.

Welcome to Zanzinet Swahili Poems

Where Swahili matters!

Poets Profile

 

 

 

 

 

Related links

 

Poets Profile

Khamis Bin Nassor Al Nabhany

Sh. Khamis Bin Nassor Bin Khamis Al Nabhany alizaliwa tarehe 18 mfungo 8 mwaka 1338H (Februari 9, 1920) katika kijiji cha Piki wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba.

Ni mtoto peke yake kwa baba na mama kwani wazazi wake waliachana muda mfupi tu baada ya kuzaliwa. Udogoni kwake alilelewa na mama yake ambae alizaa watoto wanane na mume wake wa pili na baba yake aliowa mke mwengine na kuzaa watoto tisa.

Sh. Khamis alisoma Qur-an mpaka kukhitimu chuoni kwa maalim Mtwana bin Marzouk hapo hapo Piki. Hakusoma skuli na mpaka leo hii maandishi yake alitumia herufi za kiarabu.

Sh. Khamis alianza kutunga mnamo mwaka 1940. Wakati wa udogo wake, alipenda sana kukaa na ami zake hasa wakati wa jioni kwa mazungumzo. Miongoni mwao wako ambao wakitunga mashairi jambo ambalo lilimfanya aingie katika utungaji". Siku moja katika baraza kama hiyo alikuwepo bwana mmoja jina lake Abdulla bin Muhammed ambae alikua siku hiyo hana furaha kwa khiana aliyofanyiwa na kwa sababu hiyo alikasirika sana na akatunga shairi ambalo Sh. Khamis alikumbuka beti mbili tu zifuatazo:-

Dhila iliyonifika, kwako wewe l-azizi
Kwa kila nikikumbuka, hunizidisha machozi
Maini yaunguzika, na kusubiri siwezi
Nnarudi na machozi, naliya sinyamaziki

Naliya sinyamaziki, hayakatiki machozi
Mabaya wayashiriki, ukinitenda huwazi
Usidhani siudhiki, ni kathara ya mapenz
Nnarudi na machozi, naliya sinyamaziki

Shairi hili lilimvutia sana Sh. Khamis bin Nassor na ndio khasa sababu ya yeye kuanza kutunga.

Sh. Khamis alifariki dunia tarehe 2/3/2003 na ameacha kizuka na watoto wanne wote wa kike. Hakubahatika kupata watoto wa kiume kwani mwanawe wa kwanza ambae alikuwa mwanamume alifariki alipokua mchanga. Wakati wa uhai wake, Sh. Khamis alikuwa fundi wa charahani na pia anajishughulisha na kilimo kama vile migomba, mihogo na mpunga.

Nimalizie maelezo haya mafupi kwa kunukuu maneno yake mwenyewe kama ifuatavyo:

"Mashairi kwangu si sehemu ya kazi bali ni moja ya starehe. Hutunga kutokana na matukio na visa mbali mbali ambavyo tunaviona au wakati tunaokwenda nao".

Ingawa Sh. Khamis ametutoka hapa duniani, sadaka yake ya mashairi itawafaa wengi wanaopenda kusoma tungo za Kiswahili. Mwenyeenzi Mungu ampe malazi mema peponi, Amin.

 

Ali bin Said Al Jahdhamy (Kamange)

 

Mahmoud Ahmad Mahmoud

Maelezo binafsi ya Ustadhi Mahmoud Ahmad Mahmoud:

Mahmoud Ahmed Abdulkadir (MAU) nilizaliwa Amu pwani ya Kenya mwaka 1950 nilisoma madrassa Annajah, sikwenda shule za kawaida.

Ni mwalimu wa madrassa, vile vile nahutubu Ijumaa. Nafundisha somo la dini ya Kiislamu katika shule kadhaa za msingi pia naendesha darasa la watu wazima msikitini. Naelewa vyema lugha ya kiswahili na pia kiarabu vizuri na kiengereza kwa kadiri Fulani. Kadhalika naandika mashairir na natumia lahaja ya kiamu. Naandika katika maudhui tofauti tofauti zaidi mambo ya kijamii na vile vile siasa.

Kwa mara ya kwanza nalijitokeza kusoma shairi nililoandika juu ya uhuru wa Kenya baada ya miaka kumi 12/12/1973. kuanzia hapo nilipata umashuhuri nakutangaa kuwa ni mshairi. Mwaka 1974 niliandika “WASIA WA MABANATI” Utendi wenye baiti 140 ambao ulikua ukielezea mikasa iliyompata msichana aliefanya urafiki na mvulana ambae alimtia mimba na baadae akamruka. 1975 – 1979 niliandia tendi tisa kwa jina la kimondo ambazo zilitumika kufanya kampeni wakati wa uchaguzi wa wabunge hapa Lamu. Mimi nilimsaidia Mzamil Omar Mzamil mpinzani wake alikuwa ni Madhubuti na baada ya hapo niliendelea kuandika mashairi lakini mafupi mafupi na sana huwa ni ya watu binafsi kuhusu mambo yao wenyewe k.m harusi, matanga, safari na kadhalika.

Mwaka wa 2000 niliandika tendi mbili, mmoja kwa jina la UZUNDUZI na wa pili MWANGAZA kujaribu kuwahimiza watu wazundukane na watambue haki zao na kuzitetea. Pia niliandika utendi mrefu wa baiti 700 juu ya haki za uraia vile vile niliandika tendi juu ya Ukimwi, Mihadharati na haki za watoto.

2004 niliandika tendi mbili kwa anwani ya ramani ya maisha ya ndoa, mmoja wa mume na wa pili wa mke. Pia nimeandika mashairi mafupi kadha moja ni kuhusu Ahmad Yassin na lingine kuhusu Faluja, IRAQ. Nina nia ya kuandika utendi juu ya haki za wazazi. Babangu pia alikuwa ni mshairir vile vile mamangu. Mtoto wangu wa kwanza ana kipawa cha ushairi lakini haandiki sana. Mimi nimeoa nina watoto 11, mkubwa na miaka 29 na mdogo ana miaka 8. wasichana ni 7 na wavulana ni wane. Napata mkate wangu wa kila siku kwa uwokaji mikate “BAKERY” kazi ambayo nilirithi kutoka kwa mlezi wangu Ammi yangu, Bwana Abdulghafur Abdulkadir.

Napendelea sana kusoma vitabu mbali mbali zaidi kwa kiarabu. Napenda kuogelea baharini na kusafiri. Kusoma ndio pumbao langu kubwa!! Mwaka jana 2004 nilitunukiwa tuzo ya “THE HEAD OF STATE’S COMMENDATION (HSC- CIVILAN DIVISION).

 

 

  About Us | Zanzinet Home | Contact Us | ©2004 Zanzinet