.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Awau'za Waswahili!

 

 

 

 

 

 

Related links

Awau'za Waswahili!

  1. Risala enuka hima, sikae 'kataghafali
    N'na jambo 'takutuma, ubalegheshe suali
    Nipate jawabu njema, yenye amani na kweli
    Nauliza Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  2. Lugha nyingi duniyani, zatamkwa mbalimbali
    Na zote ulimwenguni, zina wenyewe mahali
    Si Hindi Si Uzunguni, mewaumbia Jalali
    Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani ?
  3. Wakamba wana kikwao, lugha yao ya asili
    Na Wazungu piya nao, wana zao mbalimbali
    Na Wameru wana yao, wengine ni Wasomali
    Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani ?
  4. Wahindi wana Kihindi, kwa kabila mbalimbali
    Na Wanandi ni Kinandi, ndizo zao akuwali
    Wengine ni Wakilindi, wana yao ya asili
    Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  5. Kuuliza Si ujinga, musinifanye jahili
    Nautafuta niuwanga, tuzinduwane akili
    Ndipo shairi hatunga, kubaleghesha suali
    Nielezwe Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  6. Mara nyingi husikiya, kuwa hichi Kiswahili
    Hakina mtu mmoya, ambaye ni chake kweli
    Na wengine huteteya, kina wenyewe asili
    Ndipo ha'mba Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  7. Masai ana kikwao, lugha ya tangu azali
    Na Mahara wana yao, wengine Mashelisheli
    Na Waluo lugha zao, Si sawa na Maragoli
    Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  8. Na jamii wengineo, wana lugha mbalimbali
    Na kujuwa ya wenzao, ni kujifunza ya pili
    Lakini wana na zao, lugha za tangu asili
    Jee hichi Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  9. Sasa ambalo nataka, kwa wenye kujuwa hili
    Wa Kenya na Tanganyika, na walo kulla mahali
    Nipani ilo hakika, tubalegheshe ukweli
    Nambiyani Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  10. Miye mefikiri mno, kuamuwa jambo hili
    Na huona lugha hino, lazima ina asili
    Kwa sababu kulla neno, lina mwanzo wa usuli
    Ndipo ha'mba Kiswahili, hi lugha ya watu gani?
  11. Na iwapo hivi sivyo, niliyyoamuwa hili
    Nionyeshani viliyyo, mubainishe ukweli
    Nijuwe ambavyo ndivyo, tutowane mushkili
    Kifunuke Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  12. Na iwapo atakuja, wa kunijibu suali
    Namuomba jambo moja, twambiyane kiakili
    Tusionyane miuja, jambo nisilo kubali
    N'anambiye Kiswahili, ni lugha ya watu gani?
  13. Tamati ndio akhiri, na jina langu ni hili
    Ahmadi wa Nasiri, na Bhalo ndilo Ia pili
    Mtungaji mashuhuri, mpenda penye ukweli
    Nambiyani Kiswahili, ni lugha ya watu gani?

 

Ahmad Nassir (Malenga wa Mvita)

Limeletwa Zanzinet na: A. N. Mzanzibari

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet