye huuawa
118. Pana na hao kaumu - Walume waliyotimu - Katta hawatabasamu - Daima wametukiwa
119. Hao hawana kusema - Ukenda wamesimama - Na saifu njema njema - Zote wamezichomoa
120. Panga zao wameshika - Wala hawana kucheka - Na ufanyapo dhihaka - Jua utakwangamia
121. Na Ajemi wa langoni - Wana panga mikononi - Kama nyoka wa motoni - Kwa ghadhabu kuwangia
122. Ndipo ahli nadhamu - Kama simba darghamu - Kula palipo pagumu - Ndio wenyi kufungua
123. Pana wengine walume - Kabila ya Hadharume - Nyamaza usiwaseme - Afadhali kunyamaa
124. Na wengine askari - Waarabu mashuhuri - Ambao wamejikiri - Kwa upanga kuelea
125. Askari wa kimanga - Wapo wameshika panga - Huwawezi kuwawenga - Mato yako kuyenua
126. Mji wake umejengwa - Umerakibu mizinga - Na kaumu wamezinga - Kama taka za majaa
127. Mizinga ameiweka - Mjiwe umezungukwa - Wangapi wenye tafaka - Askari mashujaa
128. Baghala na marikabu - Kam hazina hisabu - Wahindi na Waarabu - Wengapi takutajia
129. Na nyingapi manuwari - zilizoko Zinjibari - Kusifu watahayari - Kwenda mno wapotea
130. Mji wake umepambwa - Na uzuri wa majumba - Na mto ameutimba - Maji mjini hungia
131. Mto u ndani ya mji - Kula utakapo maji - Kusema hakuhitaji - Wendapo utajinywea
132. Mjiwe umetakata - Una siraji zameta - Mtu mbali akipita - Kwa sura utamjua
133. Yuna wengi mashujaa - Wazoefu wa kitaa - Na wendapo kwa khadaa - Jua umekwangamia
134. Humo ndani ya biladi - Ni wangi mno junudi - Nao ni kama asadi - Na kuzidi namiriya
135. Ewe mfalme wetu - Muarabu yuna watu - Wengine ndani ya mwitu - Wamejigeuza paa
136. Hiyo bara Afrika - Watu wote wamwitika - Isilamu na Wanyika - Wote wamnyenyekea
137. Na kula alo hodari - Kwa vita na miukari - Amekwenda Zinjibari - Ili kwenda kutumia
138. Bwana nakupa khabari - Biladi ya Zinjibari - Kwa kula haufikiri - Wapita biladi pia
139. Na Sultani ni mwema - Ni mtu mwinyi huruma - Ukenda ukishasema - Utakacho wakipewa
140. Ni wengapi masikini - Walao kwa Sultani - Hata wendapo mjini - Wapata ukatukua
141. Ni nyingapi buldani - Zilo mwake mikononi - Ni wengapi shujaani - Ambao wamsikia
142. Ni kam kam kunuzi - Alo nazo mwinyi ezi - Ambazo hazina kazi - Bure zimejikalia
143. Ni kam kam taifa - Alio nao Khalifa - Ambao hawachi kufa - Harubuni wakingia
144. Ni wengapi wapatao - Chakula chema na nguo - Ni wengapi wenendao - Kiwapa bure atiya
145. E Bwana nakuradidi - Yuna kaumu Sayyidi - Na mjiwe msafidi - Wote umepigiliwa
146. Sifa zake Maulana - Nyingi sipati kunena - Nakhofu kukosekana - Kuja patwa na khatia
147. Baada sayo wenzangu - Turudi hadithi yangu - Kishakwe sema Mzungu - Sultani kasikia
148. Kimaa kuyapulika - Nakhodha alotamka - Kitwa chake kakinika - Pasiwe na kukinua
149. Kinika kitwa kwa kweli - Kwa muda wa saa mbili - Kupiga zake akili - Kuwaza na kushangaa
150. Kondokwake na kuwaza - Vita siwezi fanyiza - Labda na Mngereza - Tuwapo shauri moya
151. Mngereza akanena - Mimi siwezi pigana - Kwamba nti naiona - Sawahili naijua
152. Nililo nalo takoma - Na kuzuia watumwa - Daima hunuma numa - Na watumwa hupakiwa
153. Kwamba wataka harubu - Kuwana na Muarabu - Usije nitaharabu - Watuo wakiuliwa
154. Kwani hayo sitamani - Kumiliki buldani - Yuna nguvu Sultani - Na watuwe mashujaa
155. Kanena Mjarumani - Sinavyo vita moyoni - Kwenda jitia mjini - Bure pasipo hatia
156. Kisha sayo kudhukuri - Wakanena matajiri - Kwako twataka shauri - Ndilo tulilokujia
157. Twataka uturuhusi - Vita tutakwenda sisi - Pa mizinga na risasi - Juu yetu twakwambia
158. Zote gharama za vita - Juu yetu tutaleta - Na nti tukaipata - Ushuru tutatumia
159. Sultani kadhukuri - Endani tu mashauri - Na kila litalojiri - Siwezi ligharamia
160. Gharama zote zi kwenu - Maana vita ni vyenu - Tena nyinyi peke yenu - Mimi simo nakwambia
161. Wadachi wakaridhika - Na ahadi wakaweka - Mara ile wakandoka - Faraghani wakangia
162. Wakatakana shauri - Wakatenga wasafiri - Wa hila na tafakuri - Wenyi tambo na nakaa
163. Watu walopatikana - Wenyi hila za kuwana - Majina yao tanena - Ambao nawatambua
164. Kwanza kapatika nyundo - Ndiye muweza vishindo - Aivukaye mikondo - Kwa akili na khadaa
165. Wa pili ni kitambara - Hao ndio watu bora - Wenyi hila na busara - Na hila za kuwania
166. Na wa tatu himsema - Etwa simba wa mrima - Na wane ni Bwana Bima - Na wa tano takwambia
167. Huyo wa tano wenzangu - Etwa muhogo mchungu - Majina yao Wazungu - Ni hayo nimewambia
168. Thuma na Bwana Kirofu - Ndiye Mzungu dhaifu - Ni yeye na Asikofu - Milimani wakakwea
169. Kaja Mzungu kahati - Aitwa Bwana Lauti - Na wenginewe umati - Siwezi kuwasifia
170. Wakasema faraghani - Peke yenu enendani - Na thalathata dukhani - Zatosha kwenda wania
171. Wakaifunga safari - Wakalekeya bahari - Na thalatha manuwari - Siku haba wakangia
172. Humo safarini mwao - Wafunga shauri lao - Kama sisi twenendao - Na twenendeni kwa khadaa
173. Tukatakeni forodha - Sayyidi tumpe fedha - Itakuwa kadi madha - Zamani eshapotwaa
174. Tukishakatibiana - Mambo yetu yatafana - Hapatakuwa kuwana - Na nti tutaitwaa
175. Basi dukhani zikija - Sawasawa safu moja - Wakiwasili Unguja - Khofu moyo wakangia
176. Kuionakwe biladi - Walivyowamba junudi - Wakatetema fuadi - Ruuba kubwa ajaa
177. Wakajutia nafusi - Unguja kuletwa sisi - Wakangia kudadisi - Kwa hali ya kughumiwa
178. Kuwasili fordhani - Wakawaona zabani - Kama simba ghadhbani - Kwa ukali kuwajaa
179. Wakauzwa mwenda wapi - Lilowaleta nlipi - Wakakonda kama papi - Kwa muda wa saa moya
180. Nyundo akatakalamu - Enyi simba dharghamu - Nyumba ya mwenyi makamu - Ni ipi twahitajia
181. Tuonyeni Waarabu - Baiti 'lajaibu - Tuna jambo na sababu - Kwetu tulilokujia
182. Nawauza nambiani - Nyumba yake Sultani - Nami nijile amini - Sina shari nawambia
183. Namtaka mfalme - Tuna maneno tuseme - Wakamjibu walume - Ewe Mzungu sikia
184. Nyumba yake Maulana - Yupi asiyeiona - Kwa pambole mzayana - Na ilivyosafidiwa
185. Nyumba yake mtukufu - Ujapokuwa kipofu - Usikizapo harufu - Kwa akili waijua
186. Baiti 'lajaibu - Ujapokuwa gharibu - Huhitaji kunasibu - Ukifika waiyua
187. Mato yako hayaoni - Nyumba yake Sultani - Ujapokuwa mgeni - Huhitaji kuambiwa
188. Kwambiwa kwake Nasari - Akazidi tanadhari - Kitazama mnawari - Nyumba ilivyo tulia
189. Akajua kwa hakika - Ni nyumba yake malika - Yenye nuru na kuwaka - Ya duri na yakutiya
190. Tena nyundo atongowe - Akawambia wenziwe - Twendeni tukapumuwe - Tuzidi maarifiya
191. Twenendeni kwa balozi - Hakimu wa Kingerezi - Tuzidi kutamayazi - Na maarifa kungiya
192. Wakanenda tasihili - Kwa balozi kiwasili - Kwa hishima na jamali - Balozi kawafanyia
193. Wakaletewa khamri - Wakalewa manasari - Hata wakiwa sakari - Kwa kileo kuwajaa
194. Hata usiku mbuyaza - Balozi wakamweleza - Mambo yao tangu kwanza - Jamii wakamwambia
195. Khatima wakabaini - Tuna jambo twatamani - Atakapo Sultani - Forodha tutanunua
196. Sayyidi akakubali - Tutampa mangi mali - Chombo kikitahamali - Ushuru tutautwaa
197. Basi wakafuatana - Wakenda kwa Maulana - Kufika akawaona - Sayyidi akawajua
198. Akawajua Sayyidi - Yale yao makusudi - Yalo ndani ya fuadi - Waliyoyakusudia
199. Kuwasilikwe idadi - Mlangoni pa Sayyidi - Bawabu kamradidi - Rukhusa twahitajia
200. Tupe rukhusa bawabu - Twenende kwa Muarabu - Bawabu akawajibu - Siwezi wafungulia
201. Ngoja nende barazani - Ninde hatake idhini - Kasikia Sultani - Ambayo washindania
202. Maulana amwambieye - Bawabu siwazuiye - Wape rukhusa wangiye - Nijue walokujia
203. Bawabu akawaata - Mlangoni wakapita - Na nafsi zawavuta - Kwa fazaa kuwangia
204. Wakakweleza yuani - Waknenda barazani - Wamuene Sultani - Haibaye nawambia
205. Mzungu kenuwa macho - Awene mengi matisho - Roho ikangia kicho - Alipomuangalia
206. Wamuene yuna sefu - Kama simba maarufu - Na umbo lake tukufu - Huwezi kumlekea
207. Wakaona shujaani - Bi shimali wa yamini - Walindao Sultani - Wai wangi mashujaa
208. Makadhi na makatibu - Wapo wametakarabu - Na jamii Waarabu - Kando kando wamekaa
209. Kuonakwe miujiza - Ya mfalme muweza - Baraza kaitengeza - Wazungu wakaghumiwa
210. Maulana atamke - Roho zisifazaike - Mitima naiwashuke - Mseme mlokujia
211. Semani maneno yenu - Mnipe kusudi yenu - Kisa cha kutoka kwenu - Hata kwangu mkangia
212. Kwangu mjile takani - Au mna jambo gani - Lilowaleta ni nini - Ajilini kunambia
213. Kishakwe sema Imamu - Nyundo akatakalamu - Ya Maliku 'lhamamu - Ya Maulana sikia
214. Jambo letu makusudi - Kutaka sitak'adi - Uridhikapo Sayyidi - Forodha twahitajia
215. Sayyidi ukiridhika - Forodha yako twataka - Tukatibiane mwaka - Na fedha tutazitoa
216. Na ukitupa Mrima - Ni kheri twaona vema - Tutapata makulima - Tutajenga kwa wasaa
217. Sayyidi akamwambia - Ewe Mzungu sikia - Bandari takuwatia - Ukitaka utatwaa
218. Bandari takurukhusu - Mwaka kwa laki u nusu - Na ufanyapo ulusu - Jua umekwngamia
219. Kwamba wataka bandari - Sharti hayo ukiri - Mzungu akafikiri - Khatima akaridhia
220. Akamba nimeridhia - Yote uliyonambia - Bandari tazizuia - Fedha zako utatwaa
221. Ukomo wangu ni Tanga - Ahadi Tungi kujenga - Na miji yote tatanga - Mmoja sitabakia
222. Sayyidi akakubali - Ambapo mwanipa mali - Wala pasiwe ukali - Kwa watu kuwafanyia
223. Msiwadhiki junudi - Kwa mambo ya ufisadi - Nyinyi mjile kukodi - Nti hamkununua
224. Wazungu wakaridhika - Sayyidi alotamka - Mikataba wakandika - Na mikono wakatia
225. Wakatoka barazani - Wana furaha moyoni - Tuliyo tukitamani - Yote yametuelea
226. Baada sayo pulika - Barua zikaandikwa - Nti zote kupelekwa - Kuwaarifu jamaa
227. Sayyidi katukhubiri - Jamii zote bandari - Amezikodi nasari - Naye atawajilia
228. Sikumzidisha jambo - Ila kufuata vyombo - Na afanyapo kijambo - Sije mkamridhia
229. Azitakapo biladi - Hiyo si yetu ahadi - Waueni wasirudi - Allah Allah nawambia
230. Wala msiniarifu - Roho zenu zikakhofu - Wakija na watilifu - Wafanyapo jeuria
231. Barua zikiwasili - Zisibakiye mahali - Majumbe na maliwali - Wote wakaarifiwa
232. Tukaketi kusikiza - Ukesha mwezi wa kwanza - Na wa pili ukasoza - Khabari tukasikia
233. Tukazipiata yakini - Ya kwamba hapo Pangani - Wako Wazungu mjini - Majumbani wamekaa
234. Wako wawili kwambile - Mmoja Nyundo jinale - Ajenga nyumba akale - Na wa pili tawambia
235. Na wa pili sikiani - Ni Kitambara yuani - Ajenga n'gambo ya Bweni - Ndiko alikofikia
236. Zikapita siku mbili - Twambiwa wamewasili - Wako Wazungu wawili - Wa bara wajemelea
237. Khabari tukapulika - Na Bwagamoyo washuka - Miji yote waitaka - Ati wameinunua
238. Kilwa na Dari-'sSalama - Kuna Wazungu nakama - Mtu hapati kusema - Nti wamezizuia
239. Tanga waja kutwa kutwa - Na majumba watafuta - Wengine wanaopata - Wamo wamejikalia
240. Winde hata Saadani - Wazungu tele mjini - Na jamii bandarini - Mashua kutwa kungia
241. Na jamii ya bahari - Kula wetapo basari - Utaona manuwari - Kutwa kutwa zatembea
242. Tukaghumiwa wenzetu - Tusiweze kula kitu - Hata mfunguo tatu - Siku ya Idi sikia
243. Tukazipata yakini - Ya kama huko Pangani - Wazungu msikitini - Idi haikusaliwa
244. Walikuja wakangia - Na majibwa yao pia - Liwali akakimbia - Asihimili kukaa
245. Wakakata mlingoti - Hivi sasa uko nti - Wakazuia baruti - Jamii maduka pia
246. Wakaikunda fahamu - Bendera ya Muadhamu - Na sasa wameazimu - Kutweka yao sikia
247. Na watu wote pulika - Wanawake wametoka - Na Wazungu kama taka - Miji yote watembea
248. Tukajua ndio kweli - Wazungu kutenda feli - Zikapita siku mbili - Khabari tukasikia
249. Kwamba Wazungu wa Tanga - Wameipiga mizinga - Zahoro mwana wa Manga - Hakuweza kukimbia
250. Zahoro bin Suwedi - Akakusanya junudi - Kawapiga kawarudi - Wasiweze kutokea
251. Wakaipiga mizinga - Ndipo watu wakatenga - Twasema mambo yasonga - Yazidi kutujilia
252. Hata jua 'lasiri - Tuwene wangi jifiri - Watukuziye kishari - Wanawake wakimbia
253. Mabweta kwa majamanda - Wametukua wenenda - Mara moja wamekonda - Kama waliozuliwa
254. Tukawataka khabari - Wakatwambia ni kheri - Kwetu kujile Nasari - Wazungu kutwingilia
255. Jana wajile laili - Idadi mashua mbili - Watu wasiwakubali - Usiku wakarejea
256. Hata leo wameshuka - Wamepigwa kwa tafaka - Nao wamekhasirika - Hatujui idadia
257. Wametupiga risasi - Mizinga iso kiasi - Pasikuwa na nafasi - Hata tumewakimbia
258. Hivi watele mjini - Nasi sote tumehuni - Na merikebu zi pwani - Bandarini zimekaa
259. Tukajua kwa hakika - Nti zimeharibika - Kisha sayo kutendeka - Na mengineyo sikia
260. Baada hayo kusibu - Wakapanda merikebu - Mara wakaikalibu - Unguja waelekea
261. Maiti wakatukua - Wote waliouawa - Na waliokhasiriwa - Wote wakawapakia
262. Zinjibari wakisoza - Maiti wakacheleza - Mbali kando ya baraza - Sayyidi anapokaa
263. Wakatamka Nasari - Sayyidi tunza amri - Mrima iliyo jiri - Kwenenda tukiuliwa
264. Kwenda na shughuli zetu - Tukenda uliwa watu - Wala tusitwae kitu - Bure tukakhasiriwa
265. Zahoro liwali wako - Alituonya vituko - Kwamba ni amri yako - Twambie tupate jua
266. Sayyidi akawajibu - Labda munaharibu - Ila pasipo sababu - Hayo yasingefikia
267. Kazi tuliambiana - Sikumwambia pigana - Wala sikumpa zana - Silaha za kuwania
268. Na jamii ya Mrima - Wao si wangu watumwa - Ni watu walinandama - Wakakiri uraia
269. Leo kwamba hawataki - Mimi sikuwamiliki - Wala msije shitaki - Mwendapo mkiuliwa
270. Ahadi yetu minawe - Ni ya ushuru utowe - Miji ni yao wenyewe - Siwezi waingilia
271. Wakaondoka Nasari - Nyuso walitahayari - Wakatukua na ari - Kwa ukali kuwangia
272. Basi wakaja Pangani - Roho zili kisirani - Nyumba wakaizaini - Na mizinga wakatia
273. Na marikebu Maziwe - Mji wote unamiwe - Na Wazungu wanginewe - Mjini wakatembea
274. Mji ukanyamazana - Pasiwe mtu kunena - Jamii ya waungwana - Pasi mwinyi kutongoa
275. Mzungu kasitakimu - Akataka na hukumu - Kushitaki Isilamu - Kwenda akiwaamua
276. Pangani na kwa Mauya - Watu kawatarajia - Wende wakimwamkia - Wakubali uraia
277. Baada sayo nanena - Mambo yalotendekana - Yasije yakapandana - Nayaweka moya moya
278. Mle katika mashamba - Mna mtu ajigamba - Ushujaa kama simba - Na kuzidi namiria
279. Na jina lake fahamu - Ni Abushiri isimu - Mzaliwa ni Salimu - Kabila alHarithia
280. Huyo simba mashuhuri - Wala hataki jeuri - Na kula palipo shari - Azidi papendelea
281. Ni shujaa maarufu - Rohoye haina khofu - Mjapokuwa alufu - Hakhofu kuwangilia
282. Anaye mtu mwengine - Rafikiye wendemene - Mbaya msimnene - Afadhali kunyamaa
283. Jinale etwa Jahazi - Si mwema akibarizi - Utamboni kama kozi - Hakhofu mtu mmoya
284. Siku moja wakaketi - Usiku katika beti - Wakimaa kula kuti - Wakashukuru Taaa
285. Basi wakasimulia - Abushiri kamwambia - Jahazi umesikia - Pangani yalojiria
286. Pangani kuna kishindo - Ati amekuja Nyundo - Yuwawatenda vitendo - Visivyo kuwapasia
287. Na mlingoti wa Bwana - Wameukata laana - Nao wamenyamazana - Hapo mwnyi kutongoa
288. Jahazi akadhukuri - Nimeipata khabari - Akanena Abushiri - Ewe Jahazi sikia
289. Mambo hayo yapitayo - Yamenichoma na moyo - Na tukinyamaza sio - Bwana yatamtukiwa
290. Natamani nende kuko - Hayaole yaliyoko - Nimuonye na vituko - Nyundo apate nijua
291. Jahazi akatamka - Nami hayo nayataka - Kutezewa ni wazuka - Haifai kunyamaa
292. Kulipokucha yuani - Abushiri kabaini - Wakatelea mjini - Asubuhi wakangia
293. Abushiri katamka - Madiwani nawataka - Wote wakakusanyika - Pasisaliye mmoya
294. Jamii wakadhihiri - Ahli 'lmashuhuri - Abushiri kadhukuri - Majumbe akawambia
295. Majumbe kawauliza - Sababu ya kunyamaza - Nyundo anayofanyiza - Nanyi mkawangalia
296. Akakata mlingoti - Wa Sayyidi mwinyi nti - Naye Nyundo akaketi - Mjini akatembea
297. Majumbe wakamjibu - Kweli hayo Muarabu - Waama tuna sababu - Tuliyomnyamalia
298. Sababu yetu Liwali - Aliye kutanakali - Na sisi kutenda feli - Kwa Sayyidi twakhofia
299. Abushiri kwarudi - Mwakhofuni kwa Sayyidi - Sisi kwake tu abidi - Atakalo lajiwia
300. Na sasa shauri langu - Na tupatane wenzangu - Tupigane na Wazungu - Kwa shauri kuwa moya
301. Na mimi hapa sondoki - Na zikatimbwe khandaki - Zikutane na bunduki - Kula palipo jamaa
302. Watu na waarifiwe - Walio mbali wajuwe - Na Nyundo na azuiwe - Pasiwe kumuatia
303. Mlingoti usimame - Na Nyundo autazame - Apate neno aseme - Nasi tukamsikia
304. Kusemakwe Abushiri - Jamii wakayakiri - Majumbe na mawaziri - Wote wakafurahiwa
305. Waarabu kwa Mauya - Jamii wakateleya - Na Bweni mbili sikiya - Sahuri likawa moya
306. Hata washenzi barani - Wote wakaja Pangani - Na Nyundo yuko nyumbani - Hapati pa kutokeya
307. Bendera ikasimama - Nyundo yupo atazama - Na mlingoti dawama - Watu wapo wangojea
308. Chombo hakina nafasi - Ya kupanda maruwasi - Kwa kupigwa marisasi - Na watu kukhasiriwa
309. Mashua na marikebu - Haziji tena karibu - Kwa watu kuzidhurubu - Bunduki na madufaa
310. Nyundo kitunza dalili - Mambo yamekuwa kweli - Kapotewa ni akili - Shauri la kutumia
311. Nyumba akajifungia - Na watu wamngojea - Ambapo yuatokea - Auawe mara moya
312. Nyumbani maji hanayo - Kazi yake ni kiliyo - Hapati pa kwenda mbiyo - Kwa watu kumzuiya
313. Nyundo akatakalama - Toba jama nimekoma - Leo nataka salama - Nipate pa kutokea
314. Watu wakamba Muongo - Sharti ukatwe shingo - Au upigwe kisongo - Utembezwe mji pia
315. Siku ya tano yuani - Watu wawene dukhani - Ikipata milangoni - Ikateleza mashua
316. Mashua wakaegema - Marisasi yakavuma - Ikarudi nyuma nyuma - Isipate pa kungia
317. Na Nyundo yupo nyumbani - Akaleta Sultani - Marikebuye Shukwani - Pwani iakakaribia
318. Zikasimama bunduki - Dukhani wakaidhiki - Ajile Shekhe Lemki - Shekhe Nasoro sikia
319. Shekhe akayatazama - Unavyokaa Mrima - Kamba mimi tasimama - Mashuani tajitia
320. Akangia mashuani - Na bendera mkononi - Na kuitana amani - Watu hawakuridhia
321. Akasimama Lemki - Roho ikawa sadiki - Na risasi na bunduki - Kama matone ya mvua
322. Mashua ikaja pwani - Salama u salimini - Shekhe Nasoro yuani - Akawambia jamaa
323. Kisa cha kunidhurubu - Nasi hatuna harubu? - Madiwani wakajibu - Na Abushiri pamoya
324. Sisi tumeapiana - Pasingie chombo tena - Hata chake Maulana - Kuja kitadhurubiwa
325. Shekhe akatakalamu - Nijile na mualimu - Mushti Mafiyu fahamu - Rukhsa ahitajia
326. Yuataka aweleze - Mambo muyatengeneze - Mengine msifanyize - Yangu ni kuyasikia
327. Wakajibu wote jama - Naaje tutaja sema - Akashuka hima hima - Mushti Mafiyu kangiya
328. Pangani akiwasili - Wote akawasaili - Akhiri hata awali - Jamii wakamwambia
329. Alipokwisha pulika - Mambo yaliyotendeka - Mzungu kasikitika - Khatima akamwambia
330. Kawambia madiwani - Nataka Nyundo nipani - Na mtakalo semani - Ni mwinyi kuwaridhia
331. Majumbe wakadhukuri - Shauri kwa Abushiri - Maana ndiye Amiri - Hatuwezi mwondolea
332. Abushiri akanena - Mwalimu sikia sana - Nyundo ni jeuri sana - Hatuwezi mwatilia
333. Kwamba wamuhitajia - Yetu ni kuyaridhia - Alfu kumi rupia - Zijapo utamtwaa
334. Na tena umpakie - Na mwilini nguoye - Kingine asizidie - Atoke tukangalia
335. Mzungu akayakiri - Manenoye Abushiri - Mashua akaibari - Nyundo akampakia
336. Katoka Nyundo nyumbani - Kuona humtamani - Na watu wote mjini - Wenda wakimzomea
337. Baada sayo kujiri - Atendayo Abushiri - Akazipata khabari - Bagamoyo imengiwa
338. Winde hata Bagamoyo - Imekufa nti hiyo - Na watu wenenda mbiyo - Kwa vita kuwangilia
339. Na watu wamefikiri - Kutegemea Nasari - Kasikia Abushiri - Mno yakamtukiwa
340. Akamwambia Jahazi - Twende hapana makazi - Tutawakali Azizi - Ndiye mtawakiliwa
341. Safari wakaazimu - Na akali ya kaumu - Siku haba zikatimu - Winde wakafikilia
342. Winde walipowasili - Wawene dukhani mbili - Mji wameuatili - Nazo zipo zimekaa
343. Zikapiga darubini - Ziwene jeshi mjini - Wazungu wasiamini - Wakapiga madufaa
344. Mizinga ikatetema - Kama mwamba wa kuvuma - Majumba yakasukumwa - Kuno yakapindukia
345. Na watu wengi wenzangu - Wako juu ya mafungu - Wakatelea Wazungu - Kuja mjini kukaa
346. Hata pwani wakafika - Tafaka zikawalika - Wapigwa wakianguka - Wengi wakateketea
347. Mji wakautangua - Na wao wakauawa - Hapana mwinyi kujua - Ila ye Rabbi Jaliya
348. Baada sayo nanena - Ikawa kufuatana - Mwisumai na Mabwana - Na mzee Mwinshaha
349. Mwisumai kakalimu - Na Mbwana wa Kasimu - Ya wapi mastakimu - Mzungu katondolea
350. Twendeni na Abushiri - Bagamoyo tudhihiri - Tukampige Nasari - Ajue tu mashujaa
351. Watu wakatangamana - Shauri hilo kunenwa - Abushiri akaona - Mno akafurahiwa
352. Pamoja na Mmarika - Akamba nami nataka - Shauri mnaloweka - Afadhali kuwendea
353. Mwinyikambi Sumaili - Akamba hayo ni kweli - Mengine tusikubali - Miji yetu kutwaliwa
354. Na Mwikambi 'lAsadi - Akamba nami sirudi - Na wakapigwe junudi - Kwa mato wakangalia
355. Mwinyi Mbwana Masiku - Akamba sasa usiku - Pindi awikapo kuku - Safari tatangulia
356. Hata kukipambazuka - Safari wakaishika - Sangazero - wakafika - Wakatua wakakaa
357. Walingoja na laili - Kukicha siku ya pili - Mashamba wakawasili - Viungani wakangia
358. Wakawaona sufufu - Mwinyi Mkamba na Sefu - Na 'lAmiri tarafu - Na jamaa wamekaa
359. Khabari wakazuana - Jamii wakambiana - Wakamba ni kwenda wana - Na mengine hayafaa
360. Kabla kupambazuka - Vita vyao vikatoka - Wakapiga wakateka - Mali mingi nawambia
361. Wakateka mingi mali - Na wajakazi wa kweli - Na watu kutanakali - Pasisaliye mmoya
362. Wazungu wakakimbia - Wakenda wakajitia - Nyumba waliyofikia - Wakanyamaza jamaa
363. Tena ikawa mizinga - Hata watu wakatenga - Na mali kama mitanga - Watu waliyoyatwaa
364. Jeshi ikarudi nyuma - Wakenda lijenga boma - Kwa mijiti mema mema - Na malango yakatiwa
365. Tena ikawa vikozi - Wakatekwa wajakazi - Na wana wa Kinyamwezi - Wengi waliopotea
366. Na Mzungu Bagamoyo - Yuna nyumba moja hiyo - Hana tena apatayo - Kwa watu kumzuia
367. Daima vita vyenenda - Na Mzungu ajilinda - Kanena Mwinyi Makamba - Abushiri kamwambia
368. Mzungu atushawishi - Na tukusanyani jeshi - Ende akatiwe Moshi - Tumwondoe mara moya
369. Basi jeshi ikangia - Kem tawahisabia - Wakenda wakelekea - Mzungu kajizuia
370. Mzungu akawashunga - Abushiri akatenga - Kaikusanya mizinga - Mzungu akaitwaa
371. Wakarejea khaiba - Nyoyo bili na msiba - Pasiwe kula kushiba - Kwa hamu kuwaingia
372. Abushiri kabaini - Kawambia madiwani - Shauri jema nipani - Ambalo la kutumia
373. Mzungu ameshtadi - Na mimi nyuma sirudi - Hebu nipani muradi - Ambao wawelekea
374. Madiwani wakanena - Tusikie Maulana - Sisi tumo kupigana - Jitihadi kila ndia
375. Mali na nafsi zetu - Twafidia nti yetu - Sisi kwenenda na mwitu - Hayo hatukuzoea
376. Ama hayo Muarabu - Jambo moja twaharibu - Hatufanyi taratibu - Tukapata neno moya
377. Vita ni ukurugenzi - Kwa kupata mgonezi - Ambaye ni mmaizi - Akaja togonekea
378. Tutafute mualimu - Wa falaki na nujumu - Japokuwa Mzaramu - Ajapo tutamtwaa
379. Abushiri akajibu - Mimi hapa ni gharibu - Simjui mtibabu - Ajuaye mambo pia
380. Kwamba nyinyi mwamjua - Semani tamwamkua - Na atakacho tatoa - Si mwinyi kukizuia
381. Kanyamaa Abushiri - Wapo vijana saghiri - Mmoja etwa Amiri - Na Mwinyikombo sikia
382. Amiri katakalamu - Ewe shekhe muadhamu - Mganga twamfahamu - Yuko kijana mmoya
383. Huko upande wa kwetu - Twakufahamia mtu - Na tena ni ndugu yetu - Ni mganga hana tua
384. Jinale etwa Hemedi - Huyo mganga kazidi - Falaka na mafuradi - Unazidi kumwelea
385. Na Mwinyikombo kanena - Mimi naye twapatana - Ni sahibu yangu sana - Nisemalo aridhia
386. Aweza ngia nyumbani - Wenyewe usingizini - Au akawaghubuni - Msilifahamu moya
387. Mjapotia kufuli - Mkapiga silisili - Aweza kuzibatili - Zote akazifungia
388. Mwinyikombo keshilia - Abushiri kamwambia - Sema yapate tweleya - Tuliopo sote pia
389. Huyo ni mganga gani - Mweza ngia nyumbani - Namo mna Nasarani - Kutwa kucha wangojea
390. Akaondoka Amiri - Kamwambia Abushiri - Huyo ni mtu sahiri - Zamani twamjulia
391. Hayo na kazidi hayo - Mengapi tusikiayo - Mambo yake afanyayo - Ni ibara ukambiwa
392. Abushiri kabaini - Mwanenaje madiwani - Huyo mwana wa chuoni - Wa kuja tugonekea
393. Madiwani watongowe - Na ende akatwaliwe - Na atakacho apewe - Ambalo ahitajia
394. Na sasa tupelekeni - Rupia arubaini - Wale watoto nyumbani - Naye ayandame ndia
395. Wakaifunga safari - Mwinyikombo na Amiri - Hima hima taisiri - Pasiwe tena kukaa
396. Wakaondoka haraka - Na rupia zikatoka - Na barua wakandika - Ewe muhibu sikia
397. Ila shekhe 'lmuhibu - Ewe Hemedi sahibu - Wishapo soma kitabu - Ajili wandame ndia
398. Tuna vita twapigana - Tuna Wazungu twawana - Na sasa tumedangana - Hatuna la kutumia
399. Ajili hima muhibu - Utukue na kitabu - Tuje tuole harubu - Itakavyo tuelea
400. Basi ikaja barua - Haisoma haijua - Na rupia hazipewa - Moja kutawapungua
401. Haitazama safari - Bi 'llaili wa 'nnahari - Haona jambo kujiri - Lisijalo nifikia
402. Hatazama mfuradi - Haona jambo baidi - Na salama ya kurudi - Haona nimerejea
403. Hasema na moyo wangu - Nitatawakali Mungu - Nikawambia wenzangu - Pasiwe tena kukaa
404. Tukamuomba Jalali - Siku ya Jumapili - Pangani tukiwasili - Magharibi tukangia
405. Kuwasilikwe Pangani - Nimeketi barazani - Haona Jumbe Komani - Matoni kanipitia
406. Kwenenda kuamkiana - Khabari tukauzana - Jamii tukambiana - Tusibaki neno moya
407. Hamwambia Nimekwita - Bagamoyo kwenda vita - Hapa Pangani napita - Rabbi akinijalia
408. Akanambia Diwani - Nami taingia ndani - Nenda koma Saadani - Barua nimeletewa
409. Hata kukipambazuka - Asubuhi tukatoka - Ufukweni tukafika - Diwani akatokea
410. Tukaishika safari - Siku haba zikajiri - Bandari ya Bwana Kheri - Saadani tukangiya
411. Saadani kiwasili - Zikaniruka akili - Kwenenda nisikubali - Hatamani kurejea
412. Nikamwambia Diwani - Twenende sote bomani - Waama nami takhuni - Sivuti hatua moya
413. Diwani akayakiri - Akamba tutasafiri - Twenende kwa Abushiri - Siku haba tarejea
414. Basi tukenenda zetu - Na ndia mwitu kwa mwitu - Hata kwa siku ya tatu - Bomani tukatokea
415. Siku tuliyowasili - Tumbo likanithakili - Na uzito wa mwiili - Kwa homa iloningia
416. Hata kwa siku ya tatu - Bado sijajua mtu - Sijaweza kula kitu - Kwa uwele kuzidia
417. Siku ya tano na sita - Ndipo homa kuniata - Na chakula hakipata - Na tumbo likazuia
418. Hata sikuye yuani - Usiku tumo nyumbani - Mbwene mtu mlangoni - Akamba mwamkuliwa
419. Mwenende hima kwa bwana - Pasiwe kutafutana - Tukenda tukaonana - Faraghani tukangia
420. Tukakaa faraghani - Mimi na Jumbe Komani - Abushiri kabaini - Maneno akatwambia
421. Abushiri kanambia - Jambo nililokwitia - Khabari nimesikia - Utabibu wakwelea
422. Ati una utabibu - Ya watu kuwaghilibu - Ukafanya taratibu - Nyumba ukaifungua
423. Basi nakwamba ni kweli - Nambia tuli wawili - Na mimi yangu hakuli - Ewe Shekhe nisikia
424. Kweli nalihifanyiza - Hapo zamani za kwanza - Nyumbani hawapumbaza - Waliomo wote pia
425. Nalingafanyiza sana - Kwa ghururi za ujana - Na sasa sijui tena - Yote yamenipotea
426. Abushiri kamba ndiyo - Fanya kama ujuayo - Nawe nipa sharutiyo - Ulitakalo nambiya
427. Hamwambia Shekhe wangu - Utakapo kweli yangu - Nitawakali kwa Mungu - Kila ambalo najua
428. Numuombapo Rabbuka - Na nyumba ikafunguka - Niwapo takapo shika - Rabbi akaniongoa
429. Ufunguapo yakini - Na wenyewe wali ndani - Kila uanalotamani - Ni mwinyi kukutendea
430. Na yangu hamuarifu - Ajaalipo Latifu - Nipa rupia alufu - Moja kutawa pungua
431. Tena unipe vitwana - Viwili vyenye maana - Vya sura ya kiungwana - Vyema vilivyotulia
432. Na viwili vijakazi - Vyenye singo ya muanzi - Ndipo taitenda kazi - Yako uliyonambia
433. Na mimi na watu wangu - Nikishikacho ni changu - Usije nitaka fungu - Zamani za kuwania
434. Kitu nitachokishika - Usije ukanipoka - Ambapo umeridhika - Uganga takufanyia
435. Abushiri akakuli - Yote nimeyakubali - Ajaalipo Jalali - Mzungu akakimbia
436. Hiyo sioni sharuti - Kama ina tafauti - Bora ni kupata nti - Yote tutakufanyia
437. Nami yangu hadhukuri - Na kwamba utayakiri - Basi fanya tadbiri - Mbuzi namhitajia
438. Nataka mbuzi mweusi - Nipatie kwa upesi - Tupate omba Kudusi - Jala wa Ala Taaa
439. Mbuzi kapatikana - Akachinjwa akachunwa - Nyongo yake haiona - Kikombeni haitiya
440. Ile nyongo handikia - Kafara ya kukimbia - Siku iliyojiria - Yangu niloazimia
441. Hamwambia Shekhe letu - Bwana nipatia watu - Twende kwa adui wetu - Tupate kuwangalia
442. Leo nenda watazama - Nende nazike azima - Nizidi kuwafahama - Nipate maarifia
443. Hata usiku laili - Wakaja kumi rijali - Wamejifunga kwa kweli - Na Amiri akangia
444. Shekhe kanambia hao - Ndio watu wajuao - Haya fuatana nao - Mjini watakutia
445. Baada ya saa tatu - Hatoka nao wenzetu - Ikawa kwenda na mwitu - Ndia zimetupotea
446. Twenenda tukisimama - Twakhofu kuwa mapema - Hata mbele hitizama - Haziona sirajia
447. Haona taa zawaka - Zi ndani ya mashubaka - Nyingine zimetundikwa - Zi juu zalewalewa
448. Pale usiku wa kiza - Na taa zikaangaza - Ndudu kujitambaza - Wamuona kutambaa
449. Nikawambia jamani - Tunzani huko usoni - Kuna taa minarani - Zina nuru zaangaa
450. Hata wakatupa macho - Roho zikangia kicho - Kwa kuyaona matisho - ya Wazungu Nasariya
451. Wakamba tumeisonga - Nyumba yao walopanga - Enenda wewe mganga - Sisi twakungojelea
452. Hawambia twenendeni - Sikujui mlangoni - Wakanena abedeni - Mbele hatutasongea
453. Ila huyule Amiri - Kwenda sote akakiri - Moyo ukamdhukuri - Si vema kulimatia
454. Basi tukafuatana - Tukipata mbele sana - Kila mahali twaona - Kwa nuru ya sirajia
455. Amiri akaniuza - Mbona taa zaangaza - Ni wapi pa kujibanza - Hata tukafikilia
456. Hamwambia twende zetu - Hatutaonwa ni mtu - Lakini vua viatu - Na silaha zote pia
457. Amiri kamba sahiba - Nyumbani kuna majibwa - Wakuonapo kariba - Sharti yakubwekea
458. Nikamwambia rafiki - Leo mbwa hawabweki - Na sisi hatuoneki - Kwa amri ya Jalia
459. Viatu akavivua - Na silaha kazitua - Basi mimi haongoa - Nyuma kanifuatia
460. Basi tukaongozana - Na taa kama mchana - Mtu mbali wamuona - Kabla kukurubia
461. Mara ile mbwakhubiri - Wakaondoka Nasari - Wakasimama suturi - Wote wakatunamia
462. Wako juu sebuleni - Wote watazama chini - Amiri asiamini - Akanguka kwa fazaa
463. Hainama hamshika - Mbona Amiri wanguka - Akamba tumeoneka - Leo ndiko kwangamia
464. Tazama taa zan'gara - Nasi hatuna stara - Hakika ndiyo madhara - Leo yametufikia
465. Nikamwambia Amiri - Tuliza yako sadiri - Nami nisingejasiri - Roho naipendelea
466. Tujapongia nyumbani - Wazungu hawatuoni - Amiri akaamini - Tena tukandama ndia
467. Majibwa yakatuona - Yote yakanyamazana - Akazidi muamana - Amiri akatulia
468. Tukenda hata nyumbani - Tukafika mlangoni - Tukachimba pale chini - Azima haifukia
469. Na nyumba ina ukuta - Makile shibiri sita - Hata kombora laduta - Halondoi jiwe moya
470. Na nyuma kuna kimia - Uzi wa chuma sikia - Kufika utakungia - Hila zote hazifaa
471. Nyumaye kuna khandaki - Inachomekwa masiki - Yakukitapo hondoki - Kwa sumu iliyotiwa
472. Kuna na khandaki tena - Mtu hapati kunena - Baruti imejazana - Madari kwa madaria
473. Na mambo hayo hakika - Yote yaliyozunguka - Na mizinga imewekwa - Ukenda yakungojea
474. Moyo wangu hasadiki - Mahali hapafikiki - Kwa ukuta na khandaki - Na imara zote pia
475. Na juu kuna mizinga - Dirisha hazikufungwa - Wazungu wamo kutanga - Wenenda wakirejeya
476. Na kila umuonaye - Ni koti na bundukiye - Hapo endaye pekeye - Safu safu watembea
477. Lile lango halishika - Kuno halisukasuka - Amiri akatamka - Turudi hima ajaa
478. Haya tuliyofanyiza - Haifai kuongeza - Basi tukajitambaza - Polepole kurejea
479. Tukenenda taratibu - Kwenenda hitaajabu - Kwa nguvu za uharabu - Na nyumba ilivyokaa
480. Tukafika kwa wenzetu - Wakele ndani ya mwitu - Tena tukenenda zetu - Bomani tukarejea
481. Bomani tukadhihiri - Akatamka Amiri - Kumwambia Abushiri - Yote yaliyojiria
482. Tena Amiri kanena - Nyumba itafungukana - Kwa hayo niliyoona - Sijaonapo kataa
483. Uganga wake Hemedi - Sijaonapo abadi - Hidhani hatutarudi - Kwa yaliyotufikia
484. Nyumba twendapo ipata - Kwa kwanza mimi kupita - Nanyi mpate fuata - Nyumbani tupate ngia
485. Wakanitia hubani - Wote walio bomani - Mashekhe na madiwani - Pendo lisilo mithaa
486. Tena siku hadalili - Ya kupeleka kitali - Haiona mwezi pili - Ramadhani imengia
487. Hamwambia Abushiri - Siku njema imejiri - Mwezi pili kwenda shari - Ndiyo iliyonijia
488. Tena nipa fursani - Watimu arubaini - Ambao ni shujaani - Wazoevu wa kitaa
489. Wazungu tawapumbaza - Na mimi tangia kwanza - Wala pasiwe kuwaza - Wauawe wote pia
490. Abushiri akanena - Hao watapatikana - Tena tukatulizana - Kungoja siku kungia
491. Siku ya kundama mwezi - Hawambia wamaizi - Abushiri na Jahazi - Siku imekaribia
492. Wakasema twatafuta - Ambao waweza vita - Bado hatujawapata - Wahimilio kitaa
493. Tena kaja Mfaransa - Akaketi tukajisa - Akasema kuna kisa - Mjini kilichongia
494. Mjini kuna kioja - Huonwa nyama yuaja - Akiwapiga mapaja - Wadachi wakakimbia
495. Na nyama huyo mweusi - Ni punda au farasi - Na apigwapo risasi - Mara moja hupotea
496. Wadachi wafazaika - Na nyama amewashika - Watu wakafurahika - Abushiri na jamaa
497. Watu wakiyakariri - Wakajua ni sihiri - Kila mtu akakiri - Na kuzidi furahiwa
498. Hata kwa siku ya tatu - Hamwambia Shekhe wetu - Nawataka hao watu - Siku imefikilia
499. Abushiri katamka - Watu hawakupatika - Na vita ni kuvundika - Kwenda tukawazumbua
500. Siku ya pili yuani - Shekhe akaja nyumbani - Na barua mkononi - Yatoka kwa Nasariya
501. Tukitazama ya ndani - Mwenyewe ni Hambaroni - Na maneno sikiani - Jamii tawandikia
502. Ila Shekhe mtukufu - Abushiri maarufu - Huyo Muarabu Sefu - Mweke vema rijaa
503. Huyo Sefu bin Isa - Usije mfanya kisa - Mimi kwangu alikosa - Ndipo akanikimbia
504. Ali chini ya bendera - Hampa na mshahara - Yote hakuona bora - Ndipo yakamtukiwa
505. Tena nawe Shekhe langu - Enenda na Ulimwengu - Kula panapo Mzungu - Ajaye tutanunua
506. Kazi yako wadabiri - Kula panapo nasari - Na fedha kwetu tayari - Wenyewe tutakomboa
507. Na fundi wangu huyuno - Ulimkata mkono - Usinisahau mno - Kaa ukikumbukiya
508. Sina budi tachelea - Kuja kwako kutembea - Mambo ulonifanyia - Ukae ukitambua
509. Tukimaa kuisoma - Abushiri akasema - Hebu Hemedi tazama - Tujue la kutumia
510. Tukaipiga ramli - Tukaiona kitali - Tusikujue mahali - Ambapo kitafikia
511. Hamwambia Abushiri - Mzungu atakhasiri - Lakini tuyadabiri - Usiku tatunduia
512. Hata usiku yuani - Mimi na Jumbe Komani - Tukatazama vyuoni - Tukakiona kitaa
513. Tukakiona kitali - Na kufa wangi rijali - Na kutekwa mangi mali - Na watu kukhasiriwa
514. Na boma likavundika - Na watu kutawanyika - Na humra kumwagika - Wala isiyo mithaa
515. Waganga tukauzana - Hini fali twaiona - Na la kutenda hapana - Shauri la kutumia
516. Jumbe Komani kajibu - Tumwambie Muarabu - Tunaiona harubu - Haifai kunyamaa
517. Hata kukicha yuani - Tukamwita faraghani - Tukamwambia yakini - Harubu itatokea
518. Na vita havitimizi - Siku ashara za mwezi - Mzungu atabarizi - Na viumbe kupotea
519. Abushiri kanatiki - Moyo sikuyasadiki - Kwetu Mzungu hafiki - Hawezi kutujilia
520. La Haula tukakuli - Sote waganga wawili - Tukajua ni dalili - Ya ziumbe kupotea
521. Waganga tukanyamaza - Kuketi kusikiliza - Amri yake Aziza - Atakayotuletea
522. Tusiweze kutamka - Mwenyewe hakuridhika - Kula ambalo ataka - Sote twamfuatia
523. Wakanena madiwani - Mambo hayo mambo gani - Hawa wana wa chuoni - Kutakuwafuatia
524. Jamii tukashangaa - Kupata mwezi sabaa - Tuiwene zilizaa - Bomani kutungilia
525. Twali nyumbani tukele - Tukasikia kelele - Bunduki moja ilile - Na ya pili ikalia
526. Mara zikatwaa kasi - Tukaziona risasi - Pale tulipo jilisi - Risasi kutujilia
527. Kuionakwe zahama - Haondoka hasimama - Kushahidia Karima - Mwinyi ezi na kusaa
528. Kula hatia mkono - Kuna risasi hiino - Haya ni kama kigano - Mambo yalotujilia
529. Nili na wasia wangu - Sipewa na baba yangu - Akanambia mwanangu - Ulimwengu watembea
530. Kwenda uonapo neno - Ambalo ni kubwa mno - Fanya hivi na hivino - Rabbi atakuvuua
531. Papale hayafanyiza - Baba aloniagiza - Hatawakali Aziza - Mwinyi ezi na kusaa
532. Risasi zilizikija - Si risasi ni kioja - Na Wazungu mara moja - Bomani wamejitia
533. Wazungu wamejazana - Na ndia wameziona - Pa kupitia hapana - Ziumbe wakangamia
534. Na nje wamezunguka - Na tifaka zawalika - Akapigwa Mmarika - Risasi ikamuua
535. Watu wamesongamana - Watumwa kwa waungwana - Hapana kusikizana - Kwa watu kuwafaa
536. Amiri wetu Salimu - Kuona mambo magumu - Ndiye alotakadamu - Wa kwanza alokimbia
537. Nami nenda hitazama - Humule ndani ya boma - Haona mahali pema - Pazuri pa kurukia
538. Haruka nyuma ya pili - Punde haona jahili - Ali juu ya khaili - Farasini amekaa
539. Yuenda akadhukuri - Yuko wapi Abushiri - Nambiani askari - Leo anakokwendea
540. Amba ndimi Hambaroni - Shujaa wa Uzunguni - Namtaka nambiani - Leo namhitajia
541. Kumuonakwe Mzungu - Na wenzangu nyuma yangu - Hamtawakali Mungu - Hainama hakimbia
542. Risasi tukilemezwa - Wengine watufukuza - Na nchi kuifingiza - Kama mawingu ya mvua
543. Mizinga ikashtadi - Kutitima kama radi - Na kupigwa tukazidi - Hapo tulipokimbia
544. Kauliwa Mwasumai - Na Mbwana wa Hunei - Na wangapi mashujai - Hapo waliouliwa
545. Twenenda hatuzunguki - Kwa kivumo cha bunduki - Na risasi kama nyuki - Au matone ya mvua
546. Kuionakwe zahama - Hadhukuru Allahumma - Ndiwe mwingi wa rehema - Jalla wa Ala Taaa
547. Ndiwe mnipa salama - Kula panapo nakama - Sina mwengine Karima - Ila ni wewe Mmoya
548. Ndiwe ulonikhuluki - Ndiwe mnipa riziki - Na hapa katika dhiki - Ndiwe mwinyi kunitowa
549. Tena nikanusurika - Kwa karamaze Rabbuka - Pasiwe kukhasirika - Mungu akanivuua
550. Tukiwa mbali yuani - Tuwene moto bomani - Wazungu wagea kani - Kwa kukidhi muradia
551. Boma lote likawaka - Na mali wakayateka - Na maiti kama taka - Isilamu na juhaa
552. Idadi yao juhali - Khamsini na wawili - Ndipo mbali Wasomali - Zaidi ya watu mia
553. Na sisi kwetu idadi - Ni watu mia zaidi - Wa ama hao junudi - Wengi waliopotea
554. Nasi sote Isilamu - Tukaipana Zaramu - Hata usiku fahamu - Tukakutana jamaa
555. Jamii tulionana - Usiku tukauzana - Ndugu zangu hawaona - Wote waliopotea
556. Hapo mwinyi nguo mbili - Tukalala na laili - Kukicha siku ya pili - Abushiri hamwendea
557. Hamwambia Shekhe wangu - Nakuaga nenda zangu - Hino ni kadha ya Mungu - Iliyo kutufika
558. Amri yake Jalia - Hatuwezi izuia - Na Shekhe akanambia - Kweli ulotazamia
559. Mambo uliyoyaona - Yote yamefuatana - Na sasa ni kuagana - Rabbi na kuniombea
560. Tukishapana kwaheri - Tukayandama safari - Bi laili wa nahari - Saadani tukangia
561. Vimetupotea vyuo - Twenenda hatuna nguo - Na kula atuonao - Huruma atuonea
562. Kutuona Bwana Kheri - Nyuso zimetaghayari - Akatuuza khabari - Jamii tukamwambia
563. Akamba pumzikani - Na nguo hizi twaani - Siku mbili ni gangani - Kisha muandame ndia
564. Basi tukapumzika - Na roho zikatushuka - Makafara tukaweka - Mji wote nakwambia
565. Mji tukaufanyiza - Kila ambalo twaweza - Hayo tukesha yasoza - Tuwele kwandama ndia
566. Tukashika ndia yetu - Hata tukafika kwetu - Salimina na wenzetu - Tukaonana jamaa
567. Tena tukapumzika - Siku haba zikafika - Khabari tukipulika - Marikebu zimengia
568. Wajile Majarumani - Wamepiga Saadani - Khamasa wa sabaini - Wazungu walouliwa
569. Wamevitupa vyepeu - Na wingi wa mazibau - Na vitu wamesahau - Vingi vilivyotwaliwa
570. Zikapata siku mbili - Dukhani zikawasili - Ili kuja kudalili - Pangani wapate ngia
571. Twambiwa ziko dukhani - Zimewasili Pangani - Zimekaa milangoni - Sabaa zangojelea
572. Siku ya Jumaa tatu - Tukasikia wenzetu - Kutitima kama chatu - Mizinga mingi kulia
573. Tusikie kutitima - Kama mwamba wa kuvuma - Mizinga yanguruma - Kama raadi na mvua
574. Tukasikia kishindo - Kama cha ndovu na nyundo - Roho zikangia shondo - Kwa wingi wa madufaa
575. Jamii tukayakini - Hivyo vita ni Pangani - Bunduki kama tufani - Ambazo twazisikia
576. Magharibi yakifika - Tukamuona Msaka - Baraza kaitandika - Khabari akatwambia
577. Katwambia Wana Kwetu - Sasa Pangani si yetu - Kule kwenda na viatu - Rabbi ametwondolea
578. Tumepigwa marisasi - Na mizinga ya viasi - Tusikupata nafasi - Hata jua limetua
579. Pangani na Bweni mbili - Zote ni za majahili - Vita hatukukabili - Kwa wingi wa junudia
580. Wana mashua za chuma - Ndizo zilizokwegema - Tusiweze kusimama - Kwa risasi kutujia
581. Ila ni watu wa Bweni - Kwa Mambo Sasa Diwani - Kawambia twenendeni haifai kukimbia
582. Ndio waliopigana - Tangu ikeli mchana - Pasi nafasi kupana - Hata usiku kungia
583. Na sote tumekimbia - Mmoja hakubakia - Mzungu amezuia - Miji yote ametwaa
584. Msaka akimaliza - Mambo yale kutweleza - Tukashukuru Aziza - Ya Pangani kutwaliwa
585. Siku haba zikifika - Tanga wakaja ishika - Wakafika wakashuka - Na bunduki kutukua
586. Wote ahli biladi - Wakamtoa Rashidi - Enda kwa wao junudi - Amani twahitajia
587. Rashidi bin Hasani - Alipowasili pwani - Wote walio mjini - Wakapiga tifakia
588. Kulia kwake bunduki - Rashidi kataharuki - Wazungu wakasadiki - Mashuani kapakiwa
589. Mizinga ikatitima - Na bunduki zikavuma - Wasiweze kusimama - Wa Tanga wakakimbia
590. Rashidi bin Hasani - Akenda merikebuni - Kaona mambo launi - Aliyo kuyakutia
591. Kuwasilikwe fahamu - Kaja wao mualimu - Na huyo wao hakimu - Wakaja wakamwambia
592. Wakamuuza ni nani - Kwetu ujile takani - Akamba nina amani - Ndiyo niliyokujia
593. Mzungu kamtazama - Khatimaye akasema - Huna umbo la Mrima - U mtu gani nambia
594. Kwa kula hakunasibu - Umbolo la Kiarabu - Rashidi kataajabu - Kwa jinsi alivyojua
595. Akamba petu ni Tanga - Na watu wamenichanga - Usiwapige mizinga - Yako watakuridhia
596. Mzungu katakalama - Rudi huko hima hima - Kawete watu wazima - Katika biladi pia
597. Basi Rashidi akaja - Na watu kujikongoja - Kwenenda akiwangoja - Hata wakafikilia
598. Wasishe maneno yao - Wana khofu roho zao - Kisha wakarudi kwao - Jamii wakakimbia
599. Nasi tuliposikia - Jamii tukakimbia - Mashamba tukelemea - Pasiwe mtu mmoya
600. Sote tukakimbiana - Pasiwe kufuatana - Wadachi kushika sana - Miji yote kazuia
601. Miji imeatilika - Watu wote wametoka - Kwa Mzungu aloshika - Hapana tena wasaa
602. Allahuma ya Moletu - Mpe nguvu bwana wetu - Asingiliwe na mtu - Katika wake ulua
603. Allahuma ya Wadudi - Mjaalie Sayyidi - Awashinde mahasidi - Kwa muda wa saa moya
604. Allahuma ya Manani - Mpe nguvu Sultani - Umpe na burhani - Na ezi kumzidia
605. Rabbi mzidishe ezi - Umshindie makozi - Wafanyao virigizi - Uwondoe mara moya
606. Rabbi mzidie jaha - Umzidishe furaha - Umwondolee karaha - Ya mtu kumfanyia
607. Rabbi mzidie sifa - Sayyidi wetu Khalifa - Kwa enzi yako Latifa - Subhana wa Taaa
608. Ya Rabbi mpe umri - Na kula jambo la kheri - Umwondolee na shari - Kwa ezi Yako Jalia
609. Mhifadhi mja wako - Kwa miuja na vituko - Apate kaa kitako - Kwa rohoye kutulia
610. Azitulize biladi - Pasi mwenye kutaadi - Usowe uwe asadi - Utishe kwa watu pia
611. Mja wako mjalie - Aitulize eziye - Na adui mshindie - Ambaye amkamia
612. Mja wako mhifadhi - Kwa kula mwenye gharadhi - Umzidie na hadhi - Kwa majumbe na raia
613. Mja wako msitiri - Umpe na nyingi kheri - Pasiwe mwenye jeuri - Ambaye amfanyia
614. Mjaalie baraka - Katika wake muluka - Na kula mwinyi shabuka - Uwashinde wote pia
615. Pasiwe ajinuaye - Humo katika eziye - Kula amsikiaye - Azidi mnyenyekea
616. Wala pasiwe raia - Kumtaja kwa ubaya - Kula mwinyi kusikia - Azidi mpendelea
617. Mshindie washindani - Wa bara na baharini - Mjaalie amani - Na roho kumtulia
618. Na kula mwinyi kwinuka - Kwa vita na fashabuka - Uwashike kiwenika - Wote wawe maridhia
619. Rabbi takabali dua - Nyanda zangu nainua - Mzidishe na uluwa - Na jaha kumngilia
620. Nyanda zenu inuani - Muombe Mungu Manani - Nasi wetu Sultani - Amjalie wasaa
621. Allahuma Ya Samadi - U peke yako Wahidi - Mzidishie Sayyidi - Ezi yake na ulua
622. Tamati sitakutubu - Kwenda mbali taharibu - Hapa komele sahibu - Mbele siwezi sogea
623. Hapa nikomele basi - Yondoeni karatasi - Kula jambo ni kiasi - Na kuwa na welekea
624. Maneno yendapo sana - Nakhofu kukosekana - Hajisiri kutukana - Aibu ikaingia
625. Mwinyi kutunga utenzi - Hemedi mpelelezi - Bin Abdallah mzazi - Kabila 'lBuhriya
626. Ndimi Hemedi shairi - Bin Abdalah 'lBuhri - Nami ni mtu fakiri - Sina wasaa dunia
627. Lakini kwa Mola wangu - Hupata riziki yangu - Hala mimi na wanangu - Hamshukuru Jalia
628. Na ingawa masikini - Namshukuru Manani - Asubuhi na jioni - Anipa cha kutumia
629. AlHamdu li 'ILahi - Kula siku asubuhi - Kwanza nastafatuhi - Ndipo henda hatembea
630. Na jioni hukipata - Ambacho nala hawata - Sina kondo sina vita - Ni pangu nimetulia
631. Ndio mwisho wa utenzi - Neno wahedi songezi - Wadachi na Wangerezi - Wote nimewatajia
632. Na baitize sikia - Ni bait sitamia - Na thalathini kungia - Na wahedi kuzidia

MWISHO WA UTENZI.

Mtungaji : Hemedi Bin Abdallah Bin Said Bin Abdallah Bin Masudi El Buhry - 1307 Hijria , 1891 AD

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet